Kikatiba: Rais wa Tanzania hashtakiwi, lakini hana kinga dhidi ya yafuatayo...

MALCOM LUMUMBA

JF-Expert Member
Jul 26, 2012
20,897
63,783
Katiba ya Tanzania chini ya Ibara ya 46 inasema kwamba Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawezi kushitakiwa kwa namna yoyote ile akiwa ofisini au nje ya ofisi. Mwaka jana baada ya kesi ya kikatiba ya Ado Shaibu dhidi ya Raisi wa Magufuli na Mwanasheria Mkuu, bunge letu tukufu lilifanya mabadiliko na kuweka bayana kwamba Raisi hawezi kushitakiwa kwa namna yoyote ile. Hili nadhani tulilizungumzia kidogo hapa: Sheria inasemaje kuhusu mkuu wa nchi kufanya uhaini dhidi ya nchi anayoiongoza ?

Mabadiliko yaliyofanyika juzi ili kuongeza kinga ya Raisi yamefuata nadharia ile ya Uingereza inayosema kwamba mfalme hawezi kushitakiwa kwa jambo lolote atakalofanya kwasababu yeye ni mtakatifu. Katika lugha ya Kiingereza inasemwa hivi: " The King shall not be answerable for his actions; his person shall be sacrosanct. The Ministers shall be responsible for the conduct of the government; their responsibility shall be determined by Statute". Waingereza wameenda mbali zaidi na kusema kwamba "A King cannot be sued in his own court"

Ni jambo jema kabisa kutaka kumuwekea kinga Raisi wetu huku tukiiga wafalme wa Ulaya, lakini jambo moja muhimu ambalo tunalisahau ni kwamba tunaweza kuwa na Uraisi wa Kifalme (Imperial Presidency) na tukamlinda Raisi kama mfalme lakini ukiangalia kwa jicho la tatu Katiba hiyohiyo inayotoa kinga ya Raisi kwa upande wa pili imeacha mwanya mkubwa ambao kwa namna moja au ingine unamnyang'anya huyo Raisi kinga ya milele

Iko hivi ndugu zangu, hapa nchini Tanzania sehemu halali za kutolea adhabu siyo mahakamani tu, ambako wasomi wetu wakiongozwa na Waziri Palamagamba Kabudi na mwanafunzi wake Adelardus Kilangi wamejiaminisha kwamba ndiko sehemu pekee ambayo watanzania wanaweza kumsulubishia Raisi Magufuli. Hapana, haiko hivyo. Tumempa Raisi kinga dhidi ya kushitakiwa mahakamani, pia bunge lenye wanachama wengi wa chama cha mapinduzi haliwezi kabisa kumshitaki Raisi, lakini jambo ambalo hawajaliangalia ni kwamba Raisi akitoka madarakani anaweza kuwekwa Kizuizini (Security Detention) na Raisi ambaye ameingia ofisini. Hili ni suala ambalo liko kisheria na ndani ya mamlaka ya Raisi.

Ukiwasoma wanazuoni wakubwa wa sheria kama Chris Maina Peter wanasema kwamba tunaweza kuwa tumeondoa sheria za kuweka watu kizuizini lakini kwa upande mwingine kuna sheria ambazo bado zinampa Raisi nguvu ya kuweka mtu yeyote yule kizuizini akitumia mwamvuli wa usalama wa taifa (National Security) au Maslahi ya Ummah (Public Interest). Raisi wetu anaweza kulindwa na katiba kwa minajili ya kutoburuzwa mahakamani kwa kesi za jinai au madai, lakini sheria za mkoloni tulizorithi bado zinampa Raisi mwingine nguvu ya kukwepa hicho kigingi na kumuweka kizuizini mwenzake ambaye amestaafu bila kutoa sababu kwa mamlaka yoyote ile.

Kinga dhidi ya kushitakiwa mahakamani kwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siyo ya moja kwa moja (Not absolute), kwasababu bado anaweza kuadhibiwa kisheria kupitia njia zisizo za kimahakama (Extra-Judicial Measures) ambazo ni Kukwekwa Kizuizini au Kupelekwa Uhamishoni. Katika mtazamo wa kawaida ni bora ukashitakiwa mahakamani, huko unaweza ukapewa baadhi ya haki kama ile ya kusikilizwa (Right to be heard), haki ya kuwakilishwa (Right to legal representation) na haki ya kupewa dhamana (Right to bail): Raisi akikuweka kizuizini hakuna haki utakayopewa na wala hakuna ambaye anaweza kumkemea kwanini ameweka mtu kizuizini kwasababu sheria za nchi ndizo zimempa nguvu ya kufanya hivyo.

Ukisoma historia ya Tanzania na kufuatilia siasa za nchi hii kwa ukaribu utafahamu kwamba mwanya huu ndiyo ulitumiwa na Raisi Julius Kambarage Nyerere katika kumuweka Raisi mwenzake kizuizini Aboud Jumbe Mwinyi kwa kutumia mwamvuli wa usalama wa Taifa (National Security). Kisheria jambo alilofanya Raisi Nyerere lilikuwa sahihi kabisa kwasababu lilikuwa ndani ya mamlaka ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano. Adhabu ya kuwekwa Kizuizini au Kupelekwa Uhamishoni inatolewa kwa kufuata utashi (Personal Discretion/Pleasure) wa Raisi aliyeko madarakani, hivyo akiamua ufie kizuizini utafia kizuizini kama ambavyo ndugu Aboud Jumbe Mwinyi alifia kizuizini. Ukiwekwa kizuizini na Raisi hakuna suala za Kukata Rufaa (Right to Appeal) wala hutapelekwa mahakamani baada ya masaa 24.

Mnaweza kupuuza hili na kudhani kwamba haliwezi kutokea, lakini waswahili husema Usipoziba ufa utajenga ukuta. Ndiyo, Raisi anaweza kupewa kinga ya kutoshitakiwa mahakamani lakini hana kinga yoyote endapo mamlaka mpya itaamua kumuweka Kizuizini kwa muda ambao itataka yenyewe kama ambayo Raisi Aboud Jumbe Mwinyi alifanywa: Mamlaka hii siyo lazima iwe imetoka upinzani bali hukohuko Chama Cha Mapunduzi. Mamlaka ya Raisi kuweka mtu kizuizini kwa mwamvuli ya Usalama wa Taifa ni makubwa, hatari na inabidi yaangaliwe upya, maana yanafanya hata hiyo kinga ya Raisi anayeondoka madarakani kutokuwa na umaana wowote ule.

Kuna mwandishi wa habari alishawahi kusema hivi "Wanasiasa wa Afrika hutunga sheria ambazo mwisho wa siku huja kuwafunga wenyewe": Leo hii anaweza akaingia Raisi mwendawazimu na mwenye kisirani na hiyo kinga ya maraisi waliopita ikawa haina umaana wowote ule. Kama tunataka kumlinda Raisi hata baada ya kutoka madarakani basi tuhakikishe kwamba Ibara ya 46 ya Katiba inafanyiwa marekebisho kwamba Raisi hatashitakiwa kwa jinai yoyote au madai, lakini pia hatawekwa Kizuizini (Security Detention) au Kuhamishwa (Deported) kwa mwamvuli wa usalama wa Taifa (National Security) au Maslahi ya Ummah (Public Interest) bila chombo maalumu kupima uzito wa kosa alilofanya.

Ninalolisema lilifanyika kipindi cha vita ya pili kule visiwani Uingereza, Waziri Mkuu (Prime Minister) na Waziri wa Vita (Secretary of War) walipewa mamlaka ya kukamata mtu yoyote ambaye walihisi anafanya hujuma na uzandiki dhidi ya taifa la Uingereza kwa kushirikiana na Wajerumani. Wageni na wenyeji wengi waliohisiwa tu kama wanafanya hujuma yoyote dhidi ya Uingereza waliwekwa ndani mara moja: Lakini baada ya kuona kwamba hizi nguvu zinaweza kutumika vibaya kisiasa na watu wasio na hatia wakaumizwa, Bunge la Uingereza liliamua kuanzisha mahakama maalumu (Special Tribunal) mbayo itakuwa inapima uhusika wa hao raia ambao wanatuhumiwa kuhujumu taifa la Uingereza. Hii ilisaidia kuleta uwianisho baina ya haki za raia na usalama wa taifa la Uingereza.

Binafsi ninapenda haya mamalaka ya Raisi kuweka mtu kizuizini kwa mwamvuli wa Usalama wa Taifa na Maslahi ya Ummah yafutwe kabisa maana huwa yametumika vibaya kisiasa. Lakini kwasababu najua watawala wetu hawawezi kufanya hivyo kwasababu zao, nashauri Raisi aunde chombo maalumu na huru kitakachohusika na kutoa mwongozo wa adhabu ya mtu kuwekwa Kizuizini au kupelekwa Uhamishoni. Tukiyaacha haya mamlaka makubwa yafanywe kwa utashi wa Raisi peke yake basi watu wanaweza kuozea Kizuizini.

Hakuna anayefahamu kesho itakuwaje na nani atakuwa Mkuu wa nchi pale Chamwino Dodoma na atakuwa ni mtu wa aina gani. Mahakamani huwezi kushitakiwa kwasababu sheria inakulinda, lakini unaweza kujikuta unamalizia uzee wako Kizuizini bila kupewa haki yoyote ile na hata ukasema ni heri ungeshitakiwa mahakamani maana kuna ahueni.
 
Usiwaamshe waliolala. Japo JPM hana mpango wa kuacha kuwatumikia Watanzania...." Nimejitoa maisha yangu ( yote!?!?) kuwatumikia Watanzania..."
 
Ni kweli kabisa......

Mimi nimewahi kulisema hili mara baada ya kutungwa sheria hapa juzi kati za kuwawekea kinga Spika, Jaji Mkuu na Waziri mkuu ukiachilia mbali Rais...

Nikasema, huu ni ujinga mwingine wa binadamu wa kudhani kuwa HUKUMU ya dhambi au uovu au ubaya uliowatendea wengine unaweza kufunikwa na sheria zilizobuniwa na kutungwa na waovu hao hao...!

It's impossible.!

Kila aliyefanya ubaya dhidi ya binadamu mwenzake au dhidi ya watu wa Mungu, ni SHARTI ALIPIE GHARAMA YA UOVU WAKE sasa ama baadaye kidogo...

Hii ni kanuni ya asili, hakuna anayeweza kuikwepa hata kidogo....

Kuikwepa hii, ni kwa njia moja tu ama kwa kiingereza inasemwa; Is a one way traffic...

Nayo ni kwa wote waliopewa MAMLAKA na NGUVU ya kutenda na kuamua kwa ajili ya watu wote KUTENDA KWA HAKI kila wanaloliamua, baasi....

By all means, there's no other way round, si sheria ya kujikinga wala nini isipokuwa ni KUTII SHERIA YA MUNGU na KUTENDA HAKI tu....!!
 
Wananchi wa Tanzania ndio Wana mamlaka ya kumfanya chochote kile sio yeye kutufanyia chochote atakavyo ,sisi tuliowengi ndio wenye nchi
IMG_20200910_181034_6.jpg
 
Back
Top Bottom