Kilango anavyosaka mabadiliko kwa nguvu zote

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
56,593
30,451
Kilango anavyosaka mabadiliko kwa nguvu zote

Habari Zinazoshabihiana
• Panga lisiishie Maliasili
• Katika CCM sawa, serikalini bado
• Nionavyo: Mahakama na Polisi changamoto imebaki kwenu

*Alonga mapambano yake si na mafisadi bali mabadiliko
*Asema hawezi kupambana na majambazi kwa sauti ya upole
*Ajikita katika Kitabu cha Maombolezo 5:1 katika Biblia

Na John Daniel

NI takriban muda wa wiki tatu sasa tangu Mkutano wa 12 wa Bunge la Bajeti lilipoanza mjini Dodoma ikiwa na sura tofauti na iliyozoeleka kwa Bunge la Tanzania kuwa kimya na kubakia na kazi ya kukubali kila kinachosemwa na Serikali, hali hii ilifanya wananchi watafsiri Bunge kuwa ni mhuri lakini safari hii hali inaonekana kupungua kama si kutoweka kabisa.

Tafouti iliyopo katika Bunge la mwaka huu ni kutokana na baadhi ya wabunge wa CCM kuonesha wazi kutaka kujua kwa undani baadhi ya masuala mazito katika Taifa yanayozua maswali mengi miongoni mwa wananchi kama vile hatma ya fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (EPA), watuhumiwa wa ufisadi wa Richmond na fedha za Commodity Import Support.

Mmoja wa wabunge waliokunjua makucha kuonesha nia ya kusaka mabadiliko ni Mbunge wa Same Mashariki, Bi. Anne Kilango-Malecela, ambaye alizungumza kwa sauti ya ukali na kusababisha wengine kumtafsiri tofauti na malengo yake. Nimefanya mahojiano na mbunge huyo kama ifutavyo:

Swali: Wewe ni Mbunge wa CCM na umeonesha ukali zaidi kuzungumzia kile kinachotafsiriwa na watu kuwa ni kuchukia ufisadi, ni kweli sauti yako ya ukali ilitokana na kuchukia ufisadi au ulimaanisha kitu kingine?

Jibu: Mimi nataka nianzie mbali kidogo, ili uweze kuelewa mada yangu vizuri, kwanza ni muhimu kila mmoja aelewe kwamba Tanzania ni nchi tajiri sana kulingana na rasilimali tulizonazo, lakini ni nchi masikini sana ambayo watu wake ni masikini ikilinganishwa na wananchi wa nchi nyingine ambao hawana hata rasilimali kama sisi.

Kutokana na hali hiyo sisi wabunge tumekuwa tukifanya utafiti na kujiuliza what is our problem (tatizo letu ni nini)?.

Labda nikupe mfano mmoja rahisi tu; mimi nimebahatika kutembea katika nchi mbalimbali, kila nikukutana na Wamarekani nikiwa nimevaa hizi pete zangu zenye tanzanite au mkufu na kuwaambia natoka Tanzania wananiuliza Can you afford tanzanite (Unaweza kumudu kununua tanzanite)?

Swali hili linatokana na bei na thamani halisi ya tanzanite katika soko la kimataifa. Lakini cha ajabu ni kwamba, watu ambao ndio wanatoa madini hayo ya kipekee duniani kote ni masikini wa kutupwa, hapa lazima kuna tatizo mahali fulani.

Sisi wabunge tumekuwa tukitafuta sababu hiyo ya hali duni wakati vitu vinavyoweza kutufanya tusiwe masikini tunavyo.

Huu ni mwaka wangu wa nane ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, muda wote huo mimi na wabunge wenzangu tumekuwa tukijiuliza swali kubwa, tuna tatizo gani? Kwa nini tuwe masikini wakati tuko katika nchi tajiri? Sote tunajua kwamba utajiri wetu unatokana na rasilimali tulizopewa bure na Mungu.

Hakuna asiyejua kwamba tuna madini ya kila aina; dhahabu, almasi, makaa ya mawe, gesi asilia, misitu na mbuga za wanyama zinazovutia watalii wengi kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Sisi Tanzania pekee ndio tuna madini ambayo hayapatikani katika nchi yoyote ile duniani lakini pia ni ya thamani kubwa sana na zaidi, licha ya yote hayo bado sisi ndio masikini wa kutupwa na watu wetu wanateseka kwa umasikini.

Kutokana na hali hiyo, tumekuwa tukisema kuna kasoro mahali lakini bila kugundua tatizo liko wapi.

Kama unavyojua, mtu yeyote mwenye busara, hawezi kuzungumza bila uthibitisho, hivyo tulikuwa katika utafiti wa muda mrefu wa nini siri ya umasikini wetu, lakini sasa tumepata jibu, tunalo jibu, baada ya EPA ndio tumegundua siri ya matatizo yetu inatokana na nini.

Swali: Umesema sasa mmegundua kile mlichokuwa mkikifanyia utafiti kwa muda mrefu, ni nini hiyo siri ya umasikini wetu?

Jibu : Bado nataka ujue historia ya kwa nini nilizungumza kwa ukali, unajua nafanya hivyo ili kusaidia wenzangu ambao kwa bahati mbaya hawakuelewa.

Katika siku tuliyofarijika ni siku ambayo Katibu Mkuu Kiongozi Bw. Phelemon Luhanjo, alipotoa taarifa kuhusu EPA, siku hiyo ndio tulipata jibu la matatizo yetu, huko nyuma tulikuwa tunafikiri tu, hatukuwa na uhakika.

Hoja yangu na wabunge wenzangu, kuzungumza kwa ukali si vita kati yetu na mafisadi, hapana, hao wanaonitafsiri hivyo wamekosea sana, sisi wabunge hatuna vita na mtu yeyote na hiyo si kazi yetu, vita yetu wabunge baada ya kujihakikishia kwamba tunakuwa masikini kwa sababu mapato na rasilimali za nchi zinahodhiwa na watu wachache, sasa tunataka mapato na rasilimali hizo zitumike kwa manufaa ya Watanzania wote, hiyo ndio siri ya ukali wangu.

Kama watu wanataka kujua siri ya mimi kuzungumza kwa ukali ndiyo hiyo, sasa tunataka mabadiliko kutoka hapo tulipo na mabadiliko lazima yaanzie kwetu wabunge, kutokana na siri tuliyopata.

Inaonekana hali hii ya watu wachache kuhodhi mapato na rasilimali za watu wengi, imeota mizizi na kitu kilichoota mizizi kuing’oa si kazi rahisi, inahitaji nguvu nyingi, huwezi kuzungumza kwa upole.

Hii si vita yetu wabunge peke yetu, tunahitaji mambo matatu makubwa; moja, utayari wa Serikali kukubali mabadiliko haya; pili, mshikamano wa wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kujali itikadi na tatu, tunahitaji makanisa yote yaombee mabadiliko haya, ili yawezekane kwa uwezo wa Mungu, tunahitaji Waislamu wote watenge siku maalumu wasalie mabadiliko haya.

Ukisoma Biblia, Maombolezo 5:1: “Ee Bwana unajua yaliyotupata, utazame na kuina aibu yetu, urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni,” hicho ndicho kilio chetu sisi wabunge, si vita na mafisadi hapana, vita yetu ni kutaka mapato, rasilimali, urithi wetu ziwafaidishe Watanzania wote na si watu wachache, mstari huu wa Biblia umebeba kilio cha Watanzania.

Swali: Wewe ni Mbunge mmoja unayetaka mabadiliko, unadhani mabadiliko hayo yanawezekana kwa sasa wakati inaonekana kuna mgawanyiko kati yenu wenyewe?

Jibu: Siko peke yangu kama watu wanavyofikiri, pia hakuna mgawanyiko kati yetu, ukisoma vitabu vya Oganaizesheni, ni vizuri kila Kiongozi asome vitabu hivi, vinasaidia kujua jinsi ya kuishi na watu wa aina tofauti bila shida.

Hakuna kitu kigumu kama mabadiliko, yawe ya kisiasa, kiuchumi na kiutawala, ni kazi ngumu kweli kweli, wapo baadhi ya watu wataibuka na kutetea maslahi yao binafsi kwa sababu mabadiliko yanaingilia maslahi yao.

Wengine wanajua mabadiliko yanaweza kuwaondoa katika nyadhifa zao, hivyo hawawezi kukubali mabadiliko, hiyo ndio shida iliyopo sasa na si vita wala mgawanyiko.

Kwa mujibu wa vitabu vya Oganaizesheni, hakuna mabadiliko yanayoweza kukubaliwa na Oganaizesheni nzima, hapana. Lazima wapinzani wa mabadiliko wawepo, tena wanaweza kuwa na hoja zinazoweza kuonekana nzuri, lakini kwa kutetea maslahi yao au nyadhifa zao.

Ni kweli, kwamba mabadiliko yatachukua muda, si kitu cha leo na kesho, itachukua muda, lakini tukisimama imara na kusali, tutashinda, kwani ni lazima Mungu atusaidie katika kuleta madiliko...unajua mabadiliko haya akiyataka Rais Kikwete kama Rais mwenyewe hawezi.

Mabadiliko haya wakiyataka wananchi hata kama wana nguvu lakini lazima mhimili Bunge uwe imara kuyatetea bila kutetereka, ndiyo maana tumejua wananchi wanataka mabadiliko na sisi kama Wabunge lazima tusimame imara kuyatetea bila kurudi nyuma, nadhani najibu swali lako vizuri.

Mfano Afrika Kusini ni ya Waafrika, lakini makaburu waliamua kila Rais ni kaburu, kila kitu kizuri ni kaburu, Waafrika walipoamua kutaka mabadiliko iliwachukua muda.
Walioanza kusaka mabadiliko hawakuliona, lakini waliambizana kabisa, sisi tutakaokufa tutatangulia na watakaobaki mwendeleze mapambano mpaka mabadiliko yapatikane, walimweka Mungu karibu na wameshinda.

Hata Rais wao Mstaafu Nelson Mandela,alikubali kukaa gerezani miaka 27 kutaka mabadiliko, hivyo si kazi rahisi, na sisi tunasaka mabadiliko kwa ajili ya watoto wetu, wajukuu zetu, vituu na vijazo vijavyo.

Sasa Bunge letu linapita katika wakati mgumu wa kutaka mabadiliko, si lazima walioanza mabadiliko haya ndio wamalizie, lakini tuna bahati moja, kwamba Rais aliyeko madarakani ameunga mkono mabadiliko haya.

Swali: Lakini hata kama mnataka mabadiliko, unadhani yatawezekana wakati inaonekana wasiotaka mabadiliko wana uwezo mkubwa na mbinu nyingi za ushawishi na pia unaweza kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu sauti yako ya ukali bungeni?

Jibu: Kwanza lazima ujue kwamba kwa kuwa Serikali iliyopo madarakani inataka mabadiliko haya, inawezekana tukashinda kabisa, kitu ambacho watu hawajui ni kilekile nilichosema kuhusu Oganaizesheni.

Katika Oganaizesheni, hamwezi kufanana kimawazo, hapana, lakini nakuhakikishia kwamba karibu asilimia 90 ya wabunge, wanataka mabadiliko na wasiotaka lazima wawepo, ndio sifa ya Oganaizesheni kubwa kama Bunge.

Wapo aina nyingi za wabunge, wapo wanaunga mkono mabadiliko, lakini hawazungumzi ila wanaunga mkono hoja, wapo wanaozungumza tena kwa ukali, pia wapo ambao hawataki lakini nakuhakikishia wanaotaka mabadiliko ni wengi zaidi.

Sasa nikujibu kwa nini nazungumza kwa sauti ya ukali, unajua unapozungumza na jambazi, huwezi kuzungumza naye sauti sawa na sauti unayozungumza na mumeo au mkeo, hapana, lazima uzungumze naye sauti ya ukali kuonesha umekasirishwa na tabia yake, na pia watu hawawezi kufanana katika kusema, hakuna kitu hicho katika Oganaizesheni.

Kwa bahati nzuri mimi natoka katika familia masikini sana, pale kijijini kwetu familia yetu ni masikini sana, najua adha ya umasikini, kuna aina nyingi za umasikini, upo umasikini wa kujitakia mwenyewe wa mtu kutotaka kufanya kazi, lakini mimi nazungumzia umasikini wa kusababishiwa na mtu mwingine kwa kuhodhi mapato na rasilimali za Taifa.

Huwa najiuliza sana, kwa nini Kibabu cha Maombolezo sura ya 5:1 kiwepo kwenye Biblia? Ni kwa ajili yetu sisi Watanzania, sauti yangu lazima iwe kali zaidi ninapozungumzia mabadiliko, kwani sauti ya mabadiliko ni ya vita ya ukombozi kutaka mabadiliko haiwezi kuwa ya upole.

Hakuna mwanajeshi aneyekwenda vitani kupigana na adui wa nchi yake na kutekeleza jukumu lake kwa upole.

Ninaamini hata kama wasiotaka mabadiliko,wanaweza kutumia njia nyingi, lakini mabadiliko ni lazima hata kama si leo, wala kesho, tunataka kila mmoja ajue, kwamba kama leo hatutafanikiwa kuleta mabadiliko basi kazi iendelee 2010, 2015 mpaka 2025, lakini mwisho mabadiliko ni lazima ili kila Mtanzania afaidi matunda ya nchi yake kupitia CCM.

Nataka watu wanaodai kwamba kuna mgawanyiko kwa wabunge wa CCM nao waache kabisa, wasome Oganaizesheni, kisha watajua hakuna mgawanyiko ila kuna harakati za mabadiliko na hatuwezi kufanana kimtazamo.

Wabunge wote wa CCM na CCM yenyewe, haiwezi kuwa na mgawanyiko na anayefikiri hivyo nampa pole, ila akasome vitabu vya Oganaizesheni, ili asipate shida na asipotoshe Watanzania wanaohitaji mabadiliko kupitia Serikali yao ya CCM.

Swali: Matarajio yako kwa ujumla katika haya yote tuliyozungumza ni nini?

Jibu: Tarajio langu la kwanza ni kuondoa umasikini ambao sisi viongozi tumeuendekeza kwa ubinafsi wetu badala ya kujali maslahi ya Taifa na kuhurumia Watanzania walio masikini zaidi.

Hii itawezekana kwa kuwa Rais mwenyewe ana uchungu na watu wake akija Same anaona hali ilivyo, akienda jimbo lingine anaona hivyo, ameamua kutaka mabadiliko na sisi wabunge lazima tumsaidie kusimama kidete mpaka mabadiliko yapatikane.

Lakini kabla hatujamaliza, nitoe rai moja kwa wabunge wenzangu na Watanzania kwa ujumla, kwamba mabadiliko si kazi rahisi, wasikate tamaa wala kurudi nyuma, tuungane kwa pamoja mpaka tutakapopata mabadiliko, kutakuwa na misukosuko mingi lakini ndio njia ya kuelekea kwenye mabadiliko, wasiwe watu wa kukata tamaa wala kugeuka, waangalie mbele, daima tutashinda.

Bi. Anne Kilango-Malecela (52) alizaliwa Januari 9,1956 katika kijiji cha Kihurio Kata ya Kihurio, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro. Alijiunga na siasa rasmi mwaka 1994 baada ya kuamua kung'atuka ualimu wa sekondari.

Kabla ya kuanza siasa, Bi. Kilango alifanya kazi ya Uhasibu katika mashirika kadhaa ya ndege ikiwamo ATC na baadaye kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kata ya Kinondoni, Dar es Salaam na baadaye Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kinondoni hadi mwaka 2003 alipoanza harakati za kusaka uwakilishi wa jimbo.

Mwaka 2000 aligombea ubunge Kinondoni lakini hakuteuliwa na chama na badala yake Rais alimteua kuwa Mbunge na mwaka 2005, aliamua kugombea Jimbo lake la Same Mashariki ambapo aliibuka kidedea.
 
Alonga mapambano yake si na mafisadi bali mabadiliko

Sentensi hii iko ambiguous, inaweza kumaanisha kuwa huyu mama hataki kupambana na ufisadi ila anataka kupambana na mabadiliko.

Editor yuko wapi? Lakini sub-heading imeanza na "Alonga..." what do you expect?
 
*Alonga mapambano yake si na mafisadi bali mabadiliko
*Asema hawezi kupambana na majambazi kwa sauti ya upole

Hata mimi ananichanganya!!! au pengine hajui atendalo?

Hii ya chini nayo ina miti mingi!!!


• Katika CCM sawa, serikalini bado

Kidumu chama cha mapinduzi
 
*Alonga mapambano yake si na mafisadi bali mabadiliko
*Asema hawezi kupambana na majambazi kwa sauti ya upole

Hata mimi ananichanganya!!! au pengine hajui atendalo?

Hii ya chini nayo ina miti mingi!!!


• Katika CCM sawa, serikalini bado

Kidumu chama cha mapinduzi
 
Back
Top Bottom