Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
JESHI la Magereza hapa nchini limesema kinara wa kuuza dawa za kulevya, Ali Khatib Haji maarufu kwa jina la Shikuba amekuwa tishio katika Gereza la Lindi.
Akitoa changamoto za magereza Dar es Salaam jana kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya, Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja, alisema kutokana na hali hiyo wamelazimika kuongeza ulinzi kwa kuwa miundombinu ya gereza hilo ambako Shikuba anashikiliwa ni hafifu.
Minja alivitaka vyombo vinavyoshughulikia kesi hiyo kuharakisha upelelezi ili Shikuba aliyekamatwa mwaka 2014 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kusakwa kwa zaidi ya miaka miwili na polisi kutokana na tuhuma za dawa za kulevya huku akidaiwa kuwa na mtandao mkubwa Afrika Mashariki, China, Brazil, Canada, Japan, Marekani na Uingereza apelekwe mahakamani.
“Jeshi la Magereza limekuwa na changamoto, ..., mfano unapokuwa na mtu kama Shikuba yule ni mtu hatari hata Marekani wanamtafuta na imetulazimu kuongeza ulinzi katika Gereza la Lindi ambako yupo mahabusu. “Naomba vile vyombo vinavyohusika na kesi yake viweze kuharakisha upelelezi wa kesi ili apelekwe mahakamani,” alisema Minja.
Awali, hoja ya Shikuba ambaye hivi karibuni Marekani ilitangaza kutaifisha mali zake zilizotokana na faida haramu ya biashara zake za kuuza dawa hizo iliibuliwa katika kamati hiyo na Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu.
Mbunge huyo alishangaa kesi ya Shikuba kucheleweshwa kufikishwa mahakamani ikiwa ni mwaka wa tano tangu dawa za kulevya anazohusishwa nazo kukamatwa.
“Lazima DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) aamshwe. Haiwezekani upelelezi unafanyika kwa miaka mitano mtu hafikishwi mahakamani, Shikuba amekamatwa muda mrefu sasa tunataka tuambiwe ni lini atafikishwa mahakamani na mimi katika hili siogopi nipo tayari kufa lakini najua siwezi kufa hadi nikamilishe kazi aliyonituma Mungu,” alisema Kingu.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, alisema Shikuba alikamatwa miaka miwili baada ya dawa hizo kukamatwa na licha ya kutajwa na wale waliokamatwa mwenyewe hakukubali kwamba anahusika.
“Hii kesi inahitaji uchunguzi hatuwezi kusema kwa sababu ametajwa basi na yeye atakubali. Tulimkamata Februari, 2014 na alikana hivyo lazima tuchunguze na tuweze kuthibitisha,” alisema Mangu.
Aliwapa matumaini wabunge kuwa jeshi hilo lipo kwenye hatua nzuri ya kukamilisha upelelezi na watampeleka mahakamani.
“Tuko katika hatua nzuri ya kukamilisha upelelezi na atapelekwa mahakamani siku za hivi karibuni,” alisema Mangu.
Source: Mtanzania