Kenya: Wagombea wamiminika Tanzania kupata huduma za waganga kutwaa ushindi Agosti 8

Ghazwat

JF-Expert Member
Oct 4, 2015
23,718
66,266
Huku siku ya Uchaguzi ikizidi kukaribia, idadi ya wawaniaji kutoka Kaunti za Migori na Homa Bay wanasafiri hadi Tanzania kusaka huduma za waganga imeongezeka lengo likiwa moja, kutwaa ushindi baada ya Agosti 8 mwaka huu.

Wanasiasa wanaowania viti mbalimbali wamekuwa wakisafiri hadi miji ya Tarime, Musoma na Mwanza kutafuta usaidizi wa' nguvu za kiza' kumwezesha kupata ushindi bila jasho

Inadaiwa waganga wamekuwa wakiwapa wanasiasa hirizi ili kuwapokonya wapinzani wao wapiga kura. Wengi wa wawaniaji hao walianza kumiminika nchini Tanzania mwezi Februari kabla ya michujo kufanywa.

Ripoti ya 'Taifa leo' inaonyesha kuwa wanasiasa hao wanaamini kuwa waganga wana uwezo wa kuhakikishia ushindi katika kinyany'anyiro cha Agosti.

"Wengi wa wawaniaji wanaamini kuwa hawawezi kupata ushindi bila usaidizi wa nguvu za kishetani. Tumekuwa tukiwaona wengi wao wakipitia hapa na kuingia Tanzania", akasema Bw. George Ogwang, wakala wa ukaguzi wa mizigo katika eneo la mpakani la Isebania

"Ninamjua mmoja wa Wanasiasa ambaye alipokea huduma za waganga hao na bado akabwagwa kwenye mchujo", akaongeza.

Bw. Mohamed Yahya ambaye ni mganga wa Tarime mjini aliambia Taifa leo kwamba ni kawaida kwa biashara kunoga kila mara Kenya ikikaribia Uchaguzi Mkuu.

"Wao huja kupata huduma zetu na wanalipa pesa zozote ambazo tunawaitisha", akasema.

Wasaidizi wa karibu wa wanasiasa mbalimbali walikiri kuwa waajiri wao huamini usaidizi wa waganga.

Itakuchukua saa nne kusafiri kutoka Migori hadi Mwanza lakini ni dakika 50 tu kwa gari la kibinafsi kusafiri hadi Tarime.

Chanzo: TaifaLeo
 
Back
Top Bottom