Kikwete: Siioni kasi ya kumaliza tatizo la umeme

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,449
33,354
jk muundo.jpg
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amewataka watendaji wa Serikali yake kufanya uamuzi wa haraka kukabiliana na tatizo la umeme nchini akisema haoni kama kuna kasi ya uhakika katika kukabiliana na suala hilo.

Akizungumza katika kikao na watendaji hao alichokiitisha Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete aliwataka watendaji hao kufanya uamuzi bila ya kuwa na kigugumizi kwa manufaa ya wananchi wakitambua kuwa nchi iko katika hali ya dharura kubwa ya upatikanaji wa nishati hiyo.

"Tuko katika hali ya dharura. Sioni hisia za haraka za kuchukua uamuzi na hatua nyingine muhimu za kukabiliana na dharura ya upatikanaji wa umeme. Hatuwezi kuendeleza kuwa na kigugumizi katika kuchukua uamuzi wa kuitoa nchi katika changamoto kubwa hizi za upatikanaji wa nishati," alisema Rais Kikwete na kuongeza:

"Ubwana mkubwa wa kila mmoja wetu utatambuliwa kutokana na mafanikio ambayo kila mmoja wetu ataonyesha katika kukabiliana na hali hii ya upatikanaji wa nishati."

Rais Kikwete pia amewataka watendaji hao kuelekeza nguvu zao kwa kufanya kazi kwa karibu zaidi na wawekezaji ambao wamethibitisha umakini wao katika uzalishaji umeme.
Alisema hilo ni muhimu kwa kuwa inawezekana Serikali isiwe na uwezo wa kutosha wa kuwekeza fedha za kutosha katika uzalishaji umeme miaka mitano ijayo ili kwenda sambamba na mahitaji makubwa yanayoongezeka nchini.

Kikao hicho cha kazi kilihudhuriwa na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa Sheria na Katiba Celina Kombani, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na maofisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

Kilihudhuriwa pia na maofisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tume ya Mipango, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Kikao hicho pia kilijadili ujenzi wa bomba kubwa zaidi la kusafirisha gesi asilia kutoka Mikoa ya Mtwara na Lindi kwenda Dar es Salaam.

Bomba hilo linakusudiwa kujengwa na Serikali ili kuongeza kasi ya upatikanaji gesi kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme na matumizi ya viwandani katika sehemu mbalimbali za nchi badala ya bomba la sasa ambalo ni dogo. Shabaha na mipango ya Serikali ni kuhakikisha kuwa ujenzi wa bomba hilo unakamilika mwakani.

Tangu Novemba mwaka uliopita taifa limekuwa katika mgawo wa umeme kutokana na ukame ulioathiri kina cha maji katika mabwawa yote ya kuzalisha umeme nchini.chanzo:Gazeti la Mwananchi

Ni Jambo la aibu Nchi kubwa kama hii ya Tanzania kutokuwa na Umeme. Mpaka Rais wa Nchi anaingilia kati Masuala ya Umeme? Yuko wapi Waziri Muhusika na WaKurugenzi wa idara ya Umeme wahuisika wa Masuala ya Umeme? Nchi yetu kweli imeoza jamani hata Tatizo la umeme tunashindwa kulitatua?

Wanatushinda Majirani zetu kweli ni aibu kubwa sana.Tunaishi Mijini kiza utafikiri tupo ndani ya Makaburi? ahhh kweli Tunahitaji mabadiliko ya uongozi kwenye Serikali yetu kuna uzembe wa viongozi wahusika ndani ya Serikali kuu.Ni Aibu sana Wakuu wenzangu.
 
Back
Top Bottom