Kesi ya Kitilya na wenzake: Upande wa mashtaka haujakamilisha taarifa

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,492
9,264
Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa

Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya na wenzake wanne, wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iwape siku 14 ili waweze kukamilisha taarifa yao na kuiwasilisha Mahakama Kuu.

Wakili wa Takukuru, Leonard Swai akisaidiana na Pascal Magabe amedai leo, Alhamisi Januari 24, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili kusomema Maelezo ya mashahidi na vielelezo( Committal Proceedings).

"Kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upande wa mashtaka tupo katika hatua za mwisho za kuwasilisha taarifa yetu Mahakama Kuu, hivyo tunaomba siku 14 kuanzia leo, ili tuweze kukamilisha taarifa yetu na kuiwasilisha Mahakama Kuu, kama sheria inavyotutaka" amedai Swai.

Swai baada ya kueleza hayo, Wakili wa Utetezi Dk Masumbuko Lamwai, aliiomba mahakama tarehe ijayo, upande wa mashtaka waje wawasomee washtakiwa hao maelezo ya mashahidi na vielelezo kwa sababu upelelezi ulishakamilika.

Hakimu Shahidi baada ya kuelezwa hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 8, 2019, itakapokuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Kitilya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwemo ya kuongoza mtandao wa uhalifu, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya dola za kimarekani 6 milioni.

Mbali na Kitilya, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 2/2019 ni Miss Tanzania, mwaka 1996, Shose Sinare na Sioi Graham, ambao wote ni maofisa wa Banki ya Stanbic.

Wengine ni aliyekuwa Kamishna wa Sera na Madeni kutoka Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda, ambaye kwa sasa yuko (Ofisi ya Waziri Mkuu) na Alfred Misana, ambaye alikuwa kamishna msaidizi wa sera na madeni kutoka wizara hiyo, lakini kwa sasa yuko wizara ya afya.

Hata hivyo, Januari 11, 2019, washtakiwa, Kitilya, Sinare na Solomoni walifutiwa kesi yao ya zamani ya utakatishaji fedha iliyokuwa na mashtaka manane chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai ( CPA), sura ya 20 , iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Walifutiwa mashtaka hayo, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kueleza Mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo na kisha kuwafungulia mashtaka mapya 58.

Hata hivyo, katika mashtaka hayo mapya 58; mashtaka 49 ni ya utakatishaji fedha, matatu ya kughushi, mawili ya kutoa nyaraka za uongo, moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanyanyifu, kula njama ya kutenda kosa kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango.

Pia wanakabiliwa na shtaka moja la kuongoza mtandao wa uhalifu, uliopelekea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata hasara ya dola za kimarekani 600 milioni.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Februari 20, 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali jijini Dar ss Salam, kwa makusudi wanadaiwa kuongoza mtandao wa uhalifu, uliopelekea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata hasara ya dola za kimarekani 600milioni.

Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, washtakiwa kwa pamoja, wanadaiwa, kati ya Machi 15, 2013 na Januari 10, 2014 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya walijipatia Dola za Kimarekani 6 milioni wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd, wakati wakijua sio kweli.

Mwananchi
 
Back
Top Bottom