Kauli za wanawake wakiwa na hasira zatajwa kuwa sababu ya wanaume kupima DNA

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,010
9,874
Mwanasheria wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Abeid Kafunda ametaja baadhi ya mambo yanayochangia wazazi wanaume kutaka kujua uhalali wa mtoto au watoto kwa kutumia kipimo cha vinasaba (DNA).

Kafunda alilieleza HabariLEO ofisini kwake jijini Dar es Salaam kuwa mambo hayo kuwa ni pamoja na maneno ya baadhi ya wazazi wa kike wanayoyatamka kwa mzazi wa kiume hasa wanapokuwa na hasira.

Kafunda alisema baadhi ya wazazi wa kike huwatamkia wazazi wa kiume kwamba “Unajifanya unampenda huyu mtoto, una uhakika gani kama ni mtoto wako.”

Alisema mzazi wa kike anaweza kutoa kauli kama hiyo katika hali ya kawaida, lakini ikampa mashaka mzazi wa kiume na kumfanya atake kipimo cha DNA ili kujiridhisha kama kweli mtoto ni wa kwake au la.

Kafunda aliitaja sababu nyingine ni migogoro katika familia. Alisema migogoro katika familia inapozidi na ambayo mara nyingi husababishwa na tabia za uzinzi, humfanya mzazi wa kiume kuwa na mashaka na kutaka kujiridhisha uhalali wa mtoto anayeishi naye.

“Sababu nyingine ya wazazi kutaka kipimo cha vinasaba ni kutokufanana kwa baadhi ya watoto katika familia. Imejengeka kwenye baadhi ya jamii kwamba watoto wa mzazi mmoja wanatakiwa wafanane baadhi ya viungo, kwa hiyo inapotokea mtoto mmoja kutokufanana na wenzake inaweza kumpa mashaka mzazi wa kiume na kutaka kufanya kipimo cha vinasaba,”alisema Kafunda.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni mirathi kwenye familia. Alisema mirathi ni moja ya mambo yanayosababisha wazazi wanaume kutaka kipimo cha vinasaba ili kujua uhalali wa mtoto au watoto katika familia wanaopaswa kupata haki ya mirathi.

Alisema mirathi ni suala nyeti lakini pia ni utamaduni uliozoeleka na wa kisheria. Alisema sheria zikiwemo za kidini, utamaduni na sheria za serikali zinatambua mirathi.

Kwa mujibu wa Kafunda, sheria hizo zinampa mzazi haki ya kutaka kujiridhisha kwamba mirathi yake baada ya yeye kufariki dunia inakwenda kwa mtu anayestahili.

Kwa mujibu wa Kafunda, sababu nyingine inayosababisha wazazi wanaume kuomba kufanya kipimo cha DNA ni kutaka kujiridhisha kwenye suala la matunzo hasa kwa watoto ambao wamepatikana nje ya ndoa.

Kafunda alisema hali hiyo imewafanya baadhi ya wazazi kutaka kujiridhisha kama kweli mtoto ni wake ili atoe matunzo ikiwemo chakula, elimu, na matibabu.

Utaratibu wa DNA
Kwa kuwa suala la vinasaba vya binadamu ni suala nyeti na linalohusisha mtu mmoja mmoja, vikundi vya watu na serikali, hivyo Sheria Namba 8 ya Mwaka 2009 na kanuni zake ndizo zinazofanya suala hilo kuwa la kisheria.

Kafunda alisema Kifungu cha 25 cha sheria hiyo kimeorodhesha vyombo vinavyotambulika kisheria kwa ajili ya kumuombea mtu au taasisi kupata huduma ya kipimo cha vinasaba.

Alivitaja vyombo au mamlaka zinazoweza kuomba kipimo cha vinasaba kuwa ni Mahakama, hospitali pale inapotokea suala la kitabibu, mkuu wa wilaya yanapotokea majanga, Polisi kwenye masuala ya jinai, wanasheria wa kujitegemea na ustawi wa jamii ambao mara nyingi hupokea migogoro ya kifamilia ikiwemo kutaka kujua uhalali wa wazazi kwa mtoto.

Mtaalamu wa vinasaba wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Fedelis Bugoye alisema huduma ya uchunguzi wa vinasaba wa kubaini uhalali wa mtoto ni uchunguzi wa kitaalamu unaofanyika kwa lengo la kutaka kubaini mahusiano yaliyopo kati ya mtoto na mzazi au watoto na mzazi.

Bugoye alisema uchunguzi huo unafanyika kwa kuchukua sampuli kutoka kwa wazazi na mtoto au watoto ili kuangalia mpangilio wa vinasaba uliopo kwa watoto na kuthibitisha uhalali wa watoto hao kwa wazazi.

Sampuli inayochukuliwa
Bugoye alisema kwa kuwa vinasaba ni chembechembe za urithi hivyo sampuli inayotumika katika uchunguzi wa vinasaba ni sehemu yoyote ya mwili wa binadamu ambayo inaweza kuwa na seli kwa kuwa vinasaba vinapatikana ndani ya seli.

Alisema sehemu hizo za mwili inaweza kuwa nywele, ngozi, jino, kucha, damu na sehemu nyinginezo na isitoshe sheria inataka sampuli ya vinasaba ichukuliwe ile ambayo ni rahisi kuipata na isiyoumiza.

Bugoye alisema njia rahisi ambayo sampuli inaweza kuchukuliwa bila kumuumiza mtu ni njia ya mpanguso wa kinywa kwa kutumia kifaa maalumu kwa watu wanaotaka kujua uhalali wa mtoto japo katika mazingira yanayohusu makosa ya jinai zinaweza kuchukuliwa sampuli za aina mbalimbali ikiwemo mkono, damu, ngozi na sehemu zingine za mwili.

Alisema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inapata maombi ya huduma ya uchunguzi wa vinasaba kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuwa majibu wanayotoa yanakubalika kimataifa.

Gharama za kipimo
Kafunda alisema gharama za uchukuaji wa sampuli za vinasaba ni Sh 100,000 kwa kila mtu hivyo kama kipimo kinamhusisha baba, mama na mtoto kwa pamoja watatakiwa kulipa Sh 300,000, lakini gharama hiyo huongezeka kwa kila mtoto anayeongezeka.

Alisema baada ya sampuli kuchukuliwa, majibu ya vipimo yanatoka ndani ya siku 14 tofauti na zamani ilikuwa inachukua siku 21 kupata majibu.

Kafunda alisema majibu ya wazazi wanaotaka kujua uhalali wa mtoto katika familia yanakabidhiwa kwa mamlaka ombaji akiwemo mwanasheria wa kujitegemea au Ofisa wa Ustawi wa Jamii ambao ndiyo Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inawatambua na kisha mamlaka hizo ombaji zinakabidhi majibu kwa wazazi.

Chanzo: HabariLeo
 
Wanajiuliza mi ni msela ama niga, maana sicheki nao wakinikera napiga.../
 
Kama ndugu (brothers) wa baba na mama mmoja mmekula manzi mmoja hiyo DNA itaweza kumtambua baba halali?
 
mimi tumegombana na mke wangu ,tukatengana, mamaake mzazi (mama mkwe wangu)akanitamkia kuwa yule mtoto sio wangu anababaake, dah, hapo ni baada ya kugoma kutoa matumizi ya laki 2 kwa mwezi, yani mtoto anamiaka 2.
 
Back
Top Bottom