Kauli ya JK kuhusu elimu yakoroga wapinzani

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Date::11/23/2008
Kauli ya JK kuhusu elimu yakoroga wapinzani
Exuper Kachenje
Mwananchi

KAULI ya Rais Jakaya Kikwete kuwa serikali yake haikubaliani na matakwa ya wanafunzi kudai wakopeshwe asilimia 100 ya gharama za masomo, imepokelewa kwa hisia tofauti na wanasiasa wakieleza kuwa kwa msimamo huo taifa linaelekea gizani na kwamba athari zake hazitakawia.

Serikali imefunga vyuo vyake saba kutokana na wanafunzi kugoma kuingia madarasani wakishinikiza sera ya uchangiaji elimu ibadilishwe na kama itaendelea, basi wanafunzi wakopeshwe kwa asilimia mia badala ya mpango wa sasa (means testing) ambao huchambua uwezo wa familia ya mwanafunzi na kuwapanga kwa makundi.

Vyuo vilivyofungwa ni Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu (Duce), Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara (MUCCOBS), Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam (DIT).

Rais alikuwa akitegemewa kuingilia kati sakata hilo, lakini alipoingilia hakutoa nafuu kwa wanafunzi na wazazi baada ya kusema kuwa sera ya uchangiaji haitaondolewa, akifafanua kuwa enzi za serikali kutoa elimu bure zimeshapita.

Msimamo huo wa Rais Kikwete umepokelewa kwa hisia tofauti.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa alisema kuwa hatua hiyo inaonyesha jinsi serikali isivyotilia maanani suala la elimu na kwamba nchi yoyote isiyotoa kipaumbele kwa elimu, ipo katika giza.

Dk Slaa alisema iwapo serikali haitawekeza katika elimu kuna hatari kubwa ya kuongeza tofauti kati ya watoto wa walala hoi na wale wa vigogo ambao aliwaelezea kuwa wanapata mahitaji stahili kutoka kwa wazazi wao, hivyo kuibua matabaka na kuyakuza.

"Matunda ya kauli ya Rais Kikwete yataonekana muda mfupi ujao... nchi yoyote isiyotoa kipaumbele kwa elimu, 'future'(hali yake ya baadaye) yake ipo katika giza. Kama haiwekezi kwenye elimu itaongeza matabaka ya wenye nacho na walala hoi," alisema Slaa.

Aliongeza kuwa matokeo ya sera mbovu katika elimu na matabaka ya wenye nacho na wasio nacho yameonekana pia hivi karibuni wanafunzi wa vyuo vikuu, walipofukuzwa kutokana na watoto wa matajiri kufuatwa na magari ya kifahari kama Toyota Land Cruiser (shangingi), huku walalahoi wakiachwa vyuoni na hata kutafuta mikokoteni.

Alisema nchi hivi sasa ipo kinyume na alivyotaka Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere na kuwa hali hiyo ni hatari na kwamba, viongozi wasitafute visingizio vya matatizo yaliyopo, badala yake wawe wabunifu ili kuinusuru nchi isiangamie. Alishauri serikali itumie rasilimali zilizopo na fedha inazokusanya ili kuboresha elimu, afya na miundombinu.

Naye mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof Ibrahim Lipumba alisema kauli ya Rais Kikwete, ni matokeo ya mpango mbaya wa matumizi katika serikali yake na kwamba hali hiyo inadhoofisha elimu nchini.

Alisema tatizo ni kwamba Rais Kikwete hajatulia wala kukaa ofisini na kufanya uchambuzi wa mambo yanayolihusu taifa na kwamba akitulia na kutafakari, anaweza kupata ufumbuzi kwa manufaa ya Watanzania wote.

Alisema iwapo Kikwete na serikali yake ingekuwa na mipango mizuri ya kutumia vizuri maliasili za taifa, migogoro kama hiyo ya wanafunzi isingetokea.

"Hayo ni matokeo ya mpango mbaya wa matumizi ya serikali ya Kikwete. Hajatulia, hakai ofisini akafanya uchambuzi wa mambo... yeye kila siku safari na mikutano tu. Akitulia, kufanya uchambuzi wa mambo, akatafakari, atajua nini la kufanya kwa manufaa ya Watanzania," alisema Lipumba aliye safarini mkoani Mbeya.

Aliongeza kuwa sera ya kuchangia elimu ya juu haitekelezeki na kuwa ni bora Kikwete akatumia fedha zilizorejeshwa na watuhumiwa wa wizi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kuondoa tatizo hilo la wanafunzi wa elimu ya juu.

Alisema zinahitajika Sh23 bilioni ili kujazia katika fungu la Sh117 bilioni ambalo Bodi ya Mikopo imetengewa mwaka huu, ili kukopesha wanafunzi wote kwa asilimia 100 ya gharama za masomo.

Naye, Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Agustino Mrema alimtaka Rais Kikwete na serikali yake kuangalia upya sera hiyo ya uchangiaji ambayo imekuwa ikikumbana na vikwazo tangu mwaka 1994 ilipoanzishwa.

"Naona Kikwete analiweka pabaya taifa kutokana na kauli hiyo. Ni busara kwake na serikali kuangalia upya sera ya uchangiaji kwa maslahi ya taifa," alisema waziri huyo wa zamani wa serikali ya awamu ya pili.

"Mfumo mzima na sera ya uchangiaji elimu ya juu una dosari nyingi na umegubikwa na harufu ya rushwa kwa sababu wanaostahili mikopo wanakosa na wasiostahili wanapewa, wasiostahili alisema ni watoto wa vigogo na watu wenye uwezo kiuchumi.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Anthony Machibya alisema serikali yake itatoa tamko rasmi dhidi ya kauli hiyo ya Rais Kikwete.

Wakati huohuo, serikali imesema uamuzi wa kufunga vyuo vikuu utaisababishia serikali hasara kubwa.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Gaudensia Kabaka alikiri hayo wakati akitoa msimamo wa serikali kuhusu sera ya uchangiaji wa elimu ya juu na hatua zilizochukuliwa na serikali.

"Zipo hasara zitokanazo na kufungwa kwa vyuo vikuu hapa nchini ambazo serikali imezipata, lakini ni vigumu kubashiri kwa sasa ni kiasi gani hadi hapo tutakapofanya uchunguzi na kugundua kiasi hicho na ndipo tutaueleza umma wa Watanzania upate kuelewa," alisema Kabaka.

Alidokeza kuwa moja na hasara inayoonekana dhahiri ni mishahara ambayo inalipwa kwa wafanyakazi wa vyuo hivyo bila ya wao kufanya kazi.

Alisema kutokana na serikali kutambua hilo imeziagiza kamati za vyuo kufanya uchambuzi wa majina ya wanafunzi wanaokubaliana na sera ya uchangiaji na kuwarudisha haraka vyuoni, ili waendelee na masomo.

Kutokana na kufungwa kwa vyuo hivyo, polisi inamshikilia aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (TAHLISO), Julius Mtatilo na imemfukuza nchini mwanafunzi kutoka Uganda, Odong Kefa Odwar, ambaye amedaiwa kuvunja sheria za nchi kutokana na kujihusisha na siasa na uchochezi wa migomo vyuoni.
 
Back
Top Bottom