KILIMO: mtoto wa duma anaelelewa na kobe

Fikra Angavu

JF-Expert Member
Jul 14, 2013
301
105
Kilimo cha Tanzania kama ijulikanavyo tangu enzi na enzi kua kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa letu la Tanzania. Zaidi ya 70% ya watanzania ni wakulima na wengi kati ya hao ni wakulima wadogo (wengi wao wakiwa wanawake) ambao bado wanafanya shughuli za ukulima wakitumia mbinu za kizamani (kwa mujibu wa takwimu kutoka Bank ya maendeleo Afrika).

xUS25-WomenFarmers.jpg.pagespeed.ic.k48aKyNKd8.webp


Japokua Tanzania tuna utajiri wa ardhi kubwa yenye rutuba ikilinganishwa na nchi zingine za ukanda huu wa afrika mashariki, ni nusu yake tu ndio inatumika kwa shughuli za kilimo. Tanzania tumezungukwa na maziwa na bahari, mito inayomwaga maji vijijini na hadi baharini, bila kusahau idadi kubwa ya watu wenye nguvu za kufanya kazi, tuna mifugo, tuna bahari, maziwa na mito vilivyojaa samaki, kwa kifupi Tanzania haitakiwi kusikika kuna jamii hata moja ikilalamika kuhusu njaa.

Kila mkoa Tanzania bara mpaka visiwani una sifa kuhusu kilimo, kila mkoa una kama sio zao kuu basi kuna aidha mifugo au uvuvi kama shughuli kuu wanazo fanya, mfano Tanga ni maarufu kwa matunda, Morogoro katani, kanda ya ziwa kuna pamba, Kagera maarufu kwa ndizi, Shinyanga mifugo, Mtwara korosho, tukienda Zanzibar ni maarufu kama kisiwa cha karafuu nk.

Tukumbuke pia Raisi wetu Magufuli aliwahi kuwaambia wakuu wa mikoa kuwa asije kusikia kuna mkoa hata mmoja watu wake wakilalamikia baa la njaa, ikitokea hivyo basi mkuu wa mkoa husika hatakuwa na kazi. Kwakweli hii ni fursa kubwa kwa hawa viongozi wetu, na sisi wenye mawazo machache hatuna budi kuwakumbusha kuongeza kasi katika kuthibitisha hatuhitaji njaa na kweli kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa letu.

Japokua kuna harakati za kuiandaa Tanzania kua nchi ya viwanda pasi na shaka Kilimo, uvuvi na ufugaji ni moja ya wizara inayoweza kuchochea kasi ya ujenzi wa viwanda nchini. Ni miaka mingi sana imepita tumekua tukipiga kelele watu wajitume kwenye kilimo lakini tunakosa mikakati thabiti kutekeleza, si elimu wala matumizi ya vifaa vya kisasa vya kilimo nchini vimekua vikitolewa kwa wakulima na wafugaji kulingana na ukubwa wa sekta yenyewe na kasi inayotakiwa kuendelewa ili kuinua sekta hii kua na tija Tanzania.

Tutengeneze ushindani wa kimaendeleo baina ya wizara, mikoa, wilaya na jamii pamoja na mtu mmoja mmoja kwa faida ya taifa na mtu binasfi ili kufikia malengo ya Taifa kua nchi yenye kipato cha kati na kuondokana na umasikini tusio stahili. Kuna vijana wanao amini katika sayansi na teknolojia, ni wakati sasa wa kilimo, ufugaji na uvuvi kuongezwe usimamizi, ubunifu
na mipango kisayansi ili tutumie fursa hio kubuni na kurahisisha mambo Kupitia teknolojia.

Kabla sijasema nayowaza, niseme kwamba siamini kama kwenye umoja kunaweza
kushindikana kitu. Kwa yanayoendelea sasa katika kilimo ni wazi duma analelewa na kobe, tufanye haya kuweka mambo sawa. Ili Kilimo kiendelee kinahitaji pande 3; Wadau, wakulima wenyewe na upande wa serikali.

Mimi leo nazungumzia mchango wa serikali ikiamua iwe hivi, tutazungumziaje kilimo? Tanzania tuna idadi kubwa sana ya watu wasio na muamko wa kufaya shughuli za kujipatia kipato kwa kiwango tunachotaka, na ukweli tunapotaka wao wenyewe wajiamshe kwa maneno (kutokana mazingira na elimu yetu) tutakua tuna jidanganyana. Ila tuna watu tumewachagua/wamechaguliwa kwa ajili ya kutuongoza ambao wao ndio wana nafasi kubwa sana ya kuchagiza raia kuamka kwa vitendo.

Kuna mkuu wa mkoa, na wakuu wa wilaya, wabunge, madiwani, meya na mipango miji. Serikali kuu kuna wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuna wizara ya ardhi, nyumba na makazi, wizara ya elimu, sayansi, teknolojia na ufundi. Kwa pamoja wanaweza kushirikiana kila mmoja kuwajibika katika kuleta mapinduzi ya kilimo, uvuvi na ufugaji nchini.

Ikiwa kila mkoa una mazao/zao kuu au shughuli kuu inayo wapa sifa, nadhani wakati umefika kusimamia kwa nguvu zote. Nchi itengwe aidha kimikoa au kikanda kulingana na shughuli kuu wafanyazo ili kuleta ukaribu wa usimamizi na uongozaji thabiti kwa wakulima, wafugaji au wavuvi ili kuleta tija kwa wahusika na maendeleo ya Taifa.

Itolewe elimu kwa wakulima, wavuvi pamoja na wafugaji kuongeza ufanisi wa shughuli husika kisasa zaidi. Upatikanaji rahisi wa pembejeo za kilimo, nyavu nk. Kwa bei nafuu ili kuwezesha kufanya shughuli zao kwa ustadi mkubwa, elimu ya kilimo cha umwagiliaji, ufugaji na uvuvi wa kisasa. Tukumbuke pia asilimia kubwa ya wakulima, wavuvi na wafugaji wamepata ujuzi husika kwa kurithi kutoka kwa wazazi au watu wao wa karibu.

Ushirikiano na umoja baina ya watendaji wa mikoa pamoja na mipango miji wakikaa chini na kupanga mikakati ya kuandaa mazingira na kutenga maeneo rafiki kwa ajili ya masoko makubwa pamoja na maeneo ya kujenga viwanda vya usindikaji mazao/nyama/samaki ili kuviweka katika ubora wa kimataifa na kuleta ushindani kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi na pia kuongeza bidhaa zitokanazo na mazao, samaki na mifugo.

Maonesho kama nane nane yawe mengi mpaka ngazi ya wilaya kufanya wahusika wasikie wanayotakiwa kusikia na kuona mambo yanavyofanyika kwa vitendo, maonesho na matamasha ya kilimo yataongeza motisha kwa kiasi kikubwa kwa wakulima na wadau wote na wale wanaotamani kuingia kwenye kilimo lakini wanakosa ari na ushawishi.

Tunatakiwa tutambue ni mkoa upi au ukanda upi kuna patikana zao la aina gani kwa wingi, ila nachomaanisha sasa iwe ni kuirasimisha na kufanya kua ni biashara ili wafanyabiashara wa mazao husika wajue masoko yapi waende kufata nini wanachotaka kwa utaratibu wenye faida pande zote, upatikanaji wa mazao kwa mwaka mzima ili viwanda vifanye kazi bila ya upungufu mazao, samaki au nyama.

Wakati mikakati na maandilizi makubwa yakifanywa na ngazi ya mikoa na wilaya, serikali kuu Kupitia wizara yake ya kilimo, mifugo na uvuvi nayo isiwe nyuma katika kuhakikisha vitu vinasogea kwa utaratibu na misingi mizuri ikiwa ni kuhakikisha mambo kisheria ambayo yatahitaji kurasimishwa au kupitishwa na serikali au bunge yana fanikiwa. Bajeti yenye kukidhi mahitaji ya shughuli zote na mchango wao kama serikali kuu, ushawishi mkubwa kupata wataalamu kutoka nje watakao changia kuharakisha mipango hii iendelee na iwe bora zaidi.

Kusikiliza kero kubwa na ndogo zinazowakabili wakulima na wafanyabiashara vilevie ili kuweka mazingira mazuri pande zote, kumekuwa na malalamiko mengi sana dhidi ya miundo mbinu, kodi na ruzuku nk. Hivyo ni vyema serikali ikisimamia Kupitia wataalamu wa sheria, ardhi, wataalamu wa kilimo, mifugo na uvuvi ili kuleta tija kwa pande zote.

Usimamizi mzuri wa kisayansi katika sekta hii itepelekea takwimu nzuri za idadi ya tani ngapi zitahitajika kwa ajili ya mahitaji ya ndani na ya viwanda kwa ajili ya kuuzwa kama bidhaa ndani na nje ya nchi na si kama malighafi kwenda nje na kuletewa bidhaa zilizotokana na tulivyozalisha, ikiwa sisi tungeweza kufanya hivyo wenyewe endapo tukiamua.

Taarifa niliyosoma kwenye tovuti ya kilimo inasema ni kwa 97% Tanzania tunajitegemea kwenye chakula, ila asilimia hizi zinabadilika kutokana na kiwango cha mvua za kila mwaka. Sasa Kwanini iwe hivi ikiwa tuna wataalamu ambao wanaweza kupanga mipango ya kuhakikisha tunafikia hadi uwezo wa kulisha nchi jirani na nyingine nyingi zenye uhitaji kwa njia za kisasa bila kutegemea mvua?

Maandalizi ni kitu cha kwanza kabla ya kuamua kufanya jambo, hili suala linahitaji maandalizi makubwa ya maandishi na kitaalamu kuhakikisha mchakato uta kamilika na kufanikiwa. Wizara ya elimu, sayansi teknolojia na ufundi pamoja na wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi wahakikishe tunakua na wataalamu wengi walioandaliwa kukidhi mahitaji yao katika sekta hii.

Kuna shule za mchepuo wa kilimo nchini, kuongezwe usimamizi au ikibidi kuleta somo la kilimo na ufugaji mashuleni ili kuwaandaa vijana kitaalamu na kuwaongezea fursa nyingine ya kuchagua katika maisha yao. Kila kitu ni fursa inategemea tu na jinsi zilivyoandaliwa pamoja na uwezo wa watu kuchanganua na kujitengenezea fursa ila kwa maandalizi bora kielimu na mazingira.

Mikakati mizuri itaamsha hamasa kwa wadau na wawekezaji kujikita ipasavyo kwenye kilimo, fursa nyingi zitafunguka kutokana na uwekezaji na mipango mizuri kwenye kitu ambacho tayari kina mizizi nchini (kilimo, ufugaji na uvuvi). Huu ndio upande utakao sababisha ongezeko la viwanda nchini kwa kasi kuliko upande mwingine wowote.

Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. DUMA ana mbinu na kasi katika uwindaji lakini anarudishwa nyuma na malezi ya kobe, tuwe mama duma.

Imeandikwa na Baraka Jereko

kutoka Bongo5
 
Back
Top Bottom