Kesi dhidi ya JamiiForums(Namba 458): Jamhuri yahamia shtaka la pili. Ni kuhusu Benki ya CRDB

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,808
11,973
Kesi namba 458 ya Jamhuri vs Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media na mwenzake inayohusu kuendesha mtandao (JamiiForums.com) bila kutumia Kikoa cha do.TZ imetajwa tena leo Oktoba 25, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu.

Katika kesi hii, hati ya mashtaka ilikuwa na mashtaka mawili: Kutumia tovuti isiyosajiliwa Tanzania na Kuzuia upelelezi wa Jeshi la Polisi.

Siku ya leo, upande wa Jamhuri umewakilishwa na Wakili Mwandamizi Nassoro Katuga huku upande wa Utetezi ukiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala mbele ya Hakimu Huruma Shaidi.

Katika shauri hili, Jamhuri imekuja na shtaka jingine ambalo linaloihusu Benki ya CRDB (Count number 2).

Katika shtaka hili, Polisi ilimtaka Mkurugenzi wa JamiiForums kutoa taarifa kuhusu Wanachama wawili wa Mtandao wa JamiiForums.com walioandika kuhusu Benki ya CRDB, hata hivyo anadaiwa kukataa kutoa taarifa hizo.

Taarifa zilizotakiwa ni za Wanachama walioanzisha mijadala inayosomeka "Charles Kimei (CRDB) jiuzulu, kashfa ya kontena, tiketi TFF, wanafunzi na ujambazi CRDB" mjadala unaodaiwa kuanzishwa tarehe 18 Januari 2016 pamoja na "Wizi wa Banki ya CRDB - Part II" unaodaiwa kuanzishwa Machi 11, 2015.

Taarifa za Wanachama ambazo zilitakiwa kutolewa ni IP-Address, barua pepe, Majina Halisi ya Wanachama hao. Pia ilitakiwa zitolewe post zote zinazohusu Uhalifu unaofanyika katika benki ya CRDB.

Leo Jamhuri imekuja na shahidi wao, Inspekta Beatrice aliyekuwa akiumwa kwa muda kidogo na kushindwa kutoa ushahidi katika majuma mawili yaliyopita na kupelekea kuahirishwa kwa shauri hili.

Hata hivyo Shahidi huyu ameshindwa kutoa ushahidi leo kutokana na upande wa Jamhuri kuwakilisha shtaka hilo jipya bila kujua kuwa upande wa Utetezi pia ulikuwa umejipanga tayari kusikilizwa.

Upande wa utetezi ulikubaliana na ombi la Jamhuri kutaka kuahirisha kesi na kumuomba Hakimu Shaidi apange siku nyingine ya kusikilizwa kwa shauri hilo.

Hakimu Shaidi ameahirisha shauri hilo hadi Novemba 05, 2018 majira ya saa 5 asubuhi litakaposikilizwa tena

Ikumbukwe kuwa JamiiForums ilikuwa ikikabiliwa na Kesi Tatu katika Mahakama ya Kisutu ambapo Kesi moja iliyokuwa ikisikilizwa na Hakimu Godfrey Mwambapa, JamiiForums ilikutwa haina hatia

Licha ya kesi namba 458 kuendelea tena Novemba 05 Mwaka huu, Kesi nyingine namba 456 inayosikilizwa na Hakimu Thomas Simba itaendelea tena Katika Mahakama ya Kisutu mnamo Oktoba 31 mwaka huu

Kujua kinachoendelea katika Kesi zote dhidi ya JamiiForums, Tembelea Muendelezo wa Kinachojiri Kisutu: Kesi za Jamhuri dhidi ya JamiiForums - JamiiForums
 
Back
Top Bottom