Kikao cha NEC-CCM ngoma nzito Dodoma

jamadari

JF-Expert Member
Feb 13, 2010
295
92
MKUTANO wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), umeanza mjini hapa ukiwa umefunikwa na usiri mkubwa kutokana na mambo mazito yanayojadiliwa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba. Tofauti na mikutano iliyopita, safari hii hali inaonekana kuwa tete huku wajumbe wa wakionekana kutopenda kuzungumza lolote kwa wazi kuhusiana na mjadala wa ajenda za mkutano huo. Katika hali ambayo inadhihirisha kuwa mambo si shwari katika mwenendo mzima wa mkutano huo jana habari kutoka ndani ya kikao na ambazo hata hivyo, hazikuthibitisha mvutano wa Mbunge wa Igunga Rostam Aziz na Spika wa Bunge Samuel Sitta lilitikisa huku baadhi ya wajumbe wakiwataka wafanye suluhu ili kusudi mvutano wao unaokitikisa chama uishe. Mnamo saa 12:15 hivi jioni Spika Sitta, Mbunge wa Kyela Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango Malecela walitoka ndani ya chumba cha mikutano na kukaa kwenye chumba kimoja kwa pamoja wakijadili jambo linaloonekana kuwa ni zito kwa muda wa takribani saa nzima. Baada ya kuketi pamoja kwa muda huo, baadaye waliamua kuingia ndani ya kikao, haikufahamika kama waliitwa au la, lakini alianza kuingia Dk Mwakyembe akifuatiwa na mama Kilango na baadaye Spika Sitta. Saa moja usiku umeme ulikatika kwa dakika kama kumi hivi, lakini hakuna hata mjumbe aliyetoka ndani kwenda nje badala yake walibaki chumba cha mkutano na taa zikaingizwa huku walinzi wakiwasukumizia mbali baadhi ya watu waliokuwa na hamu ya kusikiliza nini kilijiri. Awali, Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete aliingia ukumbini katika jengo la White House saa 8:55 mchana. Punde alipoingia ukumbini alifungua mkutano baada ya kupewa taarifa kuwa idadi ya wajumbe ilikuwa imekamilika. Katibu Mkuu wa CCM Yusuf Makamba, alimwambia Rais Kikwete kwamba, idadi kamili ya wajumbe ilikuwa 211, lakini waliohudhuria katika kikao hicho walikuwa wajumbe 205 sawa na asilimia 97 ya wajumbe wote. "Mheshimiwa mwenyekiti idadi kamili ya wajumbe katika kikao hiki ni 211, lakini waliohudhuria hadi sasa ni wajumbe 205 hivyo mkutano huu ni halali naomba kukukaribisha ili ufungue," alisema Makamba. Baada ya kusomewa idadi hiyo, tofauti na siku zote Kikwete alitamka neno moja akisema: "Nimefungua" huku akiwa amekaa, kabla ya kuwaomba wajumbe wasimame kwa dakika moja kwa ajili ya kumkumbuka Rashidi Kawawa (Simba wa Vita). Mkutano huo ulio chini ya Mwenyekiti wa CCM Kikwete na kuhudhuriwa na wenyeviti wote waliomtangulia, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi unajadili ajenda kuu tatu ambazo ni kupokea na kujadili taarifa ya hali ya kisiasa nchini, taarifa ya Kamati ya Mzee Mwinyi na Uchaguzi wa kuziba nafasi mbili za wajumbe wa Nec. Mkutano wa Nec ambao ni wa siku mbili (kuanzia jana na leo), ulitanguliwa na kikao cha siku moja cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika juzi, ambacho pia kilitanguliwa na Kamati ya Maadili. Wadadisi wa mambo ya kisiasa ndani ya CCM, wanaona kuwa Nec ndiyo itatoa taswira na mwelekeo wa chama katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu; hasa baada ya kujadili kwa kina taarifa ya kamati ya mzee Mwinyi. Miongoni mwa mambo ambayo yanatarajiwa kuibuka katika ripoti ya Mwinyi ni jinsi ya kuwashughulikia wanachama wao waliochafuka kwa tuhuma za ufisadi ambao wamekuwa wakionekana kukichafua chama hicho. Baadhi ya wadadisi wa mambo wanaona mtu kama Andrew Chenge, ambaye amekuwa akituhumiwa kuhusika katika kashfa ya rada angepaswa kuvuliwa nafasi yake ya uenyekiti wa Kamati ya Maadili ya CCM. Chenge, amekuwa akipata upinzani kutoka kwa kundi linaloitwa la wapiganaji, ambalo linaona kuwa tuhuma zinazomkabili zinamfanya akose sifa ya kuongoza chombo hicho. Wengine ambao wako katika mvutano huo ingawa walivuliwa nyadhifa zao ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Nazir Karamagi na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ambao wanatuhumiwa katika kashfa ya mkataba tata kati ya Kampuni ya Richmond Development (LLC) na Tanesco, uliosainiwa Juni 23, 2006. Kuzimwa ghafla kwa sakata hilo bungeni, kunaangaliwa na wadadisi wa mambo kama hatua ya kuachia chama kiamue hatima ya waliotajwa katika mkataba wa Richmond, ikiwezekana kuwavua nyadhifa au kuwaonya na kuhakikisha chama kinakuwa na umoja. Hata hivyo, baadhi ya wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaangalia upande wa pili wa shilingi na kuamini kwamba, huenda NEC ikakosa nguvu zaidi ya ilivyotarajiwa kutokana na kutanguliwa kwa vikao vyenye nguvu ambavyo vimepunguza makali ya wajumbe. Kwa kawadia Nec, hupokea ajenda ambazo zinakuwa tayari zimeshapitishwa na CC na kutoa mapendekezo yao pamoja na kuwa na nguvu. Lakini, habari za uhakika zilizolifikia Mwananchi, zilifafanua kwamba Kamati ya mzee Mwinyi ingetoa taarifa ambayo tayari inadaiwa kuchambuliwa pamoja na misimamo ya baadhi ya wajumbe kulegeza kutokana na maazimio yaliyofikiwa na Bunge katika kulimaliza sakata la Richmond. Kwa upande wa taarifa ya hali ya kisiasa huenda ikaibuliwa hoja ya kujadili juu ya Chama Cha Jamii (CCJ), pamoja na misimamo ya CCM kuhusu ujio wa chama hicho ambacho hadi sasa kimezusha sintofahamu miongoni mwa wana- CCM na Watanzania kwa ujumla. Hadi sasa hakuna taarifa rasmi kuhusu nani hasa wahusika wakuu wa CCJ kutokana na kuwepo taarifa tata zinazohusisha watu mbalimbali ndani ya CCM na mfumo unaongoza nchi. Baadhi ya taarifa zimekuwa zikihusisha CCJ na kambi ya wapambanaji wa ufisadi ambao wanadaiwa kuwa wanajiandaa kujitoa kama watuhumiwa wa ufisadi hawatashughulikiwa ndani ya CCM na kuvuliwa nyadhifa zao. Lakini, upande wa pili CCJ inadaiwa kuandaliwa na mafisadi kwa lengo la kuwafanya wapambanaji hao kuonekana wamesaliti chama chao (CCM). Hata hivyo, Spika Sitta amekwisha weka bayana kwamba, hawezi kuzuia watu kusema kuhusu yeye kuhusika na chama hicho na kuhoji kwamba, kuna ubaya gani chama hicho kusajiliwa. Suala la makubaliano ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Visiwani), Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, kuhusu mustakabali wa kisiasa visiwani humo pia limekuwa likitarajiwa kujadiliwa kwa kina ili lisikinzane na katiba na mwongozo wa CCM. Hivi sasa Wazanzibar wanatarajia kuundwa kwa Serikali ya Mseto baada ya Seif na Karume kuafikiana kuleta amani visiwani humo na tayari suala hilo limefikishwa kwenye Baraza la Wawakilishi. Kuhusu uchaguzi, moja ya nafasi zinazozibwa ni pamoja na nafasi ya Sophia Simba ambaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho (UWT), ambapo alikata tiketi ya kuwa mjumbe moja kwa moja. http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=17959
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom