Kingatiba ya Mabusha na Matende yatolewa Dar, Kata ya Tandale yaongoza kwa maambukizi

John Haramba

JF-Expert Member
Feb 4, 2022
365
1,373
Zaidi ya wananchi milioni nne wa Dar es Salaam katika Halmashauri za Temeke, Kinondoni na Ilala kuanzia wenye umri wa miaka mitano wameanza kupatiwa tibakinga dhidi ya ugonjwa wa matende na mabusha kuanzia Kata ya Tandale ambayo ina idadi kubwa ya wagonjwa kwa Manispaa ya Kinondoni.

Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume wakati wa kuanza utekelezaji wa zoezi la utoaji wa kingatiba ya mabusha na matende kwa Halimashauri ya Kinondoni katika Kata ya Tandale ikiwa ni mpango wa kupambana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele.

Amesema katika Halmashauri zilizolengwa kupatiwa tibakinga jumla ya wananchi 4,174 wana ugonjwa wa mabusha huku wenye matende wakiwa 2221.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Kinondoni ametoa wito kwa viongozi wa Serikali za mitaa kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi hilo la upataji tibakinga ili kudhibiti ugonjwa huo.

Tayari kampeni hiyo ya utoaji tibakinga ilianza Novemba 21 na itaendelea hadi Novemba 25, 2022 lengo ni kudhibiti ugonjwa huo kwani hudhohofisha nguvu kazi ya taifa.

UFAFANUZI ZAIDI
Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume anafafanua baadhi ya mambo kutokana na maswali aliyoulizwa:

SWALI: Tandale kuna wagonjwa wengi, takwimu zipoje?
JIBU: Kuna kitu kinaitwa hali ya maambukizi, mfano katika watu 10 kukiwa na watu wawili wenye maambuki ya minyoo inayosababisha matende na mabusha kwa mujibu wa viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) hapo tunasema maambukizi yapo juu.

Tumeona kwa Kata ya Tandale utafiti unaonesha kuwa katika wastani wa watu 10, kati yao kuna watu zaidi ya watatu wenye maambukizi au vimelea vya minyoo midogomidogo inayosababisha maambukizi ya matende na mabusha.

Hiyo ndio maana tunasema kuwa Tandale hali ni mbaya zaidi ukilinganisha na maeneo mengine ya Halmashauri nyingine za Dar.”

SWALI: Kwa nini kapeni hii ifanyie sasa hivi?
JIBU: Huwa tunafanya kila mwaka, hata mwaka jana (2021) tulifanya kwa watu kumeza vidonge vya kinga tiba.

Mfano mtu ambaye ameugua Malaria akanywa dawa akapona, haimaanishi au haiondoi kuwa hawezi kuugua tena Malaria, ndivyo ilivyo katika ugonjwa huu wa Mabusha na Matende, tunachokifanya ni kutengeneza mazingira ya kuzuia minyororo ya maambukizi kutosambaa zaidi.

Pia kuwa tunaanzia kutoa dawa kwa watoto kuanzia umri wa miaka mitano, wapo waliokuwa na miaka minne mwaka jana na hawakuipata kingatiba, hivyo hii ni nafasi yao kuipata mwaka huu, pia wapo ambao hawakupata nafasi au walikuwa wagonjwa sana au walikuwa wajawazito, hawakupata hizo dawa.

SWALI: Chanzo cha Matende na Mabusha ni nini?
JIBU: Chanzo kikubwa ni vimelea vya minyoo midogomidogo jamii ya Filaria, mtu akipata minyoo hiyo inaenda kwenye damu na inaweza kusababisha madhara sehemu za haja ndogo na baadae inaweza kusababisha maji kujikusanya kwenye sehemu za korodani.

Maji yakizidi ndio unakuta sehemu hizo za siri zinavimba na baadaye hadi ngozi inaweza kuaathiri na kuweka ugumu wakati inapitakiwa kupatiwa matibabu.

SWALI: Ni kweli Maji ya Madafu ni chanzo cha Matende na Mabusha?
JIBU: Kisayansi hakuna ushahidi huo.

Wengine wanasema ukiendesha sana baiskeli unaweza kupata magonjwa hayo, si kweli labda kama mtu akiendesha apate ajali sehemu za siri.

Sababu nyingine ya magonjwa hayo ni mbu ambao ndio wanaeneza hiyo minyoo, ni sehemu zote Nchini lakini zaidi wanapatikana sehemu za Pwani.

Wakati tafiti zinaanza waligundua mbu aina ya Culex, hiyo ilibainishwa na wataalam wanaoangalia tabia za mbu na wadudu lakini baadaye ikabainika kuwa ni mbu wa aina zote wanaweza kusambaza vimelea vya minyoo midogomidogo vinavyosababisha matende na mabusha.

Hata mbu anayeeneza Malaria anaweza kusambaza vimelea hivyo vya matende na Mabusha.

Mwananchi anavyofanya bidii ya kuzuia mbu kama vile kusafisha mazingira yanayomzunguka, kufukia madimbwi ya maji, kutumia vyandarua, inamaanisha unapojikinga na mbu hujikingi na Malaria peke yake, bali unajikinga dhidi ya Homa ya Denge, Matende na Mabusha na vingine vingi…
 
Back
Top Bottom