Daniel Mbega
JF-Expert Member
- Mar 20, 2013
- 338
- 180
Na Immaculate Makilika- MAELEZO,
09/06/2016
Dar es Salaam.
SERIKALI imejipanga kukomesha mtandao wa watu wasiowaaminifu ambao wanajihusisha na biashara ya kusafirisha binadamu kwenda nchi mbalimbali duniani.
Mtandao huo unahusisha raia wa Tanzania waliopo ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na raia wa kigeni kutoka nchi za India, Malaysia, nchi za Falme za Kiarabu na Mashariki ya Kati.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
“Serikali kwa kushirikiana na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi katika nchi za Bara la Asia pamoja na baadhi ya wahanga wa biashara hiyo inashughulikia kupata majina ya wahusika wote, ikiwemo walioko kwenye Balozi ambao wanawezesha upatikanaji wa visa kuwakamata na kuwafikisha katika mkono wa sheria” alisema Mindi.
Ili kukomesha mtandao huo, Serikali imeanda utaratibu maalumu kwa wafanyakazi wanaokwenda katika nchi za ukanda huo ikiwa ni pamoja na kuandaa mikataba kulingana sheria za nchi husika.
Mindi amesema kuwa kwa nchi ya Omani tangu mwezi Machi 2011 hadi Septemba 2015, Serikali kupitia Ubalozi imeratibu ajira za Watanzania 4358 ambapo kati ya hizo ajira 4033 ni za watumishi wa majumbani.
Aliongeza kuwa, kwa upande wa nchi za Mashariki ya Kati, kuanzia mwezi Juni, 2015 Serikali ilikataza rasmi Watanzania kwenda kufanyakazi zisizo na ujuzi au za ndani katika nchi hizo hadi hapo ilipopata ufumbuzi wa changangamoto zilizokuwa zikisababishwa na mtandao uliokuwa unajihusisha na usafirishaji wa binadamu.
Aidha, ili kuwasaidia Watanzania kupata fursa za ajira nje ya nchi, Serikali inaendelea na jitihada za kusaini mikataba ya Ushirikiano na nchi hizo ikiwemo mkataba wa Tanzania na Qatar.
Mtandao huo wa kusafirisha binadamu umekua ukitoa ahadi za ajira kwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 18 na 24, kwa kuwalaghai kuwa na fursa za ajira katika mahoteli, migahawa, maduka makubwa au kazi za nyumbani, kitu ambacho si ukweli.
Hata hivyo, wengi wa Watanzania wanaoenda nje ya nchi kwa kusaidiwa na mtandao huo wamekuwa wakipata matatizo kadhaa, ikiwemo mateso, mikataba yao kukiukwa, kulazimishwa kufanya ukahaba, na hatimaye kukimbilia Ubalozini ili kupatiwa misaada mbalimbali.
Aidha, imedhihirika kuwa Watanzania walio katika nchi za Bara la Asia, Falme za Kiarabu na Mashariki ya Kati wamekuwa wakiomba misaada ya kurudishwa nchini kupitia Balozi hizo wakiwemo watanzania 500 waliopo nchini India.