Kesi ya Nestory Hussein Chigawa...pamoja na utetezi wa uwendawazimu akahukumiwa kunyongwa...! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kesi ya Nestory Hussein Chigawa...pamoja na utetezi wa uwendawazimu akahukumiwa kunyongwa...!

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, Aug 24, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  Aug 24, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Kesi hii iliyotokea mwaka 1981 na mshitakiwa katika kesi hii ni Nestory Hussein Chigawa ambaye alishitakiwa kwa kosa la kumuuwa kwa kukusudia Bonifasi Makende.

  Kesi hii ilifunguliwa kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya mauaji ya kukusudia, na ilisikilizwa na Mheshimiwa Jaji A Bahati. Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo ilibainika kuwa mnamo machi 11, 1981 mtuhumiwa Nestory Hussein Chigawa alikwenda nyumbani kwa Bonifasi Makende na akiwa njiani kuelekea huko alikutana na Paschal Makende, mtoto wa Bonifasi Makende ambaye alikuja kuwa shahidi wa pili katika kesi hii.

  Alipofika nyumbani hapo mtuhumiwa alimkuta Bonifasi Makende amekaa kwenye kiti nje ya nyumba yake. Katika hali ya kustukiza mtuhumiwa alimzaba makofi mara tatu Bonifasi makende, ambapo Bonifasi alinyanyuka na kuanza kukimbia ili kuepuka kipigo zaidi. Mtuhumiwa alichukuwa mchi na kuanza kumkimbiza na alipomfikia alimpiga na mchi huo kichwani mara kadhaa ambapo alianguka lakini mtuhumiwa aliendelea kumpiga mzee huyo hadi akatosheka kisha akautupa mchi ule na kukimbia. Tukio zima la kupigwa kwa mzee Bonifasi Makende lilishuhudiwa na binti yake aitwae Maria Makende ambaye alikuja kuwa shahidi wa kwanza katika kesi hii.

  Baada ya tukio lile mtuhumiwa alikimbilia kwa mjomba wake Eduard Chigawa ambaye nae alikuja kuwa shahidi wa tatu katika kesi hii ambapo alimjulisha kuwa amemuuwa adui yake mzee Bonifasi Makende, hivyo kumuomba mjomba wake huyo ampeleke kwa mwenyekeiti wa kijiji. Kwa mujibu wa maelezo ya Eduard Chigawa, mtuhumiwa alikuwa akitetemeka na alikuwa akipumua kwa nguvu huku akiongea kwa sauti ya juu kuwa amemuua adui yake na hivyo anataka apelekwe kwa mwenyekiti wa kijiji. Hata hivyo Eduard Chigawe alikiri kuwa tangu amfahamu mtuhumiwa hajawahi kumuona akiwa katika hali kama ile; Baada ya tukio lile la mauaji mwili wa Boniface Makende ulipelekwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi, ili kujua sababu ya kifo chake.

  Mwili ule ulifanyiwa uchunguzi na kwa mujibu wa mtaalam wa kuchunguza maiti (post-mortem) ilibainika kuwa mzee Makende alifariki kutokana na kuvunjika kwa fuvu la kichwa na kuvuja damu kwa ndani. Mtuhumiwa hakukanusha maelezo yote yaliyotolewa na mashahidi wote waliotoa ushahidi katika kesi hii bali utetezi wake ulikuwa kwamba hakujua anachokifanya kwa sababu alikuwa amechanganyikiwa. Akitoa historia ya maradhi yake mtuhumiwa alidai kuwa amekuwa akisumbuliwa na maradhi asiyoyafahamu ambapo kuna wakati mapigo ya moyo wake huenda mbio kunakoambatana na kutetemeka mwili mzima, na hali hiyo inapojitokeza huwa anachanganyikiwa na kutojitambua kuwa yeye ni nani.

  Mtuhumiwa huyo aliendelea kusema kuwa hapo nyuma aliwahi kwenda kwenye zahanati ili kupatiwa tiba ya tatizo hilo ambapo alipewa vidonge atumie lakini hali yake haikuonyesha kubadilika, hivyo ndugu zake waliamua kumpeleka kwa mganga wa miti shamba. Alipofikishwa kwa mganga wa miti shamba alipewa matibabu na kupata nafuu na tangu hapo kila tatizo hilo linapojitokeza huwa anapelekwa kwa mganga huyo na kupatiwa matibabu.Akizungumzia siku aliyomuuwa mzee Makende, mtuhumiwa huyo alidai kwamba alichanganyikiwa na hakujua ni nini alichokuwa anakifanya na alipokwenda kwa mzee Makende na kumpiga mara mbili kichwani hakuwa anajua anachokifanya, na hakuwa ni yeye kiakili.

  Mtuhumiwa huyo aliendelea kusema kwamba anachokumbuka ni pale alipojulishwa baadae kuwa ameua. Hata hivyo mtuhumiwa alidai kuwa kuna wakati mzee Makende alimwambia kwamba atamloga, na hivyo ndivyo alivyofanya kwani alimloga kweli na ndio sababu akawa mwendawazimu. Katika mahojiano ya awali mtuhumiwa alikiri kwamba wakati anakwenda kumuua mzee Makende alikutana na mtoto wa mzee huyo aitwaye Paschal Makende ambaye ni shahidi wa pili katika kesi hii, na mara baada ya kumuua mzee huyo hajawahi kuumwa tena.

  Mtuhumiwa huyo alizidi kudai kuwa hali yake kiafya imekuwa njema kwa kuwa mtu aliyekuwa anamloga ameshamuua kwa hiyo hawezi kuumwa tena, lakini hata hivyo alisisitiza kuwa hakuwa anajua anachokifanya wakati anamuua mzee Makende. Naye shahidi wa tatu kwa upande wa mashitaka katika kesi hii mzee Eduard Chigawa aliiambia mahakama kuwa anafahamu kuwa mtuhumiwa alikuwa anasumbuliwa na maradhi asiyoyafahamu ambayo yalikuwa yanamfanya aonekane kama mtu asiye wa kawaida lakini walipompeleka katika zahanati ya kijiji alionekana hana tatizo.

  Akizungumzia tatizo hilo kwa undani mzee Chigawa alisema kuwa kila mtuhumiwa huyo anapotokewa na tatizo hilo huwa anatetemeka mwili mzima na huwa anazungumza maneno yasiyoeleweka. Kwa mujibu wa maelezo ya Eduard Chigawa ni kwamba mnamo Machi 11, 1981 mtuhumiwa alikuwa shambani pamoja na yeye, na mara baada ya kumaliza shughuli za shamba wote walirejea nyumbani. Walipofika nyumbani mtuhumiwa alitoweka ghafla katika mazingira ya kutatanisha, na aliporejea alikuwa akitweta na kuongea maneno yasiyoeleweka, lakini miongoni mwa maneno yake alisema kuwa amemuua adui yake mzee Makende.

  Katika majumuisho ya ushahidi uliotolewa dhidi ya mtuhumiwa pale mahakamani mwanasheria wa serikali aliyetambuliwa kwa jina moja tu Rutashobya aliieleza mahakama kuwa mtuhumiwa hakuwa mwendawazimu kwani alikuwa na akili zake timamu wakati anamuua mzee Makende na alikuwa akijua ni nini anachokifanya kwa hiyo ana hatia kutokana na kosa aliloshitakiwa nalo. Mwanasheria huyo alinukuu vifungu vya 12 na13 vya kanuni za sheria ambavyo vinafafanua juu ya kumtambua mtu mwendawazimu na asiye mwendawazimu na ili kutetea hoja yake alitoa mfano wa kesi namba 23 EACA 622 ya Muswi Musola na kumalizia kwamba mshitakiwa anapaswa kupatikana na hatia kama alivyoshitakiwa.

  Katika majibu yake dhidi ya mwanasheria wa serikali wakili aliyekuwa akimtetea mtuhumiwa huyo ambaye naye alitajwa kwa jina moja tu la Bi Humplick aliielezea mahakama kuwa ni kweli mtuhumiwa alikuwa na hali ya kuchanganyikiwa ndiyo sababu alikuwa hajui ni nini anachokifanya. Ili kutetea hoja yake hiyo naye alirejea kesi namba A 330 ya mwaka 1957 kati ya Jamhuri na Magata Kachehekana.
  Bi Humplick aliendelea kusema imani juu ya uchawi kwa kawaida huwa inaweza kumfanya yule anaeamini kutojua kuwa ni nini anachokifanya.

  Wakili huyo Aliendelea kubainisha kwamba mtuhumiwa hakuwa anajitambua wakati alipokuwa anakwenda kumshambulia mzee Makende kwa hiyo hana haki ya kushitakiwa.
  Nao wazee wa Baraza katika kesi hii (Assessors) katika maoni yao mara baada ya kupitia kwa makini kanuni ya sheria namba 12 na 13 iliyotolewa na mwanasheria aliyekuwa akimtetea mtuhumiwa, Bi Humplick, wote kwa pamoja waliridhika kabisa kuwa mtuhumiwa anayo kesi ya kujibu kama alivyoshitakiwa.Wazee wote wa Baraza hawakuridhishwa na madai kwamba mtuhumiwa hakuwa anajua ni nini anachokifanya wakati anatekeleza mauaji.

  Mzee wa Baraza wa kwanza aliyejulikana kwa jina la Ramadhani alisema kwamba, kama mtuhumiwa alikuwa na uwendawazimu asingeweza kuzungumza yale yote aliyomueleza Eduard Chigawa kwa sababu alikuwa hajui ni nini anachokifanya. Nae mzee wa pili wa baraza aliyejulikana kwa jina la Martin alisema kwamba kwa mujibu wa vipimo vya hospitalini ilibainika kwamba mtuhumiwa alithibitishwa kuwa alikuwa na akili zake timamu na pia ugonjwa wa uwendazimu aliokuwa anadai kuwa ulikuwa ukimtokea mara kwa mara haukuwa ukifahamika pale kijijini kwao kwa sababu kwa kawaida mtu mwenye ugonjwa wa uwendawazimu angejulikana pale kijijini kwao.
  Kwa maneno yake mwenyewe mzee Martin alisema:

  "Hivi inawezekana kweli mtuhumiwa awe anaumwa uwendawazimu na awe na uwezo wa kukumbuka kwamba, kwa kuwa mzee Makende aliwahi kumwambia kuwa atamloga, kwa hiyo ndiye aliyemloga na hivyo aamue kwenda kumuua? Zaidi ya hapo mtuhumiwa pia anajua kwa usahihi kabisa kwamba alimpiga mzee Makende na mchi mara ngapi kichwani kitu ambacho hakiwezekani kufanywa na mtu mwenye wendawazimu"

  Katika hukumu yake katika kesi hii Jaji Bahati alikubaliana na maelezo yaliyotolewa na wazee wote wawili wa baraza. Katika majumuisho yake kwa maneno yake mwenyewe Jaji Bahati alianza kwa kusema "Swali la kujiuliza hapa ni Je mtuhumiwa alikuwa na uwendawazimu wakati anaua au la?" Jaji Bahati aliendelea kusema kwamba, kwa mujibu wa kanuni ya sheria kifungu cha 12 na 13 kama vilivyotumika katika kesi ya M'naghten aliyeshitakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia vimeelezea bayana kuhusu watuhumiwa wenye uwendawazimu.

  "Kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 imeeleza kwamba sheria inamchukulia mtu yeyote kuwa ni mwenye akili timamu kwa wakati wowote mpaka pale itakapoamuliwa vinginevyo. Lakini kifungu cha 13 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 imesema waziwazi kuwa mtu yeyote hawezi kuchukuliwa kuwa ametenda kosa kama kutenda kwake au kutokutenda kwake na katika muda wa kutenda au kutokutenda alikuwa anasumbuliwa naugonjwa na akili na hivyo kumfanya kutokutambua alichokuwa anakifanya."

  Baada ya kunukuu vifungu hivyo Jaji Bahati aliendelea kubainisha kwamba kwa mujibu wa vifungu hivyo jukumu la kuthibitisha kuwa mtuhumiwa alikuwa na uwendawazimu liko kwa mtuhumiwa mwenyewe kwa sababu kwa mujibu sheria inaaminika kwamba kila mtu ana akili timamu, vinginevyo labda mpaka ithibitishwe kitaalamu. Hata hivyo Mheshimiwa Jaji Bahati alikubaliana na Bi Humplick kuwa tatizo la uwendawazimu mtuhumiwa alilodai kuwa nalo halikuthibitishwa kitaalamu, lakini ili kuleta uwiano Jaji huyo alinukuu kesi kati ya Mbekule na Jamhuri ya mwaka 1971 EA 481.


  Lakini hata hivyo Jaji Bahati alizidi kusisitiza kwamba, pamoja na yote hayo bado kunahitajika ushahidi wa kitaalamu ili kuthibitisha kwamba mtuhumiwa alikuwa na uwendawazimu wakati anauwa?
  Swala la uwendawazimu limeelezwa vizuri katika kanuni ya sheria kifungu cha 13, kwa mfano kesi kati ya Muswi Musola na Jamhuri kama ilivyonukuliwa hapo juu inawiana na kesi hii. Katika kesi hiyo mtuhumiwa alimuua mkewe kwa sababu aliamini kuwa mkewe alikuwa akimloga.

  Mtuhumiwa aliieleza mahakama kwamba hakuwa anajua ni nini alichokuwa anakifanya wakati anamuua mkewe, lakini kulikuwa na ushahidi kutoka kwa Daktari aliyemchunguza mtuhumiwa na kuthibitisha kuwa alikuwa na akili zake timamu na alikuwa anajua ni nini alichokuwa anakifanya wakati anamuua mkewe. Kwa hiyo kwa kusingizia kwake kuwa alikuwa na uwendawazimu mtuhumiwa alidhani kwamba angehalalisha alichokifanya ingawa alikuwa anaweza kutofautisha baya na zuri.


  Baadae katika mahakama ya rufaa ilikuja kugundulika kuwa ushahidi ulikuwa ni finyu sana katika kuthibitisha hata uwezekano wa kuwa mtuhumiwa alishambuliwa na maradhi yaliyoathiri akili yake hivyo kutojua ni nini alichokuwa anakifanya.
  Hata hivyo mheshimiwa Jaji Bahati aliendelea kubainisha kwamba, kwa kuangalia ukweli juu ya kanuni ya sheria kifungu cha 12 na 13 alikiri kutokuona ugumu kutupilia mbali utetezi wa mtuhumiwa Nestory Hussein Chigawa kuwa alikuwa na uwendawazimu wakati anamuua mzee Makende.

  Mheshimiwa
  Jaji Bahati aliendelea kubainisha kuwa iwavyo vyovyote vile kama mtuhumiwa alikuwa hajui ni nini anachokifanya wakati anatekeleza mauaji, basi asingeweza kuonyesha tabia aliyoionyesha kabla na baada ya kutekeleza mauaji.Mtuhumiwa alikiri mwenyewe kukutana na shahidi wa pili katika kesi hii, mtoto wa mzee Makende aitwae Paschal Makende na alikiri pia kuwa alimpiga mzee Makende kwa mchi mara mbili kichwani, na kwa mujibu wa shahidi wa kwanza katika kesi hii binti wa mzee Makende aitwae Maria Makende akitoa ushahidi wake alikiri kumuona mtuhumiwa akikimbia mara baada ya kumuuwa baba yake mzee Makende.

  Pia mtuhumiwa huyo huyo alikimbilia kwa shahidi wa tatu katika kesi hii Eduard Chigawa na kumueleza kuwa amemuua adui yake mzee Makende kwa hiyo ampeleke kwa mwenyekiti wa kijiji. Mheshimiwa Jaji Bahati alikiri kuwa hayo sio matendo yanayoweza kufanywa na mtu mwenye uwendawazimu ambaye hajui ni nini anachokifanya.Jaji Bahati aliendelea kusema kwamba hakuna kitu kigeni kwa mtuhumiwa kutweta na kupumua kwa nguvu mara baada ya kumuuwa mzee Makende, kwani mtuhumiwa huyo alikuwa akimkimbiza mzee Makende , na mara baada ya kumuua alikimbia kutoka katika eneo la tukio na kwenda kwa shahidi wa tatu ambaye ni mjomba wake Eduard Chigawa. Licha ya hivyo katika kipindi chote wakati kesi hiyo inaendeshwa mtuhumiwa alionekana kuwa katika hali ya kawaida kabisa.

  Kwa maneno yake mwenyewe Jaji Bahati alisema:

  "Sikuwahi kuona hali yoyote isiyo ya kawaida kutoka kwa mtuhumiwa wakati naendesha kesi hii, hivyo nakubaliana na wazee wa baraza kuwa mtuhumiwa alikuwa anajua ni nini alichokuwa anakifanya na nimeona kuwa utetezi wa mtuhumiwa kuwa na uwendawazimu wakati akitekeleza mauaji haukuthibitishwa kabisa, kwa hiyo kama wazee wa baraza, na mimi naungana nao kuwa tuhuma za mauaji ya kukusudia kama ilivyoainishwa na kanuni ya sheria kifungu cha 196 zimethibitishwa bila shaka yoyote, kwa hiyo basi mtuhumiwa amepatikana na hatia ya kuuwa kwa kukusudia na ninamhukumu kama ifuatavyo;
  Kwa mujibu wa sheria kuna hukumu moja tu kwa makosa ya kuuwa kwa kukusudia, nayo ni adhabu ya kifo, kwa hiyo basi, nakuhukumu wewe Nestory Hussein Chigawa adhabu ya kifo kwa kunyongwa na haki ya mtuhumiwa kukata rufaa iko wazi"
   
 2. Kimbweka

  Kimbweka JF-Expert Member

  #2
  Aug 24, 2012
  Joined: Jul 16, 2009
  Messages: 8,608
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 145
  Dah haya majina " MZEE MAKENDE"
   
 3. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #3
  Aug 24, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Yaani kilichokuvutia ni hilo jina tu na si maudhui ya uzi huu....................... Una visa wewe
   
 4. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #4
  Aug 24, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Haya wadau ni hji Ijumaa nyingine tena kama kawaida nimekuja na uzi huu wa Kesi ambayo iliwahi kutokea hapa nchini miaka ya 1981.......... Sina mengi, lakini naamini kuna jambo mtajifunza kupitia kesi hii.
   
 5. Philipo Kidwanga

  Philipo Kidwanga Verified User

  #5
  Aug 24, 2012
  Joined: Jul 12, 2012
  Messages: 2,063
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  unauwa halafu unajifanya kichaa hii dunia hii ina mambo sana hii.
   
 6. Lokissa

  Lokissa JF-Expert Member

  #6
  Aug 24, 2012
  Joined: Nov 20, 2010
  Messages: 7,079
  Likes Received: 154
  Trophy Points: 160
  ba mkwe umenirudisha katika fani yangu
  ahsante kwa uchambuzi mzuri wa kesi tajwa.
   
 7. Paloma

  Paloma JF-Expert Member

  #7
  Aug 24, 2012
  Joined: Jan 22, 2008
  Messages: 5,341
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 135
  aksante......najikusanya nije kuusoma huu uzi.........
   
 8. Mr Rocky

  Mr Rocky JF-Expert Member

  #8
  Aug 24, 2012
  Joined: Oct 10, 2007
  Messages: 15,182
  Likes Received: 563
  Trophy Points: 280
  Mkuu Mtambuzi asante sana kwa kutuletea visa hivi ambavyo vinatufanya tukumbuke wajibu wetu wa kusoma kesi kama hizi mara kwa mara kupata uzoefu wa kazi zetu
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 9. Ngongo

  Ngongo JF-Expert Member

  #9
  Aug 24, 2012
  Joined: Sep 20, 2008
  Messages: 12,155
  Likes Received: 3,632
  Trophy Points: 280
  Duh mwanadamu haishi vituko unafanya mauaji unadai kichaa ... Mtambuzi asante kwa nondo zako za kila Ijumaa.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 10. Katavi

  Katavi Platinum Member

  #10
  Aug 24, 2012
  Joined: Aug 31, 2009
  Messages: 39,468
  Likes Received: 4,127
  Trophy Points: 280
  Huyo jamaa alikuwa anajitetea tu hakuwa na uwendawazimu wala nini. Maana anasema alimuua kwa sababu alimwambia kuwa atamroga, hii inaonyesha kabisa jamaa alikuwa na akili timamu alipokuwa anafanya uuaji.
   
 11. cacico

  cacico JF-Expert Member

  #11
  Aug 24, 2012
  Joined: Mar 27, 2012
  Messages: 8,392
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160
  kesi hii yatufundisha nini?? kudos kwako babu Mtambuzi.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 12. Ronn M

  Ronn M JF-Expert Member

  #12
  Aug 24, 2012
  Joined: May 2, 2012
  Messages: 1,283
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 0
  Nadhani kuna haja ya kuangalia huu utetezi wa kutokuwa na akili timamu wakati wa kufanya tukio! Mana ni ngumu kuelewa mtu anafanya kosa kwa kutumia akili halafu katika utetezi mtu anadai hakuwa na akili timamu! Hii dhana ya ukichaa wa muda 'temporary insanity' labda yafaa itazamwe upya
   
 13. GIB

  GIB JF-Expert Member

  #13
  Aug 24, 2012
  Joined: Mar 2, 2012
  Messages: 337
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Asante sana kwa uzi huu. kwa hiyo hukumu ilisha tekelezwa. yaani kwa sasa nestory husseni hatunaye tena au?
   
 14. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #14
  Aug 24, 2012
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,528
  Likes Received: 414,924
  Trophy Points: 280
  Mtambuzi...utetezi wa insanity na self-defence au hata provocation is subject to circumstantial evidence ambazo humpa mtoa maamuzi kufanya aonavyo...................ina,pa uhuru mkubwa wa aidha kutenda haki au kupindisha haki.......
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 15. Zogwale

  Zogwale JF-Expert Member

  #15
  Aug 24, 2012
  Joined: Jul 10, 2008
  Messages: 11,613
  Likes Received: 825
  Trophy Points: 280
  Asante Mtambuzi kwa mambo yako ya Ijumaa. Kweli kila Ijumaa nikiwa na nafasi ni lazima nipitie kesi zako huwa zina mafundisho sana. Jamani kuua si mchezo, roho ya mtu huwa inaita na ndiyo maana mtu akiua tu anaanza kutapatapa. Na kwa hakika fanya kosa lolote lakini la kuua epuka maana adhabu yake ni kifo tu kwa Tanzania. Muuaji wa Norway leo amehukumia miaka 21 jela kwa kuua watu 77 na hii ni kwa kuwa tu Norway ni Scandinavian Country na adhabu ya kifo hakuna. Kwa Tanzania utahukumiwa kifo na hawakunyongi ila tu ndiyo hivyo tena utakuwa umekaa gerezani hadi umauti wa either kunyongwa au natural ufike. Watch out guys!!! Hata kama una hela chafu kama Papaa Msofe but leo hii analiona jua pale tu anapoenda mahakamani au japo mwanga pale anapopelekewa msosi selo la Segerea. Ogopa Prison, epuka maovu.
   
 16. MESTOD

  MESTOD JF-Expert Member

  #16
  Aug 24, 2012
  Joined: Nov 12, 2010
  Messages: 4,640
  Likes Received: 142
  Trophy Points: 160
  Hivi Tanzania watu wananyongwa bado?
   
 17. jouneGwalu

  jouneGwalu JF-Expert Member

  #17
  Aug 25, 2012
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 2,680
  Likes Received: 62
  Trophy Points: 145
  Kwa kesi unazotusimuliaga, nilizozisoma naona za bongo zimekaa moja kwa moja kimtirirko..

  Hamna purukushani za kuumiza kichwa sana ukiringanisha na visa vya vya ulaya au marekani .....

  Labda hii nayo inachangia kwa polisi wetu "kulala", kwamba hamna changamoto za kutingisha idara nzima kwa mfano.

  Ukiangalia kesi hii kwa mfano, ipo wazi kabisa kwamba huyo mpuuzi muuaji sio chizi wala mwehu alikuwa na yake tu.

  Ahsante kwa simulizi Bro.
   
 18. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #18
  Aug 25, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  jouneGwalu unayosema ni kweli kabisa. wapo wadau waliomba niwe naweka kesi za hapa nyumbani nikawaambia kwamba hazina mvuto kama za ughaibuni, labda kama utabahatisha kesi kama za kina Asha Mkwizu au Doris Liundi, lakini kesi nyingi ambazo nimebahatika kuzipata ziko straight forward, hakuna mahali utaumiza kichwa kabisa.

  Ninajaribu kuchanganya hizi kesi ili wasomaji waone tofauti kati ya kesi za ughaibuni na za hapa nchini.

  pamoja daima
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 19. MadameX

  MadameX JF-Expert Member

  #19
  Aug 25, 2012
  Joined: Dec 27, 2009
  Messages: 7,847
  Likes Received: 64
  Trophy Points: 145
  Duuh huyo alikuwa msanii kweli, mwendawazimu halafu hapohapo anajua eti karogwa....mmmh
   
 20. jouneGwalu

  jouneGwalu JF-Expert Member

  #20
  Aug 25, 2012
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 2,680
  Likes Received: 62
  Trophy Points: 145
  Hapana mtu mzima, mi simaanishi kwamba usitusimulie kuhusu mikasa ya nyumbani!

  Nilikuwa nasemea tu kuwa kiujumla kesi za hapa ni nyepesi, ila pia ni sawa watu wazijue kama.....

  So wala usihofu mkuu, we leta a tu mkasa utakaona upo sawa then tunaenda sawa
   
Loading...