Kesi za wanaharakati 28 wa Demokrasia: Jaji Ferdinand Wambali ajitoe

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
Wanaharakati wa Demokrasia wamefungua kesi Mahakama Kuu ambapo zitaanza kusikilizwa Tarehe 9 Machi 2018. Hata hivyo wakati kesi hizo zinakwenda kusikilizwa Jaji Kiongozi Ferdinand Wambali amejipanga katika kesi zote mbili hali kadhalika amempanga pia Jaji Rose Teemba katika Kesi zote mbili.Kuna sintofahamu na mashaka juu ya Jaji Ferdinand Wambali kujipanga katika kesi zote mbili na hii inapelekea kumtaka ajitoe(nitaelezea baadaye mashaka juu ya Jaji huyu)

KESI HIZO NI ZIPI, NA NANI KAFUNGUA

Kesi hizi za Kikatiba zimefunguliwa na baadhi ya Wajumbe wa Umoja wa Wanaharakati wa Demokrasia Nchini Tanzania wenye Wajumbe wapatao 28 wa Kada mbalimbali za Kitaaluma kama vile; Wanasheria, Mawakili, Wanahabari na Wanasiasa.

1. Shauri No.4 la Mwaka 2018 limefunguliwa na Wanaharakati watatu(3) ambao ni: Baraka Mwago, Francis Garatwa na Allan Bujo Mwakatumbula.Wenye shauri hili wanasimamiwa na Jopo la Mawakili wapatao 12 wakiongozwa na Wakili Msomi JEBRA KAMBOLE

Katika Shauri hili Na.4(2018) walalamikaji tajwa hapo juu wanapinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Jeshi la Polisi vinavyowapa Polisi mamlaka ya kukamata watu hovyo na kuwaweka rumande kwa mateso na manyanyaso kwa zaidi ya masaa 24 na hata wakati mwingine bila kuwafikisha Mahakamani.

Aidha, ndani ya Shauri hilo, pia walalamikaji wanapinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Vyama vya Siasa inayowapa Polisi mamlaka ya kuzuia Mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa kwa visingizio vya hovyo ikiwa ni pamoja na Mikutano ya Madiwani na Wabunge ambao kimsingi wanayo haki ya kukutana na wananchi wao waliowachagua.

2. Shauri No.6 la Mwaka 2018 limefunguliwa na Mjumbe wa Umoja wa Wanaharakati wa Demokrasia Ndugu Bob Chacha Wangwe ambaye kwenye Shauri hilo anasimamiwa na Jopo la Mawakili 10 wakiongozwa Wakili Msomi FATUMA KARUME na anapinga Sheria ya Tume ya Uchaguzi inayowapa mamlaka (DED’s) Wakurugenzi wa Wilaya kuwa Wasimamizi wa Uchaguzi ilihali wao sio Maafisa wa Tume ya Uchaguzi.

Umoja huo wa wanaharakati umetoa Rai kwa Watanzania wote wapenda haki waunge mkono jitihada hizi muhimu kwa Mustakabali wa taifa

UHURU WA MAHAKAMA

Mihimili mikuu ya Dola lolote inahusisha Serikali (ambayo ni mtendaji), Bunge na Mahakama. Mihimili hii inatakiwa kuwa huru katika utendaji wa majukumu yake bila mhimili mmoja kuingilia mwingine katika mgawanyo wa majukumu yao.

Kwa Mahakama msingi huu ni wa mhimu sana ili siyo tu kuiwezesha itoe haki bila hofu ya kuingiliwa lakini pia kuiwezesha kujenga taswira kwa raia kuiamini kama kimbilio lao la kupata haki.

Umuhimu wa uhuru wa Mahakama ni kitu cha msingi katika utoaji haki.
Uhuru wa Mahakama
Msingi huu umewekwa katika Ibara ya 107(B) ambayo inasema " Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, Mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika tu kuzingatia masharti ya Latina na yale ya sheria za nchi".

Hata hivyo, sisi wote ni mashuhuda wa vitendo vinavyoashiria Mahakama kuingiliwa na mihimili mingine ya Dola ama kwa kutengeneza mazingira ya maamuzi ya shauri au shughuli iliyo mbele ya jaji, au kutunga sheria ambayo inafifisha uhuru wa Mahakama. Kwa hiyo waingiliaji wakubwa wa uhuru si mtu au chombo kingine chochote cha kawaida zaidi ya Mihimili hii miwili na hasa Mhimili wa SERIKALI.

KWA NINI JAJI FERDINAND WAMBALI AJITOE

Kuna mambo kadhaa ambayo yanatoa msukumo kwa Jaji Wambali kwamba ajitoe:

Mosi, Jaji Kiongozi Ferdnand Wambali amepoteza imani kufuatia maamuzi yake katika kesi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini David Kafulila, ambapo inadaiwa kuwa “alimpa ushindi” kada wa CCM huku akikataa hoja ya msingi ya kurudia kuhesabu upya kura ambazo zilionyesha kuwa DavidiKafulila(NCCR) alishinda ubunge dhidi ya mgombea wachama tawala(CCM) Ndugu Hasna Mwilima.

Pili, Kilio dhidi ya Jaji Kiongozi Wambali kinachangiwa pia na ukweli kwamba “amejipanga” kuwa kwenye paneli za kesi zote mbili. Na kutokana na wadhifa wake kama Jaji Kiongozi, anatarajiwa kuwa atakuwa mwenyekiti wa jopo la majaji katika majopo yote mawili yanayosikiliza kesi hizo.

Tatu, katika kuonesha mashaka na Jaji Wambali kuna hisia zisizo tia shaka kwamba kwa mustakabali mwema wa Demokrasia Nchini Tanzania, Jaji Kiongozi Wambali hakupaswa kuwa sehemu ya majaji wanaosikiliza kesi hizi dhidi ya Serikali ambayo Jaji huyu anahisiwa kuelemea upande wake.

Nne, Kama ilivyo kwa Jaji Kiongozi Wambali , Jaji Rose Teemba nae anahusika katika kesi zote mbili.

MSINGI WA JAJI WAMBALI KUJITOA

Kuna maswali ya kiudadisi na mashaka makubwa tunapaswa kujiuliza: Je, ni kwanini Majaji Wambali na Rose Teemba wahusike katika kesi zote mbili?

Je, kwa nini Jaji Kiongozi amejipanga mwenyewe na amempanga Jaji Teemba katika kesi zote mbili?

Ni katika mashaka na wasiwasi huo unatupa hisia kuwa huenda kuna mkakati maalum wa kuipa Serikali ushindi na ndio maana majaji hao wote wawili wakajipanga katika kesi hizo kimkakati.

HOFU KWA CHAMA TAWALA CHENYE SERIKALI

Hofu nyingine ni kwamba kuna fununu kwamba Chama Tawala kinataka kutumia sheria dhaifu zilizopo kama nyenzo ya kuwapatia ushindi katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa wa Mwakani(2019)na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Tayari kinachoitwa "Mkakati wa Siri kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019" umeshatolewa na umeelekezwa kwenda kwa MaDC na MaRC pamoja na watendaji wengine wa Serikali na chama.

Hofu kwa upande mwingine, ni pale endapo wanaharakati hao watakaposhindwa kwa sababu za wazi za kimkakati zinazoonekana kwa "marefarii" kama Wambali hususan kwenye kesi hiyo, hata wakikata rufaa, muda utakuwa haupo upande wao kwani itakuwa baada ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Nihitimishe kwa kusema,
Pale Chama Tawala Kinapojimilikisha Kauli Turufu juu ya Mambo ya Kitaifa Katika Taasisi za Umma za Maamuzi ni dhahiri udadisi, hofu na mashaka juu ya jambo hilo lazima uongezeke kwa jamii na jamii ndiyo yenye mamlaka ya kuhoji mapungufu hayo ya kikatiba.

Tunawatakia mashauri mema hayo mawili ambayo ni mwanzo mwema wa kujenga nyufa kubwa zilizopo kwenye demokrasia katika nchi yetu.
 
tunawatakia mashauri mema,wakifanikiwa kuibomoa ngome ya ' mkakati 'wa ushindi usio mkakati katu,bali kitanzi cha demokrasia!
 
Back
Top Bottom