Return Of Undertaker
JF-Expert Member
- Jun 12, 2012
- 4,572
- 26,883
Na KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
MAHAKAMA imemuachia huru mfanyabiashara Naeem Adam Gire, aliyekuwa akikabiliwa na makosa mawili, likiwamo la kughushi hati ya uwakilishi wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, hapa nchini.
Uamuzi huo, uliotolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Cyprian Mkeha, umekuja baada ya Serikali kushindwa
kuthibitisha mashitaka hayo dhidi ya Gire.
Hii ni mara ya pili kwa mshtakiwa huyo kuachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa huyo alikuwa akidaiwa Machi 13, 2006, Dar es Salaam, kwa nia ovu, alighushi hati ya uwakilishi (Power of Attorney) ya siku hiyo, kuonesha Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas ya Marekani, Mohamed Gile, amemteua kuiwakilisha kampuni hiyo hapa nchini.
Pia alikuwa akidaiwa Machi 20, 2006, eneo la Umeme Park, Barabara ya Morogoro, Dar es Salaam, kwa nia ovu alitoa hati hiyo ya uwakilishi kwa maofisa wa Serikali iliyokuwa ikionyesha imesainiwa na Mohamed Gile.
Katika uamuzi wake jana, Hakimu Mkeha alisema baada ya kusikiliza utetezi wa mshtakiwa huyo kama ilivyoelekezwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, amejikuta akifikia uamuzi wa kumwachia huru mshitakiwa huyo kama ilivyokuwa kwa hakimu wa awali.
Alisema mwaka 2011, mahakama hiyo ilimwachia huru mshitakiwa huyo baada ya kumuona hana kesi ya kujibu, hata hivyo, upande wa Jamhuri haukuridhika na kukata rufani.
Kwa sababu hiyo, Mahakama Kuu ilielekeza mshtakiwa ajitetee kwa makosa mawili, la kwanza na la pili kwa kuwa haikuwa sahihi kuachiwa bila kuwasilisha utetezi wake dhidi ya makosa yaliyokuwa yakimkabili.
Hakimu Mkeha alisema mshitakiwa aliposomewa hati ya mashtaka hayo alikana, ambapo upande wa Jamhuri ulileta mahakamani hapo mashahidi tisa na vielelezo sita.
Alisema msingi wa mashtaka kwa upande wa Jamhuri ulikuwa kwenye kile kilichofanywa na shahidi, ambaye ni mtaalamu wa maandishi.
Mtaalamu huyo ndiye aliyeonesha ulinganifu uliofanywa kati ya saini inayobishaniwa inayodaiwa ya Gire iliyoko kwenye hati ya uwakilishi na nyaraka ambazo zina saini yake.
Hakimu Mkeha alisema katika ushahidi wake, shahidi huyo alidai aligundua saini hizo zimetiwa na watu tofauti.
Kwamba ile inayobishaniwa ni ya Gire na kwa upande wa mshtakiwa aliwasilisha nyaraka zenye saini zake halisi, ikiwamo cheti cha ndoa.
Alisema mahakama hiyo katika kufikia uamuzi wake, ilijiuliza swali moja ambalo ni kwa namna gani mwandiko au saini ya mtu inaweza kusemekana imethibitika ni ya X na wala si ya Y.
Alisema kuna uthibitisho wa moja kwa moja ambao ni wa kuja mtu fulani kusema amemwona mtu fulani akiandaa nyaraka, hata hivyo, ni nyaraka chache ambazo zinaweza kuthibitishwa kwa namna hiyo.
Alisema katika kesi hiyo, vitu ambavyo walitakiwa kuchunguza ni saini za mshtakiwa na mwandiko wake ili waweze kulinganisha na hiyo iliyoko katika nyaraka inayodaiwa imeghushiwa.
Hakimu Mkeha alisema alijikuta anatoa uamuzi kama wa hakimu wa awali, kwamba mashitaka dhidi ya mshitakiwa hayajathibitishwa, hivyo anamwachia huru na kwa wale ambao hawajaridhika wana haki ya kukata rufani.
Akizungumza baada ya kutolewa uamuzi huo, Wakili Alex Mgongolwa, anayemtetea mshtakiwa huyo, alisema amefurahi sana kwa mteja wake kuachiwa na haki imetendeka katika shauri hilo, licha ya kuchukua takribani miaka saba.
Alisema mahakama imeweza kuangalia vizuri upungufu uliokuwapo kwenye shauri hilo.
Uamuzi huu kwa upande wa Mahakama umekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya sakata hilo lililogharimu uwaziri mkuu wa Edward Lowassa mwaka 2008, kuibuka tena bungeni.
Sakata hilo liliibua mzozo kati ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.
Mwakyembe, ambaye aliongoza Kamati ya Bunge kuchunguza sakata hilo mwaka 2008, alishutumiwa na Nassari kwa kitendo cha kamati yake kutomhoji Lowassa wakati kamati yake ikifanya uchunguzi na kisha kuandaa ripoti yake.
Akijibu hoja hiyo, Mwakyembe alisema hakuona umuhimu wa kumhoji Lowassa, kwa kuwa ushahidi ulikuwa wazi.
Mwakyembe hakuishia hapo, hata wakati akichangia hotuba za wizara, alisema wapinzani wanataka kumsafisha Lowassa na kushauri waliwasilishe upya suala hilo na yeye yupo tayari kuuacha uwaziri ili alishughulikie.
Kwa maneno yake, alisema yeye binafsi anaelewa ni kazi ngumu kumsafisha Lowassa na kesi ya Richmond iliishakwisha.
Alisisitiza kuwa, wakati wakiwasilisha ripoti kuhusu sakata la Richmond bungeni walikuwa na mashahidi 40 waliokuwa wakiwasubiri nje.
Alisema kamati yake ilikuwa imepata nyaraka za Serikali 104, walihoji watu 75 na waliwauliza maswali 2,717 na kwamba kumbukumbu hizo zote zipo kwenye nyaraka za Bunge.
“Hatukuona sababu ya kumhoji Lowassa, tulikuwa na ushahidi wote, mimi niombe mwenyekiti kama kuna mtu bado anakereketwa na kesi ya Richmond alete hapa kama hatujawanyoa kwa vipande vya chupa,” alikaririwa Mwakyembe juzi bungeni, ambapo pia mara kadhaa amekuwa akisisitiza kuwa Kampuni ya Richmond ni hewa.
Sakata la Richmond, ambalo linatajwa kuwa na sura nyingi, lilimlazimisha aliyekuwa Rais wa awamu wa nne, Jakaya Kikwete, kufanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri kwa mara ya kwanza mwaka 2008, baada ya Lowassa kujiuzulu.
Katika mabadiliko hayo, Kikwete alilazimika pia kuwaondoa mawaziri wake wawili, Nazir Karamagi aliyekuwa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na mtangulizi wake, Dk. Ibrahim Msabaha.
Mara kadhaa Lowassa mwenyewe amekaririwa akisema suala la Richmond lilipikwa kumchafua.