Hivi kemikali aina ya ethylene hutumika katika kuivisha ndizi? Na vipi kwenye masoko ya Dar es salaam inatumika?
- Tunachokijua
- JamiiCheck imepitia tafiti mbalimbali ikiwemo iliyochapishwa na maktaba ya taifa ya dawa nchini Marekani (NIH) ambao wanaeleza kuwa kuiva (kwa matunda) ni suala la vinasaba ambalo lisilojirudia linalojumuisha mabadiliko mengi ya kikemikali na kibaiyolojia ikiwemo kulainisha tishu, mabadiliko ya rangi, harufu na uzalishwaji wa ladha, kupunguza ukakasi, na mengine mengi. Ndizi ni moja ya matunda yanayotumiwa zaidi duniani hivyo ni muhimu kuwa makini na ndizi za biashara kuanzia uvunaji na usambazaji wake ili kuhakikisha zina rangi nzuri, umbile na muonekano unaofanana.
Tafiti hiyo inaeleza pia kuwa uivishaji wa ndizi unaweza kufanywa kwa njia za kisasa kwa kutumia kemikali mbalimbali ikiwemo ethylene, ethephon na acetylene. Lakini njia za asili pia ikiwemo moshi unaotokana na kuchoma majani mabichi au moto wa jiko la mafuta ya taa zinaweza kutumika pia. Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa ndizi zilizoiva zenyewe ki asili zinaonekana kuwa na sifa bora zaidi kuliko zilizoivishwa kwa njia za kisasa.
Ukweli upoje kuhusu matumizi ya kemikali za kuivisha ndizi Dar es salaam?
Kaimu meneja tathmini ya viatarishi katika chakula kutoka shirika la viwango nchini (TBS) Emakulata Justine alipokuwa akifanya mahojiano na Shirika la habari Tanzania kuhusiana na suala hilo alisema kuwa ndizi huwa zinaivishwa kwa joto mara baada ya kuwekwa katika kontena ambalo linakuwa na kiwango maalumu cha joto kutoka kwenye AC lakini pia alikiri wakati mwingine kemikali hutumika katika zoezi hilo la kuivisha ndizi ambapo kemikali itumikayo ni Ethylene
“Wakati mwingine unaweza ukalazimika kutumia ethylene ambayo inatengenezwa kiwandani ambayo ni salama na imeruhusiwa kitaalamu”
Shirika la viwango Tanzania (TBS) tarehe 13-10-2024 wametoa taarifa kwa umma kupitia barua waliyoiweka katika kurasa zao za mitandao ya kijamii wakieleza kuwa kutokana na uchunguzi wao wa awali katika masoko mbalimbali ya jiji la Dar es salaam wamebaini kuwa wafanyabiashara hutumia gesi ye Ethylene kwa ajili ya kuivisha matunda hayo ambapo wamesema kuwa huo ni utaratibu wa kawaida ambao unatumika duniani kote.