Ndg wanaJF,
Kwenye mojawapo ya threads zangu, niligusia suala hili kama utani tu kwamba wakati Mkapa anaingia madarakani nchi ilikuwa katika hali mbaya sana kiuchumi. Mapato ya serikali yalikuwa madogo mno ikilinganishwa na mahitaji. Migomo ya wanafunzi ilikuwa haiishi kudai siyo nyongeza ya posho bali kulipwa posho. Wafanyakazi serikalini walikuwa wanacheleweshewa sana mishahara. Ilifika hatua kesi mahakamani zilikuwa zinaandikwa kwenye makaratasi ya kaki na wakati mwingine hata kwenye vipande vya box. Fedha ilikuwa mikononi mwa wafanyabiashara wachache tena biashara za kihuni zisizo na tija kwa uchumi wa nchi yetu. Kwa ujumla, hali ilikuwa mbaya na Serikali ilikuwa haikopesheki tena.
Alipoingia Mzee Mkapa, mambo yalianza kubadilika. Japo wananchi tayari walianza kuona mabadiliko chanya, lakini miaka mitano ya mwanzo ya uongozi wa Mzee Mkapa ilitumika katika kujenga uchumi na kuongeza mapato ya Serikali. Ndani ya miaka mitano ya mwanzo, heshima ya Serikali mbele ya wananchi na jamii ya kimataifa ilianza kuongezeka. Shughuli za uzalishaji na uwekezaji zilianza kushamiri. Mbinu za kukusanya kodi zilibuniwa na kuimarishwa. Nchi ilianza kukopesheka. Uchumi ulianza kuimarika. Kwa mara ya kwanza ndani ya miaka kumi, wafanyakazi Serikalini hususan waalimu walianza kulipwa mishahara kabla hata ya tarehe 30, mwishoni mwa mwezi. Ofisi za Serikali zilianza kupendeza na kupata heshima yake. Miundombinu mingi ilianza kujengwa ikiwa ni pamoja na barabara, simu, miradi mikubwa ya maji, na mambo mengi kadha wa kadha. Ebu tujikumbushe barabara za ndani Jijini Dar zilikuwaje kabla Mkapa, barabara ya Ubungo - Mlandizi, barabara ya Chalinze - Segera, Dodoma - Mwanza, Dar - Mtwara, Daraja la Mkapa, Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria, Uwanja wa Mkapa, Uwanja wa Ndege Songwe Mbeya, Uwanja wa Mpira wa Taifa, Jengo la Bunge, Mradi wa Maji wa Wami Chalinze, n.k, n.k. Leo hii mabasi yanasafiri kutoka Dar na kufika siku hiyo hiyo Mwz kupitia Dodoma, Singida na Shinyanga na siyo kupitia Arusha, Nairobi, Kisumu na Mara. Nikikumbuka yote haya na mengine mengi, siyo siri, najisikia machozi yanaanza kutiririka.
Pamoja na mapungufu aliyofanya Mzee Mkapa mwishoni mwa utawala wake, kama vyombo vya habari vilivyotuhabarisha, kwangu mimi Mzee huyu atabaki kuwa shujaa na kadri siku zinavyokwenda, ndivyo ninavyomwona shujaa zaidi. Ukweli ni kwamba, tukiweka kwenye mizania ya mema na mabaya, kwa mimi mwananchi wa kawaida naamini kuwa Mkapa aliitendea nchi hii mema mengi kuliko mabaya. Tena basi, hata uchafu wa EPA na mengine mengi inaonekana yalifanywa kwa msukumo wa kikundi kidogo cha mafisadi ndani ya chama tawala ili kupalilia njia ya kumhakikishia ushindi Kikwete.
Baada ya kuingia Kikwete kwa mbwembwe za USHINDI WA KISHINDO nchi ilianza kuyumba taratibu na hata chama chake kilianza kuyumba. Tena basi, ni bora hata ange-maintain yale aliyofanya Mzee Mkapa ili kulinda wananchi wake. Lakini hali ya wananchi kiuchumi ilianza kuporomoka mara tu aliposhika madaraka, tena kwa kasi ya ajabu. Bidhaa muhimu anazohitaji mwananchi wa kawaida katika maisha yake ya kila siku kwa mara ya kwanza zilianza kupanda bei kwa kasi ya ajabu, tofauti na wakati wa Mzee Mkapa. Bidhaa kama unga wa sembe, sukari, unga wa ngano, mkaa wa kupikia, mchele, maharage, n.k. sasa hazishikiki. Ukienda Serikalini kasi ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo ilianza kupungua taratibu. Miradi mingi aliyoacha Mzee Mkapa imekamilishwa chini ya awamu ya kwanza ya Kikwete kwa mbinde. Kuna rafiki yangu mmoja yupo Serikalini aliniambia kwamba isingekuwa ni mikataba iliyosaini Serikali na wakandarasi, huenda hata miradi hiyo aliyoacha Mzee Mkapa inge-collapse. Kwa hiyo nguvu iliyosukuma miradi ikamilishwe ni mikataba. Chini ya awamu ya kwanza ya Kikwete jamii ya kitanzania imeshuhudia kuporomoka kwa hali ya wananchi kiuchumi na mbaya zaidi hata kijamii na kisiasa. Masuala ya udini yameibuka kwa kasi na kutishia mshikamano wa wananchi. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, wafanyakazi kupitia chama chao waligoma kuwaalika viongozi wa Serikali kuhudhuria sherehe za Mei Mosi. Kwa mara ya kwanza katika historia ya vyama vingi nchini, hotuba ya rais ya ufungzi wa Bunge inasusiwa na wabunge kwa kutoka nje ya ukumbi. Zipo rekodi nyingi sana zilizoweka chini ya uongozi wa Kikwete.
Sasa mwaka huu, Kiwete ndiyo ameanza awamu yake ya pili na ya mwisho. Hali ndiyo inaendela kuwa mbaya zaidi. Migomo mingi nchi nzima, maandamano kila kukicha, miradi ya maendeleo imesimama, bei za bidhaa zinapanda kila kukicha, mishahara imeanza kucheleweshwa, huduma muhimu kama umeme na maji zimeanza kuporomoka na bei zake kupanda, ada za shule zinaongezeka. Hivi sasa watumishi wengi wa Serikali waliokuwa busy na shughuli za miradi enzi za Mzee Mkapa wametulia maofisini wanasoma magazeti. Kwa ujumla, hali inaendelea kuwa mbaya siku hadi siku. Wananchi wengi mitaani wameanza kukata tamaa ya maisha. Wengi wanaona kama 2015 ipo mbali sana.
Sasa kwa mwenendo huu kwa nini nisiamini kwamba MKAPA ALIJENGA NA KIKWETE ANABOMOA?
huna jingine mkuu la kuongezea!???kila awamu ina mapungufu yake ni makosa kudhani kuna awamu ya utawala haikuwa na mapungufu. Awamu ya nne inaweza kuwa na mapungufu lakini kusema anabomoa kazi za mkapa ni lugha kali ambayo inaonyesha kwamba kikwete hajafanya lolote pengine kwamba hata chuo kikuu cha dodoma anabomoa kazi ya mkapa
Du hivi kweli mnasahau waandhishi wa habari walivyokuwa wanabanwa, leo dunia imepanuka vyombo vya habari vipo huru mwenye uwezo unangalia AlJazeera
Bunge letu waliokuwa wanaikosoa hasa kutoka CCMwalikuwa wanaitwa Chamwino kukosolewa na kubanwa wasiseme lolote.
JK kuachia vitu vyote kuwa na uwazi mnamfananisha na Mkapa? ni nani alimweka ROSTAM kuwa mweka hazina wa chama na kuchota hela BOT wakati JK akiwa Wizara ya NJE
Tangold,meremeta, Deep green, Kiwira, ANBEN, EPA angalieni ni za mwaka gani?
mm JK bado nampa :first:
Uliyosema ni kweli lakini mwananchi wa kawaida anayekwenda kununua unga wa sembe kwa sh. 800 kwa kilo badala ya sh. 300, sukari sh. 2,000 badala ya sh. 600 na mchele sh. 1,800 badala ya sh. 650 lazima ATAMKUMBUKA DAIMA MKAPA. Hayo masuala ya NBC, Deep Green na ANBEN mnayayujua ninyi mnaosoma magazeti.
Kila awamu ina mapungufu yake ni makosa kudhani kuna awamu ya utawala haikuwa na mapungufu. Awamu ya nne inaweza kuwa na mapungufu lakini kusema anabomoa kazi za Mkapa ni lugha kali ambayo inaonyesha kwamba kikwete hajafanya lolote pengine kwamba hata chuo kikuu cha Dodoma anabomoa kazi ya Mkapa
Hoja yako ni ya msingi na ninakubaliana na wewe. Nadhani unachotaka kieleweke ni kwamba udhaifu wa Kikwete usimtakase Mkapa. Sasa swali langu ni je, baada ya kugundua udhaifu huo ambao umepelekea umeme na huduma zingine kuwa juu, Kikwete amefanya nini ndani ya miaka takriban sita sasa ya uongozi wake? Mbona naona kama madudu yanazidi kuongezeka badala ya kupungua? Mwl. Nyerere aliwahi kutuasa kwamba kila serikali lazima itafanya makosa yake maana serikali haziongozwi na malaika. Jambo muhimu ni kwamba serikali mpya inapoingia inarekebisha makosa na kuendeleza mazuri na ya msingi ya serikali iliyopita. Kwa mtazamo ndugu yangu Nguruvi3 unadhani hali hii ndiyo inayotokea sasa chini ya uongozi wa Kikwete?? Nisaidie tafadhali.