Kingunge: Taifa lina tatizo la viongozi

mdau wetu

JF-Expert Member
Apr 20, 2011
548
58
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru, amesema Watanzania wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwa na viongozi wa namna mpya wenye uchungu na wananchi na siyo wanaofaidika na kuwa kwao nyuma kimaendeleo.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuenzi fikra na mtazamo wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye katika kipindi cha uhai wake wote alijali na kuthamini haki na maisha ya wanyonge popote waliko duniani.
Miongoni mwa wanyonge waliothaminiwa na Mwalimu Nyerere, Kingunge alisema ni pamoja na wakulima wadogo nchini, ambao alisema aliweka misingi mizuri ya kuwafanya waishi na kufanya kazi pamoja kwa kutumia maarifa ya kisasa ili kupata tija katika kazi zao.
Kingunge, ambaye ni miongoni mwa waasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema hayo katika mazungumzo kuhusu ‘Tafakuri ya Mwalimu Nyerere’ yaliyoandaliwa na Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya Mlimani jana, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya ‘Siku ya Mwalimu Nyerere’.
Wachokoza mada katika mazungumzo hayo yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa Kigoda hicho, Profesa Issa Shivji, walikuwa ni pamoja na Dk. Ng’wanza Kamata na Kingunge.
Washiriki wengine wa mazungumzo hayo, ni wahadhiri waandamizi wa UDSM, viongozi wa sasa na wastaafu wa vyama vya siasa, asasi za kiserikali na za kiraia, wasomi, akiwamo mwanaharakati na mwanazuoni, Profesa Marjolie Mbilinyi na wananchi wa kawaida,
“Lazima tuwe na viongozi wa namna mpya wenye uchungu na wananchi kuwa nyuma, siyo viongozi wanaofaidika wananchi kuwa nyuma. Ni kazi kubwa inatakiwa ifanywe,” alisema Kingunge.
Alisema ili kufikia katika hilo, ndani ya chama kunatakiwa kufanyike mageuzi makubwa ya kujisafisha.
“Ndio maana tulizungumza kwenye NEC (Halmashauri Kuu-CCM) kwamba, turudi kwenye misingi, ambayo ni Liberation (ukombozi),” alisema Kingunge.
Alisema mageuzi hayo ni muhimu, kwani licha ya kuwapo mabadiliko kwa wakulima wadogo na wafugaji katika baadhi ya maeneo, maisha yao bado ni duni.
“Mwalimu (Nyerere) alikuwa ameliona vizuri suala hili. Kwamba watu waishi na kufanya kazi pamoja, watumie maarifa ya kisasa ili wapate tija katika kazi zao. Lakini leo watu wanatumia elimu dhidi ya maendeleo ya wote. Mtu leo anainua mkono kutoa ahadi ya TANU na kuishia kutamka mdomoni, lakini moyoni haimo. Ushirika tumewaachia watu wasiokuwa waaminifu,” alisema Kingunge.
Aliongeza: “Uchumi wetu bado hatujaweza kuudhibiti. Si suala la maneno, bali maamuzi ya dhati. Tunachotaka ni mageuzi ndani ya chama. Na ndicho alichosema Mwenyekiti (wa CCM, Rais Jakaya Kikwete) tarehe 5.”
AKERWA NA WAWEKEZAJI
Kingunge alisema amekuwa akistaajabishwa kila anaposikia wakubwa wakiwaita wawekezaji wa kigeni kuja kuwekeza kwenye mashamba makubwa, huku vijana wengi nchini waliohitimu elimu ya juu wanaoweza kulima mashamba hayo wakiachwa.
Alisema matokeo yake, uchumi wa nchi hivi sasa haukui, huku kazi za kuajiriwa zikikosekana miongoni mwa vijana nchini.
“Suala la kukaribisha wawekezaji limekuwa katika ndimi za viongozi wetu…Tunataka mashamba, lakini si kwa kuleta watu kutoka nje. Hawa vijana wawezeshwe maarifa, mitaji na kumiliki ardhi, watawaajiri ndugu zao hapa hapa,” alisema Kingunge.
Aliongeza: “Mimi nimestaafu, napumzika. Nikisikia wakubwa wanawaita watu huko nje njooni hapa, nastaabu sana. Maji tunayo, lakini wanachukua ndoo na kwenda kuchota mbali.”
Alisema wakulima wadogo hapa nchini ndio wenye mchango mkubwa wa kuilisha nchi.
Kutokana na hilo, alisema kama serikali ingekuwa na mikakati endelevu kama ile iliyotumika kuleta mafanikio katika mikoa ya Iringa, Ruvuma, Rukwa na Mbeya, ambayo inalisha nchi, hivi sasa nchi ingekuwa imepiga hatua kubwa kwa chakula.
 
Huyu Mzee anafanana Kabisa na Waziri Mkuu wa Nchi ya kusadikika! Sababu ni Msanii wa Maneno tu! Heshima yako Mkuu K! ilienda Zamani sana! Kabla ya Baba ajaenda!
 
ni kweli, ni mnafiki, anauma na kupulizia, anatumia imani ya watu kwake kuwarubuni watanzania kwani na yeye ni moja wao
 
Back
Top Bottom