Kesi namba 456 (Jamhuri vs JamiiForums): Shahidi akiri mshtakiwa namba 2 yupo kimakosa...

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,746
11,875
Wakuu, Kesi namba 456 inayowakabili Maxence Melo na Micke Williams imeendelea leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu mbele ya Hakimu Thomas Simba.

Kesi imeanza kwa kubadilishwa kwa hati ya mashtaka (ingawa shahidi wa kwanza alishasikilizwa na ushahidi kuletwa mbele za mahakama). Kikubwa kilichobadilika katika hati hiyo ni kifungu cha sheria (Kifungu cha 22(1) badala ya 22(2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao).

Tayari shahidi wa kwanza kwenye kesi hii alishafanyiwa mahojiano na kutoa ushahidi wake. Alikuwa ni kaimu ZCO, Ndg. Ramadhani Kingai (Soma Yaliyojiri katika Kesi namba 456: Jamhuri dhidi ya JamiiForums - Oilcom na Uchakachuaji/Ukwepaji kodi bandarini Dar na pia soma Sehemu ya II: Jamhuri vs JamiiForums kuhusu Oilcom na Uchakachuaji mafuta/Ukwepaji Kodi bandarini Dar

Shahidi (Peter Kayumbi): Mimi ni Mkristo, nina umri wa miaka 38 na ninafanya kazi ofisi ya upelelezi Kanda Maalum tangu mwaka 2012. Nipo kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandao na nipo katika kitengo hiki tangu mwaka 2009 kwenye hicho kitengo.

Wakili wa Jamhuri(Kishenyi) anamtaka aeleze kuhusu majukumu yake.

Peter Kayumbi: Majukumu yangu ni kusikiliza wananchi na kupeleleza kesi kisha kutoa ushahidi mahakamani.

Wakili wa Jamhuri anamtaka aeleze Disemba 13, 2016 anakumbuka nini.

Shahidi: 13/12/2016 nilikuwa ofisini mida ya saa nne asubuhi niliitwa na Mkuu wa Upelelezi (ZCO) ambaye alinikabidhi jalada CD/IR/4532/2016 likiwa linahusu kosa la kuzuia upelelezi.

Kulikuwa na faili lingine namba PE/64-2016 lilikuwa shauri jingine linalohusiana ana mbalo lilifunguliwa kutokana na taarifa iliyoletwa na Ndg. Usama Mohammed ambaye ni Meneja wa Oilcom mnamo tarehe 13/02/2016 kuwa kulikuwa na habari zilizoandikwa kwenye mtandao wa JamiiForums ambazo zilikuwa na kichwa “USHUHUDA: Hivi ndivyo mafuta yanavyoibiwa Bandarini Dar...” ambamo ndani yake ilitajwa kampuni ya Oilcom.

Pia, mnamo tarehe 15/02/2016 iliandikwa taarifa nyingine kwamba “USHUHUDA: Hii ndiyo michezo hatarishi ya Kampuni ya Mafuta ya Oilcom”. Mtumaji wa taarifa zote mbili alielezwa kuwa ni Fuhrer JF Expert Member.

Wakili Kishenyi anamuuliza kama jitihada za kupata data walizoomba toka JamiiForums zilifanikiwa…

Shahidi: Nilikusanya vielelezo ambapo polisi waliomba taarifa JamiiForums na hawakujibiwa walivyotaka. Polisi waliomba kutaka kupata taarifa za Oilcom kwa urefu zaidi pia walitaka kampata Fuhrer JF Expert Member.

Wakili Kishenyi amemuuliza kama yeye ndiye alikuwa anaandika barua na alichukua hatua gani katika kupata taarifa zaidi.

Shahidi: Barua zilikuwa zikisainiwa na ASP Fatuma, sehemu nyingine tulipofuta taarifa zaidi kuhusiana na shauri hili ni kutoka BRELA ambapo tuliomba kutambua kampuni ya Jamii Forum na wakurugenzi wake. Kwengine ni Tanzania Network Information Center(TZNIC) wanaohusika na usajili wa kikoa cha .TZ kujua kama JamiiForums imesajiliwa.

Wakili Kishenyi anamuuliza kama walipata walichokuwa wanakitaka na lini waliwakamata washtakiwa.

Shahidi: Mpaka leo hatujapata ambacho tulikuwa tunatafuta. Washtakiwa sikumbuki lini walikamatwa, Maxence alikamatwa na Afande Msangi na Mike nilimpigia simu Mimi.

Wakili anamuuliza shahidi kama ana lolote la ziada la kuieleza mahakama.

Shahidi: Hatukutumia kifungu namba 32 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao kwa sababu faili lilikuwa kwenye uchunguzi. Niliandika jalada na kulipeleka kwa mwanasheria wa Serikali (DPP).

========

Sasa anaingia Wakili wa Utetezi, Benedict Ishabakaki:

Wakili: Umesema una utaalamu wa Makosa ya Kimtandao, nikisema wewe ni ‘mtaalamu’ nitakuwa sahihi?

Shahidi: Kweli

Wakili: Nikisema uanaijua Sheria ya Makosa ya Mtandao mwaka 2015, itakuwa ni kweli?

Shahidi: Kweli

Wakili: Umesema ni wewe umekuwa ukiandaa barua kwenda JamiiForums?

Shahidi: Kweli

Wakili: BRELA walikupa wakurugenzi wangapi wa Jamii Media?

Shahidi: Watatu, lakini namkumbuka mmoja, Maxence Melo Mubyazi.

Wakili: Walikujibu hao ni wakurugenzi wa Jamii Forum au Jamii Media Co. Ltd?

Shahidi: Walikuwa Wakurugenzi Jamii Media Co. Ltd

Wakili: Umewahi kupokea taarifa za Jamii Forum?

Shahidi: Ndio

Wakili: Zilisemaje?

Shahidi: Taarifa zilieleza Jamii Media ni mwamvuli ambazo ndani yake kuna Jamii Forum

Wakili: Taarifa hizo zili-specify?

Shahidi: Kama nilivyosema awali.

Wakili: Kwanini hapa mahakamani wako washtakiwa wawili kama wakurugenzi ni watatu?

Shahidi: Mike sio Mkurugenzi, Maxence ndio Mkurugenzi

Wakili: Mtu wa tatu hakuwa shareholder?

Shahidi: Katika ufutiliaji, nilibaini Maxence ni Mkurugenzi pia Shareholder.

Wakili: Nikisema Mike yupo katika mashtaka haya kimakosa naweza kuwa nimepatia?

Shahidi: Unaweza kuwa umepatia.

Hapa Hakimu anaingilia kidogo kupata ufafanuzi kabla hajaweka katika rekodi:

Hakimu: Shahidi, ni sawa nikiandika Mike ameiingizwa kimakosa katika kesi hii?

Shahidi: Ndio

Wakili anaendelea...

Wakili: Mlishawahi kujibiwa barua na Mawakili wa JamiiForums?

Shahidi: Kweli tumewahi kujibiwa.

Wakili: Unakumbuka content ya barua?

Shahidi: Nakumbuka vingi, tofauti na Kifungu Cha 32 ni Kifungu kipi kingine kinatupa mamlaka ya kutafuta data (za JamiiForums).

Wakili: Katika barua hizo toka kwa mawakili, kuna sehemu walisema ‘Mteja wao yuko tayari kulisaidia Jeshi la Polisi’?

Shahidi:
Ndio

Wakili: Mtu alisema mteja wake yuko tayari kutoa ushirikiano anakuwa amekataa kutoa taarifa?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Unajua kuna kifungu cha kisheria kinachokutaka kuiomba mahakama kudai taarifa endapo mtoa huduma kama JamiiForums anakataa kutoa ushirikiano?

Shahidi: Ndio

Wakili: Mlikuja mahakamani kufanya hivyo?

Shahidi: Hapana

Wakili: Huko kwa ZCO, hii itakuwa sio barua ya kwanza kwenda JamiiForums?

Shahidi: Ndio, zipo nyingine

Wakili: Nitakuwa sijakosea nikisema umeidanganya mahakama kwamba barua yenu ya kwanza kwa mteja wangu ilikuwa na kifungu cha 10(2) CPA wakati barua haikuwa na kifungu hicho?

Shahidi: Si kweli, barua zetu zilikuwa chini ya kifungu cha 10(2) cha CPA

Wakili: Umewahi kusikia kuwa JamiiForums walikwenda Mahakama Kuu ku-Object barua zenu?

Shahidi: Sijawahi kusikia.

Wakili: Ulisema mlitaka mjiridhishe kama taarifa za kweli? Nani anajua ukweli wa taarifa au habari ni ya kweli au uongo kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao?

Shahidi: Tulitaka tugundue Kama kuna offence.

Wakili: Barua mliyoandika BRELA kuhusu “Jamii Forum” mliandika kipindi gani?

Shahidi: Kipindi cha upepelezi.

Wakili wa Utetezi anasema amemaliza kumuuliza shahidi maswali.

Upande wa Jamhuri unasema hauna maswali zaidi na unao mashahidi wengine wa kutoa ushahidi wao.

Hakimu anamsisitiza Wakili wa Jamhuri kuhakikisha anawaleta mashahidi wote waliobaki ili kukamilisha hukumu mapema.

Kesi itasikilizwa tena siku ya Jumatatu ya tarehe 18/12/2017. Shahidi wa kwanza, Ramadhani Kingai anatarajiwa kurudi kwa ajili ya kutoa ushahidi tena siku hiyo.
 
WAKILI :-Unajua kuwa inakutaka kuiomba mahakama..........
SHAHIDI. ndiyo

WAKILI :- Mlikuja kuiomba mahakama kama sheria inavyowataka.

SHAHIDI :- Hapana.

Watu weweeeeeeeeeeeeeee.

Ushindi huo.
 
Mungu ni mwema, husimama kwenye haki, as far as Maxence amesimamia kutomtaja 'whistle blower'' Fuhrer ambaye ni JF member, hakika wewe Melo ni shujaa!

Lakini jambo moja linanishangaza sana kwenye uendeshaji wa serikali ya awamu ya 5, ni kuwa katika vita ya uchumi, utawategemea sana 'whistle blowers'

Lakini katika serikali hii ndiyo kwanza Mkulu anaombea malaika washuke toka mbinguni waje waizime JF!
 
WAKILI :-Unajua kuwa inakutaka kuiomba mahakama..........
SHAHIDI. ndiyo

WAKILI :- Mlikuja kuiomba mahakama kama sheria inavyowataka.

SHAHIDI :- Hapana.

Watu weweeeeeeeeeeeeeee.

Ushindi huo.
Hiyo ni hoja muhimu sana, sheria inawataka waiombe mahakama kufanya hiko ambacho Polisi wamekifanya JF

Polisi hawakuiomba mahakama kufanya hiko walichokifanya!

Watashindana lakini hawatashinda.....
 
Tatizo mamlaka zetu (serikali) havipendi vitu vya "made in Tanzania", JF ni mitandao ya kijamii kama ilivyo mingine tofauti yake waasisi wake ni Watz...kama ingekuwa mtu ametumia ID FAKE ya facebook alafu ameandika tuhuma kama za oilcom sijui wangemtafuta mmilki / Mkurugenzi wa facebook atoe ushirikiano?
 
Mungu ni mwema, husimama kwenye haki, as far as Maxence amesimamia kutomtaja 'whistle blower'' Fuhrer JF member, hakika wewe Melo ni shujaa!

Lakini jambo moja linanishangaza sana kwenye uendeshaji wa serikali ya awamu ya 5, ni kuwa katika vita ya uchumi, utawategemea sana 'whistle blowers'

Lakini katika serikali hii ndiyo kwanza Mkulu anaombea malaika washuke toka mbinguni waje waizime JF!
Uongozi unahitaji Akili na Maarifa na wala sio nguvu na vitisho.

Huyu Fuhrer angestahili nishani kubwa ya Uzalendo lakini kutokana na Akili ya Mtu alivyo ndio amekuwa Adui.

Hii kesi tunashinda bila wasi wasi!!
 
Uongozi unahitaji Akili na Maarifa na wala sio nguvu na vitisho.

Huyu Fuhrer angestahili nishani kubwa ya Uzalendo lakini kutokana na Akili ya Mtu alivyo ndio amekuwa Adui.

Hii kesi tunashinda bila wasi wasi!!

Ivi huyo jamaa hata wakisema wamtafute watampata wapi,,maana Iko kifaa alichotumia kuleta iyo taarifa nakujisajiri JF nadhani kashakitupa kitambo
 
16 Reactions
Reply
Back
Top Bottom