Kimya hiki kiwe na mshindo…

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,009
Kimya hiki kiwe na mshindo…

Chesi Mpilipili Machi 5, 2008
Raia Mwema

NAKIRI kufurahishwa na staili mpya ya utendaji kazi aliyokuja nayo Waziri wa zamani wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Basil Pesambili Mramba. Staili ya ukimya.

BASIL Pesambili Mramba

Angalau mpaka wakati makala hii inaandaliwa, Mramba alikuwa hajasikika kuzungumza chochote kuhusiana na taharuki inayoendelea nchini iliyosababishwa na mkataba wa Richmond na 'madudu' mengine kama EPA, IPTL, Rada na kadhalika.

Kwa hakika, katika kipindi hiki ambacho kila ambaye jina lake limeonekana kuhusika hata kwa mbali tu na sakata la Richmond la lile la EPA anajitahidi kujitetea na kujiweka mbali nalo, ukimya wa Mramba 'unazungumza' mengi.

Haijafahamika sawasawa iwapo ukimya huu umetokana na vyombo vya habari kutokuona umuhimu wa kupata kauli yoyote kutoka kwake ama ni kutokana na juhudi zake binafsi za kuweza kuvitolea nje vyombo hivyo pale vilipoomba mahojiano naye.

Iwavyo vyovyote, ukimya wa mheshimiwa huyu aliyepata kutusemea mioyo yetu kwamba tulikuwa tuko radhi kula majani ili mradi tu rais wetu apate ndege ya kisasa yenye hadhi ya urais ambayo matumizi yake sasa hayaakisi umuhimu iliyopewa wakati wa kununuliwa, unasisimua.

Tokea Rais Jakaya Kikwete alipoteua Baraza jipya la Mawaziri na kuziacha sura kadhaa ambazo zilikuwa ni kama jadi kuwamo kwenye mabaraza ya mawaziri yaliyopita, Mramba ni kama amechukua likizo ya kuzungumza na vyombo vya habari.

Pamoja na kwamba ukimya huu haumpi uhalali wa kutokutoa maelezo yanayohusu uhusika wake katika 'madudu' haya, angalau yeye anaonekana kuchukua njia tofauti kidogo katika kuyakabili tofauti na wenzake wengine walioachwa kwenye baraza jipya kwa sababu moja ama nyingine.

Wataalamu wa mambo ya saikolojia ya jamii wanatuambia kuwa njia bora ya kukabiliana na tatizo linalokupata ghafla ni kutulia na kujipa nafasi ya kutafakari kisha kutafuta njia muafaka za kukabiliana nalo na si kukurupuka na kuliweka tatizo lako kwenye mfuko wa Rambo ambamo kila unayepishana naye aliona.

Kwamba unapokuwa kwenye tatizo fulani akili yako inakuwa haijatulia sawasawa na unaweza ukajikuta ukisema ama kufanya jambo ambalo baadaye akili yako takapokuwa imetulia unaweza kulijutia.

Tunapenda kuamini kuwa ukimya wa Mramba ni hatua ya mwanzo kuelekea kuwaambia Watanzania ushiriki wake katika tuhuma zinazohusisha jina lake na hautokani na matumaini ya kutegemea kwamba tutasemaa, mwisho tutalala na kusahau kama ambavyo anaelekea kufanya rais msitaafu Benjamin Mkapa.

RAIS Mstaafu, Benjamin Mkapa

Mzee wetu huyu wa kanuni ya Ukweli na Uwazi, pamoja na kelele zote zinazopigwa kuhusiana na kufanya kwake biashara akiwa ndani ya Ikulu ameamua kufanya kile vijana wanachosema ni kuuchuna dhidi ya madongo anayorushiwa huku Watanzania tukiendelea kusisitizwa kumuacha apumzike kwa amani.

Kwa hakika, inashangaza si kidogo kwa mtu aliyekuwa na kauli kali kali wakati wa kuiingiza menejimenti ya kigeni ya Netgroup Solutions kuendesha TANESCO, wakati wa kutetea ubinafsishaji na wakati wa kuwaambia Watanzania ni wavivu wa kufikiri ghafla akaukiwe na maneno ya kutuambia wakati huu. Ndiyo, angalau tu maneno ya kujisafisha kutokana na anayotuhumiwa nayo.

Wakati, Mramba akiendelea na ukimya wake, hali imekuwa tofauti kwa waheshimiwa wenzake wengine walioachwa kwenye baraza jipya hususani wale ambao majina yao yanahusishwa kwa namna moja ma nyingine na sakata la Richmond.

Tunaendelea kusikia na kuona jinsi kila mheshimiwa aliyetajwa kwenye Ripoti ya Richmond anavyojitahidi kujiweka mbali na kampuni hiyo.

Tumesikia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa akitoa maelezo kwamba hakuhusika kwa namna yoyote ile na kampuni ya Richmond na kwa hakika alikuwa tayari kuvunja mkataba wake kama alivyofanya kwa City Water kama si wataalamu wake kutoa ushauri wa kutofanya hivyo.

Tumemsikia pia mbunge wa Igunga, Rostam Aziz akikana kuhusika kwa namna yoyote ile na kampuni ya Richmond na kuahidi kuwa maelezo zaidi, pengine kuthibitisha zaidi jinsi asivyohusika na kampuni hiyo hewa, atayatoa kwenye kikao kijacho cha Bunge.

Kwa hakika, unajikuta ukishangaa kuwa kampuni hii ya Richmond ambayo kila mtu sasa anakana kuhusika nayo na kwa maana hiyo kuthibitisha maneno ya wanaosema ni kampuni hewa, bado inaendelea kuchotewa shilingi milioni 152, kila uchao kutoka kwenye umasikini wetu!

Waama, ni jambo linaloumiza mno kwamba mpaka sasa hakuna jasiri miongoni mwa Watanzania milioni 40 ambaye amejitokeza kuzuia ubadhirifu huo ili tumuone huyo mwenye kampuni ya Richmond atakayejitokeza kushitaki ili tujue cha kumfanya!

Mtu unajiuliza; iwapo kila mtu aliyetajwa kwenye Ripoti ya Bunge anakana kuhusika, ni nini kinachozuia Rais ama Waziri Mkuu ama Waziri mhusika ama hata Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kusimamisha mara moja malipo ya kila siku ya milioni 152 wakati tukisubiri mapendekezo ya tume hiyo yafanyiwe kazi?

ibu unalopata ni kwamba ama mmiliki wa Richmond na anayefaidika na mamilioni yetu anajulikana na hivyo watu kumuonea aibu kumchukulia hatua zinazostahili ama huu ni mchezo wa kuigiza tu kama ilivyo michezo mingine ya kuigiza inayotawaliwa na kanuni kuu ya kulindana!

Kwa hakika, wakati tuna hasira ya watoto wetu kulazimika kukaa chini madarasani kutokana na uhaba wa madawati huku kampuni hewa ikilipwa shilingi zote hizo kila siku, waheshimiwa hawa wangetuacha kwanza na wakachukua staili ya mheshimiwa Basil Mramba ya kukaa kimya.

Naam, papo hapo tukitahadharisha kuwa ukimya wao ufuatwe na mshindo wa maelezo juu ya yale tunayowatuhumu nayo na si ukimya wa kutegemea usahaulifu asili wa Mtanzania unaotufanya tusemee, na usiku tukalale bila kuchukua hatua stahili dhidi ya mafisadi wetu!
 
Back
Top Bottom