Kioo kwa viongozi wa CCM, serikali na Rais

Jan 16, 2007
721
176
Uzalendo wa Nyerere unapoitwa wehu, uhuni


Joseph Mihangwa
Disemba 23, 2009
Wakongwe watoa somo, wapinga kuandamwa
Nyerere aomboleza, aliombea Taifa na kutahadharisha
Umma wahoji sifa na uadilifu wa viongozi
MAHALI: Jijini Dar es salaam, jiji linaloshikilia na kuwakilisha kila aina ya maisha ya jamii kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Ni jiji lisilo na "roho" ambamo kila mtu huishi kwa ukali wa meno yake.

Wanaonekana mabwana (waheshimiwa au ndugu?) Joseph Sinde Warioba, Dk. Salim Ahmed Salim, Joseph Butiku na wengine; wamekaa katika hali ya mawazo mazito, huku Profesa Issa Shivji akiwatazama, ameketi pembeni, naye katika hali ya kutafakari juu ya kinachoendelea.

Ni Jaji Joseph Sinde Warioba anayevunja ukimya akisema: “Tabia hii ya kubeza ukweli, kuporomosha matusi na kukejeli fikra za Baba wa Taifa, na baadhi yetu kutukanwa tunapozungumzia mambo ya msingi ya kitaifa, hasa pale tunapowasemea wanyonge wa nchi hii, inatoka wapi? Na kwa nini huyu (Yusuf) Makamba na kundi lake watuite sisi wehu na wahuni kwa kutetea maslahi ya Taifa; katumwa na nani?

Je, tumwache hivi hivi? Matusi yake yapite kwa sababu tu ilisemwa na wahenga kwamba “usibishane na mjinga kwa sababu umma unaweza kushindwa kuelewa ni nani mjinga kati yako na mjinga halisi unayebishana naye?

“Jamani; maoni na maneno yaliyozungumzwa katika Kongamano la kuadhimisha Miaka 10 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hayakuwa yetu sisi tunaoandamwa, bali ni ya washiriki. Ni maneno hayo hayo aliyoyasema Rais Jakaya Kikwete, wakati akihutubia Taifa kutoka Butiama Oktoba 2009, juu ya kuporomoka kwa maadili, uzalendo; rushwa na ufisadi uliokithiri, na hatari inayojionesha ya kusambaratika kwa umoja wa kitaifa. Kwa nini hakuandamwa, ila sisi tu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), miezi miwili baadaye?.

“Ni yale yale aliyoyasema Waziri Mkuu (Mizengo) Pinda hivi karibuni yanayokabili nchi yetu kwamba (akimnukuu) “Kuna hatari ya matajiri wachache kuendesha maisha ya masikini walio wengi kwa njia ambayo itazidi kuwaongezea utajiri, huku ikiwadidimiza zaidi masikini. Si ajabu matajiri hao wachache wakawa ndio wanaoendesha vyama vya siasa, Serikali, Mahakama, Bunge, Misikiti na Makanisa”. Kwa nini mambo hayo yanaposemwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere tunashambuliwa na kuitwa wehu na wahuni?”

Butiku, kana kwamba naye haamini ilivyotokea, huku akionyesha kukerwa dhahiri na mashambulizi dhidi yao anadakia: “Mambo ya ajabu kabisa haya; viongozi wamepoteza dira, hawana uchungu na nchi yao; kazi imebaki kuandama kila mpenda haki!. Hivi kweli wote waliotoa mawazo yao katika kongamano hili ni wehu na wahuni?”

Huku akipitia orodha ya waliohudhuria kongamano lililohusisha washiriki 200, anataja majina makubwa makubwa, taratibu: “Walikuwamo Fredrick Sumaye, Profesa Shivji, huyu hapa; Profesa Mwesiga Baregu, Balozi Daud Mwakawago, Askofu (mstaafu) Elineza Sendero, Askofu Methodius Kilaini; Wajumbe wa NEC ya CCM, Kate Kamba na Nape Nnauye; Ma-Jenerali wastaafu wa JWTZ; maprofesa na wahadhiri wa vyuo vikuu; mabalozi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za nchini na za kimataifa, orodha ni ndefu…

“Hawa ndio waliochangia mada kuu ambazo zilihusu: Watu na Uzalendo, Watu na Siasa, Uongozi, rasilimali za Taifa na utandawazi. Je, wote hawa nao ni wehu na wahuni?

“Yaliyojadiliwa ndiyo hasa yenye kuwakilisha fikra za Mwalimu Nyerere, juu ya kusimamia haki za wanyonge wa nchi hii. Na hao wanaotuandama, kwa nini wanajifanya kuzienzi fikra za Mwalimu kwa kuweka siku ya Kumbukumbu ya kifo chake, kwa gharama, lakini wanatenda kinyume, kama si unafiki mtupu? Heri Yuda Iskariote, aliyemsaliti kiongozi wake hadharani akiwa hai; kuliko msaliti wa kiongozi aliyetangulia mbele ya haki. Msaliti wa aina hii hawezi kuepuka laana ya milele; na alaaniwe kikweli kweli.

“Na kwa nini twapuuzwa sisi Mitume kumi na mmoja, watetea haki na usawa kwa wote; tukilazimishwa kuishi kwa hofu ya kujifungia ndani, baada ya kupaa kwa Bwana wetu, hadi siku ya Pentekoste? Hatuwezi kukubali kutishwa; wala matusi (ya Makamba) hayawezi kutunyima usingizi ”, anafoka akionyesha ghadhabu iliyo dhahiri.

Wakati wote huo, Profesa Shivji, ambaye ni Mkuu wa “Kigoda” cha taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, akiwatazama tu kwa fikra nzito; lakini akielewa kuwa nchi inapita kipindi kigumu mithili ya kile cha Ufaransa kabla ya Mapinduzi mashuhuri ya 1789, ambacho, Mwandishi Alex de Tocqueville, anaielezea jamii ya kipindi kile katika kitabu chake “The Ancien Regime and The French Revolution” (uk 13 na 18) kama ifuatavyo:

Ilikuwa Jamii ya Kiraia iliyoota kutu: watu wasioelewana, Taasisi zikiporomoka, mawazo kinzani yakichipuka. Kama magugu katika shamba lenye rutuba lililotelekezwa …

Lakini mapambazuko ya enzi ya demokrasia mpya tayari yalikuwa mlangoni; na ilikuwa busara kukubaliana nayo kuepuka makuu na mtafaruku wa kijamii na umwagaji damu; lakini watawala wakayabeza.

Mara wote wanakuwa kimya, wakitazamana; kila mmoja akitafakari, si tu juu ya namna ya kubaini na kupiga vita maradhi yanayoisibu jamii ya Kitanzania na yatakayoiua; bali pia namna ya kuiokoa. Anaingia Makamba, mara anatoka hima kwa kuona hali ilivyohasi kwake, akirudia “wehu hawa; wahuni hawa”. Wanamwangalia akitoka.

Kisha mmoja wa waliopo anavunja ukimya akisema: “Mabwana, nimegundua, tena si leo, bali siku nyingi zilizopita; kwamba tofauti na enzi za Serikali ya Awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere, hakuna usawa katika Tanzania ya leo, kisiasa, kijamii, kiuchumi au kisheria; Watanzania hawako huru.

“Ugonjwa wa kwanza unaoisumbua nchi ni ubinafsi, unafiki na umamluki wa viongozi ambao wako tayari hata kuwauza wananchi na uhuru wa nchi kwa ubeberu mpya wa kimataifa. Ugonjwa wa pili ni wa chama tawala na Serikali kutekwa na kikundi cha matajiri wa hapa nchini, na mafisadi ambao ndio wanaoelekeza siasa ya nchi, ili kulinda maslahi yao binafsi, kama alivyobainisha Komredi Warioba sasa hivi. Kwa sababu hii, nguvu ya uchumi na siasa sasa vimo mikononi mwa vikundi vinavyotawaliwa na uchu wa kujitajirisha kwa gharama yoyote ile. Na ni vikundi hivi hivi vinavyofanya maamuzi muhimu nchini, na wakati huo huo kujihakikisha kuwa havifahamiki kwa umma visipate kibano.

“Ni vikundi hatari kwa usalama wa nchi na kwa raia mmoja mmoja, kwani vimeweza kupenyeza watu (mamluki) wake katika vyama vya siasa, mahakama, bunge, makanisani na misikitini, kama alivyobaini Waziri Mkuu Pinda. Hili ndilo kundi lililowanunua na kuwafuga viongozi ambao sasa wanadiriki kuwaita “wehu na wahuni” wapigania haki za wanyonge wa nchi hii; watu wanaosimama kidete kupinga mbinu zote zinazofanywa kuirejesha nchi yetu utumwani kwa mara ya pili. Enzi za Mwalimu, wasingethubutu kusaliti umma kwa kiwango hiki!”

Profesa Shivji: “Wamesaliti Katiba ya nchi juu ya demokrasia na usimamizi wa uchumi wa nchi, bila hofu ya kuhojiwa wala kuwajibishwa; kwa sababu wameziteka na kuzihodhi idara za Serikali na taasisi za Umma zenye jukumu la kusimamia haki na usawa katika nchi.

Ananukuu Katiba (ibara ya 3 na 9), kisha anahoji: “Katiba ya nchi inatambua kuwa Jamhuri ya Muungano ni nchi ya demokrasia na ya Kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa; lakini uko wapi Ujamaa katika sera za leo za maendeleo? Ziko wapi taasisi za Kijamaa? Tumeziua zote kwa hila na kwa kununuliwa. Ni Ujamaa gani huo, kwa dola kujitoa katika shughuli za uchumi, pamoja na hata katika sekta za huduma za kijamii kama elimu, afya, maji, umeme na mipango ya maendeleo?

“Tunadiriki kwa ujasiri wa kifisadi, kuwaita wanaotumia haki yao ya kikatiba kuhoji, eti ni wehu na wahuni! Katiba yetu inataka ihakikishwe kwamba, matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi, na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada za kuondosha umasikini, ujinga na maradhi; na pia kwamba, shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi.

“Na ili kuhakikisha hayo, nchi (lazima) itawaliwe kwa kufuata misingi ya demokrasia na Ujamaa. Hao wanaowaita wenzao wehu na wahuni, watakeni waueleze umma, juu ya utajiri wa nchi na rasilimali zilizouzwa kwa wawekezaji chini ya mikataba mibovu, sasa zinatumika kwa maendeleo ya nani? Mbona uporaji unapodhihirika hatua hazichukuliwi, eti kwa hofu ya Serikali kushitakiwa? Tangu lini mwizi au jambazi, poraji likawa na haki ya kisheria dhidi ya mtu anayeporwa?.

“Waulizeni waeleze mbele ya kadamnasi, hao wanaowaiteni wehu na wahuni, mali na njia kuu za uchumi wa nchi zimo katika mamlaka ya nani, kufuatia ubinafsishaji usiojali, tena kwa bei ya kutupa?. Na kama haya yamewashinda, kwa nini wasirekebishe Katiba tujue moja tu, kwamba nchi imeuzwa, na wananchi wamerejeshwa utumwani, badala ya kuendelea kudanyganya.

“Lakini hawathubutu kusema hivyo, kwani wanazijua dhambi zao; wanaijua ghadhabu ya Umma! Wataendelea kuwaiteni “wehu na wahuni” kifichoni; lakini ole wao, pale Umma utakapobaini hayo, na kutenda! Furahini, asubuhi i karibu; kuna dalili za kupambazuka!. Imbeni kwa furaha, ukombozi u karibu”.

Huku wangali wakimsikiliza Profesha Shivji akimalizia maelezo yake, ghafla upepo wa msokoto unatikisa milango na madirisha, na cheche mithili ya ndimi za moto zinajaa chumbani; na bila ya kuamini macho yao, anaingia kwa kasi, Mwalimu Nyerere anawasalimia kwa majina; kisha anakaa mbele yao: “Mbona mnaonekana mu wapweke, wanyonge wenye wasiwasi na msiojiamini mfanyacho?”, anahoji Mwalimu.

Huku wangali katika hali ya mshituko na mshangao, wakitazamana nani aanze kujibu swali, ni Jaji Warioba anayejitosa kwa ujasiri wa woga akisema: “Mwalimu, tangu walipolibwaga chini Azimio la Arusha mwaka 1992 huko Zanzíbar, na tangu ulipotuhama hapa duniani; tumekuwa wakiwa kama ndege juu ya paa; tunawindwa na kuandamwa kama bundi, kwa sababu tu ya kuzienzi, kuzitetea na kuzishamirisha fikra zako katika jamii ya Kitanzania.

“Bila kuficha Mwalimu; mpaka leo, fikra zako ni silaha kamili ya mapambano dhidi ya maovu yote ya kijamii; waovu hutetemeka, wahujumu na mafisadi hulegea miguu na akili, fikra zako zinapowekwa wazi. Kila mtu, wakubwa kwa wadogo, hata wale ambao hawakuwahi kukuona au kukusikia ukiwa hai, hutulia kusikiliza hotuba zako zilizorekodiwa, nao hutoka bila swali, bali ujasiri wa kimapambano.

“Na katika hali tuliyomo, ya nchi kukosa dira, maadili ya uongozi na ya Taifa; ufisadi na mafisadi kukalia kiti cha mbele katika uchumi wa nchi; Sherehe za Kumbukumbu ya kuhama kwako zimetiwa maji kwa kuunganishwa na Sherehe za kuzima Mwenge, ili tu jina na fikra zako zisijitokeze na kuwasha moto wa kimapinduzi dhidi ya maovu yanayoinyemelea jamii yetu, na yakipigwa upatu na wasaliti wako.

“Mwalimu, nchi uliyotuachia imeota kutu na hawataki kutusaidia; badala yake wanatushambulia na kutuita wehu na wahuni. Hata wale uliodhani unawarithisha uongozi kwa manufaa ya nchi, sasa wameungana na maharamia kuangamiza nchi; na licha ya kuusaliti umma pamoja na wewe, wanataka jina lako lifutike katika historia ya nchi.

“Hata yule Mjamaa wa kutupa hapo kale, Kingunge Ngombale Mwiru, uliyetuaminisha kwamba ndiye “Mjamaa” machachari kuweza kutetea Ujamaa na Katiba, akapewa heshima ya kupata uwaziri wa chee kwenye serikali za awamu zote tatu baada ya wewe, sasa si mwenzio tena; ameingia na kunaswa katika mchezo wa mashetani, hawezi kuwasemea wanyonge tena.”

Wakati huu Butiku anaanza kuzinduka baada ya cheche za ndimi za moto na kudakiza: “Tena Mwalimu, tofauti na enzi za awamu yako, ambapo chama kiliwasemea watu, sasa chama kinawasemea, kuwalinda na kuwatetea viongozi, matajiri na wafanyabiashara wakubwa.

“Tumefikia mahali sasa fedha inanunua siasa na chama; kwa maana ya kwamba, huwezi kupata uongozi bila kuwa na fedha nyingi; na siasa inanunua fedha, kwa maana kwamba uongozi maana yake ni kuingia pepo ya utajiri mkubwa.

“Viongozi wanakuwa wanyenyekevu kwa wananchi wakati tu wa kuomba kura, na baada ya hapo huwatelekeza watu mpaka uchaguzi unaofuata. Huu ni unafiki mkubwa; na kama ulivyosema katika tafsiri yako ya Kitabu cha Julius Caesar (kitendo II Onesho la I), ukimnukuu Brutus, kwamba “Unyenyekevu ni ngazi ya mtaka cheo; ambayo anayepanda, huitazama kwa juu; bali akishakanyaga kile kipago cha mwisho; akatazama mawingu na kudharau vya chini”. Ndivyo ilivyo sampuli ya viongozi wa leo hapa nchini.

“Hatuna viongozi wa aina ya Jamhuri ya Plato, ambao, kama ulivyoeleza katika Kitabu chako “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania” (uk 8), kwamba “wenye uwezo wa kutawala, mara nyingi hawapendi kutawala; na wanapotawala, hutamani kutua mzigo haraka wanapomaliza awamu yao ya kutawala na kufurahia kurudia shughuli zao za zamani”. Watawala wetu wa leo wanapenda sana kutawala hata kama hawana uwezo; wala hawapendi kung’atuka kama ulivyofanya wewe.

“Kwa sababu hii, kazi pekee iliyobakia kwa viongozi baada ya uchaguzi mmoja hadi unaofuata, ni ya kupanga mikakati pekee na kutekeleza mapambano ya kubakia madarakani, badala ya mipango ya maendeleo ya nchi kwa manufaa ya wananchi.

“Na kwa sababu chama cha siasa ndicho njia pekee sasa ya kupatia uongozi, nacho leo kimevamiwa na kutekwa na matajiri wenye nia ya kuhodhi maamuzi ya chama na serikali kwa manufaa yao; hakiwasemei watu wadogo tena. Na hili uliliona na kuonya mapema mno tangu mwaka 1962; na ukalibainisha tena katika Kitabu chako: Tujisahihishe uliposema, “TANU hakiwezi kudumu kama chama, kama wanachama wake, na hasa viongozi, watauona utendaji wake kwa misingi ya mahitaji yao, badala ya mahitaji ya watu kwa ujumla. Huo ni ugonjwa wa hatari ndani ya chama”.

“Na ulisema tena, katika kitabu chako: Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Uk. 66) kwamba ubovu wa uongozi ndani ya CCM, ndio uliofanya upendekeze tuanzishe mfumo wa vyama vingi, ili kuondoa kansa ndani ya chama hiki”. Ulitahadharisha kuwa, bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi, chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu; na kwamba, hali ilivyokuwa nchini (hadi sasa) halikuwa jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi!

“Leo, tunapokikosoa chama na serikali, hawa kina Makamba wanatuita wehu na wahuni. Ni ujinga mtupu; ni upumbavu, kama ulivyosema, kwa viongozi wetu hivi sasa kuogopa kutumia nguvu za hoja ili kufikia maamuzi muhimu.

“Ni kweli, kama ulivyobaini, kuwa wanatumia hila zaidi kuliko hoja; vitisho kwao ni mbinu rahisi zaidi kuliko adha ya kutumia akili na kupata hoja safi ya kumjibu mpinzani katika mjadala.

“Na katika taarifa yako uliyoipa jina The Arusha Declaration: Ten years After, ulisema: Uongozi wa vitisho si uongozi hata kidogo, na unaweza kufanya kazi kwa kipindi tu. Ulisema, watu wanapohoji maamuzi (ya viongozi) ya kijinga, wanatumia haki yao hiyo ya Kikatiba kama raia. Na wanapohoji maamuzi yasiyo ya kijinga, wanaweza kuelimishwa, kwa nini maamuzi hayo yamefikiwa na yana maanisha nini”.

“Tena ulisema: viongozi wanatenda kwa ajili ya, na kwa niaba ya watu; hivi kwamba kueleza mambo mpaka wakaelewa (badala ya kufoka au kuwaita wahuni) ni sehemu muhimu ya kazi yao”.

“Na tena katika kitabu: Binadamu na Maendeleo ulisema watu wenye mawazo tofauti, hata wakiwa wachache, lazima wawe na haki ya kutoa mawazo yao katika majadiliano bila hofu ya kusumbuliwa; labda mawazo yao yashindwe katika hoja za majadiliano, na si kwa vitisho kwa mabavu. Ukaasa kwamba, uongozi hauwezi kuchukua nafasi ya demokrasia; uongozi lazima uwe sehemu ya demokrasia.

“Hivi huyu Yusuf Makamba, ametoa wapi ujasiri wa kutuita sisi “wehu na wahuni”? Tunaanza kukubali sasa kwamba chama kinaongozwa na wahuni, wacheza ndomboro.

“Makamba na kundi lake watahadharishwe, waache kutupia mawe wapita njia, wakijua wao wenyewe wanaishi kwenye nyumba za kuta za vioo; kwamba siku wapita njia hao nao watakapoamua kujibu mapigo kwa kurudisha mawe, nyumba zao zitasambaratika hima.”

Wakati wote huo, Dk. Salim amekaa kimya, mara kwa mara akionyesha kuteta jambo na Mwalimu; kisha anainua uso akiwaangalia wenzake na kusema, mithili ya mtu anayeomba dua, akimnukuu Shaaban Robert, katika shairi “Nilinde”

“Ni weledi wa kusema, watu wa leo;
Na elimu na hekima, si haba kwao.
Bali hawana huruma, katika moyo;
Na fahari na heshima, ni chache kwao.
Tamthili ya wanyama, mfano wao,
Kisha waweza kuuma, sumu wanayo,
Ee Mungu mwenye uzima; tulinde nao”

Anamtazama Mwalimu kwa huzuni na uchungu mkubwa, kisha anaendelea: “Ukweli ni kuwa, pamoja na kwamba tunazo taasisi kadhaa za kidemokrasia nchini, baadhi ya viongozi wa chama na serikali hawawasikilizi watu; wanaona rahisi kuwaambia cha kufanya bila kutoa muda wa majadiliano; hawapendi kukosolewa, na wako tayari kudhuru kwa sumu kutetea, kulinda ubinafsi na ujinga wao kwa gharama ya demokrasia nchini.

“Fikra zako Mwalimu ni kaa la moto linalounguza, ila kwa walio safi na waadilifu katika jamii, kwa fikra na kwa matendo. Ni kwa sababu hii tunawindwa na kutengwa na malimbukeni hawa wa ufisadi. Fikra zako ni “takatifu” ambazo lazima mtu ajitakase kwanza kabla ya kupanda jukwaani kuzielezea, la sivyo zaweza kukubwaga chini; yataka mtu kwanza ajikane mwenyewe kwa kubeba vema msalaba wake (na si kuwabebesha wengine msalaba wake) ili watu wamsikilize, la sivyo watamtemea mate usoni.

“Utamaduni uliozuka hivi karibuni; wa wabunge na viongozi wengine kuzomewa hadharani si wa bure, ni kwa sababu hii; na utaendelea kama viongozi hawabadiliki.

“Kuzuia changamoto kutoka kwa watu na kuendekeza utamaduni wa kutokosolewa na kutojikosoa, maana yake ni kukumbatia makosa makubwa yanayoweza kuangamiza mustakabali wa taifa na matarajio ya wananchi wema wasio na hatia. Kuna hatari kubwa mbili kwa hili, ambazo sasa zinatishia amani na utulivu katika nchi yetu. Ya kwanza ni kwa viongozi kujenga tabia ya kujipongeza (kwa unafiki), hata pale pasipostahili kupongezwa au kujipongeza, kwa mshangao wa wananchi; ambapo ukimya wa wananchi hao, unatafsiriwa kwa kupotoshwa na viongozi hao kuwa ni ishara ya amani! Je, hukuonya katika Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania, kwamba, kimya kimya tusidhani ni ishara ya amani, na kunukuu vyema Shairi la Bwana Muyaka bin Haji, juu ya jambo hili? (Anachambua maandishi yaliyopo mezani, kisha anasoma):-

“Kimya kina mshindo mkuu, ndivyo wambavyo wavyele;
Kimya chataka kumbuu, viunoni mtatile;
Kimya msikidharau, nami sikidharawile;
Kimya kina mambo mbele; tahadharini na kimya”.

“Kwa mfano, kuna nini cha kujipongeza kuhusu maendeleo, wakati serikali imejivua jukumu la kupanga na kusimamia uchumi wa Taifa kwa shinikizo la Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), yanayotaka nguvu ya soko ndiyo itawale na kuongoza uchumi?

“Kuna nini cha kujipongeza juu ya maendeleo, wakati ufa kati ya walio nacho na wasio nacho umepanuka mara dufu tangu kuzikwa kwa Azimio la Arusha huko Zanzíbar mwaka 1992?

“Halmashauri Kuu ya CCM iliketi Unguja na kufanya maasi na usaliti mkubwa kwa Umma, kwa kubadili Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni ya wananchi. Ubaya wao ni kwamba, jambo lenyewe walilifanya kwa hila na kwa “janja janja” kwa nguvu ya rupia ya mafisadi na nyang’au wanaotaka kuliangamiza Taifa na maisha ya Watanzania! Na kwa nini mpaka sasa wanaendelea kudanganya wananchi kwamba sera ya CCM bado ni ya Ujamaa na Kujitegemea wakati ni kinyume chake?

“Kuna nini cha kujipongeza au kupongezwa, wakati adui umasikini, maradhi na ujinga vinapiga hodi kwa nguvu, wakati utajiri wa nchi unahamia hima mikononi mwa vikundi vya Watanzania wachache na wageni? Kwa nini waendelee kudanganya wananchi (Katiba ya nchi, ibara ya 9 inatamka), “kwamba shughuli za Serikali zitatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla; na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine”, wakati utekelezaji ni kinyume chake? Kama huu si usanii, uzandiki, ni nini?.

“Kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi, na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umasikini, ujinga na maradhi”, wakati utekelezaji ni kinyume chake? Kama huu si usaliti kwa umma na unafiki, ni nini?

“Kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi, wakati utekelezaji ni kinyume chake? Kwa nini wanaendelea kudanganya watu kwa hilo, wakati tumebinafsisha kila kitu kilicho cha umma, tena kwa bei ya kutupa?

“Wakubwa wamejiuzia nyumba za Serikali, wananyakua kila kinachoweza kunyakulika hadi migodi ya makaa ya mawe, chini ya sera za “Chukua Chako Mapema ama maarufu kama CCM ”; kana kwamba wanajiandaa kuishi ughaibuni? Je, ni kwa sababu hii wanaandaa Muswada wa Uraia wa nchi mbili ili tuwe na watu wasiokamatika? Tangu lini popo akawa Mzalendo, mwenye msimamo thabiti?

“Ni nani mhuni na mwehu, kati ya anayepiga vita uporaji huu tunavyofanya sisi, na anayekumbatia ifisadi huu? Kuna kipi cha kujipongeza wakati idadi ya watu wasiojua kusoma wala kuandika, imeongezeka kwa asilimia 35% tangu 1992, ambapo kabla ya hapo nchi yetu iliongoza barani Afrika kwa idadi ya wanaojua kusoma na kuandika?.

“Lipi la kujivunia kwa nchi, ambayo Serikali yake inaendeshwa asilimia 50 kwa fedha ya kufadhiliwa na misaada kutoka nje, ambapo kila dola moja tunayofadhiliwa wafadhili wanavuna dola 2.5 kutokana na mikataba mibovu na uwekezaji na riba? Na katika uwekezaji, wakati wawekezaji wamekomba kila kitu kwa kutulipa asilimia tatu tu ya kivuno, wao wanabeba asilimia 97 kutokana na mikataba mibovu?

“Kuna nini cha kujivunia, wakati deni la nchi linaongezeka puta kutoka Sh. 8bn kabla ya 1992, na sasa limefikia Sh. 12 trilioni, kiwango cha kutisha tangu Uhuru; huku tukiendelea kutembeza bakuli la omba omba nje ya nchi, wakati huo huo tumefungua milango kwa utajiri wetu kuporwa, na nchi kugeuzwa Shamba la Bibi?. Iko wapi nafuu tunayodanganyiwa, ya kufutiwa madeni kwa utii wetu, wakati deni likiongezeka?

“Maendeleo gani haya, ambapo mwananchi wa kawaida hawezi kumudu hata kidonge cha aspirini au karo ya mwanaye, wakati wengine wakisomesha watoto wao kwenye Shule za Kimataifa na matibabu nchi za nje, wakila na kusaza?

“Mwalimu, ulikwishatuasa tangu mwanzo, kwamba maendeleo maana yake ni maendeleo ya watu. Mabarabara ambayo tunajitapa nayo, majumba, kuongeza mazao, (Kilimo Kwanza?), na vitu vingine vya aina hii, si maendeleo. Ulisema, maendeleo yasiyokuwa maendeleo ya watu yanaweza yakawapendeza wataalamu wa historia wa mwaka 3000, lakini kwetu sisi hayahusiani na maisha ya kesho tunayopaswa kujenga.

“Ulitoa mfano wa Mapiramidi ya Misri, na mabarabara ya Warumi yaliyoko Ulaya, kwamba yalikuwa maendeleo ya vitu ambayo mpaka leo yanatushangaza. Lakini kwa kuwa yalikuwa majengo tu, na watu wa wakati huo hawakuendelea (kama ambavyo sisi tulivyo), basi dola na utamaduni wake vimeteketea zamani. Nasi tusipojitahadhari, dola na utamaduni wetu umo hatarini kuteketea muda si mrefu. Hawa wanaotuita “wehu na wahuni” yafaa wakachunguzwe akili.

“Viongozi wasijidanganye kwamba Mtanzania wa leo ni sawa na yule wa mwaka 1947, ambaye hakujua vyema haki zake. Leo, ukiwabania watu haki zao, watazitafuta kwa njia yoyote ile.

“Kudai kwamba asilimia 70 ya Watanzania hufuata upepo, kama alivyodai kiongozi mmoja hivi karibuni, ni ishara ya kutowaelewa Watanzania; ni tamko la kuwadhalilisha. Pengine ni kwa sababu hii viongozi wetu wanajifanyia mambo watakavyo bila hofu ya kuwajibishwa kwa imani hii.

“Serikali ya Mfalme Louis wa XVI wa Ufaransa, ilipinduliwa na walala hoi mwaka 1789 kama hao asilimia 70 tunaowadharau, kwa sababu ilijidanganya kulikuwa na amani na utulivu, wakati ilikuwa ni kinyume chake; lakini kishindo kilimshutua wakati amekwishachelewa. Tamko kama hili linatokana na kutokuwapo maono miongoni mwa viongozi.

“Mwalimu, naomba nikurejeshe kwa Nicccolo Machiavelli, katika The Prince (Mtawala) juu ya umuhimu wa maono katika utawala na kwa utawala, alisema: “Katika mambo ya Taifa, kujua kwa mbali (maono, jambo ambalo ni zawadi kwa mtu mwenye busara) maovu (mitafaruku) inayowaziwa katika nchi ni vyepesi kuyaponya. Lakini kwa sababu ya kutotambulika mbele, yakaachwa yakue kila mtu apate kuyatambua, hapatakuwapo dawa zozote za kufaa”.

“Viongozi wetu wanaatamia maovu, matatizo na kero za watu. Ni wazi kwamba, kwa kufanya hivyo, wanalea au kuficha ugonjwa na kama ulivyozoea kutuasa, kilio kinachoepukika kitakuja kutuumbua na kwa gharama ya mazishi”.

“Mwalimu; sisi hatuwachukii viongozi wetu, wala hatuna sababu ya kuwaonea wivu; ila tu tunatahadharisha na kuonya. Machiavelli anafafanua pia ni wakati gani kiongozi huchukiwa na watu, anasema:

“Mtawala huchukiwa, akiwa mchoyo (hatoi matunda ya kuwa madarakani) na akanyang’anya mali iliyokuwa ya raia (ubinafsishaji usiojali, uporaji ardhi). Mtawala hudharauliwa kwa kufikiriwa kuwa mgeugeu, mpuzi, mwoga, mwenye moyo hafifu, dhaifu; mambo ambayo yanamlazimu ajilinde; na yampasa kuonyesha katika vitendo vyake ukubwa (mamlaka), ushujaa, utaratibu (kufuata Katiba, utawala wa sheria) na uvumilivu (asiyelipa kisasi); na katika vitendo vyake aonyeshe kwamba hukumu zake (maamuzi) zinatekelezeka na hazibadiliki; ahifadhi sifa zake (ili) yeyote (marafiki, wanamtandao) asiweze kutumaini (upendeleo), ama kumdanganya au kumzunguka”. Huo ni mtazamo wa Machiavelli ambao una umuhimu mkubwa nchini mwetu, hasa katika mazingira ya sasa.

“Hatari ya pili, mbali na ile ya kupongezana, ni kwa viongozi kujenga aina fulani ya aibu kwa viongozi wenzao kama tabaka, na kuanza kuogopana, ambapo hatima yake uongozi unakuwa wa “Nikune mgongo wangu, nami nitakukuna wako”, kwa maana ya kutenda maovu na kufichiana siri au kulindana.

“Katika hali ya uongozi kama huo, hakuna la manufaa kwa wananchi linaloweza kupangwa na kutekelezwa; maadili ya Taifa huyoyoma, uadilifu na uwajibikaji hutoweka, badala yake hujengeka tabia ya unafiki, utamaduni wa kujipendekeza na ubabaishaji. Hawa wanaotuita “Wehu na Wahuni” ni wa sampli hii ya uongozi”.

“Mwisho, kutokuwapo utamaduni wa kukosoa na kukosolewa huzaa maringo, majivuno na utawala wa mkono wa chuma, kutovumiliana na kukosa maridhiano. Huu ndio mwanzo wa utungu katika nchi; huu ndio mwanzo wa udikteta, uwe udikteta wa vikundi au wa chama madarakani; unaozaa chuki, ubaguzi na kusambaratika kwa umoja wa kitaifa.

“Umoja wa kitaifa unapotoweka, viongozi, watawala na wafanyabiashara wakubwa wanaoweza kukiteka chama hujihesabu kuwa ni miungu wadogo; na kwa ngazi za chini, uonevu hushamiri na haki za raia kuporwa; utamaduni wa kuabudu “Mashujaa” (hero worshiping) hujikita; ambapo “washindi” wanaweza kutenda lolote lenye machukizo kwa jamii bila hofu ya kuwajibishwa; wanaweza kupora rasilimali za taifa na mali, wakalindwa hata kupokewa kwa kuandaliwa zulia jekundu vijijini kwa ushujaa wao wa kifisadi. Haya yametokea na yanaendelea kutokea kote nchini.

“Wanaotuita wehu na wahuni ni wajinga wa kutupa, hasa wanapojifanya kwamba ukweli huu si ukweli; na zaidi, wanapojifanya kusahau usia wako katika The Arusha Declaration: Ten Years After (Uk. 8), ulipotuasa kwamba “Mambo mabaya hayawezi kutoweka kwa sababu tu tunajifanya hayapo, au kwa sababu tunawatuhumu wengine kuyavalia njuga. Sisi tumekubali kuyavalia njuga, wala kelele za akina Makamba haziwezi kutunyima usingizi. Tutazidi kuyaweka wazi makosa ya wakubwa, ili umma uelewe adui yao ni nani hasa, ili watende kwa kuchukua hatua zinazostahili, mpaka kieleweke. Je, Shaaban Robert hakutueleza kwamba maovu ya wakubwa ni lazima kutangazwa kwa sababu yanadhuru nchi? (Anasoma);

“Kosa la mtu mdogo, kutangazwa si muhimu;
Hasara yake kidogo, kama la mwendawazimu,
Kosa la mtu mkubwa, wajibu kulitangaza,
Kwa herufi kubwa kubwa, na wino wa kuangaza.

Mdogo hatendi jambo, dunia lenye kimo,
Kulitangaza uchimbo, makubwa yakiwamo,
Dunia huharibiwa, kwa makosa ya wakubwa,
Lakini husetiriwa, kwa bidii yakazibwa,
Si kinyume cha dunia, wadogo kuadhirika,
Wakubwa wenye hatia, wakazidi kutukuka.

“Mwalimu, tumetahadharisha na kuonya mara nyingi kwa misingi ya fikra zako, juu ya ukweli, kwamba UKWELI unatabia moja nzuri; kwa mkubwa na mdogo ukweli ni ule ule; na mtu mwenye kubeza ukweli mwisho ni majuto. Serikali ya Mfalme Louis wa XVI wa Ufaransa ilipinduliwa na walala hoi, si kwa sababu ilikuwa nyuma au ya kizamani; bali ni kwa sababu ilikuwa ya kisasa, kuliko zingine zote barani Ulaya; lakini ilibeza UKWELI kuhusu yaliyokuwa yakitokea katika jamii, na hasa kwa hao asilimia 70 ambao tunajidanganya kuwa ni “bendera fuata upepo”.

“Wahenga hawakukosea kwa kubaini kuwa, ugonjwa hatari unaoweza kumuua mbwa ni ule unaomziba pua; kwa maana atakosa fahamu na uwezo wa kunusa na kula sumu. Jamii yetu, na hasa viongozi, wanaugua ugonjwa huo; na kwa sababu wamepungukiwa fahamu na uwezo wa kunusa, wanadiriki kutuita wehu; uendawazimu umewapanda, wanapepesuka. Je, hawa kweli wanastahili kuongoza nchi? Angalia tunapowakumbusha ukweli, haraka haraka wanatunga sababu za ovyo dhidi yetu; eti tunamwandama Rais kwa kumuonea wivu, kwa kuwa eti tulishindwa katika kinyang’anyiro cha Urais mwaka 2005. Ni unafiki huu.

Dk. Aleck Che Mponda, ambaye alikuwa kimya tangu mwanzo akitafakari yote, anaonekana kupandisha jazba dhidi ya wanaoiandama Taasisi ya Mwalimu Nyerere, na dhidi ya viongozi wanaoonekana kuwa hawawezi kuongoza au kushika madaraka kwa heshima na uadilifu. Anaona heri serikali za wanyama, ndege, na wadudu kuliko serikali ya viongozi wenye kudhulumu wanyonge. (Akisoma shairi la Shaaban Robert);

“Serikali za Wanyama, na ndege au wadudu,
Ndani zina taadhima, kama kwamba maabudu,
Na watu wenye heshima, heri mnyama na dudu,
Vinywa vimewaachama, tamu imekuwa ngwadu,
Na heshima imehama, baki taka la mashudu,
Na madhara na dhuluma, miungu ya kuabudu,
Na mambo haya si mema, watu yanawahusudu,
Hizi husemwa ni zama, za watu kufa kibudu,
Kufa wangali wazima, na nguvu za kusujudu,
Na maudhi na hasama, kwao kashata la ladu”.

Mwalimu anaonekana kuguswa na maneno ya Che Mponda; kwa nchi aliyoiachia hali ya amani, upendo na utulivu, kushikwa na viongozi waovu kuliko serikali ya wanyama, ndege au wadudu; na hatari inayojidhihirisha kwa mustakabali wa taifa, jinsi ulivyo njia panda; anawatazama, kana kwamba anakariri maneno:

“Kweli pasipo maono, Taifa huangamia; na pasipo ushauri, Taifa huanguka.

Naiombea ncni yangu, rehema kwake Mungu – Amina!”

Anawatazama, kila mmoja kwa zamu,
Kana kwamba anatunga uraia tofauti kwa kila mmoja wao,
Kuashirikia kwamba nchi iko njia panda:

Kifo cha maji kushoto, kulia kifo cha maji moto,
Kukubali, kukataa, kila moja ni balaa!

Kote uko hatarini, hujui ufanye nini,
Ole wake Tanzania, tusipoisaidia,
Niwezalo nimefanya, kushauri kuonya,
Nimeonya, tahadhari, nimetoa ushauri.

Nimeshatoka (duniani) kitini, zaidi nifanye nini,
Namlilia jalia, atumlikie njia,
Tanzania ailinde, waovu (wahuni) wasiivunde,
Nasi tumsaidie, yote tusiyamwachie,
Amina, tena – Amina, Amina tena na tena.

(Mwalimu anatoweka ghafla na kwa kadhia na staili ile ile kama alivyoingia na kuwaacha wameduwaa).

Dk. che Mponda: “Katuachia ujumbe gani?”

Dk. Salim: Tusimamie KWELI; tuisaidie nchi, kwani Mungu mwenye haki yuko upande wetu. Na kama ilivyosemwa, ukweli una tabia moja nzuri, kwa mkubwa na mdogo, ukweli ni ule ule; ukiubeza, mwisho wake ni majuto”.

Huku akikusanya kila kilichopo mezani, anaonekana kukariri maneno fulani kwa sauti ya kusikika kwa wenzake:

“Kweli itashinda, namna tunavyoishi,
Kweli haihofu tisho, wala nguvu ya majeshi,
La uongo lina mwisho, kweli kitu cha aushi,
Kweli itashinda kesho, kama leo haitoshi”.
 
Inatia uchungu sana mkuu hii article na imegusa hasa kwenye tatizo la uongozi wa sasa na unafiki uliopo.
 
"Kweli pasipo maono, Taifa huangamia; na pasipo ushauri, Taifa huanguka.
Hatuna mtu wa kutuonya hapa...hatuna miiko...Wazee walishamalizika...Wamepotea!
 
Back
Top Bottom