Kauli ya Cleopa Msuya kuhusu umeme ifanyiwe kazi!

joseeY

Senior Member
Nov 4, 2010
108
17
HADHARI iliyotolewa juzi na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya kuhusu athari zinazoweza kutokea kufuatia uhaba mkubwa wa umeme unaolikabili taifa letu hivi sasa lazima ipewe umuhimu stahiki.

Akichangia wakati wa mjadala wa kitaifa kuhusu miundombinu, nishati na madini katika Wiki ya Maonyesho ya Miaka 50 ya Uhuru yaliyoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), kiongozi huyo alionya kwamba, hali ya uhaba wa umeme ikiendelea hivi pasipo kudhibitiwa tusishangae kutokea kwa mambo kama yaliyotokea katika nchi za Kiarabu ambazo wananchi wake wameshindwa kuvumilia ugumu wa maisha na kuamua kuandamana.

Akionekana kufadhaishwa na athari za kiuchumi na kijamii ambazo zimetokana na hali hiyo ya uhaba mkubwa wa umeme, aliitahadharisha Serikali kuwa makini na tatizo hilo, huku akisema linaweza kusababisha matatizo makubwa kiasi cha kuifanya nchi isitawalike. Kiongozi huyo ambaye alikuwa waziri mkuu kati ya mwaka 1980 na 1983 na kushika tena wadhifa huo mwaka 1994, mbali na kuongoza wizara mbalimbali, zikiwamo fedha, viwanda na biashara.

Tunalichukulia onyo la kiongozi huyo mstaafu kwa uzito mkubwa kutokana na uzoefu na utumishi wake uliotukuka alipokuwa mtumishi katika ngazi hizo za juu serikalini, kwani yeyote mwenye kumbukumbu ya rekodi yake ya utumishi atakubaliana na ukweli kwamba alisimamia vyema masuala ya kukuza uchumi alipokuwa waziri mkuu na hata alipokuwa akiongoza wizara hizo zinazoshughulikia masuala ya fedha, biashara na viwanda.

Kwa misingi hiyo, kauli yake siyo ya kubeza hata kidogo, hasa tunapotilia maanani ukweli kuwa, tangu Serikali ibanwe na Bunge na kulazimika kutangaza mpango wa dharura wa Sh1.2 trilioni kukabiliana na mgao wa umeme Agosti, mwaka huu, hadi sasa hakuna mabadiliko yoyote ya maana yaliyoonekana. Tangu kutangazwa kwa mpango huo ambao uliwapa wananchi matumaini makubwa ya kumalizika kwa tatizo hilo la umeme mapema iwezekanavyo, hali imezidi kuwa tete na kufifisha kabisa matumaini hayo ya wananchi.

Tunakubaliana na kiongozi huyo mstaafu kuwa, Serikali inalo jukumu la kuimarisha mazingira yatakayoendeleza uchumi na kwamba ipo changamoto ya kuziunganisha sekta binafsi ili kusaidia kuinua uchumi badala ya kujidanganya kwamba ni Serikali pekee inayoweza kufanya kazi hiyo. Tunakubaliana naye pia anaposema kwamba tatizo la Serikali hivi sasa ni namna ya kujipanga kukubaliana na sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wake na kuwainua wananchi kibiashara kwa sababu miundombinu ya uzalishaji, hasa umeme bado haijasambaa katika mikoa yote.

Ndiyo maana tumekuwa tukisema kwamba ni aibu na fedheha kubwa kwamba ni asilimia mbili tu ya wananchi waishio vijijini wanaopata nishati ya umeme. Ni aibu pia kuwa, sehemu kubwa ya asilimia hizo mbili za watu waishio vijijini ambayo inapata umeme inaishi katika sehemu ndogo tu ya nchi. Sehemu nyingi ya watu waishio vijijini bado wanaishi gizani, mbali na kuona nguzo za umeme zikipita angani zikipeleka umeme kwa watu waishio mijini.

Wananchi wamechoka na hadithi na ngonjera za kuwapo mipango ya kupeleka umeme vijijini ambazo zimekuwapo kwa muda mrefu sasa.
Wadau wa nishati ya umeme na mafuta ya dizeli na petroli wamekuwa wakikatwa fedha kila wanaponunua bidhaa hizo ikiwa ni kodi ya kupeleka umeme vijijini (Rural Electrification Tax). Haijulikani fedha hizo zinafanya kazi gani na ndiyo maana tunadhani kwamba Sh16 bilioni zilizotolewa na Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) juzi kama msaada wa kupeleka umeme vijijini hazitaonyesha matokeo yenye mashiko.

Tunampongeza kiongozi huyo mstaafu kwa kuitaka Serikali iiunganishe mikoa yote hapa nchini kwa kuipelekea umeme ili wananchi waweze kunufaika na kilimo cha kisasa na kufanya biashara yenye tija, hivyo kuondokana na umaskini. Ni matumaini yetu kwamba Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yake ili adha kubwa ya umeme sasa iwe historia.
 
Wewe una jipya wakati upo serikali umefanya nini cha maana mpaka taifa likukumbuke kwa mema yako au ile kauli yako, kila mtu ataubeba msalaba wake
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom