Kiongozi Afrika Hajui Atazikwa Wapi ( Makala Raia Mwema) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kiongozi Afrika Hajui Atazikwa Wapi ( Makala Raia Mwema)

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, Feb 10, 2011.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Feb 10, 2011
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Na Maggid Mjengwa,  MMACHINGA wa Afrika anajua atazikwa wapi mauti yatakapomfika, lakini, kiongozi wa Afrika hana hakika ya wapi atazikwa mauti yatakapomfika.


  Na hata kama atazikwa kwenye ardhi ya nchi yake, kwa matendo yake maovu kwa watu wake, kiongozi huyo hana hakika kama kaburi lake litabaki salama siku umma utakapofanya mapinduzi.


  Afrika tuna orodha ya marais waliolazimika, kwa matendo yao maovu kwa watu wao, kuzikimbia nchi zao. Wakaenda kuishi uhamishoni, wakafia huko huko. Idi Amin, Milton Obote, Mobutu Seseseko kwa kuwataja wachache.


  Lakini, ni katika Afrika hii, tumeshuhudia pia viongozi waliosimama upande wa watu, wakawapigania walio wengi. Kama walilazimishwa na watawala kuzikimbia nchi zao na kwenda kuishi uhamishoni, basi, nchi zao zilipokombolewa, walirudi nyumbani kama mashujaa.


  Ni Afrika hii, tuna viongozi waliokuwa na hakika, kuwa mauti yatakapowafika, watazikwa kwenye nchi zao, Mwalimu Nyerere, Edward Sokoine, Samora Machel na Kepteni Thomas Sankara ni miongoni mwa viongozi hao. Tuna viongozi pia, ambao, wana hakika, kuwa mauti yatakapowafika, watazikwa katika nchi zao. Nelson Mandela ni mmoja wa watu hao.


  Naam. Tunashuhudia sasa yanayotokea Misri. Tumeshuhudia ya Tunisia pia. Kwengineko kunafukuta moshi. Afrika kuna moto unawaka.
  Ben Ali wa Tunisia ameikimbia nchi yake. Hosni Mubarak ameshamtanguliza mwanawe na familia yake Uingereza. Siku, kama si saa, za Hosni Mubarak kubaki Ikulu ya Cairo zinahesabika.


  Mara kadhaa nimekumbushia, kuwa historia ni mwalimu mzuri. Kuna wakati, dikteta Mobutu wa iliyokuwa Zaire ya zamani alipata kumfokea Waziri wake wa Habari na Utangazaji, kisa? Waziri yule aliruhusu televisheni ya taifa kurusha mkanda ulionyesha tukio la kukamatwa na kupigwa risasi kwa dikteta Nikolai Ceaussesco wa Romania. Ilikuwa ni mwishoni mwa miaka ya 80.


  Tukio la Ceaussesco kukamatwa na kupigwa risasi lilionyeshwa dunia nzima. Waziri yule wa Mobutu hakuona sababu ya kuwaficha watu wa Zaire kuliona, maana ule ulikuwa ni ukweli wa hali halisi, kuwa wananchi waliokuwa wakikandamizwa wamesimama na kufanya mapinduzi. Lakini, kwa Mobutu, dikteta Ceaussesco hakutofautiana sana na yeye (Mobutu), hivyo, aliingiwa na hofu, kuwa kwa Wazaire kuliona tukio lile, lingewaamshia ari ya kutaka kupambana na utawala wake.


  Kama ilivyo kwa nchi nyingi za Kiafrika, serikali na vyama tawala vina vyombo vyake vya mawasiliano ikiwamo redio, televisheni na magazeti. Katika nchi nyingi za Kiafrika, hata kama huitwa ni vyombo vya umma vya mawasiliano, jukumu la kwanza la vyombo hivyo huwa ni kulinda maslahi ya watawala.


  Waziri yule wa habari wa Mobutu alimtangulia bosi wake katika kusoma alama za nyakati, akaruhusu taarifa ile ya kukamatwa na kupigwa risasi kwa Ceaussesco irushwe hewani ingawa haikulinda maslahi ya bosi wake. Ni Mobutu aliyeshindwa kusoma alama za nyakati, na zaidi, alikiogopa kivuli chake mwenyewe.


  Katika nchi zetu hizi za Kiafrika, hadi hii leo, bado tuna viongozi wenye hulka za akina Mobutu. Itakumbukwa, alipoingia madarakani, Jenerali Mobutu alianza kudhibiti vyombo vya habari, wasomi na waandishi wa vitabu. Mobutu aliwaandama wote wenye kupingana naye. Kuna Wakongo waliopoteza maisha yao kwa kupingana na Mobutu. Kuna wengi pia walioikimbia nchi yao.


  Mobutu alipenda sana Wakongo wamuimbe yeye. Wampigie makofi hata kwa kauli za kipumbavu. Alishindwa kuelewa, kuwa unaweza kumpeleka punda mtoni, lakini kamwe huwezi kumlazimisha kuyanywa maji. Kwamba unaweza kumlazimisha mwanadamu kukupigia makofi, lakini kamwe si kutabasamu. Hilo la mwisho hutoka moyoni.


  Mobutu hakuheshimiwa na watu wake, aliogopwa. Na sifa moja ya madikteta ni kuogopwa. Mobutu hakujishugughulisha na chochote kinachoitwa ujenzi wa taifa. Kinyume chake, alijaribu kuligawa taifa katika makundi kadri alivyoweza. Aliamini, kuwa kwa namna hiyo ndivyo angeweza kuwatawala vema Wakongo.


  Kwa asili Mobutu alitoka kijiji cha Badolite, huko alijenga Ikulu ya marumaru za dhahabu. Ikulu ya Badolite ilikuwa ni kama mji wa kisasa wenye kila kitu. Ilikuwa ni Ikulu ya kifahari kweli. Ikulu iliyokuwa na vyote. Lakini, ukitoka kilomita chache tu nje ya Ikulu hiyo, ulikutana na Wakongo walioshi katika umasikini wa kutupwa.


  Katika mwaka wa mwisho wa utawala wa Mobutu, wananchi masikini walioishi kandokando ya Ikulu ya Badolite walikuwa na mazoea ya kuusimamisha msafara wa Mobutu. Naye Mobutu alifahamu, kuwa angesimamishwa, alichofanya Mobutu ni kuwaelekeza Wakongo wale waende kwenye gari la nyuma kwenye msafara wake. Huko kulikuwa na wapambe wa Mobutu waliokuwa na maboksi ya fedha za Kikongo, walizigawa. Wakongo wale walibaki wakizigombania, msafara wa Mobutu uliendelea.


  Kitu ambacho Mobutu hakukitafakari ni ukweli, kuwa kugawa kwake noti zile kwa Wakongo hakukuwa jawabu la matatizo ya Wakongo. Watu wake walishawaganyika, ni yeye Mobutu aliyechangia kuwagawa.


  Mobutu aligawa utajiri wa rasilimali za Wakongo kwa wachache. Na yeye akawa mfano wa ufujaji wa rasilimali hizo. Tofauti na wakati wa mkombozi Patrick Lumumba, utaifa na moyo wa uzalendo uliporomoka kwa kasi ya ajabu miongoni mwa Wakongo.


  Hatimaye, msafara wa mwisho wa Mobutu haukusimamishwa, kila mmoja alijua kuwa ulikuwa ni msafara wa mwisho kuelekea uwanja wa ndege kutoka Ikulu yake ya Kinshasa. Mobutu aliikimbia Zaire na kufia ughaibuni, kwenye nchi ya Morocco. Inasemekana, kuwa watu waliokwenda kumzika Mobutu hawakuzidi sita.


  Kwanini kuna viongozi Afrika wanaoishia kuzikwa ughaibuni? Ni kutokana na ukweli, kuwa viongozi wengi huingia madarakani wakiwa na umma nyuma yao. Lakini, wakiwa madarakani, viongozi hawa hulewa madaraka. Huanza kujitenga na umma uliowaingiza madarakani au uliowaunga mkono. Huanza kujilimbikizia mali wao , familia zao na ‘wenzao’ wachache katika utawala.


  Viongozi hawa hugeuka vibaraka badala ya kuwa watetezi wa walio wengi. Hawaamini katika kugawana madaraka ya uongozi. Hawaamini katika demokrasia yenye kutoa uhuru mpana kwa watu kujieleza na hata kushutumu. Watatumia vyombo vya dola kuwakandamiza watu wao.
  Huishia kujenga ngome ngumu ya kuwalinda. Huingiwa hofu na wale wanaowaongoza. Viongozi hawa hushindwa kabisa kujenga utaifa. Hawataki Utaifa ambao ndio huzaa uzalendo.


  Utaifa unatokana na imani ya wananchi kwa viongozi wao. Imani hiyo inatokana na kauli na matendo ya viongozi. Ukijenga tabaka la viongozi na raia wengine wachache wenye kudhibiti na hususan kwa njia haramu, mali za umma, basi, unachangia kupunguza mapenzi ya wananchi wako kwa serikali yao. Ni vema umma ukaamini, kuwa serikali yao ni njema. Serikali njema huchangia kujenga utaifa na hatimaye uzalendo. Serikali ovu na fedhuli hupelekea kinyume chake.


  Viongozi Afrika wanapaswa kutambua sasa, kuwa Mwafrika wa mwaka 1975 si Mwafrika wa mwaka 2011. Waafrika wameamka. Viongozi Afrika wana lazima ya kuendana na mabadiliko ya wakati. Hizi ni zama za mabadiliko. Na Mabadiliko ya amani Afrika yanawezekana, mwenye kuyazuia mabadiliko ya amani, atambue, kuwa mabadiliko yenye vurugu hayaepukiki. Hilo la mwisho lina hasara kubwa. Mungu Ibariki Afrika.
  [​IMG]  [​IMG] Mwanzo [​IMG] Toleo Lilopita [​IMG] Hifadhi [​IMG] Matangazo [​IMG] Tuwasiliane
   
 2. Omuregi Wasu

  Omuregi Wasu JF-Expert Member

  #2
  Feb 10, 2011
  Joined: May 21, 2009
  Messages: 753
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Mjengwa ni mtu wa ajabu sana. Matatizo yake yanazidi mafanikio. Sioni haja ya kujadili hoja zake hata kama ni nzuri.
   
 3. b

  bagamoyo JF-Expert Member

  #3
  Feb 11, 2011
  Joined: Jan 14, 2010
  Messages: 4,530
  Likes Received: 2,113
  Trophy Points: 280
  Kwa kuwa Kada Mjengwa anawaeleza wenzie wa SISIEM labda katika hili lakuwa SISIEM wasiposikiliza wananchi basi maziko ya viongozi wa CCM yatakuwa ughaibuni watamuelewa kada Mjengwa na si hilo tu bali hata chama chao cha CCM kitakufa.
   
 4. VoiceOfReason

  VoiceOfReason JF-Expert Member

  #4
  Feb 11, 2011
  Joined: Nov 4, 2010
  Messages: 5,234
  Likes Received: 43
  Trophy Points: 0
  Kwa mtaji huu hawa Jamaa wanavyouza nchi yetu, hata sisi machinga sijui kama tutazikwa au itabidi tuchomwe moto kwa kukosa ardhi ya sehemu ya kutuzika....
   
 5. Madela Wa- Madilu

  Madela Wa- Madilu JF-Expert Member

  #5
  Feb 11, 2011
  Joined: Mar 24, 2007
  Messages: 3,074
  Likes Received: 35
  Trophy Points: 135
  Mimi nikiitwa mtu wa ajabu kamwe siwezi kushangaa kwani ninamkia.
  Siwezi kujizuia kumwona Maggid ni mtu wa ajabu na mwenye tabia ya Kambare.

  Nadhani Makala ya Maggid zaidi inawakumbusha CHADEMA siku wakishika madaraka wakumbuke usia wake. Hana haja ya kuwakumbusha CCM kuhusu hayo ayasemayo kwani wako juu ya sheria na Amani Umoja na mshikamano vinawalinda.

  Maggid!

  Viongozi wa Afrika wanajua watafia wapi???

  Nyerere alifia St Anne Hosptal UK na siyo Mwaisela Muhimbili. Je hilo ni Tatizo??
   
Loading...