Kiburi hiki cha wananchi kinatokea wapi?

G.MWAKASEGE

Senior Member
Jun 29, 2007
153
15
Na Yahya Charahani

HEBU niwaulizeni wavuja jasho wenzangu na wale waishiwa ambao mnajiita waheshimiwa au waungwana kunradhi; Hivi tunakwenda wapi jamani?


Naombeni mnipe majibu ya hilo swali na yanayofuatia, hivi ni kwanini wananchi sasa hivi wana 'kiburi' namna hii kiasi cha kuuliza maswali na kuhoji na hata kulalamika laivu mbele ya viongozi wakuu kabisa?


Hivi ni kweli kabisa kwamba wananchi wetu hawa wa hapo Buzwagi au Mwendakulima, kweli hawana adabu hadi wakaamua kushika mabango, kulala barabarani na kupiga kelele wakubwa wetu wanapozungumza? Sidhani!


Kwanini hawa watu wanapinga? Kwanini watu hawaogopi tena na wanaanza kuhoji? Kwanini hadi vijijini wavuja jasho wenzangu wameanza kuuliza "maswali ya ziada" ambayo huko nyuma majibu yake yalikuwa "yanafikirika?".


Inawezekana watu hawa wana kichaa au mzuka au tuseme nini? La hasha, kila kukicha hali inabadilika chuki inazidi kujaa ndani ya vifua vya maskini wenzangu. Wamekata tamaa.


Labda wameahidiwa visivyoahidika, wamevumilia visivyovumilika, wametumika isivyo? Sijui.


Lakini nadhani tupo katika kipindi cha mpito kutoka katika mawazo mgando na yenye woga kwenda katika kipindi cha ujasiri na kuuliza pale tusiporidhishwa.


Woga na au ile amani inatoweka tunavaa joho la mapambano, watu hawana simile awamu ya tatu ya uongozi ilijenga uchumi mkubwa ikaunda pengo kubwa kati ya maskini na matajiri.


Hali hii imetufanya tuwe na mioyo ya jiwe, wavuja jasho sasa hatuna cha kupoteza isipokuwa nguvu zetu, tunahofia nini.


Kipindi hiki ni kigumu kweli kweli. Sio rahisi kukubalika na upande wa serikali inayotawala kwa kuwa upande huo unaamini uko sahihi kuliko mtu yoyote yule.


Ndiyo maana juzi Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mwanajeshi huyu Kanali Fabian Massawe amenusurika kipigo wakati alipotoa majibu yaliyoonekana si ya kuridhisha kwa wanakijiji wa Chasimba kule Tegeta.


Kisha tumesikia mtoto wa kidato cha kwanza katika Shule ya sekondari Pius Msekwa kule Ukerewe akimuuliza Waziri Mkuu na kisha Waziri Mkuu akakaa kimya, hakujibu.


Kama haitoshi Kanali Peter Madaha amevimba mbele ya hadhara akadai kuwa yeye ni kiongozi safi na ndiyo maana kamudu kuongoza kwa miaka 24.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro naye kaonja shubiri baada ya kutoa matamko ya utozaji michango kwa wananchi katika muda ambao si muafaka.


Ametoa tamko lake hilo wakati kila mmoja kachanganyikiwa na namna hali ya maisha ilivyobadilika, mshahara hautoshi maisha hayaendi, pesa inayopatikana inatumika yote na haifiki hata katikati ya mwezi, inaisha baada ya siku moja.


Tena wakati mwingine inaisha kabla hata ya kutolewa, sasa katika mazingira hayo nani atazungumzia mchango aeleweke? Hivi mtu mwenye njaa na aliyekorogwa na maisha atakuwa na hiyari eti ashinde njaa ili ajenge madarasa?


Chanzo kikuu cha mabadiliko katika jamii bila shaka ni teknolojia hususan kuenea na kusambaa kwa mtandao wa kiintaneti na upatikanaji wa simu za mkononi, televisheni na kadhalika.


Ni katika kipindi hiki ambacho jambo linalotokea leo Marekani au Uingereza tunalipata dakika hii hii, bila ya kusubiri taarifa zichujwe.


Kwa maana hiyo hatudanganyiki sasa, akisema mtu uongo tunajua! na hata mtu akijificha sijui London akasaini mkataba tutajua tu na tutahoji.


Bahati mbaya ni kwamba upande wa watawala hautaki kukubali kwamba sasa wananchi tunajua hatutishiwi nyau na wala kudanganywa kwa kauli mbiu wakati hali halisi haieleweki.


Walipomfungia Zitto kushiriki vikao vya bunge kwa kosa la "kusema Uongo", walijihukumu wenyewe na sasa wanalipa gharama ya hukumu hiyo.


Kwa takriban nusu karne, CCM na viongozi wake hawajawahi kupambana na hali ya mabadiliko makubwa kama wanayoipata sasa, na bila ya shaka "vingunge" wa chama hicho wanajiuliza "tumekosea wapi?" na bila ya shaka wanajiuliza "kwanini wanapingwa namna hii?
 
kiburi hiki kinatokana na wananchi kuanza kutambua kuwa TAnzania yenye neema siyo hisani au huruma ya CCM ni haki yao ya kuzaliwa. Neema hiyo inaweza kuletwa na CCM au na chama kingine chochote ambacho kitakuwa tayari kuwa wazi, wakweli, na wawajibikaji.
 
Hauwezi kuwadanganya watu wote daima. Uungwana wa waTZ kutoonyesha machungu yao hadharani uliwapumbaza viongozi wakawaona raia ni wajinga sasa wamefikia tamati kuvumilia machungu hayo.Viongozi wasome alama za nyakati,kuzomewa ni mwanzo wa jambo lingine baya kufuatia. Nakumbuka hata JSM alisema kule ndani ya nyumba 'mdharau mwiba ?......'bila kujua kuwa hiyo iko pande zote.
 
Wameanza kutambua kuwa kuishi maisha bora ni haki yao ya msingi na sio hisani ya chama cha mafisadi.
 
Wananchi wa Tanzania ni wavumilivu lakini kila uvumilivu una mwisho wake ,,,,,hizi ni nyakati za mwisho....shoka lishatiwa kwenye shina...
 
Hakuna Kiburi!!Chochote...Futeni hii Thread! Haraka sana...!!
 
kiburi hiki kinatokana na wananchi kuanza kutambua kuwa TAnzania yenye neema siyo hisani au huruma ya CCM ni haki yao ya kuzaliwa. Neema hiyo inaweza kuletwa na CCM au na chama kingine chochote ambacho kitakuwa tayari kuwa wazi, wakweli, na wawajibikaji.
Mzee Mwanakijiji at his Best ......................!!!
 
kiburi hiki kinatokana na wananchi kuanza kutambua kuwa TAnzania yenye neema siyo hisani au huruma ya CCM ni haki yao ya kuzaliwa. Neema hiyo inaweza kuletwa na CCM au na chama kingine chochote ambacho kitakuwa tayari kuwa wazi, wakweli, na wawajibikaji.
Kweli kabisa kaka, nakumbuka hii uliandika enzi hizo ukiwa independent
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom