Kikwete ua mafisadi acha waandishi.

Sokomoko

JF-Expert Member
Mar 29, 2008
1,915
127
Ansbert NgurumoSISI tunaulizana: “Tuwafanyeje kina Ben Mkapa?” Rais Jakaya Kikwete na wenzake wanaulizana: “Tuwafanyeje kina Ngurumo?”


Katika makala ya Jumapili iliyopita, nilipendekeza sehemu ya majibu kwa swali la kwanza. Nilisema ni vema wananchi wafike mahali wachukue hatua kali, ikiwamo ya ‘kuwanyonga’ viongozi wa umma. Wananchi wana uwezo na ujuzi wa unyongaji huu. Wakiamua hawatashindwa.

Haidhuru watawala wana mabavu kiasi gani, hawawezi kuipiku nguvu ya umma ulioamua. Mifano ipo mingi, lakini kwa sasa, hii ya Kenya na Zimbabwe ni sehemu ya matokeo ya nguvu hiyo.

Mateso, vitisho na dhuluma ndiyo imekuwa silaha kubwa ya Rais Robert Mugabe na wengine wa aina yake dhidi ya wote wanaotofautiana naye kuhusu uongozi wa nchi, ndani na nje ya chama chake. Lakini wananchi wametumia silaha hizo hizo kumkataa.

Viongozi wa aina ya Mugabe, ambao ndio wengi Afrika, wamezigeuza serikali kuwa magenge ya wahuni wa vyama tawala na vikosi vya dhuluma dhidi ya wananchi wasio na hatia, wapinzani wa utawala mbovu na ufisadi.

Haya ya Zimbabwe yametuonyesha kuwa hata masikini wenye njaa wana uwezo. Ole wake atakayedharau hukumu yao. Kufuru ya shibe na utajiri wa kifisadi wa watawala, watoto wao, ndugu zao na wapambe wao ndilo bomu la atomiki linalowalipukia baadhi ya watawala mafisadi wastaafu na walio madarakani.

Si Zimbabwe ya Mugabe tu, bali hata Tanzania ya Kikwete. Watawala wamejitengenezea vitanzi, wakajivika kinga ya kisheria wasishitakiwe; lakini wakati umefika wananchi watumie vitanzi hivyo hivyo kuwanyonga wakiwa na kinga zao vitabuni au zikiwa zimeondolewa kwa nguvu.

Siku Rais Kikwete alipowaambia Watanzania kwamba “tumuache Mzee Mkapa apumzike” hakujua naye alikuwa ameanza kusuka kitanzi chake mwenyewe.

Ningefurahi kumsikia Kikwete akirudia maneno hayo leo, huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akitoa kauli ya ‘serikali kumchunguza’ Mkapa.

Ningependa kuamini kwamba Pinda hafanyi mzaha katika kauli hiyo, maana tutaichunguza. Kama ameitoa ili kunyamazisha wanaohoji uadilifu wa rais mstaafu; kama ametamka ili kuridhisha masikio ya Watanzania, ajiandae naye kuingizwa kwenye orodha ya ‘wanyongwaji.’

Lakini serikali hiyo hiyo anayoizungumzia Pinda, haijatoa tamko kuhusu ajira ya mtoto wa Mkapa katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambayo tunaambiwa ndiyo inafuatilia suala la Mkapa na miradi yake yenye utata.

Juu ya hayo, napata shida kuelewa ujasiri wa mshirika wa Mkapa, Daniel Yona kwamba “kama kuna mwenye ubavu aende mahakamani.” Hii ina maana hata serikali haina ubavu? Au kwa kuwa Yona ni mwanasiasa mwandamizi anajua fika kwamba si tu suala la ubavu, bali serikali haina hata nia?

Pinda na Kikwete wajue jambo moja. Wananchi wana hasira. Hasira hizi ndizo pole pole zinaanza kugeuka chuki dhidi ya watawala wao. Kisa? Ufisadi na ubabe wao!

Leo ni Mugabe na Mkapa, kesho Kikwete na wenzake. Viwango vyao vyaweza kuwa tofauti, lakini hatima yao ni moja. Watune, wanune, wacheke; umefika wakati wananchi wanataka kuona na kufaidi matunda ya uhuru wa taifa lao.

Kile kizazi cha ‘wapigania uhuru’ kinadhalilisha jitihada na nguvu zilizotumika kuleta uhuru huo katika Bara la Afrika. Badala ya uhuru, wenzetu wameleta uhuni. Ukoloni uko pale pale, utumwa wa mwananchi mnyonge unaendelea.

Watawala wanaishi katika anasa bila kutoa jasho, wananchi wanatoa jasho la damu, lakini wanaandamwa na ufukara wa kupindukia kwa sababu wamenyimwa au wamenyang’anywa fursa na nyenzo.

Wakati wa kampeni, tuliahidiwa mengi. Rais Kikwete ajue kwamba tunakumbuka ahadi zake: “Maisha bora kwa kila Mtanzania” na “Tanzania yenye neema inawezekana.”

Mfumuko wa bei unamshitaki. Maisha magumu na duni ya wananchi yanamsuta. Mwishoni mwa mwaka wa bajeti ya mwaka 2007/08 wananchi hawajaona ule uzuri wa bajeti iliyowafanya mawaziri wote kuzurura nchi nzima na kuponda posho nono.

Tuna haki ya kusema kumbe mwenzetu alimaanisha “maisha bora kwa kila fisadi.” Kama sisi Watanzania hatujayaona maisha hayo, yanatuhusu vipi?

Neema tunazoziona katika miradi ya wakubwa na watoto wa vigogo, ni bomu jingine litakalowalipukia watawala muda si mrefu kuanzia sasa.

Juzi juzi tumejadili sana matatizo na suluhu ya siasa za Kenya, hasa machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi kuvurugwa na waliokuwa madarakani. Baadhi ya watawala wetu (vipofu) wakawabeza Wakenya kwa ukabila, huku wakidai hayo hayawezi kutokea Tanzania.

Hawakutaka kuona kwamba matatizo ya Kenya yameibukia kwenye ukabila, lakini yamejikita katika uchumi; kwamba uchumi wao umejengwa katika misingi ya kutukuza kabila fulani na kulipatia kila fursa za kisiasa na kiuchumi tangu miaka ya mwanzo ya 60, huku mamilioni ya wananchi yakiishi kama tabaka la daraja la pili kwenye nchi yao.

Tanzania bado tuna bahati ya urithi tulioachiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Alitujenga katika amani, mshikamano na umoja; na alijitahidi kuweka misingi ya kuondoa matabaka, hasa ya kipato.

Bahati hiyo imefutwa pole pole na tawala zilizofuata baada ya Mwalimu Nyerere. Zimebaki kufanya ukasuku wa ‘amani, mshikamano’ lakini hazina dira ya kujenga tunu hizo. Pole pole, tumeshuhudia matabaka yakijengeka, na sasa yapo mawili: mafisadi na wananchi.

Ufisadi unapokuwa sehemu ya mfumo unaoongoza nchi, kauli za wakubwa za serikali kushughulikia ufisadi zinakosa maana kabisa.

Tumeshuhudia zaidi ya mara moja. Kwa mfano, serikali imebanwa na wapinzani, ikaita wataalamu kuchunguza uozo wa Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) Benki Kuu; ripoti ya kitaalamu ikatolewa.

Serikali imeficha ripoti hiyo hadi leo, na imeunda tume yake ‘kusafisha’ upepo wa kisiasa!

Hii inatoa picha kwamba serikali imefuga mafisadi. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinalea mafisadi; baadhi yao wakiwa ni viongozi wa chama.

Sasa imefika mahali hata baadhi ya watu wema ndani ya CCM na serikali wanaona njia ya kujinasua ni kujenga heshima zao binafsi, maana mfumo umeshaoza.

Mafisadi wanapofika mahali wakashika madaraka makubwa ya dola, hatuwezi kusema tuna taifa lenye nafuu kuliko la hao wanaochinjana kwa ukabila. Ni suala la muda tu, nasi utafika wakati tabaka la ‘wachovu’ litaamka na kusema liwalo na liwe, afaye na afe; tunataka haki zetu.

Tabaka la mafisadi, wanyonyaji limetapakaa nchi nzima. Kutokana na sababu za kihistoria zilizoisuka CCM katika nchi nzima, kama kunaibuka machafuko ya wananchi dhidi ya CCM, yatatapakaa nchi nzima na yatakuwa mabaya kuliko ‘mchezo wa kitoto’ wa Wakenya.

Katika vurugu, busara huwekwa pembeni. Wale vijana waliomfia Raila Odinga, hawakuwa wanampenda kiasi hicho. Wala hawakuwa wanamchukia Rais Mwai Kibaki kwa kiwango hicho.

Waliifia nchi yao. Walikuwa wanapambana na ufisadi na wote waliojitokeza kuutetea, waliokuwa upande wa Kibaki, ambao kwa bahati mbaya wengi ni watu wa kabila lake. Chuki na hasira za kiuchumi zikaelekezwa kwenye kabila! Bahati mbaya sana!

Kama haya yatatokea Tanzania, tabaka litakaloshambuliwa ni la kina Mkapa na Kikwete, wafuasi wao na mashabiki wao. Hapa haitaangaliwa itikadi, bali ‘nani anakula nao.’ CCM watajikuta upande mmoja na wananchi upande mwingine.

Tusidhani Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM), Mbunge wa Karatu, Dk. Willibroad Slaa (CHADEMA) na wengine waliochachamalia suala la ufisadi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa na wenzake wana ugomvi na chuki binafsi.

Dhamiri zinawasukuma, na wananchi wanasikia. Wanachukia na wanakaribia kupasuka. Wanaona wamechezewa akili na kudhalilishwa na viongozi wale wale ambao walisifika na kuheshimika na hata kudhaniwa kuwa ni safi, waamini wa dhana ya ukweli na uwazi – kumbe kwa miaka zaidi ya 10 tumeishi gizani.

Inawawia vigumu wananchi wa kawaida kukubali kwamba rais anaweza kula njama dhidi yao, akashirikiana na wapambe wake kuhujumu wananchi wale wale anaowahutubia kila mwisho wa mwezi na kuwasihi wafunge mikanda.

Kila rais anapotembelea mikoani, wananchi wanamzunguka na kutaka kumuona kwa karibu kumgusa na kupiga naye picha. Yeye anatabasamu akidhani wanampenda. Hapana!

Wanaandaa kumbukumbu muhimu za kuwasaidia kutoa hukumu dhidi yake hapo baadaye. Wanapomtazama, wanamuona mwenzao amenawiri, wao wamechakaa. Analindwa na kulishwa kama mtoto mdogo; wao wanazikana kila siku kwa magonjwa yanayosababishwa na njaa, lishe mbovu na usalama duni.

Wao wamechakaa mikono kwa kazi nzito, hata wanapompa mkono ‘wanamkwangua’ rais kwa sugu za mikono yao. Yeye ‘hawezi’ kufungua hata mlango wa gari lake. Kuna mtu analipwa manono kwa kazi hiyo!

Akisimama kuhutubia anawapa matumaini hewa, anawaahidi kushughulikia mafisadi kwa sheria zilizopo (zinazolinda mafisadi hao hao), na kuwaomba wavumilie makali ya uchumi kwa kuwa serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania yanapatikana.

Halafu kesho yake watu hao hao ndio wanagundua kwamba rais wao huyo huyo ndiye mfugaji wa mafisadi; kiasi kwamba kama si kwa kinga anayowawekea, hata sheria zilizopo zinazowalinda zingekwishafutwa au kubadilishwa ili washughulikiwe. Watamuelewa?

Inagundulika kwamba yeye au ndugu zake wanajitajirisha kwa mabilioni kila siku, ambayo yangepasa kuingia kwenye uchumi wa nchi na kusaidia maskini. Watamwelewa?

Wanagundua kwamba wakati wanasulubiwa na uongozi wa vijiji vyao kuchangia ujenzi wa shule zisizo na vitabu, maabara wala walimu – shule za kata – watawala wao wanaficha nje ya nchi kiasi ambacho kingetosha kujenga shule hizo na kulipa walimu mishahara inayostahili. Watamwelewa?

Katikati ya shida zote hizo, ndipo wanapoanza kuulizana. Tumfanyeje Mkapa? Tumfanyeje Kikwete? Bora sisi wengine tunaandika hapa watawala wanasoma. Wapo wananchi wasioandika wala kusema. Hao ndio watakaolipuka kama bomu la nyuklia.

Katika mazingira ambayo watawala wanabomoa misingi badala ya kuiimarisha; katika mazingira ambayo tumegundua watawala wenyewe ndio mafisadi; hakuna kitakachowazuia wananchi hawa kuamua kuondoa dhiki zao kwa ‘kuwanyonga’ watawala hawa.

Watawala wameshaona dalili zote hizi. Wasaidizi wao wanaziona pia, na wanajipanga. Hata hivyo, tofauti na matarjio yetu, hawajipangi kujenga nchi, kutubu na kuacha ufisadi.

Wanajipanga kuwadhuru wale wanaohoji ufisadi wao. Nao wanaulizana: “tuwafanyeje hawa?” wanatafuta cha kutufanya sisi tunaowahoji, tunaowakosoa, tunaowakumbusha wajibu wao.

Hizi ni dalili mbaya sana, na ushahidi upo sasa kwamba baadhi ya wasaidizi wa Rais Kikwete wameshaanza kumfundisha uhuni huu.

Akiwasikiliza na kutekeleza ushauri wao, ajue anachimba kaburi lake. Na siku anafukiwa kwenye kaburi hilo, wao watakuwa nje wakimcheka; kwani Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alishatuambia, na hatujasahau.

Alisema: “Mtu mwenye akili akikupa wazo la kipumbavu, huku akijua ni la kipumbavu, na wewe ukalikubali, atakudharau.”

Sasa zipo taarifa kwamba hawa ‘wenye akili’ wanamshauri Rais Kikwete aanze kuwashughulikia wanahabari ili wasizidi kutoa habari za ufisadi wa serikali yake. Wengine wanasema hata ikibidi baadhi ya waandishi ‘wapotee’ ilimradi vigogo wapone!

Wasiwasi wangu ni kwamba, inawezekana rais ameanza kuwakubalia; vinginevyo, alipaswa kuwafukuza kazi siku hiyo hiyo. Alipaswa awaambie kwamba huu ni mkakati wa kijinga, hasa katika kipindi ambacho hata waliomwagiwa tindikali majuzi hawajapona.

Yeye na wao wajue kuwa serikali adilifu haiwezi kuhusishwa na ufisadi. Wajue kuwa waandishi hawatungi habari wanazoandika, bali wanaibua kile kilichofichwa na watawala.

Zaidi ya hayo, ni vema wajue kuwa hata hicho kilichoandikwa hadi sasa ni kama tone la maji kwenye Bahari ya Hindi. Uchafu wenyewe bado haujafukuliwa.

Tunajua wakubwa wamelemewa. Kila wanachoshika kinamong’onyoka. Lakini suluhisho si kuwatafuta ubaya waandishi. Bila wao taifa hili lingekuwa kuzimu. Achana nao, pambana na mafisadi.

+447847922762
ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com
 
Katikati ya shida zote hizo, ndipo wanapoanza kuulizana. Tumfanyeje Mkapa? Tumfanyeje Kikwete? Bora sisi wengine tunaandika hapa watawala wanasoma. Wapo wananchi wasioandika wala kusema. Hao ndio watakaolipuka kama bomu la nyuklia

+447847922762
ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com

Mkuu Ngurumo anachosema ni kweli maana bora sie JF na wao kina Ngurumo wanaandika na watawala wanasoma na wengine ma member humu JF lakini hawajui wananchi walio nyamaza wanawaza nini kwenye vichwa vyao. Nasema hili ni bomu huwezi hata kulifananisha na atomiki na wataoumia watakuwa ni watu wa hali ya chini wakubwa na family zao watakimbilia ulaya! Tukaeni chonjo mida mibaya hii.
 
Waache wachochee kuni zao!
aliye juu ndio ataanguka.....tena kwa kisihindo! sisi tutawasubiri chini tuwagombanie tu!
 
Unafahamu chanzo cha kuondolewa Bokasa madarakani? Wanafunzi wa shule ambao walilazimishwa kuvaa nguo (uniform) kutoka kwa kampuni ya mke wake.

Je, unafahamu kasheshe ya Mugabe ilianzia wapi? Wauza mboga za majani kwenye suburb ya *Mabvuku au *Tafara within Harare walipogomea bei ya unga wa mahindi na yeye kupeleka tanks na paratroopers kwenda kuwanyamazisha.

Je, unafahamu sokomoko la JK lilipoanzia ………………………………….


*Sina uhakika wa majina hayo lakini Tanks zilionyeshwa CNN about 1995.
 
Unafahamu chanzo cha kuondolewa Bokasa madarakani? Wanafunzi wa shule ambao walilazimishwa kuvaa nguo (uniform) kutoka kwa kampuni ya mke wake.

Je, unafahamu kasheshe ya Mugabe ilianzia wapi? Wauza mboga za majani kwenye suburb ya *Mabvuku au *Tafara within Harare walipogomea bei ya unga wa mahindi na yeye kupeleka tanks na paratroopers kwenda kuwanyamazisha.

Je, unafahamu sokomoko la JK lilipoanzia ………………………………….


*Sina uhakika wa majina hayo lakini Tanks zilionyeshwa CNN about 1995.

90s alivyokuwa waziri wa nishati iptl....ufisadi alianza zamani huyu
 

Wao wamechakaa mikono kwa kazi nzito, hata wanapompa mkono ‘wanamkwangua' rais kwa sugu za mikono yao. Yeye ‘hawezi' kufungua hata mlango wa gari lake. Kuna mtu analipwa manono kwa kazi hiyo!

Akisimama kuhutubia anawapa matumaini hewa, anawaahidi kushughulikia mafisadi kwa sheria zilizopo (zinazolinda mafisadi hao hao), na kuwaomba wavumilie makali ya uchumi kwa kuwa serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania yanapatikana.

Halafu kesho yake watu hao hao ndio wanagundua kwamba rais wao huyo huyo ndiye mfugaji wa mafisadi; kiasi kwamba kama si kwa kinga anayowawekea, hata sheria zilizopo zinazowalinda zingekwishafutwa au kubadilishwa ili washughulikiwe. Watamuelewa?

Inagundulika kwamba yeye au ndugu zake wanajitajirisha kwa mabilioni kila siku, ambayo yangepasa kuingia kwenye uchumi wa nchi na kusaidia maskini. Watamwelewa?

+447847922762
ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com

Kaka Ugurumo umelonga haswa, huu ndiyo uchungu wangu. Unanikumbusha makala za Samsom mwigamba za 'Tanzania zipo mbili?' Watanzania wengi wanaishi maisha ya umasikini uliopindukia licha ya rasilimali nyingi ambazo Baba wa Mbinguni (Mungu) ametupatia, inatia uchungu sana. Hivi ni lini Serikali itaamua kupambambana na mafisadi?
 
Kaka Ugurumo umelonga haswa, huu ndiyo uchungu wangu. Unanikumbusha makala za Samsom mwigamba za 'Tanzania zipo mbili?' Watanzania wengi wanaishi maisha ya umasikini uliopindukia licha ya rasilimali nyingi ambazo Baba wa Mbinguni (Mungu) ametupatia, inatia uchungu sana. Hivi ni lini Serikali itaamua kupambambana na mafisadi?

Ansert Ngurumo Mafisadi wanakutamani uwe asusa yao kaa chonjo. Na usirudi nyuma tupo pamoja nanyi liwalo na liwe tumechoka.
 
Back
Top Bottom