Kilimanjaro: TAKUKURU yaingilia sakata la Meya aliyeng’olewa Moshi

Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imethibitisha kuwa inamchunguza aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu ambaye alivuliwa wadhifa huo Aprili 11, 2022, kwa tuhuma mbalimbali.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Frida Wikes alisema walipokea taarifa na tuhuma kadhaa zinazomkabili Raibu, wanaendelea kuzifanyia kazi na kukataa kuingia kwa undani aina ya tuhuma zinazochunguzwa na taasisi hiyo.

Raibu ambaye pia ni Diwai wa Kata ya Bomambuzı, baadhi ya tuhuma anazokabiliwa nazo ni matumizi mabaya ya ofisi, kuruhusu ujenzi holela eneo la kibiashara katikati ya mji (CBD) katika mazingira ya rushwa na mienendo mibaya na ukosefu wa adabu kwa madiwani wenzake.

Raibu alipigiwa kura katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani, Manispaa ya Moshi ambapo kura 18 ziliafiki ang'olewe katika nafasi hiyo kutokana na kukabiliwa na tuhuma mbalimbalı, huku kura 10 zikimkingia kifua aendelee kuwa Meya.

“Siwezi kuwaingilia katika hili, lakini baadhi ya viongozi wa chama Mkoa na Wilaya wameingilia suala hili kuhakikisha naondolewa kwa sababu nimeingilia maslahi ya chakula chao," alinukuliwa Raibu baada ya kung’olewa.

Nacho, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimedai kusikitishwa na kauli ya Raibu kuhusisha viongozi wa chama hicho na kuondolewa kwake katika madaraka hayo wakidai suala hilo ni la Kiserikali.

Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alisema utaratibu wa kumuondoa Meya madarakani ulifanywa na Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro na Halmashauri na chama hicho hakihusiki.

Aidha, Raibu aliwahi kutajwa kwenye sakata la mfanyabiashara Elioth Lyimo, aliyedai kuchukuliwa fedha zake Sh25 milioni na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kwamba wakati akizichukua alikuwa na Raibu.


Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom