Kifo cha Christina Corrigan: Je ni kubukanya au ni ugonjwa wa kurithi…?

Mtambuzi

Platinum Member
Oct 29, 2008
8,810
15,398

_46299_christina.jpg

Christina Corrigan
christinalgtxt.gif


_46299_marlene.jpg

Mama wa Christina, Marlene Corrigan


Ilikuwa ni majira ya mchana hapo mnamo Novemba 15, 1996 kitengo cha dharura cha mji wa El Cerrito, mji uliopo katika jimbo la California kilipokea simu ya dharura ya kuomba msaada kutoka kwa mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Marlene Corrigan akiwajulisha kwamba binti yake amepoteza fahamu na ameshindwa kumsaidia. Muda mfupi baadae Polisi na watu wa huduma ya dharura walipofika katika nyumba hiyo aliyokuwa akiishi mama huyo. Ukweli ni kwamba, walishtushwa na hali waliyokutana nayo.

Mwili wa Christina Corrigan ulikuwa umelala pale sebuleni mbele ya televisheni iliyokuwa imefunguliwa kwa sauti kubwa. Mwili ule ulikuwa uko uchi ukiwa umefunikwa na blanket lakini ukiwa umezungukwa na vyakula mbalmbali kama Pizza na lita mbili za Ice cream.

Mwili wake ulikuwa umeweka alama za michirizi ya kulala kwa muda mrefu kitandani na ulikuwa unanuka harufu kali ya kinyesi na mikojo. Lakini kilichowashangaza wataalamu wale wa huduma ya kwanza ni ukubwa wa mwili wa binti yule, kwani iliwachukua watu kumi kumudu kuuondoa mwili wa binti yule kutoka hapo nyumbani kwao na kuupelekea kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Kwa mujibu wa ripoti ya mtaalamu wa kuchunguza maiti, ilionyesha kwamba, Christina alikufa kutokana na moyo wake kushndwa kufanya kazi ghafla na hali hiyo ilitokana na uzito uliopitiliza aliokuwa nao binti huyo. Kwa umri wa miaka 13 aliyokuwa nayo wakati umauti ulipomfika alikuwa na uzito wa kilo 308, na unene wa mapaja yake ulikuwa na ukubwa wa sentimita 127 kila moja.

Kwa upande wa polisi, ukubwa wa umbo la mwili wake na aina ya maisha aliyokuwa akiishi, uliwashawishi kumfungulia mama yake mashitaka ya unyanyasaji wa mtoto wake wa kumzaa mwenyewe. Walimuuliza mama wa binti huyo, Marlene Corrigan, iwapo hakuona kuwa unene wa binti yake unaweza kuwa ni hatari kwa afya yake. Aliwajibu Polisi kwamba, alijua kuwa mwanaye yuko katika hatari kiafya lakini juhudi zake za kumsaidia hazikuonekana kuzaa matunda.

Afisa mmoja wa Polisi aliandika katika ripoti yake, "Mama huyu alitarajia kwamba mwanaye Christina Corrigan ataamua mwenyewe kuacha kula kupita kiasi…"

Mama huyo alikiri kwamba mwanaye Christina hakupata kumuona daktari kwa zaidi ya miaka miwili. Alihalalisha jambo hilo kwa kudai kwamba, mwanaye huyo alikuwa na Hasira za ziada zinazohusisha kuvunja vitu, hivyo pale anapotajiwa kupelekwa hospitali, alikuwa akifanya vurugu hapo nyumbani. Kuhusiana na hali mbaya ya uchafu aliyokutwa nayo binti yake, mama huyo alidai kwamba, Christina aliongezeka uzito kiasi cha kushindwa kunyanyuka kitandani kwake na kwenda chooni kujisaidia, hivyo alikuwa akimalizia haja zake hapo hapo kitandani kwake.

Makamu Mwanasheria wa wilaya ya Contra Costa jimboni California, Brian Hayes aliagiza mwili wa binti huyo ufanyiwe uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo na sababu ya kifo chake, na pia Polisi wa upelelezi waangalie historia ya maisha ya binti huyo na mama yake ili kuujua ukweli.

Mwanasheria huyo aliwaacha waandishi wa habari na wasiwasi kama kweli angeweza kumshitaki mama wa mtoto huyo. "hakuna mlezi yeyote anayeweza kuepuka kushitakiwa kwa kumwacha mtu afe kifo cha aina ile," alisema mwanasheria huyo. "Tumeshaona vifo vya aina hii kwa watu wazima, lakini hii ni mara yangu ya kwanza kuona kifo cha aina hii kwa mtoto…" alimalizia kusema mwanasheria huyo.

Ofisa mmoja katika ofisi ya mwanasheria wa wilaya hiyo, alitembelea kituo cha ustawi wa jamii na kugundua kwamba, Christina Corrigan hakuwa mgeni katika kituo hicho. Mnamo mwaka 1989 wakati huo binti huyo akiwa na miaka mitano, ofisa mmoja wa ustawi wa jamii wa kituo hicho alipokea simu kutoka kwa mtu ambaye hakutaka kujitambulisha, akawajulisha kwamba, yupo binti hapo mtaani kwao aliyemtaja kwa jina la Christina Corrigan, ambaye anaongezeka uzito kwa kasi sana na mama yake ana kawaida ya kumlisha kupita kiasi vyakula mbalimbali maarufu kama Junk Food nchini Marekani.

Afisa huyo wa ustawi wa jamii alifanya uchunguzi kwa kufuatilia taarifa hizo na ndipo alipoambiwa na mama wa mtoto huyo kwamba binti yake anatibiwa katika hospitali ya Kaizer Medical Centre, hospitali iliyopo katika eneo la Richmond jimboni California. Mama huyo alidai kwamba binti yake amekuwa akihudhuria hospitalini hapo mara kwa mara na kuonana na mtaalamu wa lishe (nutritionist) mara mbili kwa wiki. Afisa huyo wa ustawi wa jamii aliamini kwamba, mama huyo analifanyia kazi tatizo la mwanaye, hivyo kesi yake ilifungwa.

Hata hivyo Marlene Corigan, baadae wakati alipokuwa kihojiwa na afisa wa ustawi wa jamii alikiri kwamba aliacha kumpeleka mwanaye hospitalini hapo kumuona mtaalamu wa lishe kwa sababu kila mbinu aliyoshauriwa na mtaalamu huyo haikuweza kufanya kazi.

Mpaka kufikia mwaka 1991 ndugu wa karibu walianza kuingiwa na wasiwasi kutokana na hali ya afya ya Chistina. Dada wa Marlene aitwae Sandy Bickers aliwafahamisha maafisa wa ustawi wa jamii kuhusu afya ya mtoto Christina. Ilikuwa ni mara baada ya kutoka katika safari yao ya kutembelea mbuga ya wanyama ya Yosemite, alipokwenda akiwa na dada yake Marlene pamoja na binti yake Christina. Aliwaambia maofisa hao wa ustawi wa jamii kwamba, wakiwa huko, baada ya kumaliza kula mlo wao wa mchana, dada yake alimnunulia binti yake huyo aliyekuwa na umri wa miaka saba wakati huo Mikate mitatu ya nyama (Hamburgers) pamoja na bakuli tatu za tambi (Spagheti) kama vyakula vya kutuliza njaa jioni kabla ya chakula cha usiku.

Pamoja na ukweli kwamba binti huyo alikuwa ana uzito wa kilo 113, lakini mama yake alikuwa akimlisha vyakula vingi kupita kiasi bila kujali hali ya afya yake. Hata hivyo maafisa hao wa ustawi wa jamii hawakufuatilia taarifa hizo.

Christina aliendelea kukua kwa umri na kimo huku umbo lake likiendelea kuwa kubwa kiasi cha kutisha, lakini pamoja na hali yake hiyo, alikuwa ni binti mwenye akili shuleni kuliko kawaida. Akiwa darasa la sita alikuwa ni mtu wa tatu katika matokeo ya mitihani yake katika shule ya msingi ya El Cerito Fairmont, hapo mnamo mwaka 1995. Alikuwa amepangiwa kurushwa madarasa na kupekekwa moja kwa moja katika shule ya sekondari mwaka unaofuata.

Kwa mujibu wa Sandy Bickers, Christina alidai kwamba hakuweza kujiunga na shule ya sekondari kama alivyopangiwa, kutokana na kushindwa kwake kupandisha kimlima kidogo ili kufika shuleni hapo. Taarifa nyingine iliyopatikana iliyomfanya ashindwe kuendelea na masomo yake ni kutokana na wanafunzi mwenzie kumtania kupita kiasi. "Kila mmoja alikuwa anamdhihaki kupita kiasi." Alisema Hector Rodriguez, mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo aliyokuwa akisoma Christina. "Wakati wanafunzi mwengine wanaposhindwa kumalioza vyakula vyao, walikuwa wakimpa na yeye alikuwa anavichukua na kuvihifadhi kwenye begi lake la shule kwa ajili ya kuvila baadae…" Aliongeza mwanafunzi huyo.

Polisi wa upelelezi walitaka kufahamu, ni kwa nini kutohudhuria shuleni kwa Christina hakukuripotiwa katika vyombo vinavyohusika. Paul Ehara, msemaji wa shule aliyopangiwa kusoma binti huyo, alisema kwamba, alimuita mama yake Christina, siku chache baada ya uandikishwaji wa wanafunzi na alipomuuliza kwa nini binti yake hajaripoti hapo shuleni kama alivyopangiwa, mama huyo alimjibu kwamba, anamsomeshea binti yake nyumbani. Msemaji huyo alipoulizwa na askari wa upelelezi kama walifuatilia kujua kama ni kweli binti huyo anafundishiwa nyumbani kama mama yake alivyodai, msemaji huyo alikiri kwamba, hakufuatilia. "Naamini kwamba uongozi wa shule unafanya jitihada kubwa kutoa elimu kwa wanafunzi, lakini hufanya hivyo kwa wanafunzi wanaofika shuleni na si vinginevyo." Alisema msemaji huyo.

Wakati ilikuwa ni dhahiri kwamba Marlene Corrigan mama wa miaka 48 wakati huo, ambaye hakuwa na mume (Single Mother) alishindwa kumtunza mwanaye kama mzazi atakiwavyo kumlea mtoto wake, lakini pia ilionekana kwamba, hata mamlaka zinazohusika zilishindwa kumsaidia mama huyo. Jirani yake mmoja akiongea kwa hasira aliwaambia Polisi kwamba, anaamini Marlene Corrigan alikuwa ni mama mwema aliyejaribu kufanya kila linaloweza na kila lililokuwa ndani ya uwezo wake kumsaidia mwanaye lakini jitihada zake zilionekana kushindwa. "Muuguzi wa shule yuko wapi?" aliuliza mama huyo. "Wako wapi maofisa wa ustawi wa jamii? Taasisi zote zinazohusika zilishindwa kumsaidia mama huyu, na hakutokea mtu mwingine kumsaidia?"

Pamoja na kuonekana watu kumtetea, lakini, hali hiyo haikuonekana kubadili adhma ya makamu mwanasheria wa wilaya Brian Hayes kumshitaki mama huyo. Marlene Corrigan alifunguliwa mashitaka ya unyanyasaji wa mtoto wake mwenyewe wa kumzaa kwa kumuacha bila ungalizi kiasi cha kumsababishia kuongezeka uzito kupita kiasi na hivyo kusababisha kifo chake. Mashitaka hayo yamebeba hukumu ya kifungo cha miaka sita jela.

Kuanzia mwanzoni mwa usikilizwaji wa kesi hiyo, ilionekana kuvutia hisia za watu wengi nchini Marekani. Kwa upande wa magazeti ya udaku na vyombo vingine vya habari nchini humo, kesi hiyo ilionekana kuchukuliwa kisiasa zaidi, kwani wananchi wengi nchini humo walihoji kwamba, inawezekanaje kuwa na mtoto mnene iwe ni kosa? Wakati Marlene alipofikishwa katika mahakama ya manispaa ya El Carito hapo mnamo Agosti 7, 1997,alikuta umati mkubwa wa watu wakisubiri kusikilzwa kwa kesi yake. Mwanasheria aliyekuwa akimtetea , Michael Cardoza, alikanusha masitaka yake, na kesi hiyo iliahirishwa hadi hapo baadae, itakaposikilizwa rasmi katika mahakama kuu.

Baada ya kutajwa kwa kesi hiyo, Judy Freespirit, muasisi wa shirikisho la watu wenye unene nchini humo, (National Association to Advance Fat Acceptance), alielezea juu ya taasisi yake kusikitishwa na mashitaka hayo dhidi ya Marlene Corrigan. "Tunataka kuhakikisha kwamba hii siyo kesi, kwamba mama anashitakiwa kwa sababu eti ana mtoto mnene, kwanza siyo kosa mtu kuwa mnene, na siyo kosa kuwa na mtoto mnene." Alisema mama huyo.

Hata hivyo Makamu Mwanasheria wa wilaya Brian Hayes alikanusha madai hayo vikali, "Hatukumshitaki mzazi wa binti huyo eti kwa sababu binti yake alikuwa ni mnene. Tunamshitaki kwa sababu hakumlea binti yake ipasavyo kama mzazi."

Nje ya mahakama hiyo Marlene Corrigan na Mwanasheria wake walisimama na kuongea kwa kifupi na wanahabari waliokuwa wamesimama nje ya mahakama hiyo kuwasubiri. "Wanasema alimuweka binti yake katika hatari." Alisema Michael Cardoza, mwanasheria wa mama huyo. "Huyu mama hana makosa. Alijitahidi kadiri ya uwezo wake kumlea mwanaye, lakini hii ni miongoni mwa zile kesi ambazo watu humwangalia mtoto mwenye unene kupita kiasi na kuuliza. ‘Inakuwaje mzazi anamuacha mtoto anakuwa mnene kiasi hicho?' Na hapo hutafuta mtu wa kumlaumu."

Marlene alisimama tena katika mahakamani kuu ya wilaya ya Contra Costa hapo mnamo Januari 1998. Utetezi wake ulikuwa ni kwamba alikuwa hana uwezo wa kumdhibiti mwanaye asiendelee kuongezeka unene kupita kiasi.

Wakili aliyekuwa akimtetea mama huyo Bwana Michael Cardoza, akitoa taarifa za kitaalamu alisema kuwa marehemu Christina Corrigan alikuwa akikabiliwa na tatizo ambalo ni adimu sana la kizalia (genetic) linalohusiana na kichocheo kinachotoa taarifa ya mtu kujisikia kushiba wakati anapokuwa anakula, kushindwa kufanya kazi. Kitaalamu hali hiyo hufahamika kama Prader-Will Syndrome (PWS). Alibainisha kwamba muathirika wa tatizo hili hujisikia kula wakati wote na anapokula huwa hatosheki kamwe, anakuwa ni mtu wa kubukanya wakati wote. Tatizo hili kama yalivyo matatizo mengine ya kizalia bado halijapatiwa tiba maalum, na wataalamu wengi wamejaribu bila mafanikio kupata tiba ya tatizo hilo.

Kwa taarifa yako wewe msomaji ni kwamba ugonjwa huo ulipewa jina hilo kwa sababu uligunduliwa na wataalamu wawili wa tiba wa Uswizi ambao walijulikana kwa majina ya Andrea Prader na Henrich Will, ndipo lilipopatikana jila la Prader-Will Syndrome (PWS). Hiyo ilikuwa ni mwaka 1956. PWS kama unavyojulikana kwa kifupi, hutokea mara chache, kwani humpata mtoto mmoja kati ya kila watoto elfu kumi au elfu kumi na tano. Wanaozaliwa kwa mwaka. Hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa nchini Marekani miaka ya hivi karibuni. Pamoja na tatizo hili la kubukanya, pia zipo dalili ambazo mtoto anaweza kuzaliwa nazo, na hizi mara nyingi hujionyesha kabla ya tatizo la kubukanya halijajitokeza. Dalili kama za mtindio wa ubongo na hasira za ziada zinazohusisha uharibifu hujitokeza dhahiri, japokuwa zipo nyingine ambazo hujitokeza kwenye maumbile ya mwili wa muathirika. Mara nyingi hutambuliwa na wataalamu wa magonjwa ya watoto. Dalili ya kubukanya mara nyingi hujitokeza kuanzia umri wa miaka mine hadi miaka sita, lakini wengine hupata tatizo hili hata baada ya miaka 20, japokuwa ni mara chache sana.

Wakili huyo aliendelea kuiambia mahakama hiyo kwamba Marlene Corrigan alifanya kila lililo ndani ya uwezo wake kumsaidia binti yake ambaye uzito wake ulikuwa ukiongezeka kwa kiwango cha kutisha tangu alipokuwa na umri wa miaka mitano. Aliongeza kwamba, pamoja na Christina kukataa kwenda hospitalini kwa uchunguzi lakini kwa mujibu wa rekodi zilizokusanywa hospitalini hapo, Christina aliwahi kutembelea hospitalini hapo mara 90 katika hospitali hiyo ya Kaizer Medical Centre.

Makamu mwanasheria wa wilaya alipinga taarifa hiyo ya kitabibu iliyotolewa na wakili Cardoza kwa kudai kwamba, Christina Corrigan hakuonyesha dalili zozote za kuwa na tatizo hilo la Prader Will Syndrome (PWS), kama vile mtindio wa ubongo, kisukari, au matatizo ya kitabia, kama kukosa adabu. Mwanasheria huyo alidai kwamba, Marlene alitakiwa kufuatilia tiba ya mwanaye, hata kama alikuwa hawezi kunyanyuka kitandani.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili katika kesi hiyo. Mheshimiwa Jaji wa mahakama hiyo Richard E. Arnason ambaye aliisikiliza kesi hiyo bila kuwa na baraza la washauri, hakumkuta mtuhumiwa na hatia ya unyanyasaji kwa binti yake, na badala yake alimkuta na hatia ya kosa dogo la kupuuzia hatari iliyokuwa ikimkabili binti yake kiafya, kosa ambalo alimkuhumu kifungo cha miezi sita jela.

Akizungumzia hukumu hiyo, Mheshimiwa Jaji Richard Arnason alisema, "hakuna ushahidi wowote katika rekodi unaoweza kunishawishi niamini kuwa, mtuhumiwa alikuwa anajua au alitakiwa kujua kwamba kitendo chake cha kutochukua hatua kuhusiana na hali ya afya ya mwanaye kungeweza kumletea mwanaye matatizo zaidi ya kiafuya au kifo."

Pamoja na mteja wake kuhukumiwa kifungo cha miezi sita kwa kosa dogo la kupuuzia hatari iliyokuwa ikimkabili binti yake kiafya, wakili Cardoza alionekana kufurahishwa na hukumu hiyo, na kwake yeye aliichukulia hukumu hiyo kama ushindi.

"Huu ni ushindi kwetu, huyu alikuwa ni mama mwema, kama huyu binti angekuwa na tatizo la kukosa hamu ya kula, labda tusingekuwa hapa, hakukuwa na ushahidi wa kumtia hatiani kwa kosa hilo, lakini tunaweza kukubaliana na kosa alilopatikana nalo na hatia, kwa hiyo mashitaka aliyofunguliwa hayakupaswa kuwepo, mashitaka yao yalikuwa yanaonekana dhahiri kuwadhalilisha watu wanene." Alisema wakili huyo.

Kauli yake hiyo ilipokelewa na watu wengi nchini humo kwa hisia tofauti kuhusiana na kesi hiyo. Hata hivyo mwanaharakati Judy Freespirit, muasisi wa shirikisho la watu wenye unene nchini humo, (National Association to Advance Fat Acceptance), alisema,

"Ni ushindi mkubwa sana kuona kwamba Marlene Corrigan haendi jela miaka sita kwa kosa la unyanyasaji kwa mwanaye, bali anakwenda jela miezi sita kwa kosa dogo la kupuuzia hatari iliyokuwa ikimkabili binti yake kiafya. Hukumu hii inatuma ujumbe kwa wazazi wenye watoto wanene kwamba, kuwa na mtoto mnene siyo kosa…….."
 
Haya ni Ijumaa nyingine tena tunakutana hapa kwa ajili ya kujifunza kwa pamoja.
Naamini kuna mengi ya kujifunza katika kesi hii..
1. Malezi
2. Afya
3. wajibu kwa mzazi
4. Maradhi yatokanayo na kizalia (Genetic)
5. Sheria zinazowalinda watoto
 
Ulaya kuna mambo kweli kweli!
Ingekuwa huku kwetu kusingekuwa na kitu kama hiki.
Yaani ni vigumu kuona mzazi anahatia hapa, kwanin hawa watu wenye matatizo haya huwa wabishi na wadai wanasikia njaa sana, kiasi mzazi kama unahuruma inabidi umpe chakula kwani wanakuwa na njaa ya kufa mtu.
Thanks Mtambuzi
 
Last edited by a moderator:
Duniua ina mambo lukumba lukumbaaa.... paloma unaukumbuka huo wimbo...

NDio malimwengu hayo ya dunia Mtambuzi shuktani..
dunia hii mama lukumbalukumba
dunia ina mambo mwendo wa ngamia

tafutaaa eee utapata yako ni yako na yangu ni yangu (mhhh sijui napatia... Jiwe Linaloishi)

hahahaa naukumbuka ni Lady Issa huyu au?
 
Last edited by a moderator:
Mtambuzi asante sana kwa nyuzi zako za Ijumaa. Ila kwa hili yaani usiombe upate mtoto anayekula kupita kiasi!!! Ila wazazi kama mtoto ni mmoja tuna ile tendency ya kumwogopa na kila kitu anachotaka unampa!!! Tujifunze si faida ni hasara. Mleee mtoto kwa njia ile ile bora ya kumsaidia.
 
Haya ni Ijumaa nyingine tena tunakutana hapa kwa ajili ya kujifunza kwa pamoja.
Naamini kuna mengi ya kujifunza katika kesi hii..
1. Malezi
2. Afya
3. wajibu kwa mzazi
4. Maradhi yatokanayo na kizalia (Genetic)
5. Sheria zinazowalinda watoto

Kweli Dunia duara,wakati wenzetu mzazi anawajibishwa kwa kutotetekeleza wajibu wake kama mzazi huku kwetu mama atakuchamba kwa kujifanya unamuingilia katika malezi ya mwanae!
 
dunia hii mama lukumbalukumba
dunia ina mambo mwendo wa ngamia

tafutaaa eee utapata yako ni yako na yangu ni yangu (mhhh sijui napatia... Jiwe Linaloishi)

hahahaa naukumbuka ni Lady Issa huyu au?

Hahahha umepatia ila siku hizi hapo kwenye changu ni changu na chako ni changu... mwendo wa swala... hahah
 
Back
Top Bottom