Kibaki, wapambe wake tumbo joto

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Posted Date::10/4/2007
Kibaki, wapambe wake tumbo joto
Na Danny Mwakiteleko
Mwananchi


KINYANG'ANYIRO cha kuwania urais Kenya wiki hii kinaingia katika hatua muhimu wakati mgombea urais kupitia ODM, Raila Odinga, atakapozindua rasmi kampeni zake kesho katika Viwanja vya Uhuru Park.

Jumapili iliyopita, wananchi wa Kenya walipata fursa ya kushuhudia uzinduzi wa kampeni za Rais Mwai Kibaki katika Uwanja wa Taifa wa Nyayo, uzinduzi ambao ulivuta maelfu ya wakazi wa Nairobi na mikoa mingine ya Kenya.

Lakini pengine kikubwa kilichosababisha kampeni hizo kupamba moto ni matokeo ya kura ya maoni iliyoendeshwa na kampuni ya Steadman kuhusu ni mgombea yupi hasa Wakenya wanataka awaongoze katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Pamoja na kuwapo kwa hisia za chini kwa chini juu ya ni mgombea yupi hasa kati ya Mwai Kibaki wa PNU, Raila Odinga wa ODM na Kalonzo Musyoka wa ODM Kenya, anayekubalika miongoni mwa Wakenya walio wengi.

Matokeo hayo yalionyesha kuwa Raila Odinga, ambaye Wakenya wengi hawakutarajia kuwa anaweza hata kupewa nafasi ya kuongoza nchi hiyo (kutokana na kabila lake), ndiye aliyeibuka kidedea baada ya kupata kura zaidi ya zile za Kibaki na Musyoka zikijumlishwa pamoja.

Kwa mujibu wa kura ya maoni ya Steadman, Raila alijinyakulia asilimia 47 ya kura zote, akifuatiwa na Kibaki ambaye alipata asilimia 38 ya kura huku Kalonzo, akiambulia asilimia nane.

Kwa hesabu rahisi ni kwamba hata kama Kibaki na Kalonzo wangeamua kuunganisha nguvu, bado Raila alikuwa amewazidi kwa kupata asilimia 47 dhidi ya 46 za kura hizo, huku asilimia tano ya wapigakura wakiwa bado hawajaamua.

Lakini hadi sasa Kalonzo ameshikilia msimamo wake kuwa yeye ndiye anayekubalika zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote, akisema Steadman wamemua kupika matokeo hayo baada ya kununuliwa na baadhi ya wagombea.

Lakini Kibaki na wapambe wake wakubwa, akiwamo Waziri wa Barabara na Ujenzi, Simeon Nyachae na yule wa Usalama wa Ndani, John Michuki, pamoja na Waziri wa Serikali za Mitaa, Musikari Kombo, wameonekana wazi kushtushwa na kwa hakika kukanganywa na matokeo hayo.

Katika uzinduzi wa kampeni za ?Kibaki Tena Kazi Iendelee?, Jumapili iliyopita, Nyachae na Kombo walitumia muda mwingi katika hotuba zao kujaribu kumshambulia Raila, wakiwaonya Wakenya kuwa endapo watampa mamlaka ya kuongoza nchi, anaweza kusababisha machafuko katika jamii za Kenya.

Wachunguzi wa siasa za Kenya hata hivyo, walizichukulia kauli za viongozi hao wawili kama kelele za mfamaji ambaye anatapatapa baada ya kuona maji yakiimeza shingo yake.

Ingawa Rais Kibaki katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa kampeni zake aliwataka Wakenya kuacha kurushiana maneno wenyewe kwa wenyewe, bado kauli za Nyachae na Kombo zilisababisha manung?uniko miongoni mwa Wakenya, hasa mashabiki wa Raila wakisema uzinduzi huo ulilenga kumchafua mgombea wao.

Viongozi wa ODM, maarufu kama kundi la Pentagon, Joseph Nyaga, William Rutto na Musalia Mudavadi, walilazimika kuitisha mkutano na waandishi wa habari kupangua shutuma zote zilizoelekezwa kwa Raila na wapambe wa Kibaki.

Itakumbukwa kuwa Raila alikuwa azindue kampeni zake za kuusaka urais Jumamosi iliyopita, lakini polisi wakaupiga marufuku mkutano wake, wakisema kundi dogo la ?Vijana na Kibaki? lilikuwa limetangulia kuomba kuvitumia Viwanja vya Uhuru Park siku hiyo.

Pamoja na kujaribu kushikilia msimamo wa kufanya mkutano wao siku hiyo, wakitoa vielelezo kuwa waliruhusiwa na Halmashauri ya Jiji la Nairobi kufanya mkutano wao siku hiyo, baadaye viongozi wa ODM waliamua kukubali kuuahirisha hadi kesho.

Kwa kiasi fulani, uamuzi huo uliwapa ODM turufu ya ukomavu wa kisiasa kwani ni wazi kuwa endapo wangeshikilia msimamo wao, vurugu kubwa zingeutikisa Mji wa Nairobi kutokana na kinachoonekana kuwa ni ukaidi wa wafuasi wa ODM.

Lakini ukweli wa mambo ni huo kwamba Kibaki na wapambe wake sasa wameachwa tumbo joto baada ya matokeo ya kura za Steadman.

Kinachothibitisha kuwa hali si shwari tena upande wa Kibaki ni namna alivyoamua yeye mwenyewe kujituma kuanza kutafuta kura za wajumbe, tabia ambayo huko awali alikuwa hana.

Kibaki si mtu wa kushtuliwa na jambo na mara kadhaa, watu wa karibu naye wanapoonyesha kushtushwa na jambo, yeye huwa mtu wa mwisho kuonyesha mshtuko na pengine haonyeshi kabisa kuguswa na lolote.

Lakini Jumamosi iliyopita, Rais Kibaki aliamua yeye mwenyewe kutembelea mikutano mikuu ya vyama washirika na PNU iliyokuwa ikifanyika Nairobi kupitisha uamuzi wa viongozi wao wa kumuunga mkono kuwania urais wa Kenya kwa mara ya pili.

Alianza kwa kutembelea mkutano wa Ford People uliofanyika katika ukumbi wa Bomas Kenya na kuwaomba wajumbe wamuunge mkono. Kisha akaingia katika mkutano wa Kanu, katika Uwanja wa Moi Kasarani, kuwaomba kura wajumbe.

Na siku ya uzinduzi wa kampeni, Kibaki, akiwa na msafara wa mrefu wa magari, alianza kwa kutembelea vitongoji mbalimbali vya jiji la Nairobi, akisalimiana na watu mara baada ya ibada katika Kanisa la Family Holy, Basilica kabla ya kuingia Nyayo.

Wanaotazama siasa za Kenya wanajua kweli hali sasa ni ngumu na Kibaki ameamua mwenyewe kwenda mstari wa mbele kuongoza mapambano ya kumrejesha Ikulu katika kipindi kingine cha miaka mitano.

dmwakiteleko@nation.co.ke
 
Back
Top Bottom