Ufunuo wa Yohana
JF-Expert Member
- Oct 9, 2007
- 319
- 70
Wanafunzi wachoma moto shule ya Kibiti
na hamisa maganga
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari ya Kibiti iliyopo Mkoa wa Pwani, wameichoma moto shule hiyo na kusababisha uharibifu mkubwa wa majengo na mali za shule hiyo.
Kutokana na hali hiyo, serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeamua kuifunga shule hiyo kwa mwaka mmoja ili, pamoja na kuwasaka waliochochea vurugu hizo, kutoa nafasi ya kuifanyia ukarabati.
Hadi jana, moto ulikuwa ukiendelea kuteketeza moja ya bweni lililochomwa na wanafunzi hao, ambalo Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza, alisema limeteketea kabisa.
Mbali na bweni, wanafunzi hao waliokuwa na hasira, walichoma moto vyakula vilivyokuwa katika stoo kwa kutumia mafuta ya petroli ambayo haijulikani waliyatoa wapi. Pia waliingia katika maktaba ya shule na kuchoma moto vitabu vyote vilivyokuwamo. Waliharibu pia mfumo wa umeme shuleni hapo, huku wakitishia kuwaua walimu waliokuwa wakijaribu kuwazuia wasiendelee na vurugu hizo.
Vyakula vilivyochomwa moto ni pamaoja na sukari, unga na maharage. Inadaiwa kuwa asilimia kubwa ya waliofanya vurugu hizo kubwa ni wanafunzi wa kidato cha tatu ambao pamoja na mambo mengine, walikuwa wakilalamika kuwa na mwalimu dhaifu katika somo la fizikia.
Uamuzi wa kuifunga shule hiyo yenye wanafunzi 890, ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Mahiza, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, makao makuu ya Wizara ya Elimu na Ufundi.
Baada ya serikali kukaa chini na kutafakari vurugu hizo, imeamua kuifunga shule hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja na wanafunzi wote wanatakiwa kuwa wameondoka shuleni hapo ifikapo saa sita mchana wa leo (jana), alisema Mahiza.
Kwa mujibu wa Mahiza, hatua hiyo itatoa mwanya kwa serikali kuifanyia matengenezo shule hiyo na kufanya tathmini ya hasara iliyotokana na vurugu hizo kubwa.
Hadi sasa hatujui vurugu hizo zimesababisha hasara ya kiasi gani na kesho (leo) wataalamu wetu wanakwenda kutathmini gharama za mali iliyoharibiwa, alisema.
Chanzo cha vurugu hizo ni malalamiko ya muda mrefu ya wanafunzi kuhusu ufundishaji usioridhisha wa baadhi ya walimu, akiwamo mwalimu wa fizikia kidato cha tatu, ukosefu wa maji safi na kutokuwepo kwa umeme wa uhakika.
Hadi jana, moto uliowashwa katika vurugu hizo ulikuwa ukiendelea kuteketeza moja ya mabweni ya shule hiyo kutokana na ukosefu wa maji ya kuuzima.
Yako matatizo ya msingi katika shule zetu na madai ya wanafunzi wa Kibiti yalikuwa ya msingi, lakini walikosa uvumilivu. Matatizo hayo hayakuanza leo, yanatatuliwa kwa njia ya majadiliano sio kuharibu mali za shule, alisema Mahiza.
Pamoja na hatua hiyo, Serikali imeiagiza Bodi ya Shule kukutana haraka na kubaini chanzo cha vurugu hizo na kuwataja wanafunzi wote waliohusika.
Watakaobainika kuhusika sheria itachukua mkondo wake na watakaobainika kutohusika watatawanywa katika shule nyingine. Tukisha ikarabati shule hii iliyojengwa miaka 30 iliyopita kwa msaada wa serikali ya Cuba , hatutachukua tena wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne. Itakuwa na kidato cha tano na sita kwa sababu wanafunzi wa madarasa ya chini wamekuwa vinara katika vurugu, alisema.
Shule hiyo iliyounganishiwa umeme wa jua mwaka jana kutokana na jenereta yake kuharibika, ilihitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa uliohitaji zaidi ya Sh milioni 170, lakini serikali ikaahirisha ili kuifanyia ukarabati mwakani.
Naibu Waziri huyo pia alitumia fursa hiyo kuwaonya wanafunzi nchini kote kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani na vurugu zinazosababisha uharibifu wa mali.
Sourse: Mtanzania ya leo