Kilimanjaro: Mkuu wa Mkoa, Anna Mghwira akemea wapambe wa Wagombea kutekwa na kuteswa

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amekemea vitendo vya watu wanaodaiwa kuwa wapambe wa wagombea kutekwa, kuteswa na kutupwa kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo.

Zaidi ya watu wanne wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika katika matukio hayo yanayodaiwa kusababisha vurugu zinazoashiria uvunjifu wa amani wakati huu wa kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwanywesha pombe wapambe wa wagombea ili wakilewa wapate taarifa za siri kuhusu mikakati ya kupata ushindi katika nafasi za udiwani na ubunge.

Mghwira jana aliwaeleza waandishi wa habari kuwa zimetokea vurugu katika wilaya za Rombo, Hai na Moshi zenye majimbo ya Hai, Rombo, Vunjo na Moshi vijijini.

Alisema vurugu zilizotokea zinahusisha watu kutekwa, kuumizwa, kutupwa pembezoni mwa mito, mifereji, misituni na barabarani, na kwamba, zimehusisha baadhi ya wagombea.

"Kama mkoa hatutakubali kuona vitendo viovu vinaendelea na kwa namna moja au nyingine itakwamisha wagombea wa vyama tofauti kutoa sera zao lakini wananchi watashindwa kwenda kuwasikiliza"alisema Mghwira.

Alitaka wakuu wa wilaya mkoani humo kuhakikisha wagombea wa vyama vyote vya siasa kwa ngazi mbalimbali wanakuwa na ulinzi wa kutosha ili kuepuka vurugu za aina yoyote.

Mghwira alisema si uatamaduni wa wakazi wa Kilimanjaro kufanya vurugu za aina yoyote wakati wa siasa na badala yake wananchi wamekuwa makini kusikiliza sera na kuchagua viongozi wanaodhani wanawafaa.

Alisema kutokana na tishio hilo la vurugu, mkoa kwa kushirikiana na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini imeandaa kongamano la siku moja la amani ili kuwakumbusha wagombea na wananchi wajibu wao wakati wa siasa.

Hivi karibuni mgombea ubunge jimbo la Rombo (CCM), Profesa Adolf Mkenda alieleza kukerwa na kuibuka kwa vurugu katika mikutano ya kampeni.

Alidai pia kuwa, misafara ya baadhi ya wagombea imekuwa ikishambuliwa kwa mawe baada ya kumalizika mikutano.
 
Back
Top Bottom