Kina nani wanaompinga Magufuli?

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
NI wazi kuwa siyo watu wote ni mashabiki wa uongozi na aina ya uongozi wa Rais Magufuli. Ni wazi siyo wote walifurahia kuchaguliwa kwake na kwa hakika si wote wanafurahia kile ambacho kinajulikana kama Operesheni Tumbua Majipu. Ni kufanya makosa kudhania kuwa watu wote wanafurahia au wanapaswa kufurahia operesheni hii au kuchaguliwa kwa Magufuli. Wapo wenye kumpinga, na wengine wameshajitokeza wazi kumpinga. Hili kwa kweli siyo la kushangaza na lenyewe tu siyo habari.

Swali kubwa ambalo linaweza kuwa habari ni kuwa hawa wenye kumpinga ni kina nani na ni kwa nini. Je wote wenye kumpinga wanampinga kwa sababu wanataka kitu kingine au wanampinga kwa sababu wanaona hawana jinsi isipokuwa kumpinga? Je, wenye kubeza serikali hii na uongozi wa Magufuli wanafanya hivyo kwa sababu wanafurahia au wanatamani ule uongozi uliopita au wanatamani uongozi mwingine ambao haupo na haujawahi kuwepo bado?

Kwa maoni yangu, wenye kumpinga Magufuli wako kwenye makundi mbalimbali, makundi ambayo ama yanaunganishwa na baadhi ya mambo.

Kundi la wapinga mabadiliko haya si yale

Kundi hili naweza kusema ndio kundi lenye watu wengi wenye kumpinga Magufuli na ambao watajitokeza wengi wakijionesha wanafanya kwa nia njema. Hawa ni wale ambao mgombea wao alishindwa na Magufuli na ahadi zile za mabadiliko ya mtu mmoja yakakataliwa ndiyo yanasumbua kwa sababu bado hawaamini kuwa mtu wao (siyo mabadiliko yao tu) alikataliwa. Kundi hili, haliwezi na halitakuwa na sababu ya kushabikia mambo yanayofanywa na Magufuli hata akifanya nini.

Hawa mara nyingi ni watu ambao hawachelewi kuhamisha magoli. “Kama kweli Magufuli anatumbua si tuone kama atatumbua Bandari” wanasema. Bandari wanatumbuliwa na wao wanarudi “ah ile mbona rahisi sana kama kweli anataka kutumbua Bandari si atumbue Uhamiaji tuone”; uhamiaji kunatumbuliwa na hawa (hawakiri kuona kilichotokea bandari wala uhamiaji) wanarudi na goli jingine; “ah mbona yule kaonewa kama kweli ye mwanamme si aiguse Takukuru”; Takukuru inaguswa mwisho wanakuja na kusema “Vipi escrow”. Na itakapoguswa hawatakubali bado watatafuta goli jingine na jingine. Hawa ni wa mabadiliko yale; mabadiliko ya kuzungurusha mikono na hawako tayari kuacha kuzungurusha mikono.

Tukumbuke neon kubwa la hawa wakati wa kampeni lilikuwa “CCM iondoke kwanza mengine baadaye”. Tatizo ni kuwa yale mengine yameanza kutokea sasa wakati CCM iko madarakani na hili ni gumu sana kulipatanisha. Walijiaminisha kuwa yale “mengine” hayawezi kutokea CCM ikiwa madarakani na kwamba yanayotokea ni kinyume (antithesis) cha fikra zao zote na ndoto zao. Hawa hawawezi kumuunga mkono Magufuli wala kushabikia mabadiliko haya.

Kundi la wakosoaji hawa

Lipo kundi jingine la wakosoaji ‘hawa’. Hawa ni wakosoaji wa serikali. Hawa ni watu ambao kwao serikali ni ya kushukiwa wakati wote. Ni kundi zuri sana kwenye utawala wa kidemokrasia kwani kundi hili halipendi geresha na mazingaombwe; ni kundi ambalo linawaangalia wanasiasa kama viongozi wa ngoma; wanajua wanafanya burudani na kuhakikisha watu wanapokea kwa kiitikio na manyanga. Wakosoaji “hawa” wao wanaweza kufurahia mabadiliko lakini wakati huo huo wanayashuku mabadiliko hayo; hawaamini nia za wanaotaka kuleta mabadiliko na hawachelewi kutafuta kasoro ili waweze kusema “aha si unaona amefanya hivi tena”.

Kundi hili nalo kama kundi lile la mwanzo halitakoma; litaendelea kumshuku Magufuli, litaendelea kuhoji ukweli wake na malengo yake na halitochelewa kulia “kavunja katiba” “kaingilia Bunge” “kaingilia Mahakama” “dikteta n.k”. Ni kundi ambalo lipo kama mwiba wa lazima ili serikali isije kufikiri au kuishi bila kuangaliwa.

Kundi la waathirika wa haya

Kuna kundi na ninaamini litazidi kuwa kubwa zaidi kwa siku zinavyokwenda; hili ni kundi la waathirika wa mabadiliko haya. Wale watu wanaopoteza nafasi zao na watu ambao wanaaanza kuguswa na mabadiliko haya hawawezi kamwe kuwa mashabiki wa yule ambaye amesababisha jamaa, ndugu, mabodi au marafiki zao kuanza kuwa na maisha magumu. Kwa kadiri kwamba Magufuli anaanza kulazimisha uchumi wetu kujirekebisha ndivyo ambavyo wapo watu wengi ambao walikuwa wamezoea kuishi maisha fulani na sasa maisha hayo hayapo tena; na kama baadhi ya mishahara na posho zitakavyofutwa – kama inavyotarajiwa – kwenye Bunge la bajeti ni wazi kuwa Magufuli atapoteza mashabiki na marafiki wengi; na kwa vile hawa wanaweza kuwa wengi, kundi hili litazidi kumpinga na linaweza kuwa na watu wengi ndani ya serikali na ndani ya chama tawala.

Makundi haya matatu naamini ndio makubwa na yataendelea kuwepo kwa kadiri ya kwamba Magufuli anaendelea na ajenda yake ya kusafisha utumishi serikalini, kubana matumizi yasiyo ya lazima na kurejesha nidhamu na heshima kwa Watanzania. Siyo wote watafurahia na si wote watasimama na kuunga mkono. Nina uhakika hata wale ambao walipiga makofi kushangilia kutumbua majipu wanaweza leo hii wasiwe tena wa kwanza kushangilia hasa baada ya wao wenyewe kutumbuliwa. Bado kazi kubwa inakuja na ngumu zaidi lakini kama alivyosema Rais – “hakuna namna nyingine”.

Nina uhakika pamoja na watu wengi wenye kumpinga bado wapo wengine wengi ambao nao wataendelea kuunga mkono na kumtia shime kwa sababu tunajua kushindwa kwake ni hasara kwa taifa na vizazi vijavyo.

Hili tusiliruhusu litokee. -
 
Back
Top Bottom