Kikwete ni mwanasiasa, aliwaelewa chadema

mafinga kwetu

Member
Nov 21, 2010
35
3
Kikwete ni mwanasiasa, aliwaelewa chadema



kikwete.jpg
Katika makala zangu nimekuwa nikiwataka watu wafahamu kuwa siasa ndiyo nchi. Kwa bahati mbaya tafsiri hii imekuwa haipati kuanikwa sana lakini ukweli ndiyo huo. Huwezi kujenga nchi bora yenye maendeleo ikiwa siasa zinazoongoza hazina uelekeo unaotakiwa.

Utulivu, amani na mshikamano katika nchi inatokana na siasa zilizopo. Kwa mantiki hiyo wanasiasa ndiyo huamua mustakabali wa wananchi kuanzia katika uchumi, ustawi wa kijamii, maendeleo ya taifa na mtu mmoja mmoja.

Ukiona mafanikio ya Marekani, jawabu likuongoze kufahamu kuwa imefika ilipo sasa kwa sababu ya siasa zake. Ingekosa muongozo madhubuti, pengine ingekuwa maskini kuliko Tanzania.

Wanasema “Ukiona vyaelea vimeundwa”, kwa hiyo siasa bora za Marekani ziliwezesha kuunda taifa lenye mafanikio. Msemo huo una mantiki katika kila nchi inayostahili pongezi.

Nchi yetu Tanzania inaitwa Kisiwa cha Amani, lakini isingestawi kama siasa safi zisingekuwepo.

Amani inapoanza kutoweka, maana yake kuna mfumo unakosewa au ile misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa inakiukwa.
Rwanda, Burundi, DRC, Sierra Leone na nyinginezo, misingi mibaya iliyowekwa na wanasiasa wake, ndiyo kichocheo cha damu kumwagika.

Hapa kuna mkazo kuwa wanasiasa ‘koko’ ni watu hatari. Tunahitaji wanasiasa wenye akili, watulivu na wema.

Hoja inayosumbua vichwa vya watu wengi ni kuhusu wabunge wa Chadema kumsusa Rais , Jakaya Kikwete. Wakati Mkuu wa Nchi anaanza kuzungumza, wao haooo wakatimka.

Yanazungumzwa mengi lakini nami nina kitu nataka kusema. Lakini hapo hapo nataka nielekeze kwamba katika ‘ishu’ hiyo, tayari wanasiasa ‘koko’ wameanza kujitokeza. Wanakwenda mbali badala ya kutafsiri sheria au kanuni za bunge.

Chadema walifanya uamuzi wao kisiasa, vizuri ni kuwa Rais Kikwete aliwaelewa ndiyo maana badala ya kuzungumza kwa jazba, alidondosha kijembe mwishoni, “hata hao walioondoka, watakwenda watarudi mimi ndiye rais wao!”
Utaona kuwa hata JK naye alijibu kisiasa.

Wanasiasa walikutana lakini kuna wengine wanachukia kuliko hata mtendwa mwenyewe. Tunahitaji utulivu wa nchi yetu, jazba za kisiasa zinaweza kutugharimu.

Kuna baadhi ya watu walisubiri maneno makali kutoka kwa JK, akiwabeza wapinzani hasa Chadema. Walitamani kusikia akitoa amri ya kwamba washughulikiwe. Rais Kikwete ana uelewa mkubwa sana.

Bunge ni mhimili huru, hauhitaji kuingiliwa.

Kilichofanywa na Chadema hakijavunja kanuni yoyote, hakijavunja sheria wala kanuni za bunge.

Walitaka kufikisha ujumbe na hilo walifanikiwa.

Hawa wanaoshinikiza adhabu ndiyo wanataka kuvuruga amani.
Wabunge wa Chadema hawakuandama mitaani. Hawajalazimisha JK aachie nchi.

Wanamkubali Kikwete ni Amiri Jeshi Mkuu, ila wanachokikataa kwa sasa ni kile kilichotangazwa na NEC. Wanataka tume huru, katiba ibadilishwe.

Katika hoja ya Chadema, naunga mkono uwepo wa tume huru ya uchaguzi. Wakati huo huo sitaki kipengele cha kupinga matokeo ya urais mahakamani kipewe nguvu. Nalitazama hili, naona hatari kubwa mbele ya safari.

Chadema ni chama cha upinzani, kilikuwa na ilani yake kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010. Hilo peke yake linaweza kukifanya kisiwe na imani na Rais Kikwete. Wanaruhusiwa kutomuamini na kutomkubali ila ni kosa kumpinga kwa vitendo.

Kuna wabunge waliopo mjengoni leo hawajui kama bunge la mwaka 1995 liliwahi kuibua mjadala mkubwa. Wabunge wa NCCR-Mageuzi wakati huo, Mabere Nyaucho Marando na Masumbuko Lamwai walipinga kiapo cha kumtii rais.

Mwishowe walionekana wana hoja nzito. Bunge la Vyama Vingi vya Siasa, utii kwa rais aliye madarakani wa nini? Spika wakati huo Pius Msekwa akatengua kiapo hicho badala ya utii kwa rais ikasomeka: “Utiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Rais Kikwete apewe sifa kwa busara zake. Alitangaza kwamba atashirikiana na vyama vyote katika kuleta maendeleo ya nchi. Tukumbuke kwamba Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliwahi kutamka wazi kwamba hataki ushirikiano na wapinzani.

Angalau walichofanya Chadema kuondoka bungeni mbele ya JK, CUF upinzani wao ulisababisha maafa mwaka 2001 (Mungu azilaze mahali pema roho za marehemu). Hata hivyo, Chadema hawatakiwi kwenda zaidi ya hapo. Amani ikitetereka, gharama ya kuirejesha ni kubwa mno.

Nawashangaa CUF kuwabeza Chadema leo, nawashangaa wabunge wa CCM kuzomea badala ya kutafakari.

Walimsusa rais kisiasa, kwa hiyo wakabiliwe kisiasa, mabavu yakitumika ni tatizo. JK ameonesha njia kwa sababu anajua siasa, lakini itapendeza zaidi kuketi meza moja.

Tags: uwazi11
 
Back
Top Bottom