Kesi ya Constantine Petro Kizaka - Ni kweli alikuwa mwendawazimu wakati anamuua mkewe...?

Mtambuzi

Platinum Member
Oct 29, 2008
8,806
2,000

View attachment 54131

View attachment 54132

Ilikuwa ni Agosti 1, 1984, katika kijiji cha Chonwa Bwana Constantine Petro Kizaka aliondoka nyumbani kwake akiwa amefuatana na mkewe Bi, Celine Yusti Daniel kwenda porini kukata kuni, mkewe alikuwa amembeba mtoto wao mdogo aliyekuwa na umri wa miezi 7, na hapo nyumbani kwao walikuwa wamewaacha watoto wao wawili ambao hata hivyo baadae walikwenda kwa babu yao mzaa baba aitwae Petro Kizaka.

Mpaka ilipofika usiku, Constantine na mkewe Celine walikuwa hawajarudi. Baba mzazi wa Constantine alitoa taarifa pale kijijini kuhusiana na kutorejea kwa mtoto wao na mkewe na wanakijiji waliungana kuwatafuta wakiongozwa na mwenyekiti wa kijiji Bwana Iddi Mtoasala lakini jitihada zao za kuwatafuta wanandoa hao hazikuzaa matunda. Siku iliyofuata yaani tarehe 3 Agost, 1984 wanakijiji waliendelea kuwatafuta wanandoa hao lakini pia hawakuonekana.

Mnamo Agosti 3, 1984 Mzee Petro Kizaka akiwa na mkewe (wazazi wa Constantine Kizaka) walikwenda porini kutafuta kuni. Wakiwa njiani walimuona mke wa Constantine Kizaka akiwa amelala kwenye majani pembeni ya barabara, na walipomsogelea kwa karibu wakagundua kwamba amefariki, mita chache kutoka mahali mwili wa mama yule ulipolala, walimuona mtoto wa marehemu. Alikuwa hai lakini alikuwa amelegea sana, nadhani ilikuwa ni kutokana na njaa na kupigwa na baridi kali kwa siku mbili tangu atelekezwe pale porini baada ya mama yake kuuawa.

Mzee Petro Kizaka na mkewe walirudi kijijini wakiwa na mtoto yule na kuwajulisha wanakijiji wenzao. Ndugu, jamaa na wanakijiji walikwenda hadi pale mwili wa marehemu ulipokuwa umetelekezwa, na walilazimika kukesha pale, sio kwa ajili tu ya kuomboleza bali pia kuulinda mwili ule huku wakisubiri Polisi na Daktari wafike ili kufanya uchunguzi na kujua sababu ya kifo cha mama yule. Mume wa marehemu alikuwa bado hajulikani alipo.

Wakati huo huo Mume wa Marehemu Constantine Kizaka alionekana kijiji cha jirani cha Udunhu. Alikwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa mtu aliyejulikana kwa jina la Alex Mkunani majira ya saa 11:00 jioni, ambapo aliaomba apewe chakula, baada ya kulalamika kwamba anajisikia njaa sana. Pale alipewa chakula na miwa ya kutafuna. Baada ya kula aliendelea na safari yake hadi akafika kwenye kijiji chake, ilikuwa ni tarehe 5 Agosti 1984. Bwana Petro, alikwenda moja kwa moja hadi kwa kaka yake mkubwa aitwae Angoro Anthony.

Kwa mujibu wa Bwana Angoro, alimuona Constantine alikuwa amelowa sana. Alimkaribisha nyumbani mwake na wakati huo huo akatoa taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji Bwana Mtoasala. Mwenyekiti huyo wa kijiji Bwana Mtoasala akishirikiana na mgambo wa kijiji walifika kwa Bwana Angoro na kumtia mbaroni Constantine na kisha kumpeleka kituo cha Polisi kilichopo Ruhembe.

Kesi hii ni ya mwaka 1984 ya Constantine Petro Kizaka, alishitakiwa na Jamhuri kwa kosa la kumuuwa mkewe kwa kumkatakata kwa panga walipokwenda porini kutafuta kuni hapo mnamo tarehe 1 Agosti 1984. Kosa hilo la Kuuwa kwa kukusudia (Murder) limeainishwa kwenye kanuni ya adhabu (Penal Code) kifungu cha 196.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyosomwa pale mahakamani wakati wa kesi hiyo ilielezwa kwamba, Mtuhumiwa huyo Bwana Constantine aliandikisha maelezo mara mbili, katika kituo kituo hicho cha Polisi. Mara ya kwanza ilikuwa ni tarehe 7 Agosti 1984 halafu akaandikisha maelezo mengine hapo mnamo Tarehe 9 Agosti 1984.

Mahojiano hayo yalichukuliwa na Mpelelezi wa Polisi No. B 4413 Sajenti Madu (aliyekuwa shahidi wa tatu katika mkesi hii). Hata hivyo mtuhumiwa huyo alidai kutaka kuandikisha maelezo mengine kwa sababu maelezo aliyotoa awali hayakuwa sahihi. Hivyo sajenti Madu alichukua maelezo upya ya mtuhumiwa hapo mnamo mtarehe 10 Agosti 1984. Katika maelezo hayo mtuhumiwa alidai kwamba ni yeye aliyemuua mkewe lakini mauaji hayo yalikuwa yamepangwa kwa msukumo wa wazazi wake (yeye mtuhumiwa) na ndugu zake ambao walikuwa wanamchukia marehemu kutokana tabia yake ya uasherati. Katika maelezo yake hayo alidai pia kwamba marehemu alikuwa na mahusiano na wanaume tofauti tofauti tabia ambayo si kwamba ilikuwa ikimdhalilisha yeye kama mume bali pia ilikuwa ikiudhalilisha ukoo wa wa KIZAKA. Na hiyo ndiyo sababu ya wazazi wake pamoja na ndugu zake kumtaka yeye mtuhumiwa kumuua marehemu iwe ni kwa sumu au kwa njia yoyote.

Hivyo mtuhumiwa aliamua kutafuta mbinu ya kukamilisha kile alichoagizwa na ndugu zake. Mnamo Agosti 17, 1984 mtuhumiwa alijisikia kuumwa. Kulingana na maelezo, mtuhumiwa alipona kutoka katika hayo maradhi ya muda mfupi. Hata hivyo pia alijifanya kama anapata maradhi yanayoathiri akili yake.

Mnamo Agosti 1, 1984, kulingana na maelezo yake aliyoandikisha Polisi (Kidhibiti cha 5), mtuhumiwa alimshawishi mkewe waende kutafuta kuni porini. Marehemu alibeba panga na pia alimbeba mtoto wao wa kiume mgongoni aitwae Zamoyoni. Walipofika Porini marehemu alianza kukusanya kuni na mumewe alikuwa akimuangalia. Mtuhumiwa alikuwa anafikiria kumuua marehemu hapo porini lakini alisita.

Katika maelezo yake hayo alisema kwamba, wakiwa njiani kurudi nyumbani aliona kundi la watu wakija kuelekea kule walipo, akadhani ni ndugu zake ambao walikuwa wamemuonya kwamba iwapo hatamuua mkewe, basi watamuua yeye badala yake. Baada ya kuona kwamba maisha yake yako hatarini, alimnyang'anya mkewe panga na kumkata nalo. Alidai kwamba, hakumbuki alimkata katika eneo gani la mwili marehemu na hakumbulia alamkata mara ngapi. Kwa kuwa hakupewa maelezo ya kumuuwa mwanaye, hivyo alimchukua mtoto kutoka mgongoni mwa mama yake na kumuweka pembeni. Alikuwa hakumbuki ni wapi alilitupa lile panga. Hivyo alikimbilia porini. Katika maelezo yake mtuhumiwa alidai kwamba, alielekezwa na ndugu zake asilale kwa mtu yeyote kwa sababu watamsaidia kwa lolote litakalotokea. Kabla ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa alipewa kichane cha ndizi atakazokula wakati atakapokuwa amejificha porini na baba yake mdogo aitwae Lucas Kizaka.

Aliporejea hapo kijijini aliambiwa kwamba, wazazi wake walitaka kumzika marehemu lakini ndugu wa marehemu walikataa. Lakini baada muda kidogo akakamatwa na kufungwa kamba na baadae kupelekwa kituo cha Polisi ambapo aliandikisha maelezo. Mtuhumiwa katika maelezo yake alidai kwamba, alikamatwa na mwenyekiti wa kijiji na katibu wake ambao walikuwa hawajui undani wa suala lile. Alidai kwamba wazazi wake walimshauri atakapofika Polisi ajifanye kwamba anaumwa na atakapoandikisha maelezo yake aseme kwamba alikwenda porini kukusanya mabanzi (Mabaki ya mbao). Mtuhumiwa alihitimisha maelezo yake kwa kusema:-


"Maelezo yangu ya kwanza nilieleza vingine kutokana na walivyonielekeza wazazi na kusema watanisaidia. Leo tarehe 10/8/1984 nimeona nieleze ukweli mtupu nikiwa na kili zangu timamu kabisa. Mimi sikupenda kumuuwa mke wangu ila kutokana na ushauri wa ndugu zangu. Hayo ndiyo maelezo yangu na nitayazungumza popte pale.

Mimi ni: CONSTANTINE KIZAKA.

Mwili wa marehemu ulizikwa mnamo tarehe 8, Agosti 1984 baada ya kufanyiwa uchunguzi na Daktari. Silaha mbili zilipatikana katika eneo la tukio. Silaha hizo zilipatikana katika eneo hilo,la tukio wakati wa kuondoa nyasi ili kuandaa mahali pa kuchimbwa kaburi. Silaha hizo zilikuwa na panga na Mundu. Pia kulikuwa na ushahidi uliotolewa na upande wa utetezi pale mahakamani kwamba wiki mbili kabla ya mtuhumiwa kutekeleza mauaji yale alikuwa akiumwa. Aliumwa mnamo tarehe 17, Julai, 1984. Baba yake Mzee Petro Kizaka (Shahidi wa 2) na kaka yake Angoro Anthony )(Shahidi wa 5) walidai kwamba mtuhumiwa alipatwa na Malaria na kutokana na maradhi hayo mtuhumiwa alipatwa na hali ya kufanya fujo na kuongea vitu visivyoeleweka. Waliieleza Mahakama kwamba, pamoja na mtuhumiwa kutibiwa katika zahanati ya Chone, lakini hakuonekana kupata nafuu kiakili kwa sababu bado alikuwa mazungumzo yake yalikuwa hayaeleweki. Lakini hata hivyo maelezo yao hayakuonekana kuendana ya yale ya shahidi pekee wa mtuhumiwa Konrad Maumba (Shahidi wa 2 wa mtuhumiwa). (Kisheria shahidi wa kwanza ni mtuhumiwa mwenyewe).

Huyu alikuwa ni Daktari wa zahanati ya Chonwe wakati huo. Aliieleza mahakama kwamba yeye ndiye aliyekwenda nyumbani kwa mtuhumiwa kumtibu baada ya kuitwa na ndugu wa mtuhumiwa. Alisema kwamba, alipofika hakumuona mtuhumiwa akiwa amefungwa kamba kama ilivyodaiwa na baba wa mtuhumiwa na kaka wa mtuhumiwa pale mahakamani wala hakumuona mtuhumiwa akifanya vitendo vya fujo.

Alichukua vipimo vya joto la mwili wa mtuhumiwa ambapo alipata kiwango cha joto kilichofikia nyuzi joto 38. Alimtibu mtuhumiwa kwa kumpa vidonge vya klorokwin, dozi ya siku tatu mfululizo. Daktari huyo aliendelea kuileza mahakama kwamba, mnamo tarehe 20, Julai 1984 alikwenda kumtembelea mtuhumiwa na kukuta joto lake la mwili limeshuka na hali yake kiafya imetengemaa. Daktari huyo aligundua kwamba tiba yake imefanya kazi. Mtuhumiwa alipona ingawa alilalamika kwa daktari kwamba hajapata choo. Toka wakati huo daktari hakuwahi kusikia malalamiko yoyote mtuhumiwa kuumwa.

Shahidi mwingine alikuwa ni mjumbe wa nyumba kumi, kwa mujibu wa melezo yake alidai kwamba aliwahi kuambiwa kwamba mtuhumiwa alikuwa anaumwa lakini hakusikia kwamba alikuwa na tatizo la akili. Alibainisha kwamba hakuwahi kusikia kuwa mtuhumiwa aliwahi kupatwa na maradhi ambayo yalimletea matatizo ya akili kama vile malaria iliyopanda kichwani (Cerebral Malaria).

Upande wa utetezi ulileta ushahidi kuthibitisha kwamba mtuhumiwa alipatwa na Malaria iliyopanda kichwani ambayo pia ilimletea matatizo ya kiakili. Mgonjwa asingeweza kufanya vitendo vya fujo kwa sababu alikuwa amedhoofika kutokana na kusumbuliwa na malaria. Alisema mwanasheria huyo. Aliendelea kusema kwamba, mgonjwa wa aina hiyo anatakiwa matibabu wakati wote na inawezekana akapona au akafa. Hakuna mgonjwa wa aina hiyo anayeweza kupona, labda hadi pale atakapokuwa ametibiwa.

Katika maelezo yake pale mahakamani chini ya kiapo mtuhumiwa alisema kwamba, inawezekana ni yeye aliyemuua marehemu. Alisema kwamba anaamini inawezekana kuwa hivyo kwa sababu aliambiwa na wazazi wake kuwa amemuua mkewe. Na alisimuliwa stori kamili na mdogo wake aitwae Venance alipompelekea yeye mtuhumiwa nguo wakati akiwa bado yuko rumande. vinginevyo asingejua alichokifanya hadi pale aliposimuliwa na Venance. Mtuhumiwa huyo aliendaea kusema kwamba hata pale alipokuwa anaumwa hakuwa anajua chochote. Alisimuliwa tu kile kilichomtokea na vile vitendo alivyokuwa akivifanya. Alisema kwamba, kwa kipindi cha kati ya Julai 1984 na Agosti 1984 kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwake na hakumbuki chochote alichokifanya katika kipindi hicho.

Hiyo ndiyo stori kamili ya upande wa utetezi katika kesi hiyo ambapo uliegemea kwenye kipengele cha uwendawazimu (Insanity)

Akisoma hukumu ya kesi hiyo Mheshimiwa Jaji Mrema alitoa majumuisho ya kesi hiyo kama ifuatavyo:-

"Wakati nilipofanya majumuisho ya kesi hii kwa wazee wa baraza niliwaeleza kwamba, kitu kinachobishaniwa hapa ni utetezi wa uwendawazimu ambao umeibuliwa na mtuhumiwa. Kama nilivyosema upande wa utetezi nao umeafiki utetezi huo. Kifungu cha 192 cha Cr.P.A 1985 kilihusishwa katika jambo hili. Ni ukweli usiopingika kwamba, mtu aliyekufa ni Celine binti wa Yusti Daniel. Na imekubalika kwamba, mtu aliyemuuwa marehemu ni mtuhumiwa na aliyatekeleza mauaji hayo kikatili. Kifo cha marehemu hakikuwa cha kawaida."

Mheshimiwa Jaji Mrema aliendelea kusema kwamba, alichowaambia wazee wa baraza ni kuamua kulingana na madai ya muhumiwa kuwa alikuwa na ugonjwa ambao ulimsabbishia asijue anachokifanya. Mheshimiwa Jaji hakutaka kuhusisha maelezo mengine yaliyotolewa pale mahakamani kama utetezi kwamba mtuhumiwa hakujua kwamba anachokifanya ni kosa kisheria. Mheshimiwa Jaji aliendelea kusema kwamba mtuhumiwa hakutoa utetezi wa uwendawazimu, zaidi ya kudai kwamba alikuwa hajui kuwa amemuuwa marehemu..

Mheshimiwa Jaji Mrema aliendelea kusema kwamba, kwa mujibu wa kanuni ya sheria vifungu vya 12 na 13 vimeelezea bayana kuhusu watuhumiwa wenye uwendawazimu.

Kwa mujibu wa kifungu cha 12. Sheria inamchukulia mtu yeyote kuwa ni mwenye akili timamu kwa wakati wote mpaka pale itakapoamuliwa vinginevyo.

Kifungu cha 13. Mtu yeyote hawezi kuchukuliwa kuwa ametenda kosa kama kutenda kwake au kutokutenda kwake na katika muda wa kutenda au kutokutenda alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa akili na hivyo kumfanya kutokutambua alichokuwa anakifanya.

Akiendelea kufafanua Mheshimwa Jaji Mrema alisema kwamba, Katika kifungu hicho cha 13 ambacho kinahusika na kesi iliyoko mbele yake alihoji iwapo inawezekana kweli malaria au homa ambayo mtuhumiwa alikuwa akiumwa siku hiyo ya tarehe 17/7/1984 ndiyo iliyomfanya mtuhumiwa akaathirika akili na kumfanya kutokujua kwamba kitendo cha kuuwa alichokifanya ni kosa?

Mheshimiwa Jaji Mrema alizungumzia utetezi wa wakili wa mtuhumiwa Bwana Kamugisha.

Katika utetezi wake wakili Kamugisha alipinga maoni ya mwendesha mashitaka kwamba mtuhumiwa alikuwa na akili timamu wakati anatekeleza mauaji hayo. Na aliwasilisha maelezo yake kwamba mtuhumiwa alikuwa ameathirika vibaya katika akili yake kutokana na kuugua wakati alipomuuwa marehemu mkewe.

Wakili huyo alibainisha kwamba, ushahidi wa daktari Kulwa Juma alioutoa pale mahakamani usipewe uzito kwa sababu hauwezi kuchukuliwa kama ni ushahidi wa kitaalamu, pia wakili huyo alibainisha kwamba, ushahidi wa daktari huyo ulikuwa ni wa jumla.

Wakili huyo aliiomba mahakama hiyo iuangalie ushahidi wa baba wa marehemu na kaka wa mtuhumiwa alioutoa pale mahakamani kwamba mtuhumiwa alipokuwa anaumwa malaria alionekana kufanya vitendo visivyo vya kawaida na wakati mwingine kutishia usalama. Ugonjwa huo uliompata mtuhumiwa ulikuwa ni wa muda mfupi kwani ulimtokea kati ya tarhe 17/7/1984 na 1/8/1984. Pia wakili huyo aliomba mahakama iuchukulie ushahidi wa mwenyekiti wa kijiji kwa makini kwa sababu mwenyekiti huyo alikiri wazi kwamba wakati anamhoji mtuhumiwa alionekana kutokuwa katika hali ya kawaida na majibu yake yalikuwa hayapo katika mpangilio kulingana na jinsi alivyoulizwa.

Wakili Kamugisha aliendelea kusema kwamba hata repoti iliyotoka katika Hospitali ya vichaa Isanga, Dodoma (Isanga Phsychtric Institution) ambayo ilichukuliwa kama kidhibiti cha 6 iangaliwe kwa mapana zaidi kwa sababu mtuhumiwa alipelekwa katika hospitali hiyo ya vichaa Isanga miaka minne tangu kutokea kwa tukio hilo. Kwa hiyo ripoti hiyo haiwezi kuwa na majibu sahihi kuhusu hali ya mtuhumiwa kwa sababu wakati huo hali ya mtuhumiwa ilikuwa imeimarika na hakuwa akiumwa tena ule ugonjwa uliopelekea yeye kuuwa.

Pia wakili huyo alibainisha kwamba mpaka kufikia hapo mahakama ilikuwa haijathibitisha nia (motive) iliyopelekea mtuhumiwa kutekeleza mauaji hayo. Aliendelea kusema kwamba kilichoelezwa hapo mahakamni ni kwamba mtuhumiwa na marehemu walikuwa wanaishi kama mke na mume kwa furaha na amani. Hapakuwa na kutoelewana kwa wanandoa hao, kwa hiyo haiwezekani mtuhumiwa akurupuke tu na kumuua mkewe ambaye wameishi wote na kuzaa watoto watatu katika ndoa yao. Kwa sababu hiyo, wakili Kamugisha alibainisha kwamba hakuna hoja inayothibitisha kiasi cha kutosha kwamba mtuhumiwa alikuwa na akili timamu wakati akitekelza mauaji hayo, hivyo aliiomba mahakama imuone mtuhumiwa kuwa hana hatia na imuachie huru.

Akijibu hoja za wakili wa mshitakiwa, Bwana Senguji mwendesha mashitaka wa serikali alisisitiza kwamba mtuhumiwa alifanya mauaji hayo akiwa na akili timamu na alijua anachokifanya ni kosa kisheria. Aliiomba mahakama hiyo irejee ushahidi wa daktari aliyemtibu mshitakiwa ambapo katika repoti yake daktari huyo alidai kwamba mtu anayeugua malaria iliyopanda kichwani kwa kawaida huishiwa na nguvu na na hivyo haiwezekani akafanya vitendo vya kikatili au kuhatarisha usalama. Mwendesha mashitaka huyo alipinga maelezo ya upande wa utetezi kwamba mtuhumiwa alikuwa akiugua malaria kali ambayo iliathiri ubongo wake, kwa sababu kama angekuwa anaumwa ugonjwa huo asingeweza kuwa na nguvu za kumshambulia marehemu mkewe na kumuuwa. Mwendesha mashitaka huyo alisema kwamba hakuna ushahidi unaoonesha kwamba mtuhumiwa aliwahi kupata matibabu kutokana na ugonjwa huo zaidi ya kupewa klorokwin tu na baada ya siku tatu mtuhumiwa huyo alipona na kwa mujibu wa ushahidi wa daktari aliyemtibu alibainisha kwamba mtuhumiwa hakuwahi kupelekwa hospitalini, sasa iweje isemwe kwamba alikuwa na ugonjwa ulioathiri ubongo wake? "Upande wa utetezi unadanganya hapa." Alionesha kushangaa mwendesha mashitaka huyo.

Mheshimiwa Jaji Mrema, alionesha kuridhishwa na maelezo ya pande mbili upande wa mashtaka na upande wa utetezi. Mheshimiwa Jaji alisema kwamba, ni kweli sheria inataka kama mshitakiwa anakutwa na hatia, lazima iwe imeridhishwa na ushahidi uliotolewa dhidi yake pasi na shaka. Mheshimiwa Jaji alisoma malezo ya wazee wa baraza ambao walikuwa watatu. Wazee hao kwa mujibu wa sheria walitoa mtazamo wao kuhusiana na shauri hilo.

Mzee wa kwanza alikuwa mzee Said Nassoro, kwa upande wake alimuona mtuhumiwa kuwa na hatia ya mauaji ya kukusudia na alitaka ahukumiwa kwa kosa hilo kwani alikuwa anajua anachokifanya wakati akitekeleza mauaji hayo.

Mzee wa pili Salum Muhogela, na yeye maelezo yake hayakutofautiana na ya mzee Nassoro, na alitaka mshitakiwa ahukumiwe kwa mujibu wa sheria. Na Mzee wa baraza wa tatu na yeye maoni yake yalikuwa hivyo hiyo, kwamba mtuhumiwa aliuwa kwa kukusudia.

Mheshimiwa Jaji Mrema alirejea kesi ya Agnes Doris Liundi na Jamhuri (T.L.R) 1980 ukurasa wa 38 na pia alirejea rufaa ya kesi hiyo.

Mheshimiwa alinukuu kama ifuatavyo:

I. Mtuhumiwa yeyote akitoa madai kwamaba alikuwa na matatizo ya akili wakati akifanya kosa, ni lazima uwepo ushahidi wa kitaalamu utakaothibitisha kwamba alikuwa na tatizo hilo

II. Ni wajibu wa mtuhumiwa kuthibitisha kwamba alikuwa amerukwa na akili lakini hiyo itakubalika iwapo kutakuwa na kipimo chenye uwelekeo (Balance of Probability).

III. Mahakama haifungwi kukubaliana na ushahidi wa hospitalini (Medical Testimony) endapo kuna sababu madhubuti ya kutofanya hivyo.

Mheshimiwa Jaji Mrema alisema kwamba upande wa utetezi umeshindwa kuthibitisha kwamba mtuhumiwa alikuwa amerukwa na akili wakati akitekeleza mauaji hayo na alikubaliana na maoni ya wazee wa baraza kwamba mtuhumiwa alitekeleza mauaji hayo akiwa na dhamira ovu (malice aforethought) kwa hiyo anapaswa kukabiliana na hukumu kama ilivyoainishwa kwa makosa ya namna hiyo.

Mheshimiwa Jaji alimalizia kwa kusema,

"Kama ifuatavyo, namhukumu mtuhumiwa kwa kosa la kuuwa kwa kukusudia kwa mujibu wa kifungu cha sheria c/s 196. Kuna adhabu moja tu kwa makosa ya namna hiyo, nayo ni kifo kwa kunyongwa mpaka kufa."

Mtuhumiwa huyo alihukumiwa adhabu ya kifo kwa kunyongwa hadi kufa.

Haki ya mtuhumiwa kukata rufaa iko wazi.Kesi hii ilisikilizwa na Mheshimiwa Jaji Mrema huko mkoani Morogoro na hukumu ilisomwa mnamo Julai 4, 1985.
 

Attachments

  • gavel.jpg
    File size
    25.8 KB
    Views
    74

lutayega

JF-Expert Member
Feb 29, 2012
1,275
2,000
Ni Ijumaa nyingine tena, kama kawaida leo nimekuja na kesi hii ya hapa hapa nchini..............Nawatakieni usomaji mwema, na tukutane tena Ijumaa ijayo hapa hapa MMU, nitakapokuja na kesi ambayo itawashangaza wengi.............stay tune.............!
Mkuu mi ni mmoja wa wapenzi wa makala za kesi, huwa zinanifurahisha sn, usichoke kuendelea kutujuza. Be bleased
 

Mr Rocky

JF-Expert Member
Oct 10, 2007
15,188
2,000
japo kuhukumiwa kunyongwa sio dhana nzuri wala suluhisho la kosa lililofanyika ila mtuhumiwa hapa hakuwa na sababu ya kumuua mkewe kwa shinikizo la ndugu
Eti ndugu wanakuambia muue mkeo na wewe unatekeleza hukumu bila hata kujiuliza ni kwa nini
hakukuwa na ushahidi wa madai yake ya uasherati na inawezekana zilikuwa ni hear say too
Asante mkuu kwa kisa hiki
 

Ngongo

JF-Expert Member
Sep 20, 2008
15,636
2,000
Mkuu Mtambuzi.

Asante kwa kuendelea kutuletea visa vya mahakamani.Nimefurahi kwakuwa haki imetendeka na kuonekana dhahiri.Kwa mujibu wa sheria zetu Bwana Constantine Petro Kizaka ili anyongwe ni lazima Rais wa JMT atie saini sasa sijui kama hili jitu katili lilisha nyongwa au bado linaendelea kumeza kodi zetu huko magereza ?.Ikiwa mpaka leo hajanyongwa Mzee Ruksa,Mkapa na Kikwete wanastahili lawama kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.
 

ntogwisangu

JF-Expert Member
Nov 25, 2011
524
225
Ni Ijumaa nyingine tena,na kama ilivyozoeleka sasa!!!,Mtambuzi huyoooo!!!na leo tena kisa kingine kinacho-reveal migogoro katika mahusiano ya mapenzi!!!na matokeo ya migogoro hiyo!!!.Wandugu wapendwa leo ni ijumaa hakuna shaka wapo wenye mahusiano yao leo watapata fursa ya kutoka na kupumzika hapa na pale!!!
Visa hivi vya Mtambuzi vyatujuza kwamba athari za usaliti katika mapenzi ni kubwa sana!!!hivyo basi tuwe makini na yale tuyafanyayo katika mahusiano yetu!!!!
 

ntogwisangu

JF-Expert Member
Nov 25, 2011
524
225
Ngongo,

wewe ni mwanasheria!!!!!!subiri siku asali wako wa moyo atakapokuyeyusha vya kutosha na ukumkatakata nyama,ukachoma ukala ndo utajua haki zinatendeka!!!!!
 

NATA

JF-Expert Member
May 10, 2007
4,510
1,195
Thanks Gustavo, kwa kisa kingine cha ukatiri,

Jamani wale tunaowaamini na kutowaogopa ndio wanaotenda ukatiri wa kutisha sana kwa wapendwa wao.

Kwa upande mwingine nashawishika kuwa mtuhumiwa alikuwa amelukwa akili akitenda mauaji.

Kwanza kwanini Dr aitwe badala ya mtuhumiwa kumfuata Dr kama alikuwa anaumwa kawaida?

Pili maelezo ya mtuhumiwa hayajakaa sawa , pale anaposema aliona kundi la watu likimfuata yale ni mawenge ya qunini, alikuwa anasikia kuchanganyika kichwani. Mimi nilisha kunywa quinin basi kichwa kilikuwa kinaniwanga na nikawa nasikia makelele acha.

Halafu, kweli huyu kaua anarudi tena kijijini kwake?

Halafu kama ulikuwa mpango wa ndugu wote aliyeita polisi si ni kaka yake? Kwanini asimtoroshe basi?

Nashawishika kufikili aliua akiwa hajitambui!
 

Elizabeth Dominic

Platinum Member
Dec 7, 2007
4,556
2,000
Ni Ijumaa nyingine tena, kama kawaida leo nimekuja na kesi hii ya hapa hapa nchini..............
Nawatakieni usomaji mwema, na tukutane tena Ijumaa ijayo hapa hapa MMU, nitakapokuja na kesi ambayo itawashangaza wengi.............stay tune.............!
Asante Mtambuzi kwa kesi zako za kusisimua, nasubiri kwa hamu hiyo ya wiki ijayo..................kuhusiana na kesi hii natamani tungekuwa tunaenda ndani zaidi, kwanini Baba wa mtuhumiwa alikuwa anajaribu kumfanyia cover-up mtuhumiwa kwa kisingizio cha ugonjwa..........ingefaa familia ingebanwa zaidi ili kujua hasa chanzo cha mauaji hayo
 

ummu kulthum

JF-Expert Member
Feb 6, 2012
2,785
0
umekuja na staili ya ki TZ zaidi za majuu vp?big up ningekuwa na uwezo ningekujengea gorofa ufaidi matunda ya jf members.baba ngina unajitahidi sanaaa!
 

majany

JF-Expert Member
Sep 30, 2008
1,224
2,000
mkuu asante saaana...lakini naomba wana jf tujifunze,vyanzo vya kesi hizi zote ni wanandoa kukosa uaminifu...ushauri wangu ni kwamba,kama mtu anajihisi bado hajaamua kuacha makoloni yake/au kuanzisha mengine,asikubali kamwe kuingia kwenye ndoa,ni hatari sana........NIKO KWENYE NDOA and I can feel how it hurts kwa mwenzi wako kuwa mzinzi............Mungu aepushie mbali........!!!!
 

TaiJike

JF-Expert Member
Dec 14, 2011
1,485
2,000
Bado sielewi (japo sijamliza ni ndefu nimekunwa tu kuchangia) hao wanakijiji walipita pori gani wakati wa kutafuta mwili wa marehemu ambao ulionekana kirahisi tu na familia hii ya wauaji ambao walijua ni wapi walitelekeza maiti huyo, pia lile kundi la watu ambao muuaji anadai alidhani ni nduguze wao hawakusikia pulukushani zilitokea wakati huo wa kutekeleza kitendo chake hicho cha kinyama?

Alistahili adhabu hiyo ingawa sijui kama kwa tanzania zinatekelezeka. Toka awamu ya kwanza mpaka ya nne ya maraisi wa jamhuri ya tanzania ni raisi yupi aliyetekeleza hukumu hii? naomba kufahamishwa.
 

M-bongotz

JF-Expert Member
Jan 7, 2010
1,732
1,500
Hongera Mtambuzi kwa kazi nzuri.,hebu fanya mpango wa ile kesi ya Said Mwamwindi aliyemuua Dr. Kleruu maana ile kesi hadi leo kuna different school of thoughts na it is very debatable.
 

cacico

JF-Expert Member
Mar 27, 2012
8,364
1,250
Ni Ijumaa nyingine tena, kama kawaida leo nimekuja na kesi hii ya hapa hapa nchini..............
Nawatakieni usomaji mwema, na tukutane tena Ijumaa ijayo hapa hapa MMU, nitakapokuja na kesi ambayo itawashangaza wengi.............stay tune.............!
huwa unanikuna na kesi zako, ile ya liundi agness ndio ilinikuna zaidi, mtoto alipona au?? zinafundisha sana.
 

cacico

JF-Expert Member
Mar 27, 2012
8,364
1,250
mkuu asante saaana...lakini naomba wana jf tujifunze,vyanzo vya kesi hizi zote ni wanandoa kukosa uaminifu...ushauri wangu ni kwamba,kama mtu anajihisi bado hajaamua kuacha makoloni yake/au kuanzisha mengine,asikubali kamwe kuingia kwenye ndoa,ni hatari sana........niko kwenye ndoa and i can feel how it hurts kwa mwenzi wako kuwa mzinzi............mungu aepushie mbali........!!!!

amen mkuu!
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom