Elections 2010 Kingamuzi cha tume, tupe matokeo yetu.

Omulangi

JF-Expert Member
Feb 12, 2008
1,036
265
1. Nipe kalamu na wino, niseme ya king'amuzi,
Umeshaleta maneno, un'gmue king'amuzi,
Twakushangaa Chamwino, Tushafanya uamuzi,
King'amuzi chayo tume, tupe matokeo yetu.

2. Haingii akilini, hiki king'amuzi gani?
Ni cha Tigo au Zaini, chatutia matatani,
Mi ninacho cha Zaini, hung'amua ya gizani,
King'amuzi chayo tume, tupe matokeo yetu.

3. Mbeya nako Nyamagana, ni mabomu ya machozi,
Mtaani walia wana, polisi wamwaga lazi,
Ni kweli nchi ni pana, tupeleke ving'amuzi,
King'amuzi chayo tume, tupe matokeo yetu.

4. Wapinzani ni wahuni, wanasema watawala,
Wakishinda majimboni, matokeo mnayala,
Wasubiri hadi lini, hapo hakuna kulala,
King'amuzi chayo tume, tupe matokeo yetu.

5. Wapinzani wakishindwa, king'amuzi kinawahi,
Sisiemu wakishindwa, king'amuzi sio hai,
Ofisi zote zalindwa, watu wamejikinai,
King'amuzi chayo tume, tupe matokeo yetu.

6. Beti sita nimetimu, mabomu yamenitisha,
Chonde chonde sisiemu, Chadema kweli mwatisha,
Songea hadi Mugumu, king'amuzi chakatisha,
King'amuzi chayo tume, tupe matokeo yetu.
 
Back
Top Bottom