Kikwete aijaza jeuri Takukuru

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
RAIS Jakaya Kikwete amesema watakaojihusisha au kutuhumiwa kwa vitendo vya rushwa kwenye mchakato wa uchaguzi ndani ya vyama vya siasa na wakati wa uchaguzi mkuu ujao, watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alisema hayo jana jijini hapa, wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini(Takukuru) uliofanyika kwenye Chuo cha Benki Kuu.

Rais ambaye alitoa hotuba yake akiwa amekaa, alisema asingependa kuona watu au kikundi cha watu, kiongozi au mtu binafsi akijihusisha na rushwa kwenye uchaguzi mkuu ujao ndani ya chama ama vyama vyenyewe.

Aliitaka Takukuru kuhakikisha inawachukulia hatua watu hao ili kwenda sambamba na utekelezaji wa sheria ya uchaguzi ambayo muswada wake ulipitishwa bungeni hivi karibuni.

“Ningependa kuona hakuna mtu anayejihusisha au kutuhumiwa kwa rushwa katika uchaguzi au wakati wa mchakato wa uchaguzi ndani ya vyama akaachwa bila kushughulikiwa.

"Ninyi Takukuru ndio mnaotazamiwa kufanya kazi ya kukazia utekelezaji wa sheria hii mpya, na niwahakikishieni kuwa nitafanya kila linalowezekana ili muweze kufanikisha kazi ya kudhibiti rushwa katika uchaguzi nchini na msimwogope mtu,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema hivi sasa baadhi ya viongozi wa siasa ambao wengi wao ni wawakilishi wa wananchi, wameanza kupitapita majimboni kabla ya wakati muafaka kwa kisingizio cha kutoa misaada kwa wananchi na kuhoji walikuwa wapi.

“Nimeambiwa wahongaji (viongozi) hivi sasa wanajipitisha kwa wananchi kwenye matawi wakitoa misaada huku wakijenga majengo, hivi hawa walikuwa wapi hadi wajitokeze wakati huu, hawa si wanataka kuwahadaa wananchi ili wachaguliwe?”

Alihoji na kuongeza kuwa asingependa kuona mtu anayetaka kuingia kwenye uongozi akienda kwa wananchi kuwahadaa kwa fedha.

Aliitaka Takukuru ianze mchakato wa kujipanga wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, ili waanze kudhibiti viongozi wanaotumia fedha, huku akisisitiza kuwa sheria iliyopitishwa hivi karibuni inaruhusu udhibiti wa rushwa kabla na wakati wa kura za maoni ndani ya vyama vya siasa na wakati wa uchaguzi.

Alisema nia na madhumuni ni kuona kuwa wakati Serikali ya Awamu ya Nne itakapokuwa imemaliza awamu yake ya uongozi, iwe imejenga misingi imara ya utawala bora, demokrasia na maadili ya viongozi itakayojikita kwenye sheria za nchi, ili hatimaye uwepo utamaduni wa kudumu wa kuendesha shughuli za siasa bila mazingira ya rushwa.

Alitumia fursa hiyo pia kuwaasa waandishi wa habari nchini wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi, ambapo alisema baadhi yao hujenga mazingira yanayowaaminisha watoa habari kuwa nao wanajihusisha kwenye vitendo vya rushwa.

“Bahati mbaya sana waandishi wa habari nao wanaomba rushwa, mnakatisha tamaa jamii, ingawa ukiwasema hadharani waandishi wa habari wanakasirika sana, utakuta mwandishi anamwambia mtu unaona hii habari ni mbaya sasa niitoe?” Alisema.

Aliihakikishia Taasisi hiyo misaada ya hali na mali ikiwa ni pamoja na vitendea kazi vya kisasa, lakini akaonya kuwa sharti watumishi wake wafanye kazi kwa umakini wa hali ya juu wakizingatia weledi wa taaluma zao.

Aliitaka Takukuru kufanikisha azma ya kupambana na rushwa nchini, na kujihusisha kwa karibu sekta binafsi kwa maelezo kuwa wapo wakuu wa kampuni katika sekta hizo, wanaojihusisha na rushwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, alisema katika kipindi cha Januari hadi Februari mwaka huu, Kurugenzi ya Uchunguzi iliongeza kasi ya kusimamia uchunguzi na uendeshaji mashitaka na kuvuka malengo kwa kuchunguza kesi kubwa tano kwa makao makuu na moja kwa kila mwezi kwa kila mkoa.

Alisema Takukuru imeliokolea Taifa Sh 7,587,968,099.32 kupitia uchunguzi unaoendelea wa rushwa na ukaguzi wa fedha za miradi ya maendeleo uliofanyika kwenye halmashauri zote nchini.

Mkutano huo wa siku tatu unaowakutanisha viongozi na wakuu wa idara wa taasisi hiyo wapatao 169 una lengo la kufanya tathmini ya utendaji wa mwaka mzima ili kuainisha changamoto zinazoikabili taasisi hiyo na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana nayo.
 
Unajua tatizo la Rais wetu ni kuyapa kiupaumbele mambo yasiyo ya msingi sana na kuacha mambo ya msingi. Kusema kweli Rushwa katika uchaguzi hasa wa wabunge, madiwani n.k sio la msingi sana. Ni rushwa ndio, lakini sio haswa kusudio la kuiweka Takukuru. Takukuru ni chombo cha kupambana na kuzuia hasa rushwa kubwa kubwa ambayo kwa mfano inaweza kepelekea wananchi kufa kwa njaa, kukosa madawa hospitalini, kukosa barabara, kudhulumiwa haki yao ya msingi kama ulinzi, maji, nk. Hayo ndio mambo makubwa ya Rais kuyatilia mkazo. Rushwa ndogo ndogo ( khanga, pombe, sukari na chumvi) kama za uchaguzi aachiwe Waziri mkuu Pinda na Mama Sophia Simba.
 
Back
Top Bottom