Kikwete awapa mawaziri mbinu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
273
kupangua makombora bungeni *AWATAKA MAWAZIRI KUUNGANA NA KUWA NA SAUTI MOJA BUNGENI Salim Said RAIS Jakaya Kikwete amewataka mawaziri kuhakikisha wanawajibika kwa umoja wao bungeni, kutetea serikali katika hoja mbalimbali zitazowasilishwa kwenye chombo hicho cha kutunga sheria. Alisema ni wajibu wa kila waziri kuhudhuria vikao vyote vya bunge na kwamba, mawaziri wote wa serikali lazima wawajibike kwa pamoja bungeni.

Rais Kikwete alikutana na mawaziri wote 29 na manaibu wote 21, ambao aliwateua na kuwaapisha kushika nyadhifa zao hivi karibuni. “Ni muhimu ieleweke kuwa kama ilivyo kwa maamuzi ya baraza la mawaziri, uwajibikaji wa mawaziri bungeni ni wa pamoja.

Kwa hiyo, hoja ya serikali bungeni ni hoja ya mawaziri wote na sio waziri anayewasilisha hoja,” alisisitiza Rais Kikwete. Kutokana na kujaa kwa sura mpya na kuongezeka kwa sauti na nguvu ya upinzani bungeni, huenda Rais Kikwete alitoa wito huo kuweza kuhimili na kupangua hoja kutoka kwa wabunge hao waliodhamiria kuibana serikali.

Aliwaeleza mawaziri hao kuhusu dhana ya uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility) katika kuongoza nchi, akisisitiza kuwa uwajibikaji huo unaelezwa kwa ufasaha katika Hati Maalum (Instrument) ya majukumu ya kila wizara. Alitoa angalizo kwa Baraza la Mawaziri kwamba, awamu hii ya uongozi wake hatakubali utetezi kutoka kwa waziri yeyote aliyeshindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa katika Mtandao wa Habari Jamii (blog) wa Idara ya Mawasiliano Ikulu, Rais Kikwete alianza kwa kusisitiza: “Mnastahili pongezi hasa ukizingatia ukweli kwamba nyinyi mmebahatika kuteuliwa kutoka kwenye orodha ndefu ya wabunge wengi wenye sifa za kushika nafasi mlizo nazo.” Kikwete aliwaeleza mawaziri hao maana ya Baraza la Mawaziri na majukumu yake, na kutaka kila waziri ahakikishe anatayarisha kalenda yake ya masuala muhimu ambayo anataka yajadiliwe na Baraza la Mawaziri kwa mwaka.

Pia, alitaka kujengeka uhusiano mzuri kati ya Waziri na naibu wake akisisitiza: “Jambo la msingi la kuzingatia ni kwamba, uhusiano mzuri baina ya viongozi hawa ni nguzo muhimu katika mafanikio ya wizara.” Aliongeza kuwa: “Kwa hiyo, ili kuepuka migongano katika utekelezaji ni muhimu mipaka ya kazi za waziri na naibu ikaheshimika na pia wajibu wa waziri kumpangia kazi naibu wake katika wizara husika

.” Alizitaja nyaraka wanazotakiwa kukabilidhiwa kuwa, ni Taarifa ya Makabidhiano ya Ofisi, Katiba, Ilani ya Chama Tawala, Dira ya Taifa na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (Mkukuta). Rais Kikwete aliwaeleza umuhimu wao kufahamu sera, sheria, kanuni, taratibu, mikakati, mipango mikakati, mpango na bajeti ya wizara, mpango kazi wa wizara na masharti ya kazi ya waziri husika. Rais Kikwete aliwaeleza Mawaziri wake kuwa suala la vita dhidi ya rushwa ni suala la kikatiba na kuwataka kuhakikisha kuwa, mpango wa pili wa mkakati wa kitaifa wa kupambana na rushwa (NACSAP-11) unatekelezwa.

Aliwataka kuvitumia kikamilifu vitengo vya mawasiliano ya serikali katika wizara zao, ambavyo ndivyo vyenye jukumu la kutoa taarifa kuhusu wizara inavyotelekeza majukumu yake. ”Uzoefu unaonyesha kuwa mawaziri wengi ni wazito kufanya mawasiliano na wananchi hata pale ambapo wizara imefanya mambo mengi mazuri. Hivyo, lazima muwe mstari wa mbele kuelezea mafanikio ya utendaji wa serikali katika wizara zetu,” alieleza Rais Kikwete. Mwisho
 
Back
Top Bottom