Kikwete umeshindwa EPA, tunakusubiri Richmond | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kikwete umeshindwa EPA, tunakusubiri Richmond

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Aug 31, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Aug 31, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,780
  Likes Received: 83,135
  Trophy Points: 280
  Date::8/30/2008
  Kikwete umeshindwa EPA, tunakusubiri Richmond
  Na Joyce Mmasi
  Mwananchi

  HATIMAYE ile taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya bunge kuhusu zabuni ya umeme wa dharura iliyotolewa kwa kampuni tata ya Richmond Development Limited imetolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

  Kila mtu alitega masikio yake mjini Dodoma ili kusikia jinsi serikali ilivyotekeleza maazimio 23 ya bunge. Kwa ujumla ripoti hiyo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na kila Mtanzania hususani wale waliokuwa wakifuatilia kwa karibu sakata zima la mradi wa umeme wa Richmond.

  Waziri Mkuu alitoa taarifa ndefu akiligusa kila eneo kwa mujibu wa mapendekezo ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata hilo na kuridhiwa na bunge Februari mwaka huu.

  Kwa mujibu ya taarifa hiyo ya Pinda, vigogo wote waliodaiwa kuhusika katika kashfa ile kwa njia moja au nyingine, waliandikiwa barua na kutakiwa kujieleza ndani ya siku 14 na kwamba, wote walifanya hivyo.

  Pinda aliendelea kulieleza bunge kuwa, barua za kujieleza za wahusika hao, zinafanyiwa kazi na mamlaka husika na kwamba iwapo waliotajwa watabainika kuhusika watachuykuliwa hatua za kinidhamu.

  Katika taarifa hiyo ya Pinda, yametolewa maelezo kwa wahusika kila mmoja kwa nafasi yake huku baadhi ya vigogo wakiachwa mikononi mwa ofisi ya rais kwa ajili ya kuamuliwa hatma kwa kuwa watendaji hao wameteuliwa na rais na ndiye mwenye mamlaka ya kuwawajibisha.

  Vigogo ambao hatma yao iko ikulu kwa mujibu wa Pinda ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, (Takukuru) Dk Edward Hosea, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Athur Mwakapugi na Kamishna wa Nishati wa Wizara hiyo, Bashir Mrindoko.

  Pinda alisema vigogo hao wameandikiwa barua na kutakiwa kujieleza kwa misingi ya sheria ya msingi ya kujitetea kabla ya kuhukumiwa na kwamba maelezo yao yamewasilishwa na sasa yanashughulikiwa na Ikulu.

  Kwa uchache, sitanukuu taarifa nzima lakini ni vyema nikagusia maelekezo kwa baadhi ya watuhumiwa kuwa wamepewa maeneo ya kutolea maelezo ya jinsi walivyohusika katika mkataba huo uliolisababishia taifa hasara kubwa.

  Pia walitakiwa kueleza walivyoshindwa kuikagua, kuona udanganyifu wa kisheria na kuishauri serikali kuwa kampuni ya Richmond haikuwa na uwezo kifedha wala utaalam wa kupewa zabuni ya kufua umeme wa dharura megawati 100.

  Halikadhalika wametakiwa kutoa maelezo jinsi zabuni hiyo ilivyotolewa kwa kukiuka taratibu za Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA), kutokuwa makini na kutambua udanganyifu wa kampuni hiyo na jinsi ilivyojitangaza kuwa na ubia na kampuni kubwa zenye uwezo, pamoja na kujinadi kuwa na uhusiano na kampuni ya inayoendesha miradi mikubwa duniani, madai ambayo hayakuwa ya kweli.

  Hosea ametakiwa kujibu taarifa yake kuwa mchakato wa kumpata mzabuni wa Richmond ulikuwa wa wazi na hakukuwa na jinai inayowahusisha viongozi kama ilivyoeleza ripoti ya uchunguzi ya Takukuru, huku Mrindoko akitakiwa ajieleze kwenye eneo la kushindwa kumshauri Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, kuhusu udhaifu wa Richmond ambao aliujua tangia mwaka 2004.

  Kuhusu Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika, Pinda alinukuu mapendekezo ya kamati iliyosema kuwa alionekana kuwa na udhaifu wa kitaalamu na ukosefu wa umakini katika kuiwakilisha serikali na kushindwa kutambua ukosefu wa sifa huku akishindwa kuifanyia ukaguzi Richmond baada ya uteuzi.

  Sina shaka na maamuzi au utaratibu wa kuiachia Ikulu kuwashughulikia vigogo hao kwani huo ndio utaratibu, hoja yangu hapa ni kwamba rais afanye kazi yake dhidi ya watu hawa bila kuwaonea haya.

  Kitendo cha kuamua kuiacha ikulu ni kukubali kuwa watu hao kwa njia moja au nyingine wanahusika na wanapaswa kuchukuliwa hatua iwe za kinidhamu au kisheria, au adhabu nyingine yoyote itakayolingana na uzito wa makosa waliyoifanyia nchi.

  Nisionekane namfundisha Rais Kikwete kazi katika hili, lakini najua kwamba rais wetu anao utaratibu wake katika kufanya kazi zake, lakini jambo hili ni nyeti na linapaswa kushughulikiwa kwa umakini na kwa haraka na ikulu chini ya rais Kikwete ili aweze kutuliza kiu ya Watanzania walioanza kukata tamaa kwa jinsi makosa kama hayo yanavyoshughulikiwa.

  Watanzania wamekuwa wakiliangalia sakata hili kwa mtazamo tofauti, kila aliyetajwa kuhusika alitarajiwa kuchukuliwa hatua kwa ama kujiuzulu mwenyewe au kusimamishwa kazi wakati uchunguzi unaendelea au kufukuzwa kazi na mamlaka husika, achilia mbali kufikishwa mahakamani.

  Tuliona mawaziri kadhaa wakijiuzulu kufuatia kutajwa katika sakata lile. Ingawa uamuzi wa mawaziri hao haukufuta makosa yao, angalau ulipunguza hasira za Watanzania dhidi ya uzembe, wizi na udanganyifu uliokuwepo katika mazingira ya sakata lile.

  Rais Kikwete ameonekana kuwa na huruma katika suala zima la kuwawajibisha vigogo wanaotuhumiwa katika masuala mbalimbali ya kuhujumu uchumi wa nchi, hali hii mbali na kuwaudhi Watanzania pia inawakatisha tamaa wananchi hususani wale walionyesha imani yao kwa Rais Kikwete na Chama chake cha Mapinduzi na hatimaye kumchagua kwa zaidi ya kishindo¬ókwa ushindi mkubwa kuliko kiongozi yeyote katika mfumo wa vyama vingi nchini.

  Imani ya Watanzania kwa Rais Kikwete, bado ipo na inaweza kuendelea zaidi endapo atasimama kidete kuwawajibisha wote wanaoonyesha kukwamisha juhudi zake za kupambana na rushwa na kuinua uchumi wa nchi.

  Rais Kikwete hapaswi kuchoka au kuwaonea haya viongozi wanaokwamisha juhudi zake kwa namna moja ama nyingine, anachopaswa ni kufanya ni kutumia mamlaka aliyonayo kuleta heshima katika uongozi wake kwa kufanya kile kinachosubiriwa na wengi.

  Mtihani mwingine kwa Rais Kikwete ni huu aliopewa au alioachiwa na Kiongozi wa Serikali Bungeni¬óWaziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ameweka bayana kuwa baadhi ya vigogo akiwemo Mwanyika na Hosea wanasubiri maamuzi ya Ikulu.

  Hosea na Mwanyika wanahusika kwa njia moja au nyingine, ingawa wanazo sababu au utetezi wao, lakini haufuti makosa yao wala hauwapi kinga ya kuwajibishwa au kuchukuliwa hatua.

  Rais mbali na kuwa na uwezo na mamlaka katika hili, ndiye anayepaswa kisheria kubeba mzigo huu mzito, na ndio maana kwa kuzingatia uzito wake kamati ikaliacha suala hilo mikononi mwa ikulu ambapo mkuu wake ni Rais Kikwete.

  Pamoja na ukweli kuwa huenda kukawa na ugumu katika kuwachukulia hatua vigogo hao na wengine waliotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine, lakini ni vyema kwa Rais Kikwete akayatumia mamlaka aliyonayo kuwawajibisha kwa uzito ule ule ambao taifa limeingia katika hasara kuhusiana na mkataba ule wenye utata.

  Watanzania waliokupa kura Rais Kikwete wanakusubiri tena katika hili, kwa maneno mengine huu unakuwa kama mtihani mwingine kwako, je utawafumbia macho au utawachukulia hatua mara moja, tunatarajia katika hili utatufuta machozi Watanzania.

  Nakukumbusha Rais, hadi sasa umeshindwa kuonyesha njia ya kudhibiti mafisadi wa EPA sasa tunakusubiri katika Richmond, Mwanyika na Hosea ni mtihani mwingine kwako. Vinginevyo tutaanza kujiuliza, huyu kiongozi asiyefaulu mitihani miepesi kuna haja gani ya kuendelea kumpa mitihani?

  Joyce Mmasi ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi Jumapili, anapatikana kwa baruapepe:: :joycemmasi@yahoo.co.uk

  Simu: 0784253436.
   
 2. Timtim

  Timtim JF-Expert Member

  #2
  Aug 31, 2008
  Joined: Feb 9, 2008
  Messages: 603
  Likes Received: 64
  Trophy Points: 45
  Mhhhhhhhhh!
   
Loading...