Kamanda
Senior Member
- Dec 5, 2007
- 150
- 176
Shikamoo,
LEO nimeamua kuandika waraka huu kwako Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka inayokaribia mitatu sasa tangu ushinde na kuapishwa mwaka 2005 baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu.
Napenda kutumia fursa hii kukupa pole kwa kazi ngumu ya kuongoza kundi la watu wengi wenye njaa ya tumbo, njaa ya ubongo na njaa ya tiba bora.
Hakika njaa zinazowakabili Watanzania ni nyingi na hazina ukomo, hasa zikiainishwa kwa nafasi binafsi, kaya, kata, kijiji, miji, majiji na taifa kwa ujumla wake.
Ni mnafiki pekee anayeweza kukudanganya, au wewe mwenyewe kudanganyika (ingawa hili najua siyo rahisi kwako kwa kuwa umeyaishi maisha ya wengi wetu), kwamba mambo ni shwari kila mahala. Kwamba HAKUNA MATATA.
Nakumbuka vyema, na bahati nzuri bado ninaendelea kuirejea hotuba yako ya mara ya kwanza Bungeni Dodoma ambayo ilisheheni ahadi na namna nzuri ya kumpunguzia Mtanzania ufukara (unaojumuisha njaa zote alizonazo).
Kila Mtanzania aliyekusikia siku ile ukiwa umetulia na kuisoma vyema, atakubaliana nami kwamba hotuba ile ndiyo ilikuwa dira yenye mwanga wenye miali ya kuchoma na kuunguza kero nyingi za watu wako waliokuchagua, hata wale wasiokipenda chama chako CCM, kwa kura za kishindo.
Ni hotuba ile iliyohuisha hatma ya maisha yao iliyokuwa imefikia mahali pa kuonyesha kukata tamaa, hata kama waliokutangulia walikuwa wakitamba kwa hadithi za kukua na kuimarika kwa uchumi mkuu, ilhali maisha ya watu yakiendelea kudhoofika.
Kadri miaka ilivyokuwa ikisonga, hasa ule mwaka wa kwanza, matumaini ya watu wako yaliendelea kukupa muda kwamba neema ya kweli yaja. Hakuna aliyeonekana kuwa na haraka ya hiyo neema iliyoonekana katika hotuba yako na hata dhamira yako iliyojionyesha kuchukizwa na umaskini wao.
Hata hivyo, ikiwa miaka mitatu inakaribia kukatika, asilimia kubwa ya matumaini waliyokuwa nayo watu wako wengi, kwamba wewe ndiye mkombozi aliyepo, inapungua kwa kasi ya kutisha, hata kama wasaidizi wako, hasa wale wanafiki na wanaojipendekeza watakueleza vinginevyo.
Uhakika ni kwamba hata wewe unalitambua hilo kupitia kwa watu wako wengine wa karibu, wale wanaoitwa mawaziri wa jikoni wa rais-hasa wanafamilia uliowapa jukumu la kukusanya maneno ya watu wako huku kwetu mitaani.
Kasi ya kupungua kwa asilimia kubwa ya matumaini ya watu wako yanajiegemeza katika matukio mabaya yaliyoikumba nchi yetu, yakiwa yanafanywa ama na wasaidizi wako, uliowachagua kwa imani kubwa, au wafanyabiashara wenye kuhusiana nao.
Hilo halina kificho na wala hakuna haja ya kukueleza vinginevyo, kwani hata wao wenyewe walitambua na sina uhakika kama walijutia kuhusika kwao na dhambi za kuongeza ufukara kwa Watanzania, lakini angalau waliamua kuachia ngazi kwenye madaraka uliyowapa na wengine kuikimbia nchi, wakijificha huko walikotanguliza vijisenti walivyowaibia watu wako.
Ufisadi. Ufisadi. Ufisadi. Hii ni dhambi ambayo imekuwa ikilaaniwa na wapenda nchi yao, ikiwa inabeba na dhambi nyingine nyingi, ambazo zimekuwa, siyo kero tu, bali mzigo mzito wa gharama za maisha kwa watu wako.
Ni ufisadi huo ambao umeongeza bei ya umeme, bei ya vyakula, ada kwa watoto wetu, nauli kupanda na hakika umegusa kila sehemu ya maisha ya wananchi wa Tanzania, kiasi kwamba serikali nzima unayoiongoza ikaonekana inachusha kwa kila mtu, isipokuwa mafisadi wenyewe, wake zao, watoto wao na hata vimada wao.
Sasa leo wakati utakapokuwa ukilihutubia Bunge, mjini Dodoma, watu wako wenye kukata tamaa, wanataka uongee. Wanataka uzungumzie masuala yanayowakera kila uchao kwa sasa. Hawataki siasa ambazo tumezizoea zinazotolewa na viongozi wetu wanasiasa.
Wananchi wanataka kusikia namna unavyochukia ufisadi kwa dhati ya moyo wako. Wanataka kukusikia na kukuona ukikunja ndita kuwalaani na kutoa amri kuu ya kuwachukulia hatua kali mafisadi wote wanaofifisha juhudi binafsi ulizoanza kuzionyesha mwanzo wa uongozi wako.
Binafsi, msema kweli mpenzi wa Mungu, nikushangae kidogo kwa kushindwa hadi sasa kuwakemea wakuu wafuatao; Mwanasheria Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kwa kushindwa hadi sasa kuwakamata watu walioandikwa katika ripoti uliyokabidhiwa majuzi juu ya uchunguzi wa Akaunti ya Malipo ya Madeni ya je (EPA).
Kwamba kwanini hadi sasa hawajawaadabisha mafisadi wake wakati timu yao imekamilisha kazi? Nnachojua mimi ni kwamba wao kwa kazi zao wangekuwa wamewakamata watu hao kwanza na ndipo baadaye wakupe ripoti hiyo.
Polisi wanatakiwa kuwakamata wahalifu hao, baada ya Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa Takukuru kuthibitisha kuwa walihusika na wizi huo, sasa wanasubiri nini au mpaka uwaeleze wawakamate watu hao? Wao wanafanya kazi gani, yaani kukupa ripoti basi? Wanasubiri nini? Au nao tuseme wako pamoja nao kama tulivyoshuhudia baadhi yao wakitetea wizi ambao bado unasumbua kupatikana kwa neema ya Tanzania?
Kama hawajawakamata tuseme hawajawatambua hadi sasa. Ikiwa ripoti hiyo imejaa maneno matupu kama ya ukasuku wa wanasisa, tafadhali achana nayo kabisa na usiisome kwani itakuondolea zaidi asilimia za imani kwa wananchi wako.
Idadi kubwa huku mitaani tunakopita na kuzungumza na wapiga kura wako, wengi wanaonekana kushangaa timu hiyo uliyoiunda, kwamba inasubiri nini.
Mbali na hilo, wananchi wanatarajia kuwa utazungumzia na kutoa msimamo juu ya mgogoro wa Muungano, hatma ya maslahi kwa wafanyakazi na zaidi sana suala zima la neema kwa kila Mtanzania.
Rais Kikwete, vitabu vitakatifu, ambavyo naamini unavithamini na ndiyo mwongozo wako, kabla ya Katiba, vinasema kuwa ukiona maovu yanatendeka, basi yazuie hata kwa upanga ili yasiendelee, ukishindwa yakemee hata kwa ulimi na ukishindwa kabisa, basi onyesha kuchukizwa na kuchukua hatua, hata kwa kupitia wengine.
Hatua za namna hii, zimetumiwa zaidi na Rais wa Rwanda Paul Kagame na hatimaye sasa nchi hiyo iliyokuwa imegubikwa na vita, inapanda kwa kasi katika chati yake ya kuwaletea neema wananchi wake.
Utakapofaya hivyo, hakika utakuwa umemtendea haki Mungu Mkuu na waja wake Watanzania na thawabu zitarundikana katika fungu lako.
Nakutakia kila jema uwapo Dodoma na unapojiandaa kwa safari yako ya Marekani.
Wasalaam
Simon Martha Mkina
Simu: 0754 020880
Email: smkina@gmail.com
Blog:www.mkina.bloghspot.com
(Waraka huu umechapishwa katika gazeti la Kulikoni la leo) Tumeiweka hapa kwa hisani ya gazeti.