Azizi Mussa
JF-Expert Member
- May 9, 2012
- 9,172
- 7,428
Katika mazingira ambayo hata mtu akianzisha mjadala wa maana; Watanzania hawataki hata kuchangia achilia mbali kuchukua hatua; tutarajie nini?
Katika mazingira ambayo hakuna kuaminiana na ikitokea mtu anaaminiwa anageuka na anakuwa haaminiki, tutarajie nini?
Katika mazingira ambayo watanzania wengi hujikuta wakivutiwa na kutumia muda mwingi zaidi kufuatilia na kujadili udaku kuliko mambo ya msingi, tutarajie nini?
Katika mazingira ambayo kila mtu humfanyia mwenzake unafiki huku akidhani mwenzake ni mwaminifu kumbe naye mnafiki pia tutarajie nini?
Katika mazingira ambayo mwananchi na kiongozi wake wote wanaamini siasa ni ulaghai na uongo, na kupata nafasi ya uongozi maana yake ni "kuula" tutarajie nini?
Katika mazingira ambayo hakuna mtu ambaye ana hisia za ndani za kutenga angalau masaa mawili kila siku kufanya kitu chenye manufaa kwa wengine, tutarajie nini?
Dunia kwa asili yake haitupi kile tunachotamani, bali kile tunachostahili. Kujua ni kipi tunachostahili tunatakiwa tuangalie ni kipi tunapanda kwa kuwa apandacho mtu ndicho avunacho.Usifikirie atapanda mwenzako, panda wewe ili baadae tukutane kwenye kuvuna, ila kama kila mtu akidhani mwenzake atapanda, mwishowe unaweza ukakuta hakuna aliepanda, au aliepanda kapanda miiba.
Nchi hii ipo hivi leo kwa kuwa tumeamua kuwa hivi tulivyo na vile itakavyokuwa kesho, itategemeana na vile tutakavyoamua kuwa sasa. Ikumbukwe kesho huandaliwa leo. Kama hatuwazi kesho na kesho kutwa tunataka tuweje kama nchi, tunafanyaje ili tuwe na tukaanza kufanya; hali tutakayokutana nayo sasa na baadae hakutakuwa na wakumlalamikia kwa kuwa ndicho tutakachokuwa tumejichagulia.
Kila mtu aanze kutimiza wajibu wake sasa wakati anasoma uzi huu na wewe ukifanya na mwingine na mwingine hatimaye tutakuwa tunasogea lakini tukiendelea hivi hivi tutakuwa tunaendelea kupita njia mbaya.