Kifimbo Cha Mwalimu Nyerere vs Fimbo ya Moi (Fimbo ya Nyayo)

Bujibuji Simba Nyamaume

JF-Expert Member
Feb 4, 2009
74,864
155,822
HII NDIYO SIRI YA KWA NINI MWALIMU NYERERE HAKUWA AKITHUBUTU KUVIACHA VIFIMBO VYAKE.
Unapofika katika nyumba yake iliyopo jijini Dar es Salaam maeneo ya Msasani maarufu kwa Mwalimu Nyerere, kinachoyatofautisha maisha ndani ya nyumba hiyo na zile za Magomeni na Ilala ni mazingira nadhifu.

Si urithi wa mali, isipokuwa ni mapenzi kwa binadamu wenzake na hekima ambavyo, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ameviacha katika vitabu, maandiko mbalimbali na kwa familia Yake.

Wenyeji ndani ya nyumba hii kwa mwonekano na mazungumzo hawana tofauti na Watanzania wa kawaida, hawana majivuno na wanamkaribisha mgeni kama ndugu au jamaa waliyemfahamu miaka mingi.

Pamoja na kuwa nyumba ni kubwa na wenyeji ni wengi, lakini kwenye maegesho ya magari lipo gari moja tu. Mwonekano wa nje wa nyumba hii unaweza kukufanya ufikiri ndani kuna magari zaidi ya matatu tena ya kifahari.

Wanafamilia ni wakarimu sana, kwa kawaida ungetarajia kusikia wenyeji wakitumia maneno kama "Yes, No" na maneno mengine ya Kiingereza kwa kuwa hiki ni kitambulisho cha vijana waliopata elimu angalau ya sekondari, lakini hapa ni tofauti, wote wanazungumza Kiswahili na bahati mbaya wakichanganya huwa ni lugha ya Kizanaki.

Wajukuu wa Baba wa Taifa, Moringe Magige na Julius Makongoro wanasema huu ndiyo urithi ambao Baba wa Taifa aliwaachia ndugu zake wakisema kuwa walilelewa kuamini kuwa mali siyo kitu kuliko utu na ndivyo walivyo.

MAISHA YA MWALIMU NYERERE KAMA BABU
Wengi tunafahamu historia ya Baba wa Taifa hasa katika majukumu yake ya uongozi wa Tanzania na ukombozi wa bara la Afrika, lakini Moringe na Julius wanaturudisha nyumbani wakisimulia walivyomfahamu babu yao.

Moringe anasimulia akisema; "Kwanza mimi sikufahamu kwa jinsi gani babu alikuwa mtu muhimu katika nchi hii na bara la Afrika kwa ujumla, nilijua baada ya kufariki dunia na kuanza kusoma historia yake na kugundua vitu vingi alivyofanya,"

"Sikuiona tofauti yake na mababu wengine kwani shuleni nilisikia watu wakisimulia jinsi walivyoishi na babu zao na sikuona tofauti na babu yangu," anasema Moringe.

Anasema Mwalimu Nyerere aliwapenda wajukuu zake, alipenda kufanya shughuli za shamba akiwa na wajukuu zake, hakutaka hata mmoja azembee kwenda shambani.

"Babu aliipenda familia yake, tumeishi na ndugu wengi kwa sababu hakutaka kukaa mbali na ndugu zake na kila mmoja alihakikisha anapata wasaa wa kukaa naye na kuzungumza naye, mfano alikuwa na utaratibu wa kula chakula cha jioni na sisi wajukuu zake," anasema Moringe. Aidha anasema kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa akiwahimiza kuongeza juhudi shuleni hasa katika masomo ya Kiingereza na Hisabati.

"Babu alikuwa akifuatilia maendeleo yetu shuleni, kila mwisho wa muhula alikagua matokeo ya kila mmoja wetu na alikuwa akisisitiza zaidi masomo ya Kiingereza na Hesabu akisema hayo ndiyo ya msingi," anasema Moringe.

Alikuwa anapenda kupiga makonzi
Kila mtu anakumbuka adhabu gani alikuwa anapewa na bibi au babu yake pale anapokosea, lakini Julius anatuambia kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa akiwapiga makonzi wajukuu zake pale wanapokosea.

Julius anasema adhabu kubwa waliyokuwa wakipewa na babu yao ni kupigwa makonzi hata hivyo utaokoka tu kwa juhudi zako za kutoka mbio kwani ukisimama anaendelea kukupiga. "Babu alikuwa na tabia ya kutupiga makonzi hasa ukiwa mtundu au ukimpitia karibu wakati anacheza bao lazima atakupiga japo konzi moja," anasema.

Pia anasema kamwe hatasahau siku moja alipomuomba babu yake akaangalie mkanda wa video mchana;" Nilimwambia babu tunaomba kuangalia mkanda kwa sababu Tv ilikuwa inakaa Maktaba, alinikubalia na kuniambia nenda ukawaite na wenzako unaotaka kuangalia nao. Basi nikaenda kuwaita tulivyofika alitufungia na kuanza kutupiga makonzi ," anasema Julius.

Aidha anasema babu yao aliwapangia muda maalumu wa kuangalia televisheni pia aliwachagulia mikanda ya kutazama kwa kuwa alipenda wawe na maadili mema.

Vituko,utani wa babu na wajukuu zake. Pamoja na kuwapiga makonzi wajukuu zake lakini kuna wakati alikuwa akiketi chini na kufanya utani na kushuhudia vituko vya wajukuu zake.

Moringe anasema moja kati ya maswali ya utani waliokuwa wakimuuliza babu yao ni iwapo enzi za ujana wake alikuwa akifanya starehe za aina mbalimbali.

"Tulikuwa tunamuuliza babu hivi unajua kuogelea au kucheza muziki kwa sababu hatujawahi kukuona hata siku moja ukicheza, alijibu 'siwezi', tukawa tunamuuliza sasa wewe ujana wako ulikuwa unafanya nini, alisema 'kusoma tu', anasema Moringe.

Aidha wanasema utani mwingine kwa babu yao ilikuwa ni kuwa hajui kuendesha gari. Julius anasema "Tangu nimepata akili sijawahi kumuona akiendesha gari, nina wasiwasi alikuwa hajui kuendesha". Julius pia anasema babu yake hakuwa na mazoea sana ya kuvaa suti au kuchomekea huku akisema inawezekana zamani alikuwa analazimishwa kuvaa hivyo.

"Sijawahi kumuona babu amevaa suti au amechomekea shati, hata hakupenda ndugu wavae suti hasa tukiwa Butiama, alipenda kuvaa 'simple'.

Alisisitiza maadili.
Moringe na Julius wanasema wanaamini babu yao alikuwa akilinda maadili kwa kutowaachia watazame televisheni ovyo na kuwahimiza kushiriki kanisani.

"Babu hakuwa na mchezo linapokuja suala la kanisani, yaani usipoenda kanisani ni ugomvi mkubwa anaweza hata kukufukuza usile naye chakula cha jioni," anasema Moringe.

Wakizungumzia iwapo Baba wa Taifa angekuwa hai leo angebariki matumizi ya mitandao ya kijamii kama 'facebook' na 'twitter' kwa pamoja walisema asingepinga kwani alikuwa mpenda maendeleo.

"Watu wengi huwa wanazungumza wakisema kuwa babu alikuwa hataki watu waendelee kwa kutumia teknolojia, sio kweli, babu alikuwa anapenda maendeleo lakini aliheshimu utamaduni," anasema Julius.

Akitolea mfano wa dada yao mmoja aliyekuwa akiishi Ulaya walisema, babu yao hakuwa na tatizo na mavazi yake lakini alimwonya kuwa ni lazima aangalie anavaa wapi.

"Mfano tukiwa hapa Msasani babu hakumkataza kuvaa nguo zake anazopenda, lakini tulipoenda Butiama alikuwa akimrudisha pale anapovaa nguo anazoona haziendani na utamaduni wa watu wa kule," anasema Julius.

Anaongeza kuwa Mwalimu asingekuwa na tabu na mitandao hiyo au teknolojia yoyote isipokuwa pale itakapotumikwa visivyo kama wafanyavyo wengi." Ukiukwaji wa maadili unaotokana na teknolojia unawakwaza watu wengi, watu wanatumia ndivyo sivyo na hiki pengine kingemkera babu," anasema Julius.

Siri ya kifimbo cha babu yao
Moringe na Julius wanasema wamesikia hadithi nyingi kuhusu kifimbo cha Mwalimu Nyerere alichokuwa akipenda kukibeba, wengine wamediriki kusema alizikwa nacho. Julius anasema kwanza wanavyofahamu wao babu yao alikuwa nazo zaidi ya nne, nyingine alinunua mwenyewe na nyingine alipewa zawadi.

"Babu alikuwa na fimbo nyingi, alibeba yoyote anapotoka nyumbani, wakati mwingine aliweza kuisahau na kutuagiza tumpelekee nje kama ameshatoka," anasema Julius.

Aidha Moringe anasema amewahi kusikia kuwa asili ya babu yao kutembea na fimbo hiyo ilitokana na nia yake ya kuacha kuvuta sigara. "Niliwahi kusikia babu alikuwa akivuta sigara, sasa alipotaka kuacha alipewa fimbo kama njia mbadala ya kushika kitu mkononi ili aweze kuacha," anasema Moringe.

FIMBO YA MOI (FIMBO YA NYAYO)

Moi.jpg

Fimbo ya Rais wa zamani wa Kenya, Hayati Daniel Toroitich Arap Moi ilijulikana sana kama ishara ya nguvu, uongozi na mshikamano wa kitaifa.

Fimbo hiyo liyotengenezwa kwa pembe za ndovu na dhahabu, ilibatizwa jina la 'Fimbo ya Nyayo'.

Wachambuzi wanasema fimbo hiyo ilikuwa ishara ya nguvu na mamlaka aliyopewa kutoka kwa jamii yake.

Huenda fimbo ikawa ni miongoni mwa fimbo zilizowahi kusafiri zaidi nchini Kenya, kwani aliibeba kila mahali alipokwenda. Mzee Moi hakuwahi kutokea katika kazi yoyote ndani na nje ya nchi bila fimbo yake. Mara baada ya kupanda jukwaani, aliitumia kupungia umati wa watu ambao waliitikia kwa shangwe.

Mzee Moi aliithamini sana fimbo hiyo kiasi kwamba wakati mmoja mnamo mwaka 1981, alikataa kuonekana kwenye hafla ya Malkia huko Australia bila fimbo yake ambayo kwa wakati huo ilikuwa imevunjika.

Akiongea katika mahojiano mnamo Agosti 22, 2018, Msaidizi wa Mzee Moi, Lee Njiru alikumbuka jinsi ambavyo fimbo mpya ilibidi isafirishwe kwenda Australia kabla ya Mkutano wa Wakuu wa Jumuiya ya Serikali huko Melbourne.

Fimbo hiyo ilivunjika huko Los Angeles, USA, ambapo Moi alikuwa amehudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa jijini New York.

Bwana Njiru alisema walilazimika kukaa Honolulu, Hawaii, kumngojea msaidizi binafsi wa Moi, Peter Rotich, kusafirisha nyingine kabla ya mkuu huyo nchi kufika mkutanoni.

"Rotich alilazimika kuwa hapo kabla Moi hajafika Australia kwani Mzee alitaka kuwasalimia watu kwa kuwapungia na fimbo hiyo, ambayo ilikuwa sawa na mkia alioutumia Rais (Jomo) Kenyatta," Njiru aliongezea.

Hadi wakati walipofika Australia, Rotich alikuwa tayari ameshawasilisha fimbo nyingine kwa Rais Moi.

"Isingewezekana Mzee Moi kujitokeza mbele ya umma bila fimbo yake," Njiru alikumbuka.

Fimbo ya Nyayo ilijitengenezea alama yake katika historia, na nyimbo za kizalendo ziliimbwa juu yake.

fimbo.jpg

Kwaya ya Kariokor Friends waliimba wimbo uitwao Fimbo ya Nyayo, wakipongeza fimbo hiyo kumsaidia Moi kuongoza nchi. Fimbo ilikuwa ni ishara ya uongozi wa Moi kuiendesha nchi katika mwelekeo sahihi.

"Wakenya, tujali utamaduni wetu na tuungane. Wacha tusonge mbele kwani tumeunganishwa na Fimbo ya Nyayo. Umoja ndio silaha kubwa dhidi ya ukabila na ugaidi, ”yalikuwa baadhi ya mashairi ya wimbo huo.

Wimbo huo pia ulimpongeza Moi kwa kuanzisha Wizara ya Sayansi na Teknolojia iliyowezesha Wakenya wawe huru na kukuza maarifa yao ya kiteknolojia.

Wimbo huo pia uliwahimiza viongozi kufuata njia ya Moi katika kuwa mfano wa kuigwa na kuongoza nchi vizuri.

Fimbo ilikuwa maarufu sana kiasi kwamba iliwekwa nyuma ya noti za Sh20 na Sh100, ambazo zilikuwa na picha ya Moi mbele.

Sanamu kubwa kwa heshima ya rais ilijengwa katika eneo la Uhuru Park kuashiria nguvu yake, uongozi na umoja wa kitaifa.

Fimbo hiyo pia inaaminika kuashiria maono ambayo Moi alikuwa nayo kwa Kenya changa miaka ya 1970 na 80.

moi's fimbo.jpg

Fimbo moi.jpg

Kenya-20.jpg

Chanzo: The Standard
 

Attachments

  • 1603340160290.gif
    1603340160290.gif
    42 bytes · Views: 15
  • 1603340160556.gif
    1603340160556.gif
    42 bytes · Views: 11
  • 1603340160762.gif
    1603340160762.gif
    42 bytes · Views: 9
  • 1603340160973.gif
    1603340160973.gif
    42 bytes · Views: 13
Lile sanamu alilochonga kigwangala kwamba la nyerere limefanana na picha ya moi hapo juu.
 
Fimbo ya mwalimu waliwahi sema ni mti wa mpingo, kuna miaka iliongelewa humu jf.

Bujibuji vipi umefanikiwa kumkimbia yule mchumba au nikutonye dawa.
 
Back
Top Bottom