Kikwete ashauriwa kupanga upya safu ya viongozi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kikwete ashauriwa kupanga upya safu ya viongozi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Nov 9, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Nov 9, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,420
  Likes Received: 81,470
  Trophy Points: 280
  [​IMG]

  Rais Jakaya Kikwete, amepewa ushauri kupanga upya safu yake ya viongozi.

  Na Waandishi Wetu
  Mwananchi
  11/9/2009

  RAIS Jakaya Kikwete ametakiwa kutumia malumbano yanayoendelea baina ya wabunge wa CCM kupanga upya kikosi chake cha mawaziri na hasa kwa kuwa malumbano hayo yameonyesha dalili kuwa nidhamu ndani ya chama hicho imeporomoka kinadharia na kivitendo.

  Kwa miezi kadhaa sasa, wabunge na wanachama wa CCM wamekuwa wakirushiana maneno makali kutokana na baadhi kuwarushia wenzao tuhuma za ufisadi huku wengine wakieleza kuwa vitendo vya wenzao vinakichafua chama na serikali.

  Lakini, baada ya chama kuunda kamati ya watu watatu kutafuta kiini cha matatizo hayo, hali imeonekana kuwa ni mbaya zaidi kutokana na wabunge kutumia fursa ya kusikilizwa na kamati hiyo, kurushiana maneno ya kudhalilishana ambayo yanaonekana dhahiri kuwa yanakiweka chama mahali pabaya.

  Akizungumza na gazeti hili jana, mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Siasa cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema malumbano hayo ni faida kwa Watanzania na rais kwani yanatoa fursa ya kufahamu tabia za viongozi wao na kuwahukumu.

  Kwa mujibu wa Dk Bana, huu ni muda mzuri kwa Rais Kikwete kutumia malumbano hayo kujifunza na kutafakari aina ya viongozi aliowateua katika serikali yake.

  “Lakini pia wananchi wanapata kujua aina ya viongozi wanaowaongoza kwa sababu nchi yetu haina mkakati wa elimu ya uraia, basi malumbano haya yanawapa fursa ya kufanya maamuzi katika uchaguzi ujao,” alisema Prof Bana.

  Malumbano hayo si tu yamehusisha wabunge na wanachama wa CCM, bali pia baadhi ya mawaziri ambao walijitokeza kwenye vikao vya Kamati ya Mwinyi na kuonyesha dhahiri kuwa wanatetea moja ya makundi yanayopingana kwenye chama hicho.

  Mawaziri hao ni Sophia Simba na Makongoro Mahanga ambao walizungumza kwenye mikutano ya kamati hiyo kuwatetea wanachama ambao wanashambuliwa kwa tuhuma za ufisadi, akiwemo Edward Lowassa, ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu kutokaa na kashfa ya Richmond.

  Wengine ni Andrew Chenge ambaye alijiuzulu uwaziri wa Afrika Mashariki na Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi ambao walijiuzulu kutokana na kuwahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini.

  Lakini Prof Bana alichukulia maelezo, makombora na utetezi uliojitokeza kwenye vikao hivyo kuwa ni ishara ya CCM kupoteza nidhamu na kama ingekuwepo, watuhumiwa wote wangeshafukuzwa uanachama.

  Alisema nidhamu ndani ya chama hicho kikongwe nchini imeporomoka na kusababisha baadhi ya wabunge kuanza kushambuliana kwa mambo binafsi badala ya yale yenye maslahi kwa umma.

  “Zamani kulikuwa na kuheshimiana ndani ya chama, lakini sasa hakuna tena kuheshimiana wala kufichana,” alisema Dk Bana.

  “Kinachoonekana hapa ni ‘erosion of ethics(mmomonyoko wa maadili)’, maneno kama yaliyosemwa na Waziri wa Utawala Bora Sophia Simba au Samuel Malecela katika malumbano yao hayapaswi kusemwa na viongozi,” alisema Dk Bana.

  “Maneno yao machafu hayawakilishi CCM bali ni tabia ya mtu binafsi na kama ingekuwa enzi za Mwalimu Julius Nyerere, wangepoteza nyadhifa zao.”

  Naye Dk Sengondo Mvungi alisema Rais Kikwete aliteua watu wa chekechea kuwa mawaziri katika serikali yake na kwamba alishaelezwa kuwa hawafai, lakini akawatetea.

  "Tulimwambia kuwa umeteua chekechea hawafai hawa; watakwenda kujilimbikizia mali akasema wanafaa. Sasa leo wanavuruga nchi... yeye si ndiye aliwateua na si wao ndio wanaovuruga nchi, basi awajibike yeye," alisema Dk Mvungi.

  Alifafanua kuwa Rais Kikwete anapaswa kuwaangalia mawaziri wake kwa sababu hawafai na wanaivuruga nchi na kama hawezi kuwawajibisha, serikali ijiuzulu kwa sababu yeye ndiye aliyewateua.

  "
  Malumbano haya ya wabunge na mawaziri wa CCM yanatusaidia sisi kujua yale yaliyofichwa kwa muda mrefu ambayo tulikuwa hatuyajui," alisema Dk Mvungi.

  "Namshangaa Waziri Simba ana ushahidi mzuri lakini anautolea mitaani, (mfanyabiashara Jeetu) Patel si ana kesi mahakamani na haijahukumiwa, aende mahakamani kutoa ushahidi wa ufisadi wa Patel."

  Alisema kushindwa kwa rais kuipanga vizuri serikali yake ni sababu tosha kwa serikali hiyo kujiuzulu na kwamba isingoje kushinikizwa.

  Alisema migogoro na chuki ndani ya vyama vingine vya upinzani ilikuwa inapandikizwa na CCM, lakini wananchi walikuwa hawaamini.

  "Tulikuwa hatuaminiwi, sasa yamewarudia wenyewe kwa sababu wamekula nyama ya maiti na ukishakula nyama ya maiti lazima mzimu wake ukurudie tu," alisema Dk Mvungi.

  Wakati Dk Bana na Mvungi wakitoa ushauri huo, katibu wa kamati ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi iliyoundwa kuchunguza chanzo cha chuki ndani ya CCM, Pius Msekwa aliliambia gazeti hili jana kuwa kazi hiyo bado inaendelea, lakini kikubwa kinachofanyika sasa ni kupitia hoja mbalimbali za wabunge hao na kuandaa ripoti.

  Wachambuzi wanaona kuwa mikutano ya kamati hiyo na wabunge imekoleza chuki badala ya kupunguza, lakini Msekwa alisema wanaotilia shaka kile kinachofanywa na kamati hiyo, wanapiga ramli na kuwataka wawe na subira hadi wamalize kazi hiyo na kuikabidhi kwenye Halmashauri Kuu (Nec).

  "Mambo bado ni mabichi. Kilichofanyika ilikuwa ni kuwasikiliza ili kujua kulikoni. Kazi hiyo tumemaliza. Kazi kubwa sasa ni kuyatafakari hayo waliyotueleza," alisema Msekwa ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa CCM.

  Alipotakiwa kueleza siku ambayo watakamilisha kazi hiyo, Msekwa alisema ni vigumu kutaja muda kwa sababu kamati yake imesimamisha kazi zake kutokana na mwenyekiti wao, Ali Hassan Mwinyi kusafiri nje ya nchi.

  "Tunasubiri akiregea tutaendelea na kazi," alidokeza.

  Msekwa alisema kwamba hakuna haja ya watu kuwa na wasiwasi kwa sasa bali wasubiri kamati hiyo imalize kazi yake na kwamba, suala lolote litakalozungumzwa kuhusu utendaji wa kamati yake ni sawa na kupiga ramli, akimaanisha kuwa wanaofanya hivyo, wanabahatisha.

  "Mimi siwezi kusema lolote kwa sasa, labda muendelee kuwauliza hao maana mimi siwezi kupiga ramli," alisema Msekwa huku akionya kwamba wananchi wanapaswa kuwa na subira.

  Mgawanyiko ndani ya CCM ulizuka baada ya kuibuka makundi mawili, moja likiwa ni lile linalojieleza kuwa liko mstari wa mbele katika kupambana na ufisadi wakati jingine linajihami kwa kudai kuwa vita hiyo inakichafua chama na serikali.

  Baadhi ya wananchi walitoa maoni yao wakieleza kwamba kamati hiyo ya Mwinyi imechochea mambo baada ya Waziri Simba kutoa tuhuma nzito dhidi ya Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango na mumewe, John Malecela wakidai kuwa harusi yao na kampeni za urais za mbunge huyo wa Mtera zilifadhiliwa na fedha za mtuhumiwa wa ufisadi, Jeetu Patel.

  Alimtuhumu pia Kilango kuwa si mtu safi na ni mnafiki na kwamba kama isingekuwa rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa asingeolewa na Malecela.

  Alimshambulia Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, akiwatuhumu kuwa ni watu wenye njaa na kwamba wanalipwa fedha kufanya kazi ya kupambana na ufisadi. Pia alimtuhumu mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi kuwa anatumia vyombo vyake kukichafua chama na serikali kwa maslahi yake binafsi.

  Watu hao waliotuhumiwa na Waziri Simba hawakujibu tuhuma hizo na badala yake walimtuhumu kuwa ni mgonjwa wa akili, mnafiki na ambaye hastahili kuzungumza lolote katika vita dhidi ya ufisadi.

  Suala la kashfa ya utoaji zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development LLC lilionekana kutawala kwenye vikao hivyo na watetezi wa watuhumiwa walitumia nafasi hiyo kumtuhumu mwenyekiti wa kamati teule iliyochunguza kashfa hiyo, Dk Harrison Mwakyembe kuwa alimuonea waziri huyo mkuu wa zamani na kwamba ana njaa.

  Pia Spika Samuel Sitta alielezewa kuwa aliendesha mijadala dhidi ya Lowassa kwa kuwa alizidiwa kete na mbunge huyo wa Monduli katika kinyang'anyiro cha uwaziri mkuu.

  Hata hivyo, Dk Mwakyembe amemuelezea mbunge wa Ukonga, Dk Makongoro Mahanga, ambaye alitoa tuhuma hizo, kuwa ana ufahamu mdogo. Habari hii imeandaliwa na Leon Bahati, Salim Said na Hashim Gulana
   
 2. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #2
  Nov 9, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,420
  Likes Received: 81,470
  Trophy Points: 280
  Mtamlaumu dobi bure kumbe kaniki ndiyo rangi yake. Kikwete kishapanga safu mpya zaidi ya mara tatu sasa. Kulinusuru Taifa na uongozi wake mbovu ni bora atangaze mapema kwamba 2010 hatagombea tena nafasi ya Urais arudi Bwagamoyo akalime minazi na mananasi.
   
 3. Lyangalo

  Lyangalo JF-Expert Member

  #3
  Nov 9, 2009
  Joined: Sep 10, 2009
  Messages: 681
  Likes Received: 77
  Trophy Points: 45
  Tatizo hapa si kupanga safu ya viongozi, tuabadili viongozi na viongizi lakini wapi, wangeshauri atumie urais wake kubadili mfumo wa uongozi ndo uliooza unaotoa nafasi kwa hao viongozi kufanya wanayotaka wakiwa kwenye ofisi za umma. Halafu na yeye ajipunguzie madaraka, wewe raisi anateuwa hadi watendaji wa kata! anawafahamu vizuri kweli? huo ni mfani mdogo tu. Watu walishasema akitoka Mungu kwa TZ mwenye madaraka makubwa ni rais. Kama tukibadili mifumo hakika tutafika mbali sana.
   
 4. MaxShimba

  MaxShimba JF-Expert Member

  #4
  Nov 9, 2009
  Joined: Apr 11, 2008
  Messages: 35,816
  Likes Received: 129
  Trophy Points: 160
  Kikwete ashauriwa kupanga upya safu ya viongozi
   
 5. M

  Mwafrika JF-Expert Member

  #5
  Nov 9, 2009
  Joined: Nov 20, 2006
  Messages: 5,490
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  Mkuu,

  Ungesoma vizuri threads za wengine, labda usingemaliza bandwith kwa hii thread mpya. Hii topic tayari ipo.
   
Loading...