Kikwete, hili ni lako, usiwaachie wenzako

Quinty

JF-Expert Member
Mar 25, 2010
462
74
Kikwete, hili ni lako, usiwaachie wadogo zako


Jenerali Ulimwengu
Aprili 20, 2011

BAADA ya kukaa wiki kadhaa bila kuonekana katika safu hii, wiki hii narejea ulingoni kuendeleza mjadala ule ule tuliokuwa nao kabla sijachukua likizo fupi, nao ni mjadala unaohusu uandikaji wa Katiba mpya, mjadala ambao umeshika kasi na kuwagusa wananchi lukuki wenye ari ya kuchangia katika maendeleo ya Taifa lao.

Ni jambo jema kwamba ari ya kiwango hiki imejitokeza kwa sababu hiyo ni dalili ya ukomavu wa kisiasa miongoni mwa wananchi. Ina maana wanayajali masuala yanayohusu mustakabali wa nchi yao na wanafuatilia kwa karibu.

Inaashiria pia kwamba wananahci walio wengi wanaachana na utamaduni wa kuwasabilia watu wachache ili wawaamulie kuhusu maslahi yao. Utashi wa kushiriki katika mjadala huu ni mkubwa mno, na unatia moyo.

Kwa muda niliokuwa nimesimama kuandika katika safu hii, mambo kadhaa yametokea, baadhi yakiwa ni ya kukatisha tamaa huku mengine yakiwa ni ya kurejesha imani.

Jambo mojawapo lililoelekea kukatisha tamaa ni ile lililohusu muswada uliopelekwa Bungeni minajili ya kuandika sheria ambayo ndiyo ingeelekeza mchakato wa kuandika Katiba mpya. Ingawaje muswada huo umeondolewa mbele ya Bunge kwa sasa ili ujadiliwe zaidi na wananchi, bado ni muhimu kusema mawili au matatu kuhusu muswada wenyewe na jinsi ulivyokuwa umeletwa, lengo langu likiwa ni kutoa hadhari huko tuendako.

Mara tu muswada ule ulipochapishwa, wadau wa kila aina nchini walitamka kwamba haufai, na walifanya hivyo kwa njia ambayo ingemfanya mtu asiyejua kudhani kwamba walikuwa wameshauriana na kuratibu misimamo yao ili ishabihiane, kumbe si kweli. Kilichowafanya waukatae muswada ule kwa sauti moja ni kile kilichoonekana kama kutokuwa makini kwa Serikali katika kuandaa muswada ule.

Baadhi ya walioukosoa muswada ule ni wale waliodhani kwamba Serikali ilikuwa inafanya mzaha, inaleta mambo ya utani kazini, kama vile ilitaka watu wacheke, wafurahi kisha iwaambie, ah, msijali, huo ulikuwa ni utani tu, muswada wenyewe si huo, hilo ni boya tu, muswada wenyewe ni huu hapa.

Tatizo ni haitarajiwi kwamba Serikali yetu itafanya utani wa gharama kubwa kama huo, gharama kwa fedha zinazoteketea kila kikao cha Bunge kinapoitishwa, lakini gharama kubwa zaidi na ya kutisha inayoweza kutokea iwapo zitazuka zahma, vurugu na uvunjaji wa amani kutokana na wananchi kuamini kwamba Serikali waliyoiajiri iwafanyie kazi sasa "inawacheza shere".

Hata hivyo, wale waliodhani muswada huo ulikuwa ni aina ya utani wa Serikali waligundua kwamba Siku ya Majuha, Aprili Mosi, ambayo huwa ndiyo siku ya kuchezana shere kimataifa, ilikuwa imekwisha kupita. Kwa kuwa dhana ya Serikali kufanya utani ilikuwa haiyumkiniki, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa walijaribu kuangalia sababu nyingine ambazo zilikuwa zimeifanya Serikali kuwasilisha muswaada wa kipuuzi kiasi kile.

Miongoni mwa wachambuzi hao, baadhi waliueleza udhaifu wa muswada kwamba ni zao halisi la Serikali inayoendeshwa na watu wavivu wa kufikiri, watu waliozoea kufanya mambo yao 'fasta fasta' kwa sababu wa na shughuli zao binafsi ambazo ni muhimu kuliko kazi za ofisi zao rasmi; kila mara wamo katika harakati za kutengeneza 'dili' na hawana muda kudurusu makabrasha yanayohusu majukumu muhimu ya ofisi zao.

Wanaosema hivyo wanaeleza hisia zao hizo kwa kuonyesha jinsi muswada ulivyoandikwa kwa kulipua. Watu wengi wameukosoa muswaada huo kwa kuandikwa katika lugha ya kigeni, jambo ambalo bila shaka ni la aibu kwa shughuli kama hii. Lakini pia, angalau hata hicho Kiingereza kilichotumika kingeonyesha kwamba maofisa hawa wa Serikali wanao uwezo wa kuandika katika lugha hiyo waliyoiteua wao. Uwezo huo haukujitokeza.

Sasa, basi, ni jinsi gani watu wazima waliokabidhiwa ofisi nyeti za Serikali wanaweza 'kupuyanga' na kuandaa 'madudu' na kuyaanika kadamnasi bila haya? Tumezoea kuwaambia waandishi wachanga katika vyumba vya habari kwamba wanahitaji kufanya hadhari kabla ya kuweka majina yao juu ya makala iliyoandikwa hovyo na isiyohaririwa kwani kufanya hivyo ni kujisababishia fedheha mbele ya wasomaji.

Kama waandishi chipukizi wanatakiwa kuona haya kuhusu machapisho ya hovyo, inakuwaje wanasheria waandamizi na wanasiasa wanaowaelekeza hawaoni haya kuhusishwa na upuuzi?

Kisha kuna wachambuzi wengine wanaoamini kwamba sakata yote hii kuhusu muswada haikutokana na uvivu wa kufikiri au udhaifu wa kiuandishi au uhariri, bali ulikuwa ni mpango wa makusudi ulioandaliwa kwa lengo la kuzima ari iliyoanza kujitokeza katika mjadala kuhusu Katiba mpya. Hawa wanasema kwamba wanasiasa hawakuwa na nia ya kuleta muswada ambao ungekuwa ni chanzo cha kufanya mabadiliko ya kweli katika utawala wa nchi.

Wananaukuu matamko ya wakuu wawili wa wizara inayohusika moja kwa moja na masuala ya kikatiba, waziri na mwanasheria wake, ambao wote wawili waliwahi kusema hadharani kwamba hakukuwa na sababu ya kuandika Katiba mpya, kwani mabadiliko yakihitajika yanaweza kufanyika kwa njia ya siku zote ya kupachika 'viraka'. Hiyo ilikuwa ni kabla ya tajiri wao, Rais Jakaya Kikwete hajatamka wazi kwamba angeanzisha mchakato wa kuandika Katiba mpya.

Wanaoshuku dhamira ya maofisa hawa wa Serikali wamesema kwamba hawaoni ni jinsi gani wale wale waliosema kwa kutamba kwamba hakukuwa na haja ya Katiba mpya wangekuwa ndio hao hao ambao wangepewa jukumu la kuandaa sheria za kutekeleza jambo wasiloliamini. Hata dhana ya mchawi mpe mwana amlee haiendi hivyo.

Tukifika hatua hii ya tafakuri tunalazimika kujiuliza ni maagizo gani hawa wakuu wa Sheria walipewa na tajiri yao, Rais Kikwete. Ni dhahiri kwamba Rais Kikwete alijua misimamo ya maofisa wake hao, na yumkini alijua kwamba msimamo wake alioutangaza ulikuwa unatofautiana na misimamo yao. Sasa, ni maelekezo gani aliwapa?

Swali hili lina umuhimu wake kwa sababu jibu lake litatusaidia kujua namna gani tuenende katika mwendelezo wa mjadala wa Katiba. Kama Rais Kikwete alijua kwamba alichotamka hakikuendana na walichoamini maofisa wake, na ni dhahiri kwamba alijua, alikuwa na wajibu wa kuwa na shaka wakati akiwakabidhi majukumu ya kuandaa mswada, hata kama aliwajibika kuwapa majukumu hayo kwa sababu ni kazi yao.

Shaka hiyo ingemtaka Rais Kikwete afuate utaratibu wa utumishi wa umma. Inapotokea kwamba mkuu na mdogo wake wanatofautiana kuhusu suala fulani, na mkuu anamtaka mdogo wake aifanye kazi hiyo kama anavyotaka mkuu, mkuu anawajibika kumpa mdogo wake "maagizo mahsusi." Hamwachii achague ni nini afanye na nini asifanye, kwa sababu anajua akimruhusu hilo, mdogo wake atafanya anavyotaka yeye na si anavyotaka mkuu wake.

(Utaratibu huu wa kiutawala unatumika pia iwapo mdogo anaamini kwamba maelekezo ya mkuu, mara nyingi kwa mdomo, yanaweza kumwingiza mdogo katika hatia itakapokuja kuonekana kwamba alikiuka utaratibu. Mdogo anayo haki ya kumtaka mkuu wake ampe "maagizo mahsusi" kwa maandishi ili kusiwe na utata kuhusu chanzo cha uamuzi. Wale waliohusika na sakata la Richmond, ama kwa kutuhumiwa kufanya hili na kutofanya lile ama kwa kufuatilia malumbano yaliyoibuka wakati ule, watagundua umuhimu wa utaratibu huu kati ya mkuu na mdogo katika utumishi wa umma. Kwa bahati mbaya, ni utaratibu uliosahaulika katika Serikali yetu hivi sasa).

Iwapo Rais Kikwete hakuwapa maofisa wake maagizo mahsusi alikosea kwani aliwapa carte blanche kufanya watakavyo ilhali akijua kwamba hawakuwa na utashi wa kuifanya kazi hiyo. Vinginevyo, akiri kwamba hivyo walivyofanya ndivyo alivyowatuma, ambalo litakuwa ni jambo la kushangaza, kwani itabidi aeleze ni kwa mini muswaada huo umeondoshwa Bungeni.

Iwapo aliwapa maagizo mahsusi na wakakaidi, tutalazimika kujiuliza ni vipi bado wamo ndani ya ofisi zake (zake, nasema, si zao) baada ya kuwa wamekataa kutimiza matakwa yake. Je, ni kweli kwamba maofisa wa Serikali wanaweza kupokea maagizo ya Rais, wakayapuuza na bado wakaendelea kuwa serikalini? Hiyo itakuwa ni Serikali gani?

Ni muhimu kuyajadili masuala haya kwa umakini mkubwa kwani mustakabali wa Taifa letu utaamuliwa kwa kiasi kikubwa na hatua tutakazozichukua kati ya sasa na hapo tutakapokuwa tumekamilisha rasimu ya Katiba itakayokidhi matarajio ya wananchi. Ni rai yangu kwamba hii ni fursa kwa Rais Jakaya Kikwete kufanya kile anachotarajiwa kufanya na kuacha urithi wenye fahari.

Sidhani kwamba haelewi kwamba rekodi yake imeingia madoa mengi mengi na kwamba baadhi ya changamoto zinazomkabili zimetokana na kule kuonekana kama hajali na kuwaachia walio chini yake wafanye wanavyotaka.

Kama Rais Kikwete atashindwa kusimamia kwa dhati zoezi hili, ambalo amelitangaza mwenyewe bila hata chama chake kujua, atakuwa ameshindwa kazi katika idara nyingine muhimu.

Haifai hata kidogo kukubali wazo kwamba Rais amewatuma watu wake waandike muswaada wa hovyo ili ukataliwe na kila kundi, kisha uondolewe Bungeni, na mchakato wa kuandaa muswada mpya uendelee kwa muda mrefu, hadi yeye amalize muhula wake, na mzigo mzito wa kuandika Katiba mpya awaachie hao watakaokuja baada yake, ambao ndio hao hao wanaodai Katiba mpya, na ambao si wa chama chake! Hili ni jukumu la Rais; hawezi kulikwepa.
 
Back
Top Bottom