Kurzweil
JF-Expert Member
- May 25, 2011
- 6,622
- 8,410
Uchaguzi Mkuu wa Uingereza ni nini hasa?
Ni utaratibu ambao Waingereza wanachagua wawakilishi wao bungeni, na kuiongoza nchi kwa ujumla. Wagombea katika uchaguzi huo mkuu hutokana na vyama vya siasa, lakini pia kuna wagombea huru. Mgombea atakayepata kura nyingi zaidi katika jimbo husika, atachaguliwa kuwa Mbunge, na atawakilisha jimbo husika katika Bunge la ‘House of Commons’ (Bunge jingine ni ‘House of Lords’ ambalo ‘wabunge’ wake hawachaguliwi kwa kura)
Waziri Mkuu anapatikanaje kupitia uchaguzi mkuu?
Kiongozi wa chama cha siasa kitakachoshinda viti vingi vya ubunge, ataombwa na Malkia kuwa Waziri Mkuu na baadaye kuunda serikali. Kiongozi wa chama kitakachoshika nafasi ya pili ndiye anatarajiwa kuwa ‘kiongozi wa kambi ya upinzani.’
Kuna jumla ya viti 650, na ili kuunda serikali ya peke yake, chama husika kitahitaji viti 326 au zaidi.
Nini kinatokea baada ya mbunge kushinda?
Baada ya kushinda uchaguzi, mbunge hufanya kazi jimboni kushughulikia masuala mbalimbali yanayowahusu wakazi wa eneo husika, na pia hufanya kazi bungeni ambako wabunge hupiga kura na kuunda sheria.
Kwanini uchaguzi huo mkuu unafanyika leo (maana kulikuwa na uchaguzi mkuu mwaka 2015)?
Uchaguzi huu mkuu ‘ujao’ ulipaswa kufanyika Juni mwaka 2020, lakini Waziri Mkuu Theresa May alitangaza April 18 mwaka huu kuwa ataitisha uchaguzi wa ghafla (snap election). Siku moja baadaye, Bunge lilipiga kura na kuidhinisha uamuzi huo wa Waziri Mkuu.
Nani ataibuka mshindi?
Kwanza, kama ilivyoelezwa awali, ushindi si kama ule wa huko nyumbani ambapo, kwa mfano, Rais John Magufuli aliibuka mshindi baada ya kumshinda mpinzani wake mkubwa Edward Lowassa (bila kujali matokeo ya wabunge). Kwa hapa, ushindi unatokana na idadi ya viti vya ubunge. Kwahiyo ili Theresa May ‘amshinde mpinzani wake Jeremy Corbyn’ itamlazimu chama chake cha Wahafidhina (Conservatives) kishinde idadi kuwa ya viti vya ubunge.
Kuhusu kura za maoni, chama tawala cha Conservative kinaongoza kwa takriban pointi 12. Hata hivyo, kwa kuzingatia kura za maoni (opinion polls) ‘zilivyoingia boya’ kwenye kura ya maoni (referendum) ya Uingereza kubaki au kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya Brexit na pia jinsi kura za maoni zilivyobashiri ‘ndivyo sivyo’ kwenye uchaguzi wa Rais wa Marekani, haitokuwa ajabu kushuhudia Labour wakiibuka na ushindi dhidi ya Conservatives.
Idadi ya waliojiandikisha ikoje?
Jumla ya watu milioni 46.9 wamejiandikisha kupiga kura katika vituo 40,000 vya kupigia kura. Idadi hiyo ni kubwa kiasi kulinganisha na uchaguzi mkuu uliopita ambapo idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ili milioni 46.4
Baadhi ya waliojiandikisha wameshapiga kura kupitia mfumo wa kupiga kura kwa njia ya posta.
Moja ya mambo yanayoweza ‘kufanya miujiza’ kuwezesha Labour kushinda ni jinsi hamasa iliyoongoza na kiongozi wake Jeremy Corbyn kuhusu kujiandikisha kupiga kura, itakavyoweza kutafsiri katika idadi ya watakaojitokeza kupiga kura, na kukipigia kura chama hicho.
Hali ikoje Uskochi?
Chama tawala cha SNP kinatarajiwa kupoteza viti kadhaa. Vyama vya Scottish Conservatives and Scottish Labour vinachuana vikali kushika nafasi ya pili. Matokeo kwa SNP ni muhimu mno kuhusiana na ajenda ya chama hicho kuitisha kura nyingine ya maoni kwa ajili ya ‘uhuru wa Uskochi.’ SNP ikishinda kwa wingi, itajenga taswira nzuri kuhusu ajenda yake ya kura ya maoni ya pili ya ‘uhuru wa Uskochi.’ Ikipata matokeo yasiyoridhisha, inaweza kujenga taswira kuwa hata wazo la ‘uhuru wa Uskochi’ litafeli pia.
Nani anaruhusiwa kupiga kura?
Raia wa Uingereza mwenye miaka 18 au zaidi, na aliyejiandikisha kupiga kura; raia wa Jamhuri ya Eire wanaoishi Uingereza, na raia wa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Madola (ikiwemo Tanzania) wenye umri wa miaka 18 au zaidi, na waliojiandikisha kupiga kura.
Vipi hatma ya Brexit kuhusiana na uchaguzi huu mkuu?
Theresa May na Conservative yake wakishinda, ni habari njema zaidi kwa mchakato wa kuitoa Uingereza kwenye Umoja wa Ulaya (Brexit). Lakini hata kama Jeremy Corbyn atashinda, Brexit itaendelea, ila tofauti kati ya vyama hivyo viwili ni katika vipengele mbalimbali vya utekelezaji wa suala hilo. Kwahiyo kwa kifupi, Brexit itaendelea bila kujali chama gani kitashinda na kuunda serikali.
Vipi kuhusu kura ya maoni ya ‘uhuru wa Uskochi’?
Kama nilivyoeleza awali, matokeo ya uchaguzi huu mkuu kwa huku Uskochi yatatoa taswira nzuri kuhusu kiwango cha kukubalika au kutokubalika kwa wazo la kura ya pili ya maoni (referendum) ya ‘uhuru wa Uskochi.’ Iwapo SNP itashinda kwa wingi itakuwa ishara nzuri kwa ajenda hiyo, lakini chama hicho tawala kisipofanya vizuri sana, si habari njema kwa ajenda hiyo. Kwa kifupi, kwa SNP sio suala la kushinda tu (na kwa vyovyote vile chama hicho kitashinda) bali ushindi huo ni mkubwa au mdogo kiasi gani.
Je matokeo yataanza kufahamika saa ngapi?
Upigaji kura utamalizika leo saa nne usiku (saa sita usiku kwa saa za Afrika Mashariki). Kwa vile wenzetu wamewekeza mno kwenye teknolojia ya uchaguzi, vituo vikuu vya runinga vitafanya ubashiri wao kuhusu mshindi wa uchaguzi huo mara tu baada ya upigaji kura kumalizika rasmi leo saa nne usiku.
Chanzo: Uchambuzi huu umefanywa na Evarist Chahali, mmiliki na afisa mtendaji mkuu wa kampuni ya AdelPhil Consultancy ya Glasgow, Uskochi, ambayo pamoja na masuala mengine, inajihusisha na ushauri wa kitaalamu wa masuala ya siasa (political consulting). Kampuni hii pia inajihusisha pia na ushauri wa kitaalamu kuhusu intelijensia na usalama, elimu, nyenzo za kidigitali, biashara na masoko ya kimataifa.