Tumaini Makene
JF-Expert Member
- Jan 6, 2012
- 2,642
- 6,070
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kwa niaba ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) natoa mwito kwa watumishi wa umma kote nchini kupuuza maagizo yaliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu wake wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye ya kuwalazimisha kuhudhuria mikutano ya CCM na kutoa taarifa za kiserikali kama yalivyotolewa katika baadhi redio na televisheni tarehe 2 Disemba 2012 na kunukuliwa na magazeti mbalimbali tarehe 3 Disemba 2012.
Pia namshauri Rais Jakaya Kikwete kwa mamlaka yake ya mkuu wa nchi na kiongozi wa Serikali ambaye ndiye mwajiri wa watumishi wa umma wenye kulipwa mishahara kwa kodi za wananchi wasio na vyama na ambao ni wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa kukemea kauli kama hizo zilizo kinyume na haki za kikatiba, misingi ya utawala bora, sheria na waraka wa utumishi wa umma.
Aidha, CCM kutaka kujitwalia mamlaka ya Serikali kutoa maagizo kwa watumishi wa umma badala ya vyombo vya usimamizi kwa niaba ya wananchi kama bunge, baraza la mawaziri, mabaraza ya madiwani, kamati za ushauri za wilaya, kamati za ushauri za mikoa, bodi za mashirika mbalimbali na mamlaka nyingine ambapo wapo viongozi waliotokana na chama hicho ni ishara ya udhaifu na uzembe wa viongozi wanaotokana na chama hicho katika mikutano ya vyombo hivyo.
Maagizo hayo ya CCM yanazidi kuongeza sababu za wananchi kufanya mabadiliko ya kweli kwa kuunga mkono CHADEMA ikiwa ndicho chama mbadala chenye kuweza kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Maagizo haya ya CCM yanaashiria ulegelege wa chama hicho na kuzidiwa na vuguvugu la mabadiliko linaloongozwa na CHADEMA na madai ya uwajibikaji toka kwa umma kwa kiwango cha kutaka kuirejesha nchi katika maagizo yamfumo wa siasa wa chama kimoja ambapo kundi lote la watumishi wa serikali na vyombo vyake walikuwa wakilazimishwa kushiriki katika shughuli za CCM wakati ambapo kwa sasa watumishi hao wengine ni wanachama wa CHADEMA na wapo ambao sio wanachama wa chama chochote cha siasa.
Rais Kikwete aikumbushe CCM kuwa mapendekezo ya Tume ya Nyalali ya mwaka 1991 na marekebisho ya Katiba ya mwaka 1992 kuingia katika mfumo wa vyama vingi na marekebisho ya sheria yaliyofuata yameweka uhuru wa watumishi wa umma katika kujiunga na vyama vya siasa (isipokuwa watumishi wa kada maalum) na mipaka ya mahusiano kati ya kazi zao za kiserikali na shughuli za vyama vya siasa kikiwemo chama kinachotawala.
Naitaka CCM izingatie kuwa utumishi wa umma katika nchi yetu unaongozwa na Sheria ya Utumishi Serikalini namba 16 ya mwaka 1989 na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma Toleo la 1994 pamoja na marekebisho yake. Kifungu cha 4(1) cha Sheria hiyo kinampa mamlaka Mkuu wa Utumishi wa Umma, ambaye ni Katibu Mkuu kiongozi kutoa waraka kuhusu taratibu mbalimbali za utumishi wa umma.
Chini ya Mamlaka hayo, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Martem Y.C. Lumbanga tarehe 26 Juni, 2000 alitoa Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma na. 1 wa mwaka 2000 wenye kumb. Na. SHC/C.180/2/113 uliohusu maadili ya Watumishi wa Umma katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Waraka huo unawataka watumishi wa umma kutekeleza wajibu wao wa utumishi bila kufanya upendeleo wala ubaguzi wa chama chochote cha siasa. Waraka huo unawakataza watumishi wa umma kuzungumza na kutoa taarifa kwenye mikutano ya vyama vya siasa na haujatoa ruhusa kwa watumishi hao kuzungumza katika mikutano ya CCM pekee; hivyo maagizo yaliyotolewa na chama hicho ni kinyume maagizo ya Serikali inayoongozwa na chama hicho hicho.
Ikiwa Rais Kikwete atahalalisha maagizo hayo haramu ya CCM, watumishi wa umma watawajibika pia kuitwa na kutoa taarifa kwenye mikutano ya CHADEMA na vyama vingine vya upinzani nchini.
Imetolewa na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
04/12/2012
@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@
Ps
Sheria ya 1989 ilifutwa na Sheria ya 2002 na marekebisho yake ya mwaka 2007. Na kanuni za mwaka 1994 zilifutwa na kanuni za mwaka 2009. Hata hivyo hoja ya Waraka wa Watumishi wa Umma katika mfumo wa vyama vingi inabakia pale pale.