kikwazo cha kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
SIO wazazi wote wanaoshindwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni.Wapo wanaotamani kufanya hivyo na hata kuwasaidia kimasomo lakini wanakwazwa na matumizi ya lugha inayotumika shuleni.

Hivi karibuni, shirika la HakiElimu, lilifanya utafiti ambao pamoja na mambo mengine, ulilenga kubaini ushiriki wa wazazi na jamii katika maendeleo ya watoto.

“Umuhimu wa ushiriki wa jamii katika maendeleo na utekelezaji wa mtaala hauwezi kupuuzwa. Ushahidi unaonyesha kwamba, kadri familia na jamii zinavyoshirikishwa zaidi, ndipo mafanikio ya wanafunzi yanavyopatikana,” inaeleza sehemu ya ripoti ya utafiti huo.

Katika utafiti huo, ilidhihirika kuwa idadi kubwa ya wazazi hasa wenye watoto wanaosoma sekondari, hawana uwezo wa kuwasaidia watoto wao kwa kuwa hawana maarifa ya kutosha kufanya hivyo. Wazazi hawa wanashindwa kuwasaidia kutokana na kikwazo cha lugha.

Wazazi wengi wanalalamika kuwa masomo mengi ya sekondari yanafundishwa katika lugha ya Kiingereza ambayo wengi hawaimudu.

Ikiwanukuu wazazi bila ya kutaja majina yao, ripoti inasema baadhi yao walisema kwa hali ilivyo, wameamua kuwaachia mzigo walimu kwa kuwa lugha ya Kiingereza imekuwa kikwazo kwao.

“ Kwa kuwa hatufahamu ni kwa kiwango gani watoto wetu wanajifunza, wanaenda shuleni wanarudi na vitabu, sasa nitajuaje wanachojifunza wakati mimi mwenyewe sikwenda shule?” alisema kwa kuhoji mzazi mmoja kutoka Malangani.

Mzazi mwingine aliyehojiwa kutoka wilayani Bukombe anasema: “…. hakuna mtu aliyewahi kuniuliza kuhusu nini watoto wangu wanajifunza shuleni. Nadhani hiyo ni kazi ya walimu, wao ndiyo wanapaswa kufahamu kuhusu kile watoto wetu hujifunza shuleni.”

Akaongeza: “Ninachofahamu ni vitabu na vifaa vya shule ambavyo watoto wangu hubeba wanapokwenda shuleni, huwa nawaona wakibeba mabegi ya shule.”

Mzazi kutoka Ushirombo anaeleza kuwa anachofahamu yeye ni kwamba watoto wake wakienda shule, hubeba madaftari, vitabu na vitu vingine vya shule katika mikoba yao, lakini masuala mengine haelewi…… “Kusema kwamba nafahamu wanachofundishwa shuleni nitakuwa nadanganya.”

Mzazi mwingine kutoka Mufindi anasema ni vigumu kujua kile ambacho watoto wake wanafundishwa kwa kuwa kila kitu kimeandikwa katika lugha ya Kiingereza.

“Na hata unapouliza iwapo wanawasaidia watoto katika masomo yao, nitawasaidiaje wakati masomo yao yapo katika lugha ya Kiingereza?” anahoji mzazi huyo.

Ripoti inatoa mapendekezo kadhaa kama inavyosema: “Suala la lugha ya kufundishia limekuwa likiibua mijadala mizito na kwamba muafaka umekuwa haufikiwi katika suala hili. Kuna haja kwa serikali kuchukua hatua madhubuti katika kuongoza majadiliano kuhusu lugha ya kufundishia katika mfumo wetu wa elimu.”

“Watoto hujifunza vizuri zaidi iwapo wataimudu lugha ya kufundishia. Suala hili linapaswa kutazamwa kwa umakini zaidi, ili kuhakikisha kuwa lugha ya kufundishia inafahamika vema kwa walimu na wanafunzi.”

Utafiti huo pia ulihusisha suala la mitalaa na kubaini kuwa pamoja na mitalaa kupaswa kwenda sambamba na matarajio na mahitaji ya jamii iliyolengwa, ushiriki wa wazazi na hata walimu katika maandalizi yake ni mdogo.

“Matokeo haya yalitarajiwa kwa kuwa hata walimu ambao ndiyo watekelezaji wa mtalaa wenyewe, hawahusishwi kwa kiwango cha kutosha katika maendeleo na utekelezaji wa mtalaa,” inafafanua ripoti.
 
Back
Top Bottom