Kila la kheri Chiligati, nenda kachume janga

engmtolera

JF-Expert Member
Oct 21, 2010
5,151
2,000
DEMOKRASIA ni dhana pana. Ni haki ya kila mtu kufanya kile atatakacho almradi havunji sheria.

Dhana hii chimbuko lake ni haki ya binadamu ambayo haiombwi kwa yeyote.
Inafahamika kuwa kila binadamu aliyezaliwa ana haki hizo, hakuna kujaza fomu kuiomba, hakuna kuisomea ili ufikie. Ni haki kwa sifa ya kuwa tu, wewe ni binadamu.
Pamoja na uzuri wa dhana hii, mara nyingi wengi wameshindwa kuitumia; ama kwa kujua au kwa kutokujua na hivyo kutumiwa.


Kwamba demokrasia imekuwa ni njia mojawapo ambayo mazuzu kujitutumua ili nao waheasabiwe mbele ya watu kwamba wamo miongoni mwa binadamu.
Mwaka 2006 ulikuwa mwaka wenye sekeseke nyingi nchini, mbali ya kuwa na baa la njaa, ukame mkubwa uliosababisha mgawo wa umeme, haki ya kidemokrasia iliamsha umma kuonyesha uzuzu wao juu ya kile walichokuwa wanakifanya.


Hili ni lile tukio la watu kuandamana kulaani filamu ya Darwin’s Nightmare, ambayo iliandaliwa na Mfaransa ajilikanaye kwa jina la Hubert Sauper.
Katika filamu hii alionyesha jinsi mataifa yaliyoendelea yanavyonufaika na rasilimali za ziwa Victoria hasa samaki wakati wananchi waliozunguza ziwa hili wakiishi maisha mithiri ya kuku wa kienyeji.

Wannachi wanakula mabaki ya samaki ambayo yamekwisha kutolewa minofu, haya ni mabaki ya mifupa na kichwa. Hakuna mnofu wa maana. Wakazi wa mikoa inayozunguka ziwa hili, waliibatiza mapanki.
Baada ya filamu hiyo kutolewa, utawala wa Tanzania ulikasirishwa na kuzungumza kwa ukali kuonyesha kwamba ilikuwa imetia chumvi; ilisisitiza “hakuna Mtanzania anayekula mapanki.”


Kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia wakazi wa Jiji la Mwanza walifanya maandamano wakiilaani filamu hiyo na wote walioshiriki kuifanikisha; lakini kubwa zaidi wananchi waliokuwa wanaandamana walikuwa wanasema “hawali mapaki.”
Nilikuwa miongoni mwa watu waliojisumbua kuitazama filamu hiyo, kusema ukweli hata kama kulikuwa na la kukera hapa na pale, lakini kulikuwa hakuna uhalali wa kukasirika kwa kiwango kile.


Waliokuwa wanajishugulisha na “mapanki” ni raia wa nchi hii na walikuwa wanafanya hivyo kujitafutia kipato. Mapanki yanaliwa na watu, lakini pia yanatumika kutengeneza chakula cha mifugo.


Kwa maana hiyo, ingawa Sauper anaweza kushutumiwa kwamba katika mambo yote yaliyoko Tanzania aliloona ni mapanki tu, lakini ukweli unabaki palepale, kwamba sehemu kubwa ya utajiri unaopatika Ziwa Victoria, haunufaishi wananchi.


Wakati wananchi wanaolizunguka eneo hili wakiishia kwenye shughuli ya mapanki minofu inapanda ndege kwenda Ulaya. Kimsingi katika hili, serikali ilitakiwa kukiri kwamba kuna changamoto ya sera na mikakati ya taifa katika kuwawezesha watu wake.


Tukiweka mengine pambeni kitendo cha wananchi kuandamana na kuimba hawali mapanki wakati wanajua fika wanakula, na pengine baada ya maandamano hayo kitoweo pekee kilichokuwa kinawasubiri nyumbani kwao ni mapanki, nilikiona kama kihoja cha mwaka na uzuzu wa hali ya juu wa kisingizio cha demokrasia.


Uzuzu huo huo ndio nimeanza kuuona ukiibuka tena sasa baada ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kususa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, bungeni mjini Dodoma.


Wabunge hawa walifanya jambo moja ambalo katika taratibu za siasa za vyama vingi ni haki yao; walionyesha kile ambacho wanaamini hawajatendewa haki.


Walitoka nje ya ukumbi wa Bunge mara rais Kikwete alipoanza kuhutubia.
Waliondoka bila kufanya vurugu, hawakuzomea mtu, hawakumng’ong’a yeyote.
Walitoka kimya kimya. Hata pale wenzano waliobaki walikosa uvumilivu na kuwazomea na kwa kuwakejeli, wao hawakujibu mapigo.


Baada ya tukio lile, watu wametaharuki, wapo wanaopanga kuwasilisha azimio bungeni, wapo waliopanga maandamano kana kwamba wabunge wa CHADEMA wamevunja sheria, au kanuni yoyote inayoelekeza jinsi ya kushiriki katika siasa za nchi hii.


Wote wanaolalama ukiwauliza wanapata wapi ujasiri wa kulalama, hakuna mwenye majibu. Kukurupuka huku nakufananisha na wale walioandamana kulaani mapanki ambayo pengine wengine walikuwa wameyala muda mfupi uliopita na wengine yalikuwa yanawasubiri nyumbani.


Dhana ya domokrasia ni nzuri, lakini demokrasia bia kutumia akili ni uzuzu. Ndiyo maana mtu anapotafakari siasa zetu anagundua kwamba kama taifa hatuwezi kipiga hatua mbele kwa kuwa wengi tunatumiwa tu.


Tunatumika na kuchakaa mno, lakini kinachoumiza zaidi ni pale mchaakaji anaposhindwa kutambua amechakaa, na kwamba maslahi yake yanahitaji kutazamwa, anahitaji kufikiriwa, anahitaji mambo yake yatengenezewe taratibu na kaununi ambazo zitaponya wote katika jamii.


Tatizo kubwa la taifa hili ni uzuzu. Wapo watu wameamua kuwa mazuzu hata pale wanapoona miili yao inateketea. Hawa bado wanaamini watamfurahisha mkubwa na aliyefurahi ataona huruma.
Wenye fikra za namna hii ni watu sawa na wafu, hawawezi kujikomboa wengine na kwa maana hiyo hawatarajiwi wala kuhesabiwa kwamba wanaweza kusaidia mapambano ya kukomboa wengine.


Jaribu kufikiri, mtu anakula mapanki lakini anathubutu kusema hali, anaandamana na kulaani kuambiwa amekula panki ambalo limo tumboni mwake saa hiyo. Je, mtu wa aina hii, anatii hisia zake binafsi au ni mtu wa kuagizwa? Je, akiambiwa tuletee kidole chako komoja nini kitamzuia kukikataa na kukikabidhi?


Kama mtu hawezi kujionea huruma mwenyewe hiyo demokrasia ya kuandamana inakupa faida gani? Inakuongezea shibe ipi? Inakupa nguvu gani?

Kwa nini jamii kwa ujumla wake, haitaki kujadili msingi wa wabunge hawa kutoka nje ya ukumbi wa bunge? Je, wamezusha madai yao, au umma unataka kisingizio cha demokrasia kitumike kuwakaza wengine kuonyesha hisia zao hata katika mambo ya msingi?

Duniani kote watu wana njia mbalimbali za kuwasilisha hisia zao juu ya jambo fulani, ama kuliunga mkono, kulikataa au hata kushinikiza liwepo kama halikuwapo. Kufanya hivyo ni haki, na haiwezi kuminywa na yeyote.


Ni kwa msingi huo watu kama akina John Chiligati, katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, alipaswa kujua vilivyo kwamba wabunge wa CHADEMA kwa maana ya kanuni, sheria na taratibu za kisiasa hakuna kosa lolote walilofanya kwa hatua yao ya kutoka nje ya ukumbi wa bunge wakati rais anahutubia.

Hivyo anapaswa kuelewa kuwa kutafuta azimio la kuwasilisha bungeni dhidi yao, ni kutaka kuwasha moto ambao hawataweza kuuzima.

Chiligati na wenzake, ni vema wakacheza siasa ndani ya ukumbi wa bunge, ambako kwa bahati nzuri kuna kanuni na sheria za kubanana, lakini wakifanya kosa kama lile la kumfukuza Zitto Kambwe baada ya kuwasilisha hoja ya Buzwagi.


Na kwa jinsi mambo yanavyokwenda, hakuna ambaye anaweza kukiondoa chama chao na serikali yake katika kina kirefu na kujinasua huko itakuwa ni kilio na kusaga meno.
Sijui kama sekretariati ya CCM inafahamu hili, kwa kuwa siku nyingi walikwisha kuaharisha kutumia bongo zao sawa sawa, lakini kwa kuwa wamekuwa sikio la kufa, tunawatakia kila la kheri katika safari hii ya kwenda kuchuma janga.

Chiligati alidokeza, sasa chama chake kinamsubiri katibu mkuu wake, Yusuf Makamba atamke kwamba wamekwisha tayarisha azimio, hapo tutajua tupo msibani na matanga hayataisha leo wala kesho.
Binafsi, namtakia kila la kheri Chilgati katika safari ya kupeleka chama chake kabulini.


chanzo mwanahalisi

mapinduziiiii daimaaaaaaa
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom