Kero lukuki, wajumbe mmh!

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Kero lukuki, wajumbe mmh!

Ncheme, nchicheme? Novemba 7, 2007
Raia Mwema

KWA tuliofuatilia, kwenye luninga, Mkutano Mkuu wa CCM, uliomalizika Dodoma, mwishoni mwa wiki, ‘poa’ ndiyo neno moja sahihi la kuelezea hali ya mkutano huo wa siku mbili ilivyokuwa.

Mambo yalikuwa ‘poa’ kweli kweli; kana kwamba nchi nzima ni ‘poa’kabisa na hakuna kero wala dhiki yoyote inayowakabili wanachama wa chama hicho tawala; achilia mbali Watanzania wasio wanachama wa chama chochote cha siasa.

Katika hali ya kawaida, ripoti ya utendaji ya mkutano mkuu wowote, uwe wa chama cha siasa, cha ushirika au hata NGO, huzua majadiliano makali na hoja zinazokinzana hadi mwafaka unapopatikana. Lakini si Mkutano Mkuu wa CCM; angalau sivyo tulivyoshuhudia, majuzi, mjini Dodoma.

Mkutano huo ulikuwa ‘poa’ mno. Bila shaka ni ‘poa’ya wajumbe wa mkutano huo katika kuijadili ripoti ya utendaji ya chama hicho iliyomfanya, baadaye, Mwenyekiti Kikwete kuchezacheza kitini wakati Banana Zorro na wenzake walipoimba, ukumbini, ule wimbo maarufu wa Bongo Flavour wa “Presha eeh Presha”, ukiwa na vidokezo vya kwamba wapinzani wanapata presha.

Kwa hakika, Kikwete alikuwa na kila sababu ya kuchezacheza kitini wakati Banana Zorro na wenzake wakiimba wimbo huo. Hakuwa na presha. Hakuwa amekalia kiti moto; hakupata presha yoyote hata pale ripoti ya utendaji ya chama hicho ilipowasilishwa.

“Ukurasa wa kwanza?” (kimya), ukurasa wa pili? (kimya), ukurasa wa tatu? (kimya), ukurasa wa nne? (kimya)…. ukurasa wa 20? (kimya)…ukurasa wa 40? (kimya); hivyo hivyo Mwenyekiti Kikwete akamaliza ripoti nzima ya utendaji bila mjadala wowote mzito. Ripoti ikapitishwa kama ilivyowasilishwa.

Ni dhahiri wanetu na wajukuu zetu watakapokuja, miaka ijayo, kufanya utafiti na kupitia rejea (miniti) za mkutano huo mkuu wa CCM, watatushangaa, na pengine watatukana kwamba wao si uzao wetu.

Na watakuwa na kila sababu ya kufanya hivyo. Watajiuliza: Iweje mkutano mkuu wa chama tawala, wenye wajumbe 1,922, upoe kiasi hicho? Iweje ripoti yake ipitishwe hivi hivi bila mjadala wowote?

Inakuaje mkutano mkuu wa chama tawala, unaofanyika katika kipindi ambapo kuna hoja lukuki za wananchi, kuanzia za ufisadi hadi za kupanda kwa gharama za maisha (kumbuka bei ya mafuta ya taa), saruji n.k), utawaliwe tu na hotuba za viongozi zisizojadiliwa?

Kero na hoja ni nyingi. Kuna madai (kwa mfano) kutoka kwa watu kama Joseph Butiku kwamba CCM hakina dira. Akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti Kikwete aliwakejeli wanaotoa madai hayo, lakini hakuwafafanulia wajumbe dira ya CCM ni ipi.

Kama mmoja wa wanachama wa siku nyingi wa Chama anasema kwamba hakuna dira, ilikuwa ni juu wa wajumbe kumbana Mwenyekiti wao ili suala hilo lijadiliwe: Kuna dira au hakuna dira, na kama ipo ni ipi? Lakini halikujadiliwa kwa sababu hakuna mjumbe aliyeomba ufafanuzi. Wote kimya.Lakini pia yapo madai ambayo yametanda nchi nzima kwamba CCM kimewakumbatia matajiri na kuwatosa wanyonge, na kwamba si chama tena cha wafanyakazi na wakulima. Hilo nalo lilipaswa kujadiliwa, lakini halikujadiliwa kwa sababu wajumbe waliamua kukaa kimya.

Jingine ni suala la kuongezeka kwa kasi kwa pengo kati ya matajiri na masikini, kati ya walio nacho na wasio nacho. Hili nalo lilipaswa kuibuliwa na wajumbe wa mkutano mkuu ili lijadiliwe, lakini wapi! Najua kuna watakaosema kwamba CCM haina utamaduni wa kujadili au kuulizana maswali kwenye mkutano wake mkuu, lakini katika dunia ya sasa na changamoto za leo zinazoikabili, hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa?

Yaani; mjumbe asafiri kwa taabu kwa treni kutoka Kasulu (kwa mfano) hadi Dodoma, akiwa na zigo la kero za wananchi anaowawakilisha, tena akifika Dodoma alale nje kwa kukosa chumba, na kisha wakati wa mkutano akae kimya muda wote! Si bora angebaki tu Kasulu?

Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba mkutano huo mkuu ulikuwa poa mno, na kwamba mpaka ulipomalizika si Mwenyekiti Kikwete au viongozi wenzake, waliweza kupata hisia zozote za wajumbe wa mkutano ule kuhusu masuala ya chama na kero za wananchi, hususan wale wa vijijini.

Kama huo ndiyo utamaduni wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM; kwamba wao ni watu wa kuwasikiliza tu viongozi wakisoma ripoti zao, basi, huo ni utamaduni uliopitwa na wakati.

Hotuba tamu tamu za Mwenyekiti Kikwete, au ripoti za utendaji za Katibu Mkuu, Yusuf Makamba na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, hazikustahili kupita hivi hivi bila kujadiliwa na wajumbe waliotoka mbali wakiwa na zigo la kero za wananchi wa huko walikotokea.

Kama mjadala ungekuwepo na ukapamba moto, hisia halisi za wananchi, hususan wa vijijini, zingefahamika. Wakulaumiwa kwa hili ni wajumbe wenyewe. Ni dhahiri ni waoga, hawajiamini, si jasiri, na bila shaka waliogopa kuitwa wasaliti au kuambiwa “huyu si mwenzetu”.

Kina Kikwete na viongozi wenzake lazima waibadilishe hali hii kwa kuwapa wajumbe mazingira ya kujiamini na ujasiri wa kuuliza na kuhoji.

Maana, hizi si zama za “zidumu fikra za mwenyekiti”. Hizi ni za zama za www.com. Hizi ni zama za kufikiri yale ambayo yalikuwa hayafikiriwi mwanzoni. Hizi ni zama za kuhoji yale ambayo zamani yalikuwa hayahojiwi. Ni zama za kupinga, kubisha, kuomba ufafanuzi na kurekebishana.

Mwenyekiti Kikwete alisema CCM si chama cha migogoro; kwamba migogoro si mila au utamaduni wa CCM. Sawa. Lakini kuhoji yasiyoeleweka au yasiyokwenda sawa ni kukaribisha migogoro? Nionavyo ni kinyume chake. Kuhoji na kujadiliana huzuia migogoro isiibuke.

Hali hii ya wajumbe kukaa kimya si afya nzuri kwa chama chochote cha siasa. Afya ni kujadiliana na kuambizana ukweli hadi mwafaka unapatikana.

Mungu jalia Makamu mpya wa Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa ameiona kasoro hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano huo, Msekwa alisema kwamba katika uongozi wake atahamasisha uhuru wa mawazo na kuruhusu mijadala kwa viongozi na wanachama hata kama una mtazamo tofauti.

“Chama kinapenda wanachama wake wakue kihoja, wawe ni watu ambao wanakuwa na maoni tofauti yenye lengo la kuimarisha chama, kwa kweli hilo ni moja ya mambo muhimu sana katika Chama”, alisema mzee huyo.

Na kama Msekwa hakuyasema hayo kufurahisha genge (la waandishi), kama atasimamia uanzishwaji wa utamaduni huo mpya ndani ya chama, basi, pengine mkutano mkuu wa mwaka 2012 utakuwa na uhai zaidi kuliko huu wa mwishoni mwa wiki. Na hiyo ndiyo itakuwa salama ya chama chenyewe.
 
Back
Top Bottom