beth
JF-Expert Member
- Aug 19, 2012
- 3,879
- 6,356
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk Khamis Kigwangalla amewapa siku 60 viongozi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya (MRH) wawe kununua mashine ya CT-scan.
Dk Kigwangalla alitoa agizo hilo, baada ya kuwasili jijini Mbeya ghafla na kwenda moja kwa moja kwenye hospitali hiyo na kupokea taarifa iliyoeleza pia kwamba ni ya kanda, lakini haijawahi kupata mashine za CT scan.
Kukosekana kwa CT-scan kumesababisha wagonjwa kwenda Dar es Salaam au watumie mashine ya mtu binafsi iliyofungwa jijini hapa miaka miwili iliyopita.
“Haingii akilini mtu binafsi hapahapa Mbeya anamiliki CT-scan, lakini hospitali kubwa kama hii imekosa,”alisema.
Dk Kigwangalla alishangazwa zaidi aliposikia kuwa mapato ya hospitali hiyo ni zaidi ya Sh500 milioni kwa mwezi.
“Sasa nawapa siku 60 nataka kuona mashine hiyo imefungwa, vinginevyo mtakuwa mmeshindwa kazi, nitakula sahani moja na nyie viongozi,” alisema.
Aliwataka watumishi wa hospitali hiyo kuwa na mawazo chanya kwa maendeleo na kutoa mfano wa CT-scan nzuri na ya kisasa kama ile iliyonunuliwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MHN) inauzwa Sh3 bilioni jambo ambalo wanaweza kulitekeleza badala ya kusubiri Serikali iwapelekee.
Awali, Mkuu wa Kitengo cha Maabara cha hospitali hiyo, Abednago Mwakila alisema mbali ya kukosa mashine hiyo kwa miaka yote, nyingine zilizopelekwa hapo hazifanyi kazi baada ya kuharibika na hawajui mafundi wanapatikana wapi.
Alitoa mfano wa mashine ya kuangalia mgando wa damu aliyodai ni kifaa muhimu, lakini haifanyi kazi kwa zaidi ya miaka minne kutokana na kukosekana kwa fundi.
Baada ya kuelezwa hivyo, Dk Kigwangala aliuagiza uongozi wa hospitali hiyo kuorodhesha mashine ambazo hazifanyi kazi na kumpelekea ofisini aweze kufanya utafiti na kubaini watu walioingia mkataba na Serikali wapeleke mashine hizo.
Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Idsory Thomas alisema agizo lililotolewa na Dk Kigwangalla litatelekezwa kwa wakati.