Elections 2010 Kauli mbiu mpya ya JK 2010

"Serikali haina hela" huu ndio wimbo ambao nimeusikia sana katika awamu hii. Unajua kuna watu ambao wana external locus of control, yaani wao kila kitu wanasukumizia upande mwingine, they can't accept their mistakes. Wewe unakimbilia kusingizia mapato ya TRA, gharama za serikali (ambazo for sure ni fuel costs za ma-V8 ambayo sijaona sababu mpaka kesho ya kuwa nayo mengi kiasi hiki), wakati hali ya hospitali zetu ni chovu namna hiyo. Then leo tunakuja danganywa na Rais kuwa by 2015 kila mwalimu atakuwa ana computer wakati ameshindwa kutimiza simple tasks kama elimu, huduma safi za afya na kuishia kushangilia wimbo wenye kibwagizo cha "kwa hisani ya watu wa Marekani, China, n.k."

Mkuu hapo haujaweka Mishahara na posho za Mawaziri 60 ambao si watendaji bali wanasiasa. Miradi ya kipuuzi kama vitambulisho, yaani unatumia mabilioni kwenye issue kipuuzi tu.

Kama tungeamua hasa kwa dhati kuwa makini na matumizi basi nchi kama TZ ilitakiwa kuwa na mawaziri wasiozidi 15 tu. wengine wote ni redundant!
 
Ifuatayo ni hotuba ambayo Rais Kikwete ameitoa leo Dodoma akitangaza nia yake ya kugomea tena Urais.

Je, Kikwete amewafanyia nini Watanzania kwenye kipindi cha miaka mitano iliyopita 2000-2010 ili kustahili apewe miaka mitano mingine? Naomba maoni yenu wana JF...



HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE HAFLA YA KUDHAMINIWA FOMU YA KUGOMBEA URAIS KWA TIKETI YA CCM, OFISI YA CCM DODOMA

TAREHE 21 JUNI, 2010

Ndugu Wana-CCM wenzangu,

Muda mchache uliopita nimechukua fomu ya kuomba kuteuliwa tena na Chama chetu kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mambo matatu yamenipa moyo wa kufanya uamuzi huu. Kwanza, ushawishi wa Watanzania wenzangu wengi: wana-CCM na wasiokuwa wana-CCM, wanawake kwa wanaume, vijana kwa wazee wa Mikoa yetu na Wilaya zetu zote kwa kunitaka nigombee tena. Pili, nimeridhika kwamba katika miaka mitano hii, pamoja na kukabiliana na changamoto nyingi, Serikali chini ya uongozi wangu imefanya kazi nzuri ya kusukuma maendeleo ya taifa letu na kuimarisha umoja, amani na utulivu katika nchi yetu. Na tatu, Katiba inaniruhusu, kwani naweza kuwa Rais kwa vipindi viwili mfululizo. Nimemaliza kimoja, hivyo naweza kuomba kupata kipind kingine cha pili.

Nawashukuru sana wana-CCM wenzangu hususan wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kwa imani kubwa waliyonipa mwaka 2005 ya kubeba bendera ya Chama chetu katika uchaguzi wa mwaka ule. Nimejitokeza tena safari hii kuwaomba mnipe ridhaa nyingine. Nilitembea nchi nzima kunadi Ilani ya uchaguzi na Sera za Chama cha Mapinduzi na kwa ushirikiano na wagombea wenzangu wa nafasi za Ubunge na Udiwani tukiongozwa pamoja na viongozi wa Chama wa ngazi zote tangu Taifa hadi Shina na kuungwa mkono na wana-CCM wenzetu na wananchi tulipata ushindi mkubwa. Naahidi kuwa mkiniteua tena safari hii nitafanya hivyo hivyo na naamini kwa dhati kabisa na hasa kama wana-CCM tutaendelea kushikamana na kukipigania Chama chetu kama tulivyofanya mwaka 2005 tutapata ushindi mkubwa kama ule au hata kuzidi ule.

Niliahidi, wakati ule kwamba katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi mliyonikabidhi kuinadi kwa Watanzania, tutatengeneza mipango na programu mbalimbali za utekelezaji wa shabaha na malengo ya Ilani hiyo. Wana-CCM wenzangu wote na Watanzania wote ni mashahidi kwa kiasi gani nilikuwa muaminifu kwa ahadi hiyo. Tumeitekeleza Ilani kwa umakini mkubwa na matokeo yake yanaonekana pembe zote. Takriban mambo yote tuliyoahidi tumetekeleza na pale ambapo yapo ambayo hatujatekeleza, ambayo kwa kweli si mengi, ni kwa sababu za msingi. Hata hivyo, yale ambayo hatukujaaliwa kuyatekeleza safari hii tutayakamilisha tukipewa heshima ya kuliongoza taifa letu katika awamu ijayo.

Ndugu Wana-CCM wenzangu,

Baada ya kuchaguliwa niliahidi kuwa nitatumia vipaji vyangu vyote nilivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuitumikia nchi yangu na watu wake. Ninyi ni mashahidi kwa kiasi gani nimefanya kazi kwa kujituma usiku na mchana, ndani na nje ya nchi yetu kwa ajili hiyo.

Katika miaka mitano hii, hakuna Wilaya au Jimbo la Uchaguzi katika nchi yetu ambalo sikufika. Nimetembea vijiji, vitongoji na maeneo mengi sana kuona mengi. Nimekutana na kuzungumza na wananchi na kujua raha zao, mafanikio yao na karaha zao. Yapo masuala mengi yanayowatatiza wananchi ambayo yameweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia hiyo. Nimeiacha wazi simu yangu kwa wananchi kuwasiliana nami na nimeambiwa mengi ya ushauri na yanayotaka kuchukuliwa hatua. Nimesikiliza na kuchukua hatua muafaka. Hata waliokuwa na shida binafsi niliwasikiliza na kuwasaidia kwa kile nilichoweza. Katika kipindi cha miaka mitano hii tumeshuhudia demokrasia nchini ikizidi kustawi na taasisi za kidemodrasia na utoaji wa haki kama vile Bunge, Mahakama na vyombo vya habari vikiimarika. Watu wamekuwa huru zaidi kutoa maoni yao na uhuru wa kuabudu umeendelea kuheshimiwa. Vyombo vya ulinzi na usalama vimeendelea kuimarishwa na mapambano dhidi ya uhalifu na maovu mengine katika jamii ikiwemo rushwa yaliendelea kwa uthabiti zaidi.

Na kwa kweli tumepata mafanikio makubwa katika kutimiza yale tuliyowaahidi Watanzania. Kote ninakotembea katika nchi yetu, napata faraja kuwasikia wananchi wenzangu wengi wakiyazungumzia, wakiyafurahia na wakinufaika na mafanikio tuliyoyapata katika kipindi hiki cha uongozi wangu. Hata mimi mwenyewe ninapotazama na kuona tuliyoweza kufanya katika kipindi hiki nashangaa. Hakika pamoja na juhudi zetu kuna baraka za Mwenyezi Mungu. Naamini Mungu asipotuacha mkono kipindi kijacho tutafanya makubwa zaidi.

Ndugu Wana-CCM wenzangu,

Upo msemo kwamba kama unavuka mto ukiwa umepanda farasi sio busara kushuka na kubadili farasi katikati ya mto, hasa kama farasi huyo amehimili mawimbi.

Katika miaka mitano iliyopita, tumehimili mawimbi makubwa yaliyotishia umoja wa nchi yetu. Tanzania yetu leo hii bado ni ile ile nchi yenye amani na utulivu tunayoijua sote na ambayo dunia inaijua hivyo. Tumejifunza mengi, na tumepikwa katika tanuru la moto na tumeiva kama chuma cha pua. Na tumefaulu mtihani na changamoto za uongozi wa Taifa letu. Na tumedhihirisha kwamba tunao uwezo wa kuivusha nchi yetu kuelekea kwenye neema.

Leo hii kuna shule nyingi zaidi za msingi na sekondari na vijana wengi zaidi wanaingia shule za msingi, Sekondari na Vyuo Vikuu kuliko 2005 na kuna walimu wengi zaidi. Huduma ya afya ni bora zaidi na zipo hospitali, vituo vya afya na zahanati nyingi zaidi na upatikanaji wa dawa umeboreka zaidi. Afya za Watanzania zinaimarika na watu wachache zaidi wanakufa kwa malaria, Ukimwi, TB na maradhi mengine ambayo huko nyuma yalikuwa yanauwa watu wengi. Barabara nyingi zaidi vijijini na mijini zimejengwa na kuimarishwa na kufanya maeneo mengi zaidi kufikika na kupitika mwaka mzima. Barabara za lami na changarawe zimeongezeka na madaraja mengi zaidi yametengenezwa. Kuna visima vingi, mabwawa mengi yaliyochimbwa na miradi mingi ya maji ya bomba imejengwa na kuimarishwa. Idadi ya watu wanaopata maji safi na salama imeongezeka zaidi mijini na vijijini kuliko mwaka 2005. Umeme umeendelea kusambazwa na kufika kwenye wilaya nyingi zaidi nchini kuliko mwaka 2005.

Mfuko wa ruzuku ya mbolea na pembejeo nyingine kwa wakulima na wafugaji umeongezewa sana pesa. Matokeo yake wakulima wengi wameongeza matumizi ya mbolea, mbegu bora, madawa ya kuulia wadudu na wafugaji wanapata dawa za kinga na tiba ya mifugo yao. Mfumo wa ununuzi wa mazao ya wakulima umeboreshwa na kufanya wakulima wa mazao yetu makuu kupata masoko ya uhakika na bei nzuri.

Uchumi wa taifa, pato la taifa na pato la Mtanzania limeendelea kuongezeka na kuwa kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 2005 na idadi ya Watanzania wanaoishi katika umaskini uliokithiri imepungua, ingawa sio kwa kasi tuliyotarajia. Bajeti ya Serikali nayo imeongezeka sana kutoka shilingi trilioni 4.8 mwaka 2005/2006 hadi shilingi trilioni 11.1 mwaka 2010/2011. Tumezidi kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje katika bajeti yetu. Mafanikio ni mengi sana, na itakapofika wakati wa kampeni tutayaeleza yote kwa kina.

Ndugu Wana-CCM wenzangu,

Naomba niwashukuru wanachama wa CCM wote walionishawishi kuchukua fomu pamoja na ninyi mliofika hapa kunidhamini. Nimefarijika sana kuona kwamba ninyi, pamoja na wana-CCM wenzangu wengine wengi nchini, mmeniamini kwamba ninafaa kuendelea kuliongoza Taifa letu kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Hayo yote ndiyo yaliyonishawishi nami kushawishika kujitokeza kuomba tena kupewa nafasi ya kuliongoza taifa letu. Safari ile nilisema mkinichagua nitafanya kazi kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na kasi Mpya na matokeo yake tumeyaona. Safari hii nasema mkinichagua nitawatumikiwa Watanzania kwa Ari Zaidi, Nguvu Zaidi na Kasi Zaidi katika dhamira yetu ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania. Kwa pamoja tuzidi kusonga mbele.

Ndugu Wana-CCM,

Napenda kuwashukuru wanachama wote wa CCM walionichangia fedha za kuchukua fomu hii. Nawashukuru sana. Wamejinyima ili kunichangia. Nauthamini sana mchango wenu.

Ndugu Wana-CCM wenzangu,

Naomba nimalizie kwa kuwaahidi kwamba, mkinipa nafasi ya kuwa mgombea wa Chama chetu, sitawaangusha. Nitatumia bidii yangu yote kufanya kampeni ya kukipigania Chama chetu kipate ushindi mkubwa.

Na, mara tutakapofanikiwa, vipaumbele vya Serikali ijayo vitasukumwa na misingi kumi na moja ifuatayo:

1. Kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kuwa na umoja, amani na usalama, na Muungano wetu unaendelea kuimarika.

2. Kujenga misingi ya uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea kwa kuchukua hatua madhubuti za kuharakisha zaidi mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda. Nataka tuanze safari ya kuelekea kuwa taifa la uchumi wa kati, ambalo viwanda ndio mhimili mkuu.

3. Kuongeza jitihada na mipango zaidi ya kuwawezesha kiuchumi wananchi hasa wa hali ya chini, ili waweze kushiriki na kunufaika na uchumi wetu unaokua. Lakini vilevile tutaweka mkazo katika kulitambua na kuliwezesha kwa namna yake kundi la wajasiriamali wa tabaka la kati ili waweze kushiriki katika uwekezaji mkubwa katika nchi yetu.

4. Kutumia fursa ya kijiografia ya nchi ya nchi yetu kwa kuifanya lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika ya Mashariki, Kusini na Kati, hasa kwa kuimarisha ufanisi wa reli na bandari zetu.

5. Kuongeza jitihada za kuhakikisha Taifa letu linanufaika zaidi na rasilimali za asili za nchi yetu, kuanzia madini, misitu, wanyamapori hadi vivutio mbalimbali vya utalii.

6. Kuweka mkazo sasa kwenye kuboresha elimu ya msingi na sekondari, na kupanua elimu ya ufundi na elimu ya juu, hasa katika masomo ya sayansi.

7. Kuongeza jitihada za kupanua na kuboresha huduma muhimu za kijamii hasa huduma za afya na maji, na huduma za kiuchumi hasa umeme, miundombinu ya usafirishaji na mawasiliano na huduma ya fedha.

8. Kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria, na demokrasia nchini, hasa kwa kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, na ubadhirifu wa mali ya umma; na kuendelea kuviwezesha kirasilimali, kitaasisi/kimuundo na kisheria vyombo vya kutoa na kusimamia haki nchini;

9. Kuipa dola na vyombo vyake husika uwezo mkubwa zaidi wa kupanga mipango ya uchumi na kusimamia uchumi wa nchi kwa ufanisi, bila kuingilia sekta binafsi, ili kulinda maslahi ya nchi yetu na watu wake.

10. Kulinda mafanikio tuliyoyapata katika nyanja zote tangu uhuru wa nchi yetu, ikiwemo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na kukamilisha yale tuliyoyaahidi mwaka 2005 ambayo, kwa sababu moja au nyingine, hatukuweza kuyakamilisha katika miaka hii mitano.

11. Kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi yetu na majirani zetu, na mataifa mengine duniani, pamoja na taasisi mbalimbali za kimataifa, na kuendelea kutafuta marafiki wapya kwa manufaa ya nchi yetu.

Ndugu Wana-CCM wenzangu,

Haya ni mambo ya msingi kwa maendeleo ya Taifa letu. Nitahakikisha kwamba Ilani ya Uchaguzi tutakayoitengeza na mipango ya Serikali baada ya hapo inayabeba yote haya.

Naomba nimalize tena kwa kuwashukuru kwa mara nyingine kwa kujitokeza kushuhudia tukio hili. Nawashukuru kwa imani mliyoionyesha kwangu. Ninayo nguvu, ari na dhamira ya kuitumikia nchi yangu. Na niko tayari kuendelea kuwa mtumishi wenu. Pamoja, Tuzidi Kusonga Mbele!

Kidumu Chama cha Mapinduzi!

Mungu Ibariki Afrika!

Mungu Ibariki Tanzania!
 
Hivi kuna mategemeo yoyote ya Chadema kuweka mgombea wa Urais na kumshinda Jakaya?Au ndiyo yale yale ya Vuvuzela?
 
Na wabongo wataimba hiyo tu, huruma!

Je ana maana kuwa madudu yote tuliyoyashuhudia toka aingie madarakani yataongezeka kwa ari zaidi nguvu zaidi na kasi zaidi - yaani tutegemee ufisadi zaidi, wizi zaidi, usanii zaidi na uzembe kama kazi au?

Yaani ari zaidi kwa safari kama za Vasco Dagama, matumizi kama ya mlevi vile na utawala usiojali sheria, wenye ubia na mafisadi na upendeleo kwa washikaji hadi 2015 ?

Mbona hapo tutakuwa tumeliwa au ndio tunajitafuna wenyewe kama mapunguani ? Talk of the dumb, the blind and the stupid, that's what we are for sure.
 
What Speed?

There is zero sense of urgency with anything the government does.

MORE CORRUPTION, MORE INCOMPETENCE, MORE LAZINESS
 
Ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi kwenye lipi?

Aliahidi kuipitia upya mikataba ya kuchimba dhahabu ambyo ilikuwa inalalamikiwa na Watanzania kwamba haina maslahi kwa Tanzania. Baada ya miaka mitano ya kuwepo madarakani bado tunaambulia 3% ya mapato yote yanayotokana na dhahabu yetu na wachukuaji kuendelea kufaidi 97%. Pamoja na kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia ongezeko hilo halina manufaa yoyote kwa Watanzania wanaofaidi na Wachukuaji na shareholders wao.

Alipoingia madarakani wagonjwa wengi na hata waja wazito walikuwa ama wanashare vitanda au kulala chini na baada ya miaka mitano hakuna ahueni yoyote katika hali hii.

Alipoingia madarakani hospitali zetu nyingi zilikuwa hazina madawa au vitendea kazi muhimu nah ii kusababisha waheshimiwa wengi kukimbilia nje kwa ajili ya matibabu yao. Baada ya kuwepo madarakani kwa miaka mitano hali hii bado iko vile vile hakuna ahueni yoyote.

Alipoingia kulikuwa na manung'uniko mengi toka kwa Wafanyakazi wa sekta mbali mbali nchini kuhusu kuhusiana na mishahara midogo ambayo haiendani na hali halisi ya gharama za maisha hadi hii leo hakuna lolote lililofanywa la kuongeza mishahara ili ilingane na gharama halisi za maisha na kama mtakumbuka hivi karibuni kulikuwa na tishio la mgomo wa Wafanyakazi kote nchini. Kwa maneno mengine hili nalo pamoja na kuwepo madarakani miaka mitano halijafanyiwa kazi.

Alipoingia madarakani Wanafunzi wengi katika shule za msingi na sekondari katika mikoa yote nchini walikuwa wanakaa chini na na wengi hawana hata madarasa na hivyo kusomea chini ya miti. Halii hii baada ya kuwepo madarakani kwa miaka mitano haijapatiwa ufumbuzi wowote.

Alipoingia madarakani alisema atapambana na rushwa na ufisadi lakini hali nalo halijafanyiwa kazi maana rushwa badi imekithiri nchini na mafisadi wote waliohusika na EPA, Richmond, Kiwira, Ununuzi wa rada, Ununuzi wa ndege ya Rais na heli za jeshi n.k.

Alipoingia madarakani nchi ilikuwa na matatizo mengi ya umeme na upatikanaji maji safi kwa matumizi ya binadamu. Hadi hii leo baada ya kukaa madaraki kwa miaka mitano bado matatizo haya ni sugu na kero kubwa kwa Watanzania.

Sasa Rais anaposema "mmetutuma tumetekeleza" hivi ni kipi walichotekeleza ikiwa matatizo yote ambayo aliingia madaraka na kutakuta baada ya miaka mitano yako vile vile na hakuna ahueni yeyote?

Kama huu siyo usanii ndugu Watanzania sijui tuite nini!!! Kwanini CCM hawataki kuwa wakweli hata pale ambapo ukweli umedhihiri?
 
What???? naota au ni kweli!! Hivi tujiite ni wajinga tumekosa akili tumekosa uelewa au ni vipi? kazi ipo wajameni...
 
Hapo tayari Komba keshaitungia nyimbo!...na wabongo wataiandika hadi kwenye magari yao!...Ni kauli za kupitisha muda na kuhalalisha uwizi wa mchana kweupe!
 
Kasi Mpya, Nguvu Mpya na Ari Mpya 2005 yazaa Ari Zaidi, Nguvu Zaidi na Kasi Zaidi 2010. Kaazi kweli kweli - kwa habari zaidi soma hapa;

JK aboresha kaulimbiu, AJA NA ARI ZAIDI, NGUVU ZAIDI NA KASI ZAIDI

Kwa kaulimbiu hatuwezekani - bahati mbaya kaulimbiu peke yake haiondoi umasikini wala haizimi njaa !


Hivi ndani ya Sekretarieti ya Propaganda ya CCM kuna waimbaji wa taarabu wangapi? To hii kauli mbiu inanikumbusha nyimbo za Bi Hadija Kopa na Nasma Hamis!
 
Nani tumlaumu ? Ata angekuja na slogan mbaya kuliko tulizowahi kusikia lakini bado atachukua hiyo nafasi. Upinzani upinzani...upizani my a**
 
Katika WANASIASA HALISI wa Tanzania JK ni mmoja wao. Kila analolitamka ni GUMZO humu ndani na kwingineko!! Hii inanikumbusha enzi zile za Mwalimu kuanzia mwaka 1967 Azimio la Arusha lilipoanzishwa.

Tuliimba sana, tukatembea sana. Ikaja Mwongozo Mpya wa TANU, vijiji vya ujamaa, siasa ni kilimo, ambayo yoote aliondoka nayo madarakani hatimaye akafa nayo.
 
Wana JF,

Katika pitapita yangu leo nimeweza kugudua kauli mbiu ya Mh Jakaya atakayo tumia katika uchaguzi mkuu mwaka huu kama ifuatayo:

KASI ZAIDI
NGUVU ZAIDI
ARI ZAIDI
TULIAHIDI TUMETEKELEZA!


Hii ndio kauli mbiu itakayotumika mwaka huu ktk uchaguzi

"Mvinyo wa Zamani Ndani Ya Chupa Mpya" Hakuna dodose hapo.
 
Back
Top Bottom